< Amosi 1 >

1 Maneno ya Amosi, mmoja wa wachunga wanyama wa Tekoa: yale aliyoyaona kuhusu Israeli miaka miwili kabla ya tetemeko la ardhi, wakati Uzia alikuwa mfalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yehoashi alikuwa mfalme wa Israeli.
Haya ni mambo yanayoihusu Israeli ambayo Amosi, mmoja wa wachungaji katika Tekoa, aliyapokea katika ufunuo. Alipokea haya mambo katika siku za Uzia mfalme wa Yuda, na pia katika siku za Yeroboamu mwana wa Yoashi mfalme wa Israeli, miaka miwili kabla ya tetemeko la aridhi.
2 Alisema: “Bwana ananguruma toka Sayuni, pia ananguruma kutoka Yerusalemu; malisho ya wachunga wanyama yanakauka, kilele cha Karmeli kinanyauka.”
Alisema, “Yahwe atanguruma kutoka Sayuni; atainua sauti yake kutoka Yerusalemu. Malisho ya wachungaji yatanyamaza kimya; kilele cha Karmeli kitanyauka.”
3 Hili ndilo asemalo Bwana: “Kwa dhambi tatu za Dameski, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu aliipura Gileadi kwa vyombo vya chuma vyenye meno.
Hivi ndivyo Yahwe asemavyo: “Kwa dhambi tatu za Damaskasi, hata kwa nne, sintobadilisha adhabu, kwa sababu wameipura Gileadi kwa vyombo vya chuma.
4 Nitatuma moto juu ya nyumba ya Hazaeli ambao utateketeza ngome za Ben-Hadadi.
Nitapeleka moto kwenye nyumba ya Hazaeli, na utaiteketeza ngome za Ben Hadadi.
5 Nitalivunja lango la Dameski; nitamwangamiza mfalme aliyeko katika Bonde la Aveni, na yeye ambaye anaishika fimbo ya utawala katika Beth-Edeni. Watu wote wa Aramu watakwenda uhamishoni huko Kiri,” asema Bwana.
Nitazivunja komeo za Damaskasi na kumkatilia mbali mtu ambaye aishiye katika Biqati Aveni, na pia yule mtu ashikaye fimbo ya kifalme katika Beth Edeni. Na watu wa shamu watakwenda utumwani hata Kiri,” asema Yahwe.
6 Hili ndilo asemalo Bwana: “Kwa dhambi tatu za Gaza, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu walichukua mateka jumuiya nzima na kuwauza kwa Edomu,
Hivi ndivyo Yahwe asemavyo: “Kwa dhambi tatu za Gaza, hata nne, sintobadilisha adhabu, kwa sababu waliwachukua mateka watu wote, kuwaweka juu ya mkono wa Edomu.
7 nitatuma moto juu ya kuta za Gaza ambao utateketeza ngome zake.
Nitatuma moto kwenye kuta za Gaza, na kuziteketeza ngome zake.
8 Nitamwangamiza mfalme wa Ashdodi na yeye aishikaye fimbo ya utawala katika Ashkeloni. Nitaugeuza mkono wangu dhidi ya Ekroni, hadi Mfilisti wa mwisho atakapokufa,” asema Bwana Mwenyezi.
Nitamkatilia mbali yule mtu aishiye katika Ashdodi na mtu ashikaye fimbo ya kifalme kutoka Ashkeloni. Nitaugeuza mkono wangu dhidi ya Ekroni, na mabaki ya Wafilisti wataangamia,” asema Bwana Yahwe.
9 Hili ndilo asemalo Bwana: “Kwa dhambi tatu za Tiro, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu ameuza jumuiya nzima ya mateka kwa Edomu, na kutokujali mapatano ya undugu,
Hivi ndivyo Yhawe asemavyo: “Kwa dhambi tatu za Tiro, hata kwa nne, sintobadili adhabu, kwa sababu waliwapelekea watu wote wa Edomu, na wamevunja agano lao la undugu.
10 Nitatuma moto kwenye kuta za Tiro ambao utateketeza ngome zake.”
Nitapeleka moto kwenye kuta za Tiro, nao utaziteketeza ngome zake.”
11 Hili ndilo Bwana asemalo: “Kwa dhambi tatu za Edomu, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu alimfuatia ndugu yake kwa upanga, alikataa kuonyesha huruma yoyote, kwa sababu hasira yake kali iliendelea kupanda wakati wote na ghadhabu iliwaka bila kuzuiliwa.
Hivi ndivyo Yahwe asemavyo, “Kwa dhambi tatu za Edomu, hata kwa nne, sintobadilisha adhabu, kwa sababu alimfuatilia ndugu yake kwa upanga na kutupilia mbali huruma zote. Hasira yake ikaendelea kuwa kali, na ghadhabu yake ikabaki milele.
12 Nitatuma moto juu ya Temani ambao utateketeza ngome za Bosra.”
Nitapeleka moto juu ya Temani, na utaziteketeza nyumb a za kifalme za Bozra.”
13 Hili ndilo asemalo Bwana: “Kwa dhambi tatu za Amoni, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu aliwatumbua wanawake wajawazito wa Gileadi ili kuongeza mipaka yake.
Hivi ndivyo Yahwe asemavyo, “Kwa dhambi tatu za watu wa Amoni, hata kwa nne, sintobadilisha adhabu, kwa sababu wamewapasua wanawake wa Gileadi wenye mimba, ili waweze kupanua mipaka yao.
14 Nitatuma moto kwenye kuta za Raba ambao utateketeza ngome zake katikati ya vilio vya vita katika siku ya mapigano, katikati ya upepo mkali katika siku ya dhoruba.
Nitawasha moto katika kuta za Raba, nao utaziteketeza nyumba za kifalme, pamoja na kupiga kelele katika siku ya vita, pamoja na dhoruba katika siku ya kimbunga.
15 Mfalme wake atakwenda uhamishoni, yeye pamoja na maafisa wake,” asema Bwana.
Mfalme wao ataenda utumwani, yeye na maafisa wake pamoja,” asema Yahwe.

< Amosi 1 >