< Amosi 5 >

1 Sikia neno hili, ee nyumba ya Israeli, ombolezo hili ninalifanya kuwahusu ninyi:
Sikilizeni hili neno ambalo nisemalo kama maombelezo juu yenu, nyumba ya Israeli.
2 “Bikira Israeli ameanguka, kamwe hatainuka tena, ameachwa pweke katika nchi yake, hakuna yeyote wa kumwinua.”
Bikira wa Israeli ameanguka; hatoinuka tena; ametoroka kwenye nchi yake, hakuna mtu wa kumwinua.
3 Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: “Wakati mmoja wa miji yako utakapopeleka watu elfu moja vitani kwa ajili ya Israeli, mia moja tu watarudi; wakati mji utakapopeleka mia moja, kumi tu ndio watarudi hai.”
Kwa kuwa hivi ndivyo Yahwe asemavyo: “Mji ambao umetoka nje kwa elfu watabaki mia, na walioenda nje mia watabaki kumi wa mali ya nyumba ya Israeli.”
4 Hili ndilo Bwana asemalo kwa nyumba ya Israeli: “Nitafuteni mpate kuishi;
Kwa kuwa hivi ndivyo Yahwe asemavyo kwa nyumba ya Israeli: “Nitafuteni na mtaishi!
5 msitafute Betheli, msiende Gilgali, msisafiri kwenda Beer-Sheba. Kwa maana kwa hakika Gilgali itakwenda uhamishoni, na Betheli itafanywa kuwa si kitu.”
Msimtafute Betheli; wala kuingia Gilgali; msisafiri kwenda Bersheba. Kwa kuwa Gilgali watakwenda utumwani hakika, na Betheli haitakuwa kitu.
6 Mtafuteni Bwana mpate kuishi, au atafagia nyumba ya Yosefu kama moto; utawateketeza, nayo Betheli haitakuwa na yeyote wa kuuzima.
Mtafuteni Yahwe mtaishi, au atawaka kama moto kwenye nyumba ya Yusufu. Utateketeza, na hakutakuwa na mtu hata mmoja kuuzima katika Betheli.
7 Ninyi ambao mnageuza haki kuwa uchungu na kuiangusha haki chini
Wale watu wageuzao haki kuwa jambo chungu na kuiangusha haki chini!”
8 (yeye ambaye alifanya Kilimia na Orioni, ambaye hugeuza giza kuwa mapambazuko na mchana kuwa usiku, ambaye huyaita maji ya bahari na kuyamwaga juu ya uso wa nchi: Bwana ndilo jina lake;
Mungu aliiumba Pleidezi na Orioni; amebadilisha giza kuwa asubuhu; hufanya siku kuwa giza na usiku na kuita maji ya bahari; yeye huyamwaga juu ya uso wa dunia. Yahwe ndilo jina lake!
9 yeye hufanya maangamizo kwenye ngome na kufanya mji uliozungushiwa ngome kuwa ukiwa),
Yeye huleta uharibifu wa ghafla juu ya waliohodari ili kwamba uharibifu uje juu ya ngome.
10 mnamchukia yule akemeaye mahakamani, na kumdharau yule ambaye husema kweli.
Wanamchukia kila awasahihishaye katika lango la mji, nao humchukia sana yeyote asemaye ukweli.
11 Mnamgandamiza maskini na kumlazimisha awape nafaka. Kwa hiyo, ingawa mmejenga majumba ya mawe ya fahari, hamtaishi ndani yake; ingawa mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu, hamtakunywa divai yake.
Kwa sababu mnamkanyaga chini maskini na kuchukua sehemu ya ngano kutoka kwake- ingawa mmejenga nyumba za mawe yaliyochongwa, hamtaishi kwenye nyumba hizo. Mmependezwa na mashamba ya mizabibu, lakini hamtakunywa mvinyo wake.
12 Kwa kuwa ninajua hesabu ya makosa yenu na ukubwa wa dhambi zenu. Mmewaonea wenye haki na kupokea rushwa na kuzuia haki ya maskini mahakamani.
Kwa kuwa najua ni jinsi gani mlivyo na makosa mengi na jinsi dhambi zenu zilivyo kubwa- ninyi mnaowaonea wenye haki, chukueni rushwa, na kuwageuza wahitaji kwenye lango la mji.
13 Kwa hiyo mtu mwenye busara hunyamaza kimya nyakati kama hizo, kwa kuwa nyakati ni mbaya.
Kwa hiyo kila mtu mwenye busara atanyamaza kimya kwenye wakati kama huo, kwa kuwa ni wakati wa uovu.
14 Tafuteni mema, wala si mabaya, ili mpate kuishi. Ndipo Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote atakuwa pamoja nanyi, kama msemavyo yupo nanyi.
Tafuteni mazuri na sio mabaya, ili kwamba mpate kuishi. Hivyo Yahwe, Mungu wa majeshi, atakuwa na ninyi tayari, kama msemavyo yeye ndiye.
15 Yachukieni maovu, yapendeni mema; dumisheni haki mahakamani. Yamkini Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote atawahurumia mabaki ya Yosefu.
Chukieni uovu, imarisheni haki katika lango la mji. Huenda Yahwe, Mungu wa majeshi, atawafadhili mabaki ya Yusufu.
16 Kwa hiyo hili ndilo Bwana, Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, asemalo: “Kutakuwepo maombolezo katika barabara zote na vilio vya uchungu katika njia kuu zote. Wakulima wataitwa kuja kulia, na waombolezaji waje kuomboleza.
Kwa hiyo, hivi ndivyo Yahwe asemavyo, Mungu wa majeshi, Bwana, “Kutakuwa na maombolezo kwenye miraba yote, na watasema kwenye mitaa yote, 'Ole! Ole!' Watawaita wakulima kuomboleza na walio hodari wa kulia na kuomboleza.
17 Kutakuwepo kuomboleza katika mashamba yote ya mizabibu, kwa kuwa nitapita katikati yenu,” asema Bwana.
Katika mashamba yote ya mizabibu kutakuwa na kilio, kwa kuwa nitapita katikati yako,” asema Yahwe.
18 Ole wenu ninyi mnaoitamani siku ya Bwana! Kwa nini mnaitamani siku ya Bwana? Siku hiyo itakuwa giza, si nuru.
Ole wenu ninyi mnaoitamani siku ya Yahwe! Kwa nini mnaitamani? Itakuwa giza na sio nuru,
19 Itakuwa kama vile mtu aliyemkimbia simba kumbe akakutana na dubu, kama vile mtu aliyeingia nyumbani mwake na kuupumzisha mkono wake kwenye ukuta, kumbe akaumwa na nyoka.
kama wakati mtu anamkimbia simba na kukutana na dubu, au aliingia katika nyumba na kuweka mkono wake kwenye ukuta na kung'atwa na nyoka.
20 Je, siku ya Bwana haitakuwa giza, na si nuru: giza nene, bila mwonzi wa mwanga?
Je siku ya Yahwe itakuwa giza na sio nuru? Huzuni na sio furaha?
21 “Ninachukia, ninazidharau sikukuu zenu za dini; siwezi kuvumilia makusanyiko yenu.
“Nachukia, nazidharau sikukuu zenu, naichukia mikutano yenu ya dini.
22 Hata ingawa mnaniletea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za nafaka, sitazikubali. Ingawa mnaniletea sadaka nzuri za amani, sitazitambua.
Hata kama mnanitolea sadaka ya kuteketeza na sadaka za unga, sintozipokea, wala kuzitazama kwenye sadaka za ushirika wa wanyama walionona.
23 Niondoleeni kelele za nyimbo zenu! Sitasikiliza sauti za vinubi vyenu.
Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; sintosikiliza sauti za vinubi vyenu.
24 Lakini acheni haki itiririke kama mto, na uadilifu uwe kama kijito kisichokauka!
Badala yake, acheni haki itiririke kama maji, na haki kama mkondo utiririkao siku zote.
25 “Je, mliniletea dhabihu na sadaka kwa miaka arobaini kule jangwani, ee nyumba ya Israeli?
Je mmeniletea dhambihu na sadaka za kuteketeza jangwani kwa mda wa miaka arobaini?
26 Mmeyainua madhabahu ya mfalme wenu, Sikuthi mungu wenu mtawala, na Kiuni mungu wenu wa nyota, ambao mliwatengeneza wenyewe.
Mtamwinua Sikuthi kama mfalme wenu, na Kiuni, nyota yenu ya miungu-ambayo mmeifanya kwa ajili yenu wenyewe.
27 Kwa sababu hiyo nitawapeleka uhamishoni mbali kupita Dameski,” asema Bwana, ambaye jina lake ni Mungu Mwenye Nguvu Zote.
Kwa hiyo nitawahamisha upande wa pili wa Damaskasi,” asema Yahwe, ambaye jina lake ni Mungu wa majeshi.

< Amosi 5 >