< Amosi 3 >

1 Sikilizeni neno hili alilosema Bwana dhidi yenu, enyi watu wa Israeli, dhidi ya jamaa nzima niliowapandisha toka Misri:
Sikieni neno la Yahwe aliloongea juu yenu, watu wa Israeli, juu ya familia nzima ambayo niliwatoa kutoka nchi ya Misri,
2 “Ni ninyi tu niliowachagua kati ya jamaa zote za dunia; kwa hiyo nitawaadhibu kwa ajili ya dhambi zenu zote.”
“Nimewachagua ninyi tu kutoka familia zote za dunia. Kwa hiyo nitawaadhibu kwa dhambi zenu zote.”
3 Je, watu wawili hutembea pamoja wasipokubaliana kufanya hivyo?
Je wawili wanaweza kutembea pamoja isipokuwa wamekubaliana?
4 Je, simba hunguruma katika kichaka wakati hana mawindo? Aweza kuvuma katika pango wakati ambao hajakamata chochote?
Je simba huunguruma msituni wakati hakuna mawindo? Je mwana simba ataunguruma kutoka pangoni mwake kama hajakamata kitu?
5 Je, ndege aweza kuanguka kwenye mtego ulio ardhini ambapo hajategewa chambo? Je, mtego unaweza kufyatuka toka ardhini wakati ambapo hakuna chochote cha kunasa?
Je ndege ataanguka kwenye mtego aridhini wakati hakuna chambo kimewekwa kwa ajili yake? Je mtego utafyatuka juu aridhini wakati hakuna kitu cha kukamata?
6 Je, tarumbeta inapopigwa mjini kujulisha hatari, watu hawatetemeki? Mji upatwapo na maafa, je, si Bwana amesababisha?
Je tarumbeta itapigwa mjini na watu wasitetemeke? Je janga laweza kuja mjini lisiyoletwa na Yahwe?
7 Hakika Bwana Mwenyezi hatafanya neno lolote bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.
Hakika Bwna Yahwe hatafanya kitu vinginevyo amewafunulia mpango watumishi wake manabii.
8 Simba amenguruma: je, ni nani ambaye hataogopa? Bwana Mwenyezi ametamka: je, ni nani awezaye kukosa kutoa unabii?
Simba ameshaunguruma; nani hatoogopa? Bwana Yahwe amekwisha ongea; nani hatotabiri?
9 Tangazeni katika ngome za Ashdodi na katika ngome za Misri: “Kusanyikeni juu ya milima ya Samaria; angalieni wingi wa wasiwasi ulio ndani yake, na uonevu ulio miongoni mwa watu wake.”
Tangaza hii katika ngome huko Ashdodi, na katika ngome za nchi ya Misri; sema, “Kusanyikeni kwenye milima ya Samaria na oneni vile mchafuko ulivyomkubwa kwake, na ukandamizaji uliopo katika yeye.
10 Bwana asema: “Hawajui kutenda lililo jema, wale ambao hujilundikia nyara na vitu vilivyotekwa katika ngome zao.”
Kwa kuwa hawajui jinsi ya kufanya haki -hivi ndivyo Yahwe asemavyo- hao watunzao nguvu na uharibifu katika ngome zao.”
11 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: “Adui ataizingira nchi; ataangusha chini ngome zenu na kuteka nyara maboma yenu.”
Kwa hiyo, hivi ndivyo Yahwe asemavyo, “Adui ataizunguka nchi. Atazivuta chini nguvu zako na ngome zenu zitatekwa nyara.”
12 Hili ndilo asemalo Bwana: “Kama vile mchungaji aokoavyo kinywani mwa simba vipande viwili tu vya mfupa wa mguu au kipande cha sikio, hivyo ndivyo Waisraeli watakavyookolewa, wale wakaao Samaria kwenye kingo za vitanda vyao, na katika Dameski kwenye viti vyao vya fahari.”
Hivi ndivyo Yahwe asemavyo,” Kama mchungaji aokoavyo miguu miwili tu kwenye mdomo wa simba, au kipande cha sikio, ndivyo wana wa Israeli watakavyookolewa wale waishio katika Samaria, pamoja na pembe ya kulalia, au pembe ya kitanda.”
13 “Sikia hili na ushuhudie dhidi ya nyumba ya Yakobo,” asema Bwana, Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote.
Sikieni na kushudia juu ya nyumba ya Yakobo -hivi ndivyo Yahwe asemavyo, Mungu wa majeshi,
14 “Siku nitakapomwadhibu Israeli kwa sababu ya dhambi zake, nitaharibu madhabahu za Betheli; pembe za madhabahu zitakatiliwa mbali na kuanguka chini.
“Kwa kuwa katika siku ambayo nimeadhibu dhambi za Israeli, pia nitaziadhibu madhabahu za Betheli. Pembe za madhabahu zitakatwa na kuanguka chini.
15 Nitabomoa nyumba ya wakati wa masika, pamoja na nyumba ya wakati wa kiangazi; nyumba zilizonakshiwa kwa pembe za ndovu na majumba makubwa ya fahari yatabomolewa,” asema Bwana.
Nitaiharibu nyumba ya baridi pamoja na nyumba ya hari. Nyumba za pembe zitaangamia, na nyumba kubwa zitatoweka, -hivi ndivyo Yahwe asemavyo.”

< Amosi 3 >