< Amosi 3 >
1 Sikilizeni neno hili alilosema Bwana dhidi yenu, enyi watu wa Israeli, dhidi ya jamaa nzima niliowapandisha toka Misri:
2 “Ni ninyi tu niliowachagua kati ya jamaa zote za dunia; kwa hiyo nitawaadhibu kwa ajili ya dhambi zenu zote.”
3 Je, watu wawili hutembea pamoja wasipokubaliana kufanya hivyo?
4 Je, simba hunguruma katika kichaka wakati hana mawindo? Aweza kuvuma katika pango wakati ambao hajakamata chochote?
5 Je, ndege aweza kuanguka kwenye mtego ulio ardhini ambapo hajategewa chambo? Je, mtego unaweza kufyatuka toka ardhini wakati ambapo hakuna chochote cha kunasa?
6 Je, tarumbeta inapopigwa mjini kujulisha hatari, watu hawatetemeki? Mji upatwapo na maafa, je, si Bwana amesababisha?
7 Hakika Bwana Mwenyezi hatafanya neno lolote bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.
8 Simba amenguruma: je, ni nani ambaye hataogopa? Bwana Mwenyezi ametamka: je, ni nani awezaye kukosa kutoa unabii?
9 Tangazeni katika ngome za Ashdodi na katika ngome za Misri: “Kusanyikeni juu ya milima ya Samaria; angalieni wingi wa wasiwasi ulio ndani yake, na uonevu ulio miongoni mwa watu wake.”
10 Bwana asema: “Hawajui kutenda lililo jema, wale ambao hujilundikia nyara na vitu vilivyotekwa katika ngome zao.”
11 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: “Adui ataizingira nchi; ataangusha chini ngome zenu na kuteka nyara maboma yenu.”
12 Hili ndilo asemalo Bwana: “Kama vile mchungaji aokoavyo kinywani mwa simba vipande viwili tu vya mfupa wa mguu au kipande cha sikio, hivyo ndivyo Waisraeli watakavyookolewa, wale wakaao Samaria kwenye kingo za vitanda vyao, na katika Dameski kwenye viti vyao vya fahari.”
13 “Sikia hili na ushuhudie dhidi ya nyumba ya Yakobo,” asema Bwana, Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote.
14 “Siku nitakapomwadhibu Israeli kwa sababu ya dhambi zake, nitaharibu madhabahu za Betheli; pembe za madhabahu zitakatiliwa mbali na kuanguka chini.
15 Nitabomoa nyumba ya wakati wa masika, pamoja na nyumba ya wakati wa kiangazi; nyumba zilizonakshiwa kwa pembe za ndovu na majumba makubwa ya fahari yatabomolewa,” asema Bwana.