< Amosi 2 >
1 Hili ndilo asemalo Bwana: “Kwa dhambi tatu za Moabu, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu alichoma mifupa ya mfalme wa Edomu, ikawa kama chokaa.
2 Nitatuma moto juu ya Moabu ambao utateketeza ngome za Keriothi. Moabu ataanguka kwa ghasia kubwa katikati ya vilio vya vita na mlio wa tarumbeta.
3 Nitamwangamiza mtawala wake na kuwaua maafisa wake wote pamoja naye,” asema Bwana.
4 Hili ndilo asemalo Bwana: “Kwa dhambi tatu za Yuda, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu wameikataa sheria ya Bwana na hawakuzishika amri zake, kwa sababu wamepotoshwa na miungu ya uongo, miungu ambayo babu zao waliifuata.
5 Nitatuma moto juu ya Yuda ambao utateketeza ngome za Yerusalemu.”
6 Hili ndilo asemalo Bwana: “Kwa dhambi tatu za Israeli, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Wanawauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu.
7 Wanakanyaga juu ya vichwa vya maskini, kama vile juu ya mavumbi ya nchi, na kukataa haki kwa walioonewa. Baba na mwanawe hushiriki msichana mmoja, kwa hivyo hulinajisi Jina langu takatifu.
8 Watu hulala kando ya kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani. Katika nyumba ya mungu wao hunywa mvinyo ulionunuliwa kwa fedha walizotozwa watu.
9 “Nilimwangamiza Mwamori mbele yao, ingawa alikuwa mrefu kama mierezi, na mwenye nguvu kama mialoni. Niliyaangamiza matunda yake juu na mizizi yake chini.
10 “Niliwapandisha toka Misri, na nikawaongoza miaka arobaini jangwani niwape nchi ya Waamori.
11 Pia niliinua manabii kutoka miongoni mwa wana wenu na Wanadhiri kutoka miongoni mwa vijana wenu. Je, hii si kweli, enyi watu wa Israeli?” asema Bwana.
12 “Lakini mliwafanya Wanadhiri kunywa mvinyo na kuwaamuru manabii wasitoe unabii.
13 “Sasa basi, nitawaponda kama gari lipondavyo wakati limejazwa nafaka.
14 Mkimbiaji hodari hatanusurika, wenye nguvu wataishiwa nguvu zao, na shujaa hataweza kuokoa maisha yake.
15 Mpiga upinde atakimbia, askari wapiga mbio hawataweza kutoroka, na mpanda farasi hataokoa maisha yake.
16 Hata askari walio mashujaa sana siku hiyo watakimbia uchi,” asema Bwana.