< Matendo 9 >

1 Wakati ule ule, Sauli alikuwa bado anazidisha vitisho vya kuua wanafunzi wa Bwana, akamwendea kuhani mkuu,
Wakati huo Saulo alikuwa akizidisha vitisho vikali vya kuwaua wafuasi wa Bwana. Alikwenda kwa Kuhani Mkuu,
2 naye akamwomba kuhani mkuu ampe barua za kwenda kwenye masinagogi huko Dameski, ili akimkuta mtu yeyote wa Njia Ile, akiwa mwanaume au mwanamke, aweze kuwafunga na kuwaleta Yerusalemu.
akaomba apatiwe barua za utambulisho kwa masunagogi ya Kiyahudi kule Damasko, ili akikuta huko wanaume au wanawake wanaofuata Njia ya Bwana, awakamate na kuwaleta Yerusalemu.
3 Basi akiwa katika safari yake, alipokaribia Dameski, ghafula nuru kutoka mbinguni ikamwangaza kotekote.
Lakini alipokuwa njiani karibu kufika Damasko, ghafla mwanga kutoka angani ulimwangazia pande zote.
4 Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli, mbona unanitesa?”
Akaanguka chini na kusikia sauti ikimwambia: “Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?”
5 Sauli akajibu, “U nani wewe, Bwana?” Ile sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu unayemtesa.
Naye Saulo akauliza, “Ni nani wewe Bwana?” Na ile sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa.
6 Sasa inuka uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.”
Lakini simama sasa, uingie mjini na huko utaambiwa unachopaswa kufanya.”
7 Watu waliokuwa wakisafiri pamoja na Sauli wakasimama bila kuwa na la kusema, kwa sababu walisikia sauti lakini hawakumwona aliyekuwa akizungumza.
Wale watu waliokuwa wanasafiri pamoja na Saulo walisimama pale, wakiwa hawana la kusema; walisikia ile sauti lakini hawakumwona mtu.
8 Sauli akainuka kutoka pale chini na alipojaribu kufungua macho yake hakuweza kuona kitu chochote. Basi wakamshika mkono wakamwongoza mpaka Dameski.
Saulo aliinuka, na alipofumbua macho yake hakuweza kuona chochote; hivyo wale watu wakamwongoza kwa kumshika mkono mpaka mjini Damasko.
9 Naye kwa muda wa siku tatu alikuwa kipofu naye hakula wala kunywa chochote.
Saulo alikaa siku tatu bila kuona, na wakati huo hakula au kunywa chochote.
10 Huko Dameski alikuwepo mwanafunzi mmoja jina lake Anania. Bwana alimwita katika maono, “Anania!” Akajibu, “Mimi hapa Bwana.”
Basi, huko Damasko kulikuwa na mfuasi mmoja aitwaye Anania. Bwana akamwambia katika maono, “Anania!” Anania akaitika, “Niko hapa, Bwana.”
11 Bwana akamwambia, “Ondoka uende katika barabara iitwayo Nyofu ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu kutoka Tarso, jina lake Sauli, kwa maana wakati huu anaomba,
Naye Bwana akamwambia, “Jitayarishe uende kwenye barabara inayoitwa Barabara ya Moja kwa Moja, na katika nyumba ya Yuda umtake mtu mmoja kutoka Tarso aitwaye Saulo. Sasa anasali;
12 katika maono amemwona mtu aitwaye Anania akija na kuweka mikono juu yake ili apate kuona tena.”
na katika maono ameona mtu aitwaye Anania akiingia ndani na kumwekea mikono ili apate kuona tena.”
13 Anania akajibu, “Bwana, nimesikia kutoka kwa watu wengi habari nyingi kuhusu mtu huyu na madhara yote aliyowatendea watakatifu wako huko Yerusalemu.
Lakini Anania akajibu, “Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kutoka kwa watu wengi; nimesikia juu ya mabaya aliyowatendea watu wako huko Yerusalemu.
14 Naye amekuja hapa Dameski akiwa na mamlaka kutoka kwa viongozi wa makuhani ili awakamate wote wanaotaja jina lako.”
Na amekuja hapa akiwa na mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu kuwatia nguvuni wote wanaoomba kwa jina lako.”
15 Lakini Bwana akamwambia Anania, “Nenda! Mtu huyu ni chombo changu kiteule nilichokichagua, apate kulichukua Jina langu kwa watu wa Mataifa na wafalme wao na mbele ya watu wa Israeli.
Lakini Bwana akamwambia, “Nenda tu, kwa maana nimemchagua awe chombo changu, alitangaze jina langu kwa mataifa na wafalme wao na kwa watu wa Israeli.
16 Nami nitamwonyesha jinsi impasavyo kuteseka kwa ajili ya Jina langu.”
Mimi mwenyewe nitamwonyesha mengi yatakayomlazimu kuteswa kwa ajili ya jina langu.”
17 Kisha Anania akaenda kwenye ile nyumba, akaingia ndani. Akaweka mikono yake juu ya Sauli akasema, “Ndugu Sauli, Bwana Yesu aliyekutokea njiani amenituma kwako ili upate kuona tena na ujazwe Roho Mtakatifu.”
Basi, Anania akaenda, akaingia katika hiyo nyumba. Kisha akaweka mikono yake juu ya Saulo, akasema, “Ndugu Saulo, Bwana ambaye ndiye Yesu mwenyewe aliyekutokea ulipokuwa njiani kuja hapa, amenituma ili upate kuona tena na kujazwa Roho Mtakatifu.”
18 Ghafula vitu kama magamba vikaanguka chini, kutoka machoni mwa Sauli, akapata kuona tena. Akasimama, akabatizwa.
Mara vitu kama magamba vikaanguka kutoka macho ya Saulo, akaweza kuona tena. Akasimama, akabatizwa.
19 Baada ya kula chakula, akapata nguvu tena. Sauli akakaa siku kadhaa pamoja na wanafunzi huko Dameski.
Na baada ya kula chakula, nguvu zake zikamrudia. Saulo alikaa siku chache pamoja na wafuasi huko Damasko.
20 Papo hapo akaanza kuhubiri kwenye masinagogi kwamba “Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu”
Mara alianza kuhubiri katika masunagogi kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu.
21 Watu wote waliomsikia Sauli walishangaa na kuuliza, “Huyu si yule mtu aliyesababisha maangamizi makuu huko Yerusalemu miongoni mwa watu waliolitaja jina hili? Naye si amekuja hapa kwa kusudi la kuwakamata na kuwapeleka wakiwa wafungwa mbele ya viongozi wa makuhani?”
Watu wote waliomsikia walishangaa, wakasema, “Je, mtu huyu si yuleyule aliyewaua wale waliokuwa wanaomba kwa jina hili kule Yerusalemu? Tena alikuja hapa akiwa na madhumuni ya kuwatia nguvuni watu hao na kuwapeleka kwa makuhani!”
22 Sauli akazidi kuwa hodari na kuwashangaza Wayahudi walioishi Dameski kwa kuthibitisha kuwa Yesu ndiye Kristo.
Saulo alizidi kupata nguvu, na kwa jinsi alivyothibitisha wazi kwamba Yesu ndiye Kristo, Wayahudi wa huko Damasko walivurugika kabisa.
23 Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi wakafanya shauri kumuua Sauli.
Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi walikusanyika na kufanya mpango wa kumwua Saulo.
24 Lakini shauri lao likajulikana kwa Sauli. Wayahudi wakawa wanalinda malango yote ya mji, usiku na mchana ili wapate kumuua.
Lakini Saulo alipata habari ya mpango huo. Usiku na mchana walilinda milango ya kuingia mjini ili wapate kumwua.
25 Lakini wafuasi wake wakamchukua usiku wakamshusha akiwa ndani ya kapu kupitia mahali penye nafasi ukutani.
Lakini wakati wa usiku wanafunzi wake walimchukua, wakamteremsha chini ndani ya kapu kubwa kwa kupitia nafasi iliyokuwako ukutani.
26 Sauli alipofika Yerusalemu akajaribu kujiunga na wanafunzi lakini wote walimwogopa, kwa maana hawakuamini kwamba kweli naye alikuwa mwanafunzi.
Saulo alipofika Yerusalemu alijaribu kujiunga na wale wanafunzi. Lakini wote walimwogopa, na hawakuweza kuamini kwamba yeye amekuwa mfuasi.
27 Lakini Barnaba akamchukua, akampeleka kwa wale mitume. Akawaeleza jinsi Sauli akiwa njiani alivyomwona Bwana, jinsi Bwana alivyosema naye na jinsi alivyohubiri kwa ujasiri kwa jina la Yesu huko Dameski.
Hapo, Barnaba alikuja akamchukua Saulo, akampeleka kwa mitume na kuwaeleza jinsi Saulo alivyomwona Bwana njiani na jinsi Bwana alivyoongea naye. Aliwaambia pia jinsi Saulo alivyokuwa amehubiri bila uoga kule Damasko.
28 Kwa hiyo Sauli akakaa nao akitembea kwa uhuru kila mahali huko Yerusalemu, akihubiri kwa ujasiri katika jina la Bwana.
Basi, Saulo alikaa pamoja nao, akatembelea Yerusalemu yote akihubiri neno la Bwana bila hofu.
29 Alinena na kuhojiana na Wayahudi wenye asili ya Kiyunani lakini wao walijaribu kumuua.
Pia aliongea na kubishana na Wayahudi wasemao Kigiriki, lakini wao walijaribu kumwua.
30 Wale ndugu walipopata habari wakampeleka hadi Kaisaria, wakamsafirisha kwenda Tarso.
Wale ndugu walipogundua jambo hilo walimchukua Saulo, wakampeleka Kaisarea, wakamwacha aende zake Tarso.
31 Ndipo kanisa katika Uyahudi wote, Galilaya na Samaria likafurahia wakati wa amani. Likatiwa nguvu, na kwa faraja ya Roho Mtakatifu, idadi yake ikazidi kuongezeka, na likaendelea kudumu katika kumcha Bwana.
Wakati huo kanisa likawa na amani popote katika Yudea, Galilaya, na Samaria. Lilijengwa na kukua katika kumcha Bwana, na kuongezeka likitiwa moyo na Roho Mtakatifu.
32 Petro alipokuwa akisafiri sehemu mbalimbali, alikwenda kuwatembelea watakatifu walioishi huko Lida.
Petro alipokuwa anasafirisafiri kila mahali alifika pia kwa watu wa Mungu waliokuwa wanaishi Luda.
33 Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Ainea, ambaye alikuwa amepooza na kwa muda wa miaka minane alikuwa hajaondoka kitandani.
Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Enea ambaye kwa muda wa miaka minane alikuwa amelala kitandani kwa sababu alikuwa amepooza.
34 Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo anakuponya, inuka utandike kitanda chako.” Mara Ainea akainuka.
Basi, Petro akamwambia, “Enea, Yesu Kristo anakuponya. Amka utandike kitanda chako.” Enea akaamka mara.
35 Watu wote wa Lida na Sharoni walipomwona Ainea akitembea wakamgeukia Bwana.
Wakazi wote wa Luda na Saroni walimwona Enea, na wote wakamgeukia Bwana.
36 Huko Yafa palikuwa na mwanafunzi jina lake Tabitha (ambalo kwa Kiyunani ni Dorkasi). Huyu alikuwa mkarimu sana, akitenda mema na kuwasaidia maskini.
Kulikuwa na mfuasi mmoja mwanamke mjini Yopa aitwaye Tabitha (kwa Kigiriki ni Dorka, maana yake, Paa). Huyo mwanamke alikuwa akitenda mema na kuwasaidia maskini daima.
37 Wakati huo akaugua, akafa na wakiisha kuuosha mwili wake wakauweka katika chumba cha ghorofani.
Wakati huo ikawa kwamba aliugua, akafa. Watu wakauosha mwili wake, wakauzika katika chumba ghorofani.
38 Kwa kuwa Yafa hapakuwa mbali sana na Lida, wanafunzi waliposikia kwamba Petro yuko huko waliwatuma watu wawili kwake ili kumwomba, “Tafadhali njoo huku pasipo kukawia.”
Yopa si mbali sana na Luda; kwa hiyo wafuasi waliposikia kwamba Petro alikuwa Luda, wakawatuma watu wawili kwake na ujumbe: “Njoo kwetu haraka iwezekanavyo.”
39 Kwa hiyo Petro akainuka akaenda nao, naye alipowasili, wakampeleka hadi kwenye chumba cha ghorofani alipokuwa amelazwa. Wajane wengi walisimama karibu naye wakilia na kuonyesha majoho na nguo nyingine ambazo Dorkasi alikuwa amewashonea alipokuwa pamoja nao.
Basi, Petro akaenda pamoja nao. Alipofika alipelekwa ghorofani katika kile chumba. Huko wajane wengi walimzunguka Petro wakilia na kumwonyesha makoti na nguo ambazo Dorka alikuwa akitengeneza wakati alipokuwa hai.
40 Petro akawatoa wote nje ya kile chumba, kisha akapiga magoti akaomba, akaugeukia ule mwili akasema, “Tabitha, inuka.” Akafumbua macho yake na alipomwona Petro, akaketi.
Petro aliwatoa nje wote, akapiga magoti, akasali. Kisha akamgeukia yule maiti, akasema, “Tabitha, amka” Naye akafumbua macho yake na alipomwona Petro, akaketi.
41 Petro akamshika mkono akamwinua, ndipo akawaita wale watakatifu na wajane akamkabidhi kwao akiwa hai.
Petro akamsaidia kusimama, halafu akawaita wale watu wa Mungu na wale wajane, akamkabidhi kwao akiwa mzima.
42 Habari hizi zikajulikana sehemu zote za Yafa na watu wengi wakamwamini Bwana.
Habari ya tukio hili ilienea kila mahali huko Yopa, na watu wengi wakamwamini Bwana.
43 Petro akakaa Yafa kwa siku nyingi akiishi na Simoni mtengenezaji ngozi.
Petro alikaa siku kadhaa huko Yopa, akiishi kwa mtu mmoja mtengenezaji wa ngozi aitwaye Simoni.

< Matendo 9 >