< Matendo 7 >

1 Ndipo kuhani mkuu akamuuliza Stefano, “Je, mashtaka haya ni ya kweli?”
Basi, Kuhani Mkuu akamwuliza, “Je, mambo haya ni kweli?”
2 Stefano akajibu, “Ndugu zangu na baba zangu, nisikilizeni! Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Abrahamu, alipokuwa bado yuko Mesopotamia, kabla hajaishi Harani,
Naye Stefano akasema, “Ndugu zangu na akina baba, nisikilizeni! Mungu alimtokea baba yetu Abrahamu alipokuwa kule Mesopotamia kabla hajaenda kukaa kule Harani.
3 akamwambia, ‘Ondoka kutoka nchi yako na kutoka kwa jamii yako, uende hadi nchi nitakayokuonyesha.’
Mungu alimwambia: Ondoka katika nchi yako; waache watu wa ukoo wako; nenda katika nchi nitakayokuonyesha!
4 “Hivyo aliondoka katika nchi ya Wakaldayo akaenda kukaa Harani. Baada ya kifo cha baba yake, Mungu akamtoa huko akamleta katika nchi hii ambayo mnaishi sasa.
Kwa hivyo, Abrahamu alihama nchi ya Kaldayo, akaenda kukaa Harani. Baada ya kifo cha baba yake, Mungu alimtoa tena Harani akaja kukaa katika nchi hii mnayokaa sasa.
5 Mungu hakumpa urithi wowote katika nchi hii, hakumpa hata mahali pa kuweka wayo mmoja. Bali Mungu alimwahidi kuwa yeye na uzao wake baada yake wangeirithi hii nchi, ingawa wakati huo Abrahamu hakuwa na mtoto.
Mungu hakumpa hata sehemu moja ya nchi hii iwe mali yake; hata hivyo, alimwahidia kumpa nchi hii iwe yake na ya wazawa wake, ingawaje wakati huu hakuwa na mtoto.
6 Mungu akasema naye hivi: ‘Wazao wako watakuwa wageni kwenye nchi ambayo si yao, nao watafanywa watumwa na kuteswa kwa miaka mia nne.’
Mungu alimwambia hivi: Wazao wako watapelekwa katika nchi inayotawaliwa na watu wengine, na huko watafanywa watumwa na kutendewa vibaya kwa muda wa miaka mia nne.
7 Mungu akasema, ‘Lakini mimi nitaliadhibu taifa watakalolitumikia kama watumwa, na baadaye watatoka katika nchi hiyo na wataniabudu mahali hapa.’
Lakini mimi nitalihukumu taifa hilo litakalowafanya watumwa. Kisha nitawatoa katika nchi hiyo ili waje kuniabudu mahali hapa.
8 Ndipo akampa Abrahamu Agano la tohara. Naye Abrahamu akamzaa Isaki na kumtahiri siku ya nane. Baadaye Isaki akamzaa Yakobo, naye Yakobo akawazaa wale wazee wetu kumi na wawili.
Halafu Mungu aliifanya tohara iwe ishara ya agano. Hivyo, Abrahamu alimtahiri mtoto wake Isaka, siku ya nane baada ya kuzaliwa. Na Isaka, vivyo hivyo, alimtahiri Yakobo. Naye Yakobo aliwatendea wale mababu kumi na wawili vivyo hivyo.
9 “Kwa sababu wazee wetu walimwonea wivu Yosefu ndugu yao, walimuuza kama mtumwa huko Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye.
“Wale mababu walimwonea wivu Yosefu, wakamuuza utumwani Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye,
10 Akamwokoa kutoka mateso yote yaliyompata, tena akampa kibali na hekima aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri, ambaye alimweka kuwa mtawala juu ya Misri na juu ya jumba lote la kifalme.
akamwokoa katika taabu zake zote. Mungu alimjalia fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri, hata Farao akamweka awe mkuu wa ile nchi na nyumba ya kifalme.
11 “Basi kukawa na njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, ikasababisha dhiki kubwa, nao baba zetu wakawa hawana chakula.
Kisha, kulizuka njaa kubwa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, ikasababisha dhiki kubwa. Babu zetu hawakuweza kupata chakula chochote.
12 Lakini Yakobo aliposikia kwamba kuna nafaka huko Misri, aliwatuma baba zetu, wakaenda huko kwa mara yao ya kwanza.
Basi, Yakobo alipopata habari kwamba huko Misri kulikuwa na nafaka, aliwatuma watoto wake, yaani babu zetu, waende huko Misri mara ya kwanza.
13 Walipokwenda mara ya pili, Yosefu alijitambulisha kwa ndugu zake, nao ndugu zake Yosefu wakajulishwa kwa Farao.
Katika safari yao ya pili, Yosefu alijitambulisha kwa ndugu zake, na Farao akaifahamu jamaa ya Yosefu.
14 Ndipo Yosefu akawatuma kumleta Yakobo baba yake pamoja na jamaa yake yote, jumla yao walikuwa watu sabini na watano.
Yosefu alituma ujumbe kwa baba yake na jamaa yote, jumla watu sabini na tano, waje Misri.
15 Hivyo Yakobo akaenda Misri ambako yeye na baba zetu walifia.
Hivyo, Yakobo alikwenda Misri ambako yeye na babu zetu wengine walikufa.
16 Miili yao ilirudishwa Shekemu na kuzikwa katika kaburi ambalo Abrahamu alinunua kutoka kwa wana wa Hamori kwa kiasi fulani cha fedha.
Miili yao ililetwa mpaka Shekemu, ikazikwa katika kaburi Abrahamu alilonunua kutoka kwa kabila la Hamori kwa kiasi fulani cha fedha.
17 “Lakini wakati ulipokuwa unakaribia wa kutimizwa kwa ile ahadi ambayo Mungu alikuwa amempa Abrahamu, watu wetu walizidi kuongezeka sana huko Misri.
“Wakati ulipotimia Mungu aitimize ahadi aliyompa Abrahamu, idadi ya wale watu kule Misri ilikwisha ongezeka na kuwa kubwa zaidi.
18 Ndipo mfalme mwingine ambaye hakujua lolote kuhusu Yosefu akatawala Misri.
Mwishowe, mfalme mmoja ambaye hakumtambua Yosefu alianza kutawala huko Misri.
19 Huyu mfalme akawatendea watu wetu hila na kuwatesa baba zetu kwa kuwalazimisha wawatupe watoto wao wachanga ili wafe.
Alilifanyia taifa letu ukatili, akawatendea vibaya babu zetu kwa kuwalazimisha waweke nje watoto wao wachanga ili wafe.
20 “Wakati huo Mose alizaliwa, naye hakuwa mtoto wa kawaida. Akalelewa nyumbani kwa baba yake kwa muda wa miezi mitatu.
Mose alizaliwa wakati huo. Alikuwa mtoto mzuri sana. Alilelewa nyumbani kwa muda wa miezi mitatu,
21 Waliposhindwa kumficha zaidi, wakamweka nje mtoni na binti Farao akamchukua akamtunza kama mtoto wake mwenyewe.
na alipotolewa nje, binti wa Farao alimchukua, akamlea kama mtoto wake.
22 Mose akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa mtu hodari kwa maneno na matendo.
Mose alifundishwa mambo yote ya hekima ya Wamisri akawa mashuhuri kwa maneno na matendo.
23 “Mose alipokuwa na umri wa miaka arobaini aliamua kuwatembelea ndugu zake Waisraeli.
“Alipokuwa na umri wa miaka arobaini aliamua kwenda kuwaona ndugu zake Waisraeli.
24 Aliona mmoja wao akidhulumiwa na Mmisri, akamtetea yule aliyeonewa, akampiga yule Mmisri akamuua kulipiza kisasi.
Huko alimwona mmoja wao akitendewa vibaya, akaenda kumwokoa, na kulipiza kisasi, akamuua yule Mmisri.
25 Mose alidhani kuwa ndugu zake wangetambua kwamba Mungu anamtumia ili kuwaokoa, lakini wao hawakuelewa.
(Alidhani kwamba Waisraeli wenzake wangeelewa kwamba Mungu angemtumia yeye kuwakomboa, lakini hawakuelewa hivyo.)
26 Siku iliyofuata Mose aliwakuta Waisraeli wawili wakigombana, akajaribu kuwapatanisha kwa kuwaambia, ‘Enyi watu, ninyi ni ndugu, mbona mnataka kudhulumiana?’
Kesho yake, aliwaona Waisraeli wawili wakipigana, akajaribu kuwapatanisha, akisema: Ninyi ni ndugu; kwa nini basi, kutendeana vibaya ninyi kwa ninyi?
27 “Lakini yule mtu aliyekuwa akimdhulumu mwenzake akamsukuma Mose kando, akamuuliza, ‘Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu?
Yule aliyekuwa anampiga mwenzake alimsukuma Mose kando akisema: Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wa watu?
28 Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?’
Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?
29 Mose aliposikia maneno haya, alikimbilia huko Midiani alikokaa kama mgeni, naye akapata watoto wawili wa kiume.
Baada ya kusikia hayo Mose alikimbia, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani na huko akapata watoto wawili.
30 “Basi baada ya miaka arobaini kupita, malaika wa Mungu akamtokea Mose jangwani karibu na Mlima Sinai katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto.
“Miaka arobaini ilipotimia, malaika wa Bwana alimtokea Mose katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto kule jangwani karibu na mlima Sinai.
31 Alipoona mambo haya, alishangaa yale maono. Aliposogea ili aangalie kwa karibu, akaisikia sauti ya Bwana, ikisema:
Mose alistaajabu sana kuona jambo hilo hata akasogea karibu ili achungulie; lakini alisikia sauti ya Bwana:
32 ‘Mimi ndimi Mungu wa baba zako, Mungu wa Abrahamu, Isaki na Yakobo.’ Mose alitetemeka kwa hofu na hakuthubutu kutazama.
Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo! Mose akatetemeka kwa hofu na wala hakuthubutu kutazama zaidi.
33 “Ndipo Bwana akamwambia, ‘Vua viatu vyako kwa maana mahali unaposimama ni patakatifu.
Bwana akamwambia: Vua viatu vyako maana hapa unaposimama ni mahali patakatifu.
34 Hakika nimeona mateso ya watu wangu huko Misri. Nimesikia kilio chao cha uchungu, nami nimeshuka ili niwaokoe. Basi sasa njoo, nami nitakutuma Misri.’
Nimeyaona mabaya wanayotendewa watu wangu kule Misri. Nimesikia kilio chao, nami nimekuja kuwaokoa. Basi sasa, nitakutuma Misri.
35 “Huyu ndiye Mose yule waliyemkataa wakisema, ‘Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu?’ Alikuwa ametumwa na Mungu mwenyewe kuwa mtawala na mkombozi wao, kwa njia ya yule malaika aliyemtokea katika kile kichaka.
“Huyu Mose ndiye yule watu wa Israeli waliyemkataa waliposema: Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wetu? Kwa njia ya yule malaika aliyemtokea katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto, Mungu alimtuma Mose huyo awe kiongozi na mkombozi.
36 Aliwaongoza wana wa Israeli kutoka Misri, baada ya kufanya ishara na maajabu mengi huko Misri, katika Bahari ya Shamu, na katika jangwa kwa muda wa miaka arobaini.
Ndiye aliyewaongoza wale watu watoke Misri kwa kufanya miujiza na maajabu katika nchi ya Misri, katika bahari ya Shamu na jangwani kwa muda wa miaka arobaini.
37 “Huyu ndiye yule Mose aliyewaambia Waisraeli, ‘Mungu atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu wenyewe.’
Mose ndiye aliyewaambia watu wa Israeli: Mungu atawateulieni nabii kama mimi kutoka katika ndugu zenu ninyi wenyewe.
38 Huyu ndiye yule Mose aliyekuwa katika kusanyiko huko jangwani, ambaye malaika alisema naye pamoja na baba zetu kwenye Mlima Sinai, naye akapokea maneno yaliyo hai ili atupatie.
Wakati watu wa Israeli walipokutana pamoja kule jangwani, Mose ndiye aliyekuwako huko pamoja nao. Alikuwa huko pamoja na babu zetu na yule malaika aliyeongea naye mlimani Sinai; ndiye aliyekabidhiwa yale maneno yaletayo uzima atupe sisi.
39 “Lakini baba zetu walikataa kumtii Mose, badala yake wakamkataa na kuielekeza mioyo yao Misri tena.
“Lakini yeye ndiye babu zetu waliyemkataa kumsikiliza; walimsukuma kando, wakatamani kurudi Misri.
40 Wakamwambia Aroni, ‘Tufanyie miungu watakaotuongoza, kwa maana mtu huyu Mose aliyetutoa nchi ya Misri, hatujui yaliyompata.’
Walimwambia Aroni: Tutengenezee miungu itakayotuongoza njiani, maana hatujui yaliyompata Mose huyu aliyetuongoza kutoka Misri!
41 Huu ni ule wakati walitengeneza sanamu katika umbo la ndama, wakailetea sadaka kufanya maadhimisho kwa ajili ya kile kitu walichokitengeneza kwa mikono yao wenyewe.
Hapo ndipo walipojitengenezea sanamu ya ndama, wakaitambikia na kukifanyia sherehe kitu ambacho ni kazi ya mikono yao wenyewe.
42 Ndipo Mungu akageuka, akawaacha waabudu jeshi lote la mbinguni, kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Manabii: “‘Je, mliniletea dhabihu na sadaka kwa miaka arobaini kule jangwani, ee nyumba ya Israeli?
Lakini Mungu aliondoka kati yao, akawaacha waabudu nyota za anga, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha manabii: Enyi watu wa Israeli! Si mimi mliyenitolea dhabihu na sadaka kwa muda wa miaka arobaini kule jangwani!
43 La, ninyi mliinua madhabahu ya Moleki, na nyota ya mungu wenu Refani, vinyago mlivyotengeneza ili kuviabudu. Kwa hiyo nitawapeleka mbali’ kuliko Babeli.
Ninyi mlikibeba kibanda cha mungu Moloki, na sanamu ya nyota ya mungu wenu Refani. Sanamu mlizozifanya ndizo mlizoabudu. Kwa sababu hiyo nitakupeleka mateka mbali kupita Babuloni!
44 “Baba zetu walikuwa na lile Hema la Ushuhuda huko jangwani. Lilikuwa limetengenezwa kama Mungu alivyokuwa amemwelekeza Mose, kulingana na kielelezo alichoona.
Kule jangwani babu zetu walikuwa na lile hema lililoshuhudia kuweko kwa Mungu. Lilitengenezwa kama Mungu alivyomwambia Mose alifanye; nakala kamili ya kile alichoonyeshwa.
45 Baba zetu wakiisha kulipokea hema kwa kupokezana wakiongozwa na Yoshua katika milki ya nchi kutoka kwa yale mataifa ambayo Mungu aliyafukuza mbele yao, nalo likadumu katika nchi mpaka wakati wa Daudi,
Kisha babu zetu walilipokezana wao kwa wao mpaka wakati wa Yoshua, walipoinyakua ile nchi kutoka kwa mataifa ambayo Mungu aliyafukuza mbele yao. Hapo lilikaa mpaka nyakati za Daudi.
46 ambaye alipata kibali kwa Mungu, naye akaomba kwamba ampatie Mungu wa Yakobo maskani.
Daudi alipata upendeleo kwa Mungu, akamwomba Mungu ruhusa ya kumjengea makao yeye aliye Mungu wa Yakobo.
47 Lakini alikuwa Solomoni ndiye alimjengea Mungu nyumba.
Lakini Solomoni ndiye aliyemjengea Mungu nyumba.
48 “Hata hivyo, Yeye Aliye Juu Sana hakai kwenye nyumba zilizojengwa kwa mikono ya wanadamu. Kama nabii alivyosema:
“Hata hivyo, Mungu Mkuu haishi katika nyumba zilizojengwa na binadamu; kama nabii asemavyo:
49 “‘Mbingu ni kiti changu cha enzi, nayo dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu. Mtanijengea nyumba ya namna gani? asema Bwana. Au mahali pangu pa kupumzikia patakuwa wapi?
Bwana asema: Mbingu ni kiti changu cha enzi na dunia ni kiti changu cha kuwekea miguu.
50 Je, mkono wangu haukufanya vitu hivi vyote?’
Ni nyumba ya namna gani basi mnayoweza kunijengea, na ni mahali gani nitakapopumzika? Vitu hivi vyote ni mimi nimevifanya, au sivyo?
51 “Enyi watu wenye shingo ngumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, daima hamwachi kumpinga Roho Mtakatifu, kama walivyofanya baba zenu.
“Enyi wakaidi wakuu! Mioyo na masikio yenu ni kama ya watu wa mataifa. Ninyi ni kama baba zenu. Siku zote mnampinga Roho Mtakatifu.
52 Je, kuna nabii gani ambaye baba zenu hawakumtesa? Waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki. Nanyi sasa mmekuwa wasaliti wake na wauaji.
Je, yuko nabii yeyote ambaye baba zenu hawakumtesa? Waliwaua hao Mungu aliowatuma watangaze kuja kwake yule Mwenye Haki. Na sasa, ninyi mmemsaliti, mkamuua.
53 Ninyi ndio mlipokea sheria zilizoletwa kwenu na malaika, lakini hamkuzitii.”
Ninyi mliipokea ile Sheria iliyoletwa kwenu na Malaika, lakini hamkuitii.”
54 Waliposikia haya wakaghadhibika, wakamsagia meno.
Wale wazee wa Baraza waliposikia hayo, walighadhibika sana, wakamsagia meno kwa hasira.
55 Lakini yeye Stefano, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alikaza macho mbinguni, akaona utukufu wa Mungu, na Yesu akiwa amesimama mkono wa kuume wa Mungu.
Lakini Stefano akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akatazama juu mbinguni, akauona utukufu wa Mungu na Yesu amekaa upande wa kulia wa Mungu.
56 Akasema, “Tazameni! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama upande wa kuume wa Mungu.”
Akasema, “Tazameni! Ninaona mbingu zimefunuliwa na Mwana wa Mtu amesimama upande wa kulia wa Mungu.”
57 Lakini wao wakapiga kelele kwa sauti kubwa, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja.
Hapo, watu wote katika kile kikao cha Baraza, wakapiga kelele na kuziba masikio yao kwa mikono yao. Kisha wakamrukia wote kwa pamoja,
58 Wakamtupa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka mavazi yao miguuni mwa kijana mmoja ambaye jina lake aliitwa Sauli.
wakamtoa nje ya mji, wakampiga mawe. Wale mashahidi wakayaweka makoti yao chini ya ulinzi wa kijana mmoja jina lake Saulo.
59 Walipokuwa wakimpiga mawe, Stefano aliomba, “Bwana Yesu, pokea roho yangu.”
Waliendelea kumpiga mawe Stefano, huku akiwa anasali: “Bwana Yesu, ipokee roho yangu!”
60 Kisha akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii.” Baada ya kusema hayo, akalala.
Akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa: “Bwana, usiwalaumu kwa sababu ya dhambi hii.” Baada ya kusema hivyo, akafa.

< Matendo 7 >