< Matendo 6 >

1 Basi ikawa katika siku hizo, wakati idadi ya wanafunzi ilipokuwa ikiongezeka sana, palitokea manungʼuniko kati ya Wayahudi wa Kiyunani, dhidi ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahaulika katika mgawanyo wa chakula wa kila siku.
Baadaye, idadi ya wanafunzi ilipokuwa inazidi kuongezeka, kulitokea manung'uniko kati ya wanafunzi waliosema Kigiriki na wale waliosema Kiebrania. Wale waliosema Kigiriki walinung'unika kwamba wajane wao walikuwa wanasahauliwa katika ugawaji wa mahitaji ya kila siku.
2 Wale mitume kumi na wawili wakakusanya wanafunzi wote pamoja wakasema, “Haitakuwa vyema sisi kuacha huduma ya neno la Mungu ili kuhudumu mezani.
Kwa hiyo, mitume kumi na wawili waliita jumuiya yote ya wanafunzi, wakasema, “Si vizuri sisi tuache kulihubiri neno la Mungu ili tushughulikie ugawaji wa mahitaji.
3 Kwa hiyo ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, watu wenye sifa njema, waliojawa na Roho Mtakatifu na hekima, ambao tunaweza kuwakabidhi kazi hii,
Hivyo, ndugu zetu, chagueni miongoni mwenu watu saba wenye sifa njema, waliojawa na Roho na wenye hekima; nasi tutawakabidhi jukumu hilo.
4 nasi tutatumia muda wetu kuomba na huduma ya neno.”
Sisi, lakini, tutashughulika na sala na kazi ya kuhubiri neno la Mungu.”
5 Yale waliyosema yakawapendeza watu wote, nao wakamchagua Stefano (mtu aliyejawa na imani na Roho Mtakatifu) pamoja na Filipo, Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena na Nikolao, mwongofu kutoka Antiokia.
Jambo hilo likaipendeza jumuiya yote ya waumini. Wakawachagua Stefano, mtu mwenye imani kubwa na mwenye kujawa na Roho Mtakatifu, Filipo, Prokoro, Nikanora, Timona, Parmena na Nikolao wa Antiokia ambaye hapo awali alikuwa ameongokea dini ya Kiyahudi.
6 Wakawaleta watu hawa mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono juu yao.
Wakawaweka mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono.
7 Neno la Mungu likazidi kuenea. Idadi ya wanafunzi ikazidi kuongezeka sana katika Yerusalemu hata makuhani wengi wakaitii ile imani.
Neno la Mungu likazidi kuenea na idadi ya waumini huko Yerusalemu ikaongezeka zaidi, na kundi kubwa la makuhani wakaipokea imani.
8 Stefano, akiwa amejaa neema na nguvu za Mungu, alifanya ishara na miujiza mikubwa miongoni mwa watu.
Mungu alimjalia Stefano neema tele, akampa nguvu nyingi hata akawa anatenda miujiza na maajabu kati ya watu.
9 Hata hivyo, ukainuka upinzani wa watu wa Sinagogi la Watu Huru (kama lilivyokuwa linaitwa), la Wayahudi wa Kirene na wa Iskanderia, na wengine kutoka Kilikia na Asia. Watu hawa wakaanza kupingana na Stefano.
Lakini watu fulani wakatokea ili wabishane na Stefano. Baadhi ya watu hao walikuwa wa sunagogi moja lililoitwa “Sunagogi la Watu Huru”, nao walitoka Kurene na Aleksandria; wengine walitoka Kilikia na Asia.
10 Lakini hawakuweza kushindana na hekima yake wala huyo Roho ambaye alisema kwake.
Lakini hawakuweza kumshinda kwa sababu ya hekima yake na kwa sababu ya yule Roho aliyeongoza maneno yake.
11 Ndipo kwa siri wakawashawishi watu fulani waseme, “Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kufuru dhidi ya Mose na dhidi ya Mungu.”
Kwa hiyo waliwahonga watu kadhaa waseme: “Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kumkashifu Mose na kumkashifu Mungu.”
12 Wakawachochea watu, wazee na walimu wa Sheria, nao wakamkamata Stefano wakamfikisha mbele ya baraza.
Kwa namna hiyo, waliwachochea watu, wazee na walimu wa Sheria. Basi, wakamjia Stefano, wakamkamata na kumleta mbele ya Baraza kuu.
13 Wakaweka mashahidi wa uongo ambao walishuhudia wakisema, “Mtu huyu kamwe haachi kusema dhidi ya mahali hapa patakatifu na dhidi ya Sheria.
Walileta Barazani mashahidi wa uongo ambao walisema, “Mtu huyu haachi kamwe kusema maneno ya kupakashifu mahali hapa patakatifu na Sheria ya Mose.
14 Kwa maana tumemsikia akisema kwamba Yesu wa Nazareti atapaharibu mahali patakatifu na kubadili desturi zote tulizopewa na Mose.”
Kwa maana tulikwisha msikia akisema eti huyo Yesu wa Nazareti atapaharibu kabisa mahali hapa na kufutilia mbali desturi zile tulizopokea kutoka kwa Mose.”
15 Watu wote waliokuwa wameketi katika baraza wakimkazia macho Stefano, wakaona uso wake unangʼaa kama uso wa malaika.
Wote waliokuwa katika kile kikao cha Baraza walimkodolea macho Stefano, wakauona uso wake umekuwa kama wa malaika.

< Matendo 6 >