< Matendo 5 >
1 Lakini mtu mmoja jina lake Anania pamoja na mkewe Safira waliuza kiwanja.
Mtu mmoja aitwaye Anania na mkewe Safira waliuza shamba lao vilevile.
2 Huku mkewe akijua kikamilifu, Anania alificha sehemu ya fedha alizopata, akaleta kiasi kilichobaki na kukiweka miguuni pa mitume.
Lakini, mkewe akiwa anajua, Anania akajiwekea sehemu ya fedha alizopata na ile sehemu nyingine akawakabidhi mitume.
3 Petro akamuuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja?
Basi, Petro akamwuliza, “Anania, mbona Shetani ameuingia moyo wako na kukufanya umdanganye Roho Mtakatifu kwa kujiwekea sehemu ya fedha ulizopata kutokana na lile shamba?
4 Je, kabla hujauza hicho kiwanja si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, fedha ulizopata si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu bali Mungu.”
Kabla ya kuliuza lilikuwa mali yako, na baada ya kuliuza, bado hizo fedha zilikuwa zako uzitumie utakavyo. Kwa nini basi, uliamua moyoni mwako kufanya jambo la namna hii? Hukumdanganya mtu; umemdanganya Mungu!”
5 Anania aliposikia maneno haya akaanguka chini na kufa. Hofu kuu ikawapata wote waliosikia jambo lililokuwa limetukia.
Anania aliposikia hayo, akaanguka chini, akafa. Watu wote waliosikia habari ya tukio hilo waliogopa sana.
6 Vijana wakaja, wakaufunga mwili wake sanda, wakamchukua nje kumzika.
Vijana wakafika wakaufunika mwili wake, wakamtoa nje, wakamzika.
7 Saa tatu baadaye mkewe Anania akaingia, naye hana habari ya mambo yaliyotukia.
Baada ya muda wa saa tatu hivi, mke wake, bila kufahamu mambo yaliyotukia, akaingia mle ndani.
8 Petro akamuuliza, “Niambie, je, mliuza kiwanja kwa thamani hii?” Akajibu, “Ndiyo, tuliuza kwa thamani hiyo.”
Petro akamwambia, “Niambie! Je, kiasi hiki cha fedha ndicho mlichopata kwa kuuza lile shamba?” Yeye akamjibu, “Naam, ni kiasi hicho.”
9 Ndipo Petro akamwambia, “Imekuwaje mkakubaliana kumjaribu Roho wa Bwana? Tazama! Nyayo za vijana waliomzika mumeo ziko mlangoni, wewe nawe watakuchukua nje.”
Naye Petro akamwambia, “Mbona mmekula njama kumjaribu Roho wa Bwana? Sikiliza! Wale watu waliokwenda kumzika mume wako, sasa wako mlangoni na watakuchukua wewe pia.”
10 Saa ile ile akaanguka chini miguuni mwake na kufa. Nao wale vijana wakaingia, wakamkuta amekufa, wakamchukua wakamzika kando ya mumewe.
Mara Safira akaanguka mbele ya miguu ya Petro, akafa. Wale vijana walipoingia, walimkuta amekwisha kufa; hivyo wakamtoa nje, wakamzika karibu na mume wake.
11 Hofu kuu ikalipata kanisa lote pamoja na watu wote waliosikia juu ya matukio haya.
Kanisa lote pamoja na wote waliosikia habari ya tukio hilo, waliogopa sana.
12 Mitume wakafanya ishara nyingi na miujiza miongoni mwa watu. Walioamini wote walikuwa wakikusanyika katika ukumbi wa Solomoni.
Mitume walifanya miujiza na maajabu mengi kati ya watu. Waumini walikuwa wakikutana pamoja katika ukumbi wa Solomoni.
13 Hakuna mtu mwingine aliyethubutu kuambatana nao ijapokuwa waliheshimiwa sana na watu.
Mtu yeyote mwingine ambaye hakuwa mwamini hakuthubutu kujiunga nao. Hata hivyo, watu wengine wasiokuwa wa imani hiyo waliwasifu.
14 Hata hivyo, waliomwamini Bwana wakazidi kuongezeka, wanaume na wanawake.
Idadi ya watu waliomwamini Bwana, wanaume kwa wanawake, iliongezeka zaidi na zaidi.
15 Hata wakawa wanawaleta wagonjwa na kuwalaza kwenye magodoro na kwenye vitanda barabarani ili yamkini Petro akipita kivuli chake kiwaguse baadhi yao.
Kwa sababu hiyo, watu walikuwa wakipeleka wagonjwa barabarani na kuwalaza juu ya vitanda na mikeka ili Petro akipita, walau kivuli chake kiwaguse baadhi yao.
16 Pia watu wakakusanyika kutoka miji iliyokuwa karibu na Yerusalemu, wakileta wagonjwa na watu walioteswa na pepo wachafu. Hao wote wakaponywa.
Watu wengi walifika kutoka katika miji ya kando kando ya Yerusalemu, wakiwaleta wagonjwa wao na wale waliokuwa na pepo wachafu, nao wote wakaponywa.
17 Kisha kuhani mkuu na wenzake wote waliokuwa pamoja naye, waliokuwa wa kundi la Masadukayo, wakajawa na wivu.
Kisha, Kuhani Mkuu na wenzake waliokuwa wa kikundi cha Masadukayo wa mahali hapo, wakawaonea mitume wivu.
18 Wakawakamata mitume na kuwatia gerezani.
Basi, wakawatia nguvuni, wakawafunga ndani ya gereza kuu.
19 Lakini wakati wa usiku, malaika wa Bwana akaja, akafungua milango ya gereza na akawatoa nje. Akawaambia,
Lakini usiku malaika wa Bwana aliifungua milango ya gereza, akawatoa nje, akawaambia,
20 “Nendeni, mkasimame Hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya uzima huu mpya.”
“Nendeni mkasimame Hekaluni na kuwaambia watu kila kitu kuhusu maisha haya mapya.”
21 Waliposikia haya wakaenda Hekaluni alfajiri wakaendelea kufundisha watu. Kuhani mkuu na wale waliokuwa pamoja nao walipowasili, alikusanya baraza na wazee wote wa Israeli wakatuma wale mitume waletwe kutoka gerezani.
Mitume walitii, wakaingia Hekaluni asubuhi na mapema, wakaanza kufundisha. Kuhani Mkuu na wenzake walipofika, waliita mkutano wa Baraza kuu, yaani halmashauri yote ya wazee wa Wayahudi halafu wakawatuma watu gerezani wawalete wale mitume.
22 Lakini wale walinzi wa Hekalu walipokwenda gerezani hawakuwakuta mitume mle. Kwa hiyo wakarudi na kutoa habari.
Lakini hao watumishi walipofika huko hawakuwakuta mle gerezani. Hivyo walirudi, wakatoa taarifa mkutanoni,
23 Wakasema, “Tumekuta milango ya gereza imefungwa sawasawa na askari wa gereza wamesimama nje ya mlango, lakini tulipofungua milango hakuwepo mtu yeyote ndani.”
wakisema, “Tulikuta gereza limefungwa kila upande na walinzi wakilinda milango. Lakini tulipofungua hatukumkuta mtu yeyote ndani.”
24 Basi mkuu wa walinzi wa Hekalu na viongozi wa makuhani waliposikia haya, wakafadhaika na kushangaa sana kwa ajili yao kwamba jambo hili litakuwaje.
Mkuu wa walinzi wa Hekalu na makuhani wakuu waliposikia habari hiyo wakawa na wasiwasi, wasijue yaliyowapata.
25 Ndipo mtu mmoja akaja akawaambia, “Tazameni watu mliowatia gerezani wako Hekaluni wakiwafundisha watu.”
Akafika mtu mmoja, akawaambia, “Wale watu mliowafunga gerezani, hivi sasa wamo Hekaluni, wanawafundisha watu.”
26 Ndipo yule mkuu wa walinzi wa Hekalu wakaenda pamoja na askari wakawaleta wale mitume, lakini bila ghasia kwa sababu waliogopa kupigwa mawe na watu.
Hapo mkuu wa walinzi wa Hekalu pamoja na watu wake walikwenda Hekaluni, akawaleta. Lakini hawakuwakamata kwa kutumia nguvu, maana waliogopa kwamba watu wangewapiga mawe.
27 Wakiisha kuwaleta mitume wakawaamuru kusimama mbele ya baraza ili kuhani mkuu awahoji.
Basi, wakawapeleka, wakawasimamisha mbele ya Baraza. Kuhani Mkuu akawaambia,
28 “Tuliwaonya kwa nguvu msifundishe kwa jina hili, lakini ninyi mmeijaza Yerusalemu yote mafundisho yenu na tena mmekusudia kuleta damu ya mtu huyu juu yetu.”
“Tuliwakatazeni waziwazi kufundisha kwa jina la mtu huyu; sasa mmeyaeneza mafundisho yenu pote katika Yerusalemu na mnakusudia kutuwekea lawama ya kifo cha mtu huyo.”
29 Petro na wale mitume wengine wakajibu, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.
Hapo Petro, akiwa pamoja na wale mitume wengine, akajibu, “Lazima tumtii Mungu, na siyo binadamu.
30 Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu, ambaye ninyi mlimuua kwa kumtundika kwenye msalaba.
Mungu wa babu zetu alimfufua Yesu baada ya ninyi kumwua kwa kumtundika msalabani.
31 Mungu alimtukuza, akamweka mkono wake wa kuume kuwa Kiongozi na Mwokozi ili awape Israeli toba na msamaha wa dhambi.
Huyu ndiye yule aliyekwezwa na Mungu mpaka upande wake wa kulia, akawa kiongozi na Mwokozi, ili awawezeshe watu wa Israeli watubu, wapate kusamehewa dhambi zao.
32 Nasi tu mashahidi wa mambo haya, vivyo hivyo na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii.”
Sisi ni mashahidi wa tukio hilo, naye Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii, anashuhudia pia tukio hilo.”
33 Wale wajumbe wa baraza la wazee waliposikia haya, walijawa na ghadhabu, wakataka kuwaua mitume.
Wajumbe wote wa lile Baraza waliposikia hayo, wakawaka hasira, hata wakaamua kuwaua.
34 Lakini Farisayo mmoja, jina lake Gamalieli, aliyekuwa mwalimu wa sheria, aliyeheshimiwa na watu wote, akasimama mbele ya baraza akaamuru mitume watolewe nje kwa muda.
Lakini Mfarisayo mmoja aitwaye Gamalieli ambaye alikuwa mwalimu wa Sheria na aliyeheshimika sana mbele ya watu wote, alisimama mbele ya lile Baraza, akataka wale mitume watolewe nje kwa muda mfupi.
35 Ndipo alipowaambia wajumbe wa baraza, “Enyi watu wa Israeli, fikirini kwa uangalifu mnayotaka kuwatendea watu hawa.
Kisha akawaambia wale wajumbe wa Baraza, “Wananchi wa Israeli, tahadhari kabla ya kutekeleza hicho mnachotaka kuwatenda watu hawa!
36 Kwa maana wakati uliopita, aliinuka mtu mmoja jina lake Theuda, alijidai kuwa yeye ni mtu maarufu, akapata wafuasi wapatao 400 walioambatana naye. Lakini aliuawa, na wafuasi wake wote wakatawanyika, wakawa si kitu.
Zamani kidogo, kulitokea mtu mmoja jina lake Theuda, akajisema kuwa mtu wa maana na watu karibu mia nne wakajiunga naye. Lakini aliuawa, kisha wafuasi wake wote wakatawanyika na kikundi chake kikafa.
37 Baada yake, alitokea Yuda Mgalilaya wakati wa kuorodhesha watu, naye akaongoza kundi la watu kuasi. Yeye pia aliuawa, nao wafuasi wake wakatawanyika.
Tena, baadaye, wakati ule wa kuhesabiwa watu, alitokea Yuda wa Galilaya. Huyu naye, aliwavuta watu wakamfuata; lakini naye pia aliuawa, na wafuasi wake wakatawanyika.
38 Kwa hiyo, kwa habari ya jambo hili nawashauri, jiepusheni na watu hawa. Waacheni waende zao! Kwa maana kama kusudi lao na shughuli yao imetokana na mwanadamu, haitafanikiwa.
Na sasa pia mimi nawaambieni, msiwachukulie watu hawa hatua yoyote; waacheni! Kwa maana, ikiwa mpango huu au shughuli hii yao imeanzishwa na binadamu, itatoweka yenyewe.
39 Lakini ikiwa imetoka kwa Mungu, hamtaweza kuwazuia watu hawa. Badala yake mtajikuta mnapigana na Mungu.”
Lakini kama imeanzishwa na Mungu, siyo tu kwamba hamtaweza kuwashinda, bali mtajikuta mnapigana na Mungu.” Basi, wakakubaliana naye.
40 Wakapokea ushauri wa Gamalieli. Wakawaita mitume ndani, wakaamuru wachapwe mijeledi, kisha wakawaagiza wasinene tena kwa jina la Yesu, wakawaachia waende zao.
Hivyo wakawaita wale mitume, wakaamuru wachapwe viboko na kuwaonya wasifundishe tena kwa jina la Yesu; kisha wakawaacha waende zao.
41 Nao mitume wakatoka nje ya baraza, wakiwa wamejaa furaha kwa sababu wamehesabiwa kustahili kupata aibu kwa ajili ya jina la Yesu.
Basi, mitume wakatoka nje ya ule mkutano wa halmashauri wakiwa wamejaa furaha, kwani walistahili kuaibishwa kwa ajili ya jina la Yesu.
42 Kila siku, Hekaluni na nyumba kwa nyumba, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema kwamba Yesu ndiye Kristo.
Wakaendelea kila siku kufundisha na kuhubiri Habari Njema ya Kristo, Hekaluni na nyumbani mwa watu.