< Matendo 3 >
1 Siku moja Petro na Yohana walikuwa wanapanda kwenda Hekaluni kusali yapata saa tisa alasiri.
Sasa Peter na Yohana walikuwa wanaelekea katika hekalu wakati wa maombi, saa tisa.
2 Basi palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa kiwete tangu kuzaliwa. Alichukuliwa na kuwekwa kwenye lango la Hekalu liitwalo Zuri, kila siku ili aombe msaada kwa watu wanaoingia Hekaluni.
Mtu fulani, kiwete tangu kuzaliwa, alikuwa akibebwa kila siku na alikuwa akilazwa katika mlango wa hekalu uitwao mzuri, ili aweze kuomba sadaka kutoka kwa watu waliokuwa wakielekea hekaluni.
3 Huyu mtu alipowaona Petro na Yohana wakikaribia kuingia Hekaluni, akawaomba wampe sadaka.
Alipowaona Petro na Yohana wanakaribia kuingia hekaluni, aliomba sadaka.
4 Wakamkazia macho, kisha Petro akamwambia, “Tutazame sisi.”
Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, alisema,”tutazame sisi.”
5 Hivyo yule mtu akawatazama, akitazamia kupata kitu kutoka kwao.
Kiwete akawatazama, akitazamia kupokea kitu fulani kutoka kwao.
6 Ndipo Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!”
Lakini Petro akasema, “fedha na dhahabu mimi sina, lakini kile nilichonacho nitatoa kwako. Katika jina la Yesu Kristo wa Nazareth, tembea.”
7 Petro akamshika yule mtu kwa mkono wa kuume akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikapata nguvu.
Petro akamchukua kwa mkono wake wa kulia, na akamwinua juu: mara moja miguu yake na vifundo vya mifupa yake vikapata nguvu.
8 Akaruka juu na kusimama, akaanza kutembea. Kisha akaingia Hekaluni pamoja na Petro na Yohana, huku akitembea na kurukaruka na kumsifu Mungu.
Akiruka juu, mtu kiwete alisimama na akaanza kutembea; akaingia hekaluni pamoja na Petro na Yohana, akitembea, akiruka, na kumsifu Mungu.
9 Watu wote walipomwona akitembea na kumsifu Mungu,
Watu wote walimwona akitembea na akimsifu Mungu.
10 wakamtambua kuwa ni yule mtu aliyekuwa akiketi nje ya Hekalu penye lango liitwalo Zuri akiomba msaada, nao wakajawa na mshangao, wakastaajabu juu ya yale yaliyomtukia.
Wakatambua kwamba alikuwa ni yule mtu ambaye alikuwa akikaa akiomba sadaka kwenye mlango mzuri wa hekalu; walijawa na mshangao na kustaajabu kwa sababu ya kile kilichotokea kwake.
11 Aliyeponywa alipokuwa akiambatana na Petro na Yohana, watu wote walishangaa mno, wakaja wakiwakimbilia pale ukumbi wa Solomoni.
Namna alivyokuwa amewashikilia Petro na Yohana, watu wote kwa pamoja wakakimbilia kwenye ukumbi uitwao wa Sulemani, wakishangaa sana.
12 Petro alipoona watu wamekusanyika akawaambia, “Enyi Waisraeli, kwa nini mnastaajabu kuhusu jambo hili? Mbona mnatukazia macho kwa mshangao kana kwamba ni kwa uwezo wetu au utakatifu wetu tumemfanya mtu huyu kutembea?
Petro alipoliona hili, yeye akawajibu watu, “Enyi watu wa Israel, kwa nini mnashangaa? Kwa nini mnayaelekeza macho yenu kwetu, kama kwamba tumemfanya huyu atembee kwa nguvu zetu wenyewe au uchaji wetu?”
13 Mungu wa Abrahamu na Isaki na Yakobo, Mungu wa baba zetu amemtukuza Mwanawe Yesu, ambaye ninyi mlimtoa ahukumiwe kifo na mkamkana mbele ya Pilato, ingawa yeye alikuwa ameamua kumwachia aende zake.
Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Yakobo, Mungu wa Baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu. Huyu ndiye ambaye ninyi mlimkabidhi na kumkataa mbele ya uso wa Pilato, japo yeye alikuwa ameamua kumwachia huru.
14 Ninyi mlimkataa huyo Mtakatifu na Mwenye Haki mkaomba mpewe yule muuaji.
Mlimkataa Mtakatifu na Mwenye Haki, na badala yake mkataka muuaji aachwe huru.
15 Hivyo mkamuua aliye chanzo cha uzima, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. Sisi tu mashahidi wa mambo haya.
Ninyi mlimuua Mfalme wa uzima, ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu - Sisi ni mashahidi wa hili.
16 Kwa imani katika jina la Yesu, huyu mtu mnayemwona na kumfahamu ametiwa nguvu. Ni kwa jina la Yesu na imani itokayo kwake ambayo imemponya kabisa huyu mtu, kama ninyi wote mnavyoona.
Sasa, kwa imani katika jina lake, mtu huyu ambaye mnamwona na kujua, alifanywa kuwa na nguvu. Imani ambayo inapitia kwa Yesu imempa yeye afya hii kamilifu, mbele yenu ninyi nyote.
17 “Sasa ndugu zangu, najua ya kuwa ninyi mlitenda bila kujua, kama walivyofanya viongozi wenu.
Sasa, Ndugu, najua kwamba mlitenda katika ujinga, ndivyo pia walivyofanya viongozi wenu.
18 Lakini kwa njia hii Mungu alitimiza kile ambacho alikuwa ametabiri kwa vinywa vya manabii wake wote, kwamba Kristo atateswa.
Lakini mambo ambayo Mungu aliwaambia mapema kwa vinywa vya manabii wote, kwamba huyu Kristo atateseka, sasa ameyatimiza.
19 Tubuni basi mkamgeukie Mungu, dhambi zenu zifutwe, ili zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwepo kwake Bwana,
Kwa hiyo, tubuni na mgeuke, ili kwamba dhambi zenu ziweze kuondolewa kabisa, kusudi zije nyakati za kuburudika kutokana na uwepo wa Bwana;
20 naye apate kumtuma Kristo, ambaye ameteuliwa kwa ajili yenu, yaani Yesu.
na kwamba aweze kumtuma Kristo ambaye ameshateuliwa kwa ajili yenu, Yesu.
21 Ilimpasa mbingu zimpokee mpaka wakati wa kufanywa upya kila kitu, kama Mungu alivyoahidi zamani kupitia kwa vinywa vya manabii wake watakatifu. (aiōn )
Yeye ndiye ambaye lazima mbingu zimpokee mpaka wakati wa kurejeshwa kwa vitu vyote, ambavyo Mungu alizungumzia zamani za kale kwa vinywa vya manabii watakatifu. (aiōn )
22 Kwa maana Mose alisema, ‘Bwana Mungu wenu atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu. Itawapasa kumtii huyo kwa kila jambo atakalowaambia.
Hakika Musa alisema, 'Bwana Mungu atainua nabii kama mimi kutoka katika ndugu zenu. Mtamsikiliza kila kitu ambacho atawaambia ninyi.
23 Mtu yeyote ambaye hatamsikiliza huyo nabii, atatupiliwa mbali kabisa na watu wake.’
Itatokea kwamba kila mtu ambaye hasikilizi kwa nabii huyo ataangamizwa kabisa atoke kati ya watu.'
24 “Naam, manabii wote tangu Samweli na waliokuja baada yake, wote walitabiri kuhusu siku hizi.
Ndiyo, na manabii wote tokea Samweli na wale waliofuata baada yake, walizungumza na walitangaza siku hizi.
25 Ninyi ndio wana wa manabii na wa Agano ambalo Mungu alifanya na baba zenu, akimwambia Abrahamu, ‘Kupitia kwa uzao wako, watu wote wa ulimwengu watabarikiwa.’
Ninyi ni wana wa manabii na wa agano ambalo Mungu alilifanya pamoja na mababu, kama alivyosema kwa Abrahamu, 'Katika mbegu yako familia zote za dunia zitabarikiwa.'
26 Mungu alipomfufua Yesu Mwanawe, alimtuma kwenu kwanza, ili awabariki kwa kumgeuza kila mmoja wenu kutoka njia yake mbaya.”
Baada ya Mungu kumwinua mtumishi wake, alimtuma kwenu kwanza, ili awabariki ninyi kwa kugeuka kutoka katika uovu wenu.”