< Matendo 24 >
1 Baada ya siku tano, kuhani mkuu Anania akashuka akiwa amefuatana na baadhi ya wazee pamoja na mwanasheria mmoja aitwaye Tertulo, nao wakaleta mashtaka yao dhidi ya Paulo mbele ya mtawala.
Baada ya siku tano, Kuhani Mkuu Anania aliwasili Kaisarea pamoja na wazee kadhaa na wakili mmoja wa sheria aitwaye Tertulo. Walimwendea yule mkuu wa mkoa wakamweleza mashtaka yao juu ya Paulo.
2 Paulo alipoitwa aingie ndani, Tertulo akaanza kutoa mashtaka akisema, “Mtukufu Feliksi, kwa muda mrefu tumefurahia amani na matengenezo mengi mazuri yamefanywa kwa ajili ya watu hawa kwa sababu ya upeo wako wa kuona mambo ya mbele.
Paulo aliitwa na Tertulo akafungua mashtaka hivi: “Mheshimiwa Felisi, uongozi wako bora umeleta amani kubwa na marekebisho ya lazima yanafanywa kwa manufaa ya taifa letu.
3 Wakati wote na kila mahali, kwa namna yoyote, mtukufu sana Feliksi, tumeyapokea mambo haya yote kwa shukrani nyingi.
Tunalipokea jambo hili kwa furaha daima na kutoa shukrani nyingi kwako kila mahali.
4 Lakini nisije nikakuchosha zaidi, ningekuomba kwa hisani yako utusikilize kwa kifupi.
Lakini, bila kupoteza wakati wako zaidi, tunakusihi kwa wema wako, usikilize taarifa yetu fupi.
5 “Tumemwona mtu huyu kuwa ni msumbufu, anayechochea ghasia miongoni mwa Wayahudi duniani pote. Yeye ndiye kiongozi wa dhehebu la Wanazarayo,
Tumegundua kwamba mtu huyu ni wa hatari mno. Yeye huanzisha ghasia kati ya Wayahudi kila mahali duniani na pia ni kiongozi wa kile chama cha Wanazareti.
6 na hata amejaribu kulinajisi Hekalu, hivyo tukamkamata; [tukataka kumhukumu kufuatana na sheria zetu.
Tena alijaribu kulikufuru Hekalu nasi tukamtia nguvuni. Kama ukimhoji wewe mwenyewe, utaweza kubainisha mambo haya yote tunayomshtaki kwayo.” Tulitaka kumhukumu kufuatana na Sheria yetu.
7 Lakini jemadari Lisia alitujia na nguvu nyingi, akamwondoa mikononi mwetu,
Lakini Lusia, mkuu wa jeshi, aliingilia kati, akamchukua kwa nguvu kutoka mikononi mwetu.
8 akiwaamuru washtaki wake waje mbele yako: ili] kwa kumchunguza wewe mwenyewe unaweza kujua kutoka kwake mambo yote tunayomshtaki kwayo.”
Kisha akaamuru washtaki wake waje mbele yako.
9 Pia wale Wayahudi wakaunga mkono wakithibitisha kuwa mashtaka yote haya ni kweli.
Nao Wayahudi waliunga mkono mashtaka hayo wakisema kwamba hayo yote yalikuwa kweli.
10 Mtawala Feliksi alipompungia Paulo mkono ili ajitetee, yeye akajibu, “Najua kwamba wewe umekuwa hakimu katika taifa hili kwa miaka mingi, hivyo natoa utetezi wangu kwa furaha.
Basi, mkuu wa mkoa alimwashiria Paulo aseme. Naye Paulo akasema, “Nafurahi kujitetea mbele yako nikijua kwamba umekuwa hakimu wa taifa hili kwa miaka mingi.
11 Unaweza kuhakikisha kwa urahisi kuwa hazijapita zaidi ya siku kumi na mbili tangu nilipopanda kwenda Yerusalemu kuabudu.
Unaweza kujihakikishia kwamba si zaidi ya siku kumi na mbili tu zimepita tangu nilipokwenda kuabudu Yerusalemu.
12 Hawa wanaonishtaki hawakunikuta nikibishana na mtu yeyote Hekaluni au kuchochea umati wa watu katika sinagogi au mahali pengine popote mjini.
Wayahudi hawakunikuta nikijadiliana na mtu yeyote. Hawakunikuta nikichochea watu Hekaluni wala katika masunagogi yao, wala mahali pengine popote katika mji huo.
13 Wala hawawezi kabisa kukuthibitishia mashtaka haya wanayonishtaki kwayo.
Wala hawawezi kuthibitisha mashtaka waliyotoa juu yangu.
14 Lakini, ninakubali kwamba mimi namwabudu Mungu wa baba zetu, mfuasi wa Njia, ile ambayo wao wanaiita dhehebu. Ninaamini kila kitu kinachokubaliana na Sheria na kile kilichoandikwa katika Manabii,
Ninachokubali mbele yako ni hiki: Mimi ninamwabudu Mungu na wazee wetu nikiishi kufuatana na Njia ile ambayo wao wanaiita chama cha uzushi. Ninaamini mambo yote yaliyoandikwa katika vitabu vya Sheria na manabii.
15 nami ninalo tumaini kwa Mungu, ambalo hata wao wenyewe wanalikubali kwamba kutakuwa na ufufuo wa wafu, kwa wenye haki na wasio na haki.
Mimi namtumainia Mungu, na wao wanalo tumaini hilo, kwamba watu, wema na wabaya, watafufuka.
16 Kwa hiyo ninajitahidi siku zote kuwa na dhamiri safi mbele za Mungu na mbele za wanadamu.
Kwa hiyo ninajitahidi daima kuwa na dhamiri njema mbele ya Mungu na mbele ya watu.
17 “Basi, baada ya kutokuwepo kwa miaka mingi nilikuja Yerusalemu ili kuwaletea watu wangu msaada kwa ajili ya maskini na kutoa dhabihu.
“Baada ya kukaa mbali kwa miaka kadhaa, nilirudi Yerusalemu ili kuwapelekea wananchi wenzangu msaada na kutoa dhabihu.
18 Nilikuwa nimeshatakaswa kwa taratibu za kiibada waliponikuta Hekaluni nikifanya mambo haya. Hapakuwa na umati wa watu, pamoja nami wala aliyehusika kwenye fujo yoyote.
Wakati nilipokuwa nikifanya hayo ndipo waliponikuta Hekaluni, nilipokuwa nimekwisha fanya ile ibada ya kujitakasa. Hakukuwako kundi la watu wala ghasia.
19 Lakini kulikuwa na baadhi ya Wayahudi kutoka Asia, ambao wangelazimika wawepo hapa mbele yako ili watoe mashtaka kama wanalo jambo lolote dhidi yangu.
Lakini kulikuwa na Wayahudi wengine kutoka mkoa wa Asia; hao ndio wangepaswa kuwa hapa mbele yako na kutoa mashtaka yao kama wana chochote cha kusema dhidi yangu.
20 Au, watu hawa walioko hapa waseme ni uhalifu gani walioniona nao waliponisimamisha mbele ya baraza,
Au, waache hawa walio hapa waseme kosa waliloliona kwangu wakati niliposimama mbele ya Baraza lao kuu,
21 isipokuwa ni kuhusu jambo hili moja nililopiga kelele mbele yao kwamba, ‘Mimi nashtakiwa mbele yenu leo kwa sababu ya ufufuo wa wafu.’”
isipokuwa tu maneno haya niliyosema niliposimama mbele yao: Mnanihukumu leo hii kwa sababu ya kushikilia kwamba wafu watafufuliwa!”
22 Basi Feliksi ambaye alikuwa anafahamu vizuri habari za Njia ile, akaahirisha shauri lile kwa maelezo yake akisema, “Wakati jemadari Lisia atakapoteremka huku, nitaamua shauri lako.”
Hapo, Felisi, ambaye mwenyewe alikuwa anaifahamu hiyo Njia vizuri, aliahirisha kesi hiyo. Akawaambia, “Nitatoa hukumu juu ya kesi hiyo wakati Luisa, mkuu wa jeshi, atakapokuja hapa.”
23 Ndipo akaamuru kiongozi wa askari amweke chini ya ulinzi lakini ampe uhuru na kuwaruhusu rafiki zake wamhudumie.
Kisha akamwamuru yule jemadari amweke Paulo kizuizini, lakini awe na uhuru kiasi, na rafiki zake wasizuiwe kumpatia mahitaji yake.
24 Baada ya siku kadhaa, Feliksi alikuja pamoja na Drusila mkewe, ambaye alikuwa Myahudi. Alituma aitiwe Paulo, naye akamsikiliza alipokuwa akinena juu ya imani katika Kristo Yesu.
Baada ya siku chache, Felisi alifika pamoja na mkewe Drusila ambaye alikuwa Myahudi. Aliamuru Paulo aletwe, akamsikiliza akiongea juu ya kumwamini Yesu Kristo.
25 Naye Paulo alipokuwa akinena juu ya haki, kuwa na kiasi na juu ya hukumu ijayo, Feliksi aliingiwa na hofu na kusema, “Hiyo yatosha sasa! Waweza kuondoka. Nitakapokuwa na wasaa nitakuita.”
Lakini wakati Paulo alipoanza kuongea juu ya uadilifu, juu ya kuwa na kiasi na juu ya siku ya hukumu inayokuja, Felisi aliogopa, akasema, “Kwa sasa unaweza kwenda; nitakuita tena nitakapopata nafasi.”
26 Wakati huo Feliksi alitazamia kwamba Paulo angempa rushwa. Hivyo akawa anamwita mara kwa mara na kuzungumza naye.
Wakati huohuo alikuwa anatumaini kwamba Paulo angempa fedha. Kwa sababu hii alimwita Paulo mara kwa mara na kuzungumza naye.
27 Baada ya miaka miwili kupita, Porkio Festo akaingia kwenye utawala mahali pa Feliksi, lakini kwa kuwa Feliksi alitaka kuwapendeza Wayahudi, akamwacha Paulo gerezani.
Baada ya miaka miwili, Porkio Festo alichukua nafasi ya Felisi, akawa mkuu wa Mkoa. Kwa kuwa alitaka kujipendekeza kwa Wayahudi, Felisi alimwacha Paulo kizuizini.