< Matendo 22 >
1 “Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni utetezi wangu.”
“Ndugu na baba zangu, sikilizeni utetezi wangu nitakaofanya kwenu sasa.”
2 Waliposikia akisema kwa lugha ya Kiebrania, wakanyamaza kimya kabisa. Ndipo Paulo akasema,
Makutano walipo sikia Paulo akiongea nao kwa kiebrania, wakanyamaza. Akasema,
3 “Mimi ni Myahudi, niliyezaliwa Tarso huko Kilikia, lakini nimelelewa katika mji huu. Miguuni mwa Gamalieli, nilifundishwa kikamilifu katika sheria ya baba zetu, na nikawa mwenye juhudi kwa ajili ya Mungu kama kila mmoja wenu alivyo leo.
“Mimi ni myahudi, nimezaliwa mji wa Tarso eneo la Kilikia, ila nilipata elimu katika mji huu, miguuni pa Gamalieli. Nilifundishwa kulingana na njia sahihi za sheria za baba zetu. Mimi ninabidii ya Mungu, kama ninyi nyote mlivyo leo.
4 Niliwatesa watu wa Njia hii hadi kufa, nikiwakamata waume kwa wake na kuwatupa gerezani,
Niliwatesa kwa njia hii hadi kufa; nikawafunga wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani.
5 kama kuhani mkuu na baraza zima la wazee wanavyoweza kushuhudia kunihusu. Hata nilipokea barua kutoka kwao kwenda kwa ndugu wale wa Dameski, nami nikaenda huko ili kuwaleta watu hawa Yerusalemu kama wafungwa ili waadhibiwe.
Hata kuhani mkuu na wazee wote wanaweza kutoa ushahidi kwamba nilipokea barua kutoka kwao kwa ajili ya ndugu walio Dameski, kwangu mimi kusafiri kwenda huko. Ilikuwa niwalete watu Yerusalemu wa njia ile ili wafungwe na kuadhibiwa.
6 “Nilipokuwa njiani kuelekea Dameski, yapata saa sita mchana, ghafula nuru kubwa kutoka mbinguni ikanimulika kotekote.
Ilitokea kwamba pale nilipokua nikisafiri nakaribia Dameski, majira ya mchana ghafla nuru kuu ikatokea mbinguni ikaanza kuniangaza.
7 Nikaanguka chini, nikasikia sauti ikiniambia, ‘Sauli, Sauli! Mbona unanitesa?’
Nikaanguka chini na kusikia sauti ikiniambia, 'Sauli, Sauli kwanini unaniudhi?'
8 “Nikajibu, ‘Wewe ni nani Bwana?’ “Naye akaniambia, ‘Mimi ni Yesu wa Nazareti unayemtesa.’
Nikajibu, 'wewe ni nani, Bwana?' Akaniambia, 'Mini ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi.'
9 Basi wale watu waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia sauti ya yule aliyekuwa akisema nami.
Wale waliokuwa na mimi waliiona nuru, ila hawakusikia sauti ya yule alie ongea na mimi.
10 “Nikauliza, ‘Nifanye nini Bwana?’ “Naye Bwana akaniambia, ‘Inuka uingie Dameski, huko utaambiwa yote yakupasayo kufanya.’
Nikasema, 'Nifanye nini, Bwana?' Bwana akaniambia, 'Simama na uingie Dameski; huko utaambiwa kila kitu unachopaswa kufanya.'
11 Kwa kuwa nilikuwa siwezi kuona kwa ajili ya mngʼao wa ile nuru, wenzangu wakanishika mkono wakaniongoza kuingia Dameski.
Sikuweza kuona kwa sababu ya muangaza wa nuru ile, ndipo nikaenda Dameski kwa kuongozwa na mikono ya wale waliokuwa na mimi.
12 “Mtu mmoja mcha Mungu, jina lake Anania, alikuja kuniona. Alizishika sana sheria zetu, na aliheshimiwa sana na Wayahudi waliokuwa wakiishi huko Dameski.
Huko nikakutana na mtu aitwaye Anania, alikuwa mtu aliyeshika sheria na mwenye kuheshimika mbele ya Wayahudi wote walioishi huko.
13 Akasimama karibu nami, akasema, ‘Ndugu Sauli, pata kuona tena!’ Saa ile ile nikapata kuona tena, nami nikaweza kumwona.
Akaja kwangu, akasimama mbele yangu, na kusema, 'Ndugu yangu Sauli, upate kuona.'Kwa muda ule ule nikamuona.
14 “Akasema, ‘Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe ili ujue mapenzi yake, umwone yeye Aliye Mwenye Haki na upate kusikia maneno kutoka kinywani mwake.
Akasema, 'Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, kumuona yule mwenyehaki, na kusikia sauti itokayo kwenye kinywa chake.
15 Kwa kuwa utakuwa shahidi wake kwa watu kuhusu kile ulichokiona na kukisikia.
Kwa sababu utakuwa shahidi kwake kwa watu wote juu ya uliyoyaona na kusikia.
16 Sasa basi, mbona unakawia? Inuka, ukabatizwe na dhambi zako zikasafishwe, ukiliita Jina lake.’
Basi sasa kwa nini unasubiri? Amka, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliita jina lake.'
17 “Baada ya kurudi Yerusalemu, nilipokuwa ninaomba Hekaluni, nilipitiwa na usingizi wa ghafula
Baada ya kurejea Yerusalemu, na nilipokuwa nikisali ndani ya hekalu, ikatokea kwamba nikapewa maono.
18 nikamwona Bwana akiniambia, ‘Harakisha utoke Yerusalemu upesi, maana hawataukubali ushuhuda wako kunihusu mimi.’
Nikamuona akiniambia, 'Hima na utoke Yerusalemu haraka, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako kuhusu mimi.'
19 “Nami nikasema, ‘Bwana, wao wenyewe wanajua jinsi nilivyokwenda kwenye kila sinagogi ili kuwatupa gerezani na kuwapiga wale waliokuamini.
Nikasema, 'Bwana, wao wenyewe wanajua niliwafunga gerezani na kuwapiga wale waliokuamini katika kila sinagogi.
20 Wakati damu ya shahidi wako Stefano ilipomwagwa, mimi mwenyewe nilikuwa nimesimama kando, nikikubaliana na kitendo hicho na kutunza mavazi ya wale waliomuua.’
Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, Mimi pia nilikuwa nimesimama karibu na kukubali na nilikuwa nalinda nguo za wale waliomwua.'
21 “Ndipo Bwana akaniambia, ‘Nenda, kwa maana nitakutuma mbali, kwa watu wa Mataifa.’”
Lakini aliniambia, 'Enenda, kwa sababu mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa mataifa.”'
22 Ule umati wa watu wakamsikiliza Paulo mpaka aliposema neno hilo, ndipo wakapaza sauti zao na kupiga kelele wakisema, “Mwondoeni duniani, hafai kuishi!”
Watu wakamruhusu aongee juu ya neno hili. Lakini baadaye walipaza sauti na kusema, “mwondoe mtu huyu katika nchi: kwa sababu sio sahihi aishi.”
23 Walipokuwa wakipiga kelele na kutoa mavazi yao huku wakirusha mavumbi juu hewani,
Walipokuwa wakipaza sauti, na kutupa mavazi yao na kutupa mavumbi juu,
24 yule jemadari akaamuru Paulo aingizwe kwenye ngome. Akaelekeza kwamba achapwe viboko na aulizwe ili kujua kwa nini watu walikuwa wanampigia kelele namna hiyo.
jemedari mkuu akaamuru Paulo aletwe ngomeni. Akaamuru aulizwe huku anapigwa mijeledi, ili yeye mwenyewe ajue kwa nini walikuwa wanampigia kelele namna ile.
25 Lakini walipokwisha kumfunga kwa kamba za ngozi ili wamchape viboko, Paulo akamwambia kiongozi wa askari aliyekuwa amesimama pale karibu naye, “Je, ni halali kwenu kwa mujibu wa sheria kumchapa mtu ambaye ni raiya wa Rumi hata kabla hajapatikana na hatia?”
Hata walipokuwa wamemfunga kwa kamba, Paulo akamwambia yule akida aliye simama karibu naye, “Je! ni haki kwenu kumpiga mtu aliye Mrumi na bado hajahukumiwa?”
26 Yule kiongozi aliposikia maneno haya, alimwendea yule jemadari na kumwambia, “Unataka kufanya nini? Kwa maana huyu mtu ni raiya wa Rumi.”
Yule akida aliposikia maneno haya, akaenda kwa jemedari mkuu na kumwambia, akisema, “Unataka kufanya nini? Kwa maana mtu huyu ni mrumi.”
27 Yule jemadari akaja akamuuliza Paulo, “Niambie, wewe ni raiya wa Rumi?” Paulo akajibu, “Naam, hakika ndiyo.”
Jemedari mkuu akaja na kumwambia, “Niambie, je wewe ni raia wa Rumi?” Paulo akasema, “Ndiyo.”
28 Ndipo yule jemadari akasema, “Mimi ilinigharimu kiasi kikubwa cha fedha kupata uraia wangu.” Paulo akasema “Lakini mimi ni raiya wa Rumi kwa kuzaliwa.”
Jemedari akamjibu, “Ni kupitia kiasi kikubwa cha pesa ndipo nilipata uraia.” Lakini Paulo akamwambia, “Mimi ni mrumi wa kuzaliwa.”
29 Mara wale waliokuwa wanataka kumhoji wakajiondoa haraka, naye yule jemadari akaingiwa na hofu alipotambua ya kuwa amemfunga Paulo, ambaye ni raia wa Rumi, kwa minyororo.
Basi wale waliokuwa tayari kwenda kumuuliza wakaondoka na kumwacha wakati huo huo. Na jemedari naye akaogopa, alipojua kuwa Paulo ni Mrumi, na kwa sababu amemfunga.
30 Kesho yake, kwa kuwa yule jemadari alitaka kujua hakika kwa nini Paulo alikuwa anashutumiwa na Wayahudi, alimfungua, na akawaagiza viongozi wa makuhani na baraza lote likutane. Kisha akamleta Paulo, akamsimamisha mbele yao.
Siku iliyofuatayo, jemedari mkuu alitaka kujua ukweli kuhusu mashtaka ya Wayahudi dhidi ya Paulo. Hivyo akamfungua vifungo vyake akaamuru wakuu wa makuhani na baraza lote wakutane. Akamleta Paulo chini, na kumweka katikati yao.