< Matendo 21 >

1 Tulipokwisha kujitenga nao, tukaanza safari kwa njia ya bahari moja kwa moja mpaka Kosi. Siku ya pili yake tukafika Rodo na kutoka huko tukaenda Patara.
Tulipokwisha agana nao, tulipanda meli tukaenda moja kwa moja mpaka Kosi. Kesho yake tulifika Rodo, na kutoka huko tulikwenda Patara.
2 Hapo tukapata meli iliyokuwa inavuka kwenda Foinike tukapanda tukasafiri nayo.
Huko, tulikuta meli iliyokuwa inakwenda Foinike, hivyo tulipanda, tukasafiri.
3 Tulipokiona kisiwa cha Kipro, tukakizunguka tukakiacha upande wetu wa kushoto, tukasafiri mpaka Shamu, tukatia nanga katika bandari ya Tiro ambapo meli yetu ilikuwa ipakue shehena yake.
Baada ya kufika mahali ambapo tuliweza kuona Kupro, tulipitia upande wake wa kusini tukaelekea Siria. Tulitia nanga katika mji wa Tiro ambapo ile meli ilikuwa ipakuliwe shehena yake.
4 Baada ya kuwatafuta wanafunzi wa huko, tukakaa nao kwa siku saba. Wale wanafunzi wakiongozwa na Roho wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu.
Tulikuta waumini huko, tukakaa pamoja nao kwa muda wa juma moja. Waumini hao wakawa waongea kwa nguvu ya Roho, wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu.
5 Lakini muda wetu ulipokwisha, tukaondoka tukaendelea na safari yetu. Wale wanafunzi pamoja na wake zao na watoto wakatusindikiza hadi nje ya mji. Wote tukapiga magoti pale pwani tukaomba.
Lakini muda wetu ulipokwisha tuliondoka. Wote pamoja na wanawake na watoto wao walitusindikiza mpaka nje ya mji. Tulipofika pwani, sote tulipiga magoti tukasali.
6 Baada ya kuagana, tukapanda melini, nao wakarudi majumbani mwao.
Kisha tuliagana; sisi tukapanda meli nao wakarudi makwao.
7 Tukaendelea na safari yetu toka Tiro tukafika Tolemai, tukawasalimu ndugu wa huko, tukakaa nao kwa siku moja.
Sisi tuliendelea na safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai ambapo tuliwasalimu ndugu zetu, tukakaa nao siku moja.
8 Siku iliyofuata tukaondoka, tukafika Kaisaria. Huko tukaenda nyumbani kwa mwinjilisti mmoja jina lake Filipo, aliyekuwa mmoja wa wale Saba, tukakaa kwake.
Kesho yake tuliondoka tukaenda Kaisarea. Huko Kaisarea tulikwenda nyumbani kwa mhubiri Filipo. Yeye alikuwa mmoja wa wale saba waliochaguliwa kule Yerusalemu.
9 Filipo alikuwa na binti wanne mabikira waliokuwa wanatoa unabii.
Alikuwa na binti watatu ambao walikuwa na kipaji cha unabii.
10 Baada ya kukaa kwa siku kadhaa, akateremka nabii mmoja kutoka Uyahudi jina lake Agabo.
Baada ya kukaa huko siku kadhaa, nabii mmoja aitwaye Agabo alifika kutoka Yudea.
11 Alipotufikia akachukua mshipi wa Paulo akajifunga, akautumia kufunga mikono na miguu yake mwenyewe akasema, “Roho Mtakatifu anasema: ‘Hivi ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mwenye mshipi huu na kumkabidhi kwa watu wa Mataifa.’”
Alitujia, akachukua mkanda wa Paulo, akajifunga mikono na miguu, akasema “Roho Mtakatifu asema hivi: Wayahudi kule Yerusalemu watamfunga namna hii mtu mwenye ukanda na kumtia mikononi mwa watu wa mataifa.”
12 Tuliposikia maneno haya sisi na ndugu wengine tukamsihi Paulo asiende Yerusalemu.
Tuliposikia hayo, sisi na wale watu wengine waliokuwa hapo tulimsihi Paulo asiende Yerusalemu.
13 Lakini Paulo akajibu, “Kwa nini mnalia na kunivunja moyo? Mimi niko tayari si kufungwa tu, bali hata kufa huko Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana Yesu.”
Lakini yeye alijibu, “Mnataka kufanya nini? Mnataka kuvunja moyo wangu kwa machozi? Niko tayari siyo tu kutiwa ndani kule Yerusalemu, ila hata kufa kwa ajili ya Bwana Yesu.”
14 Alipokuwa hashawishiki, tukaacha kumsihi, tukasema, “Mapenzi ya Bwana na yatendeke.”
Tuliposhindwa kumshawishi tulinyamaza, tukasema tu: “Mapenzi ya Bwana yafanyike”
15 Baada ya haya, tukajiandaa, tukaondoka kwenda Yerusalemu.
Baada ya kukaa pale kwa muda, tulifunga mizigo yetu, tukaendelea na safari kwenda Yerusalemu.
16 Baadhi ya wanafunzi kutoka Kaisaria wakafuatana nasi na kutupeleka nyumbani kwa Mnasoni, ambaye tungekaa kwake. Yeye alikuwa mtu wa Kipro, mmoja wa wanafunzi wa zamani.
Wengine kati ya wale wafuasi wa Kaisarea walienda pamoja nasi, wakatupeleka nyumbani kwa Mnasoni ambaye tulikuwa tunakwenda kukaa naye kwa muda. Mnasoni alikuwa mwenyeji wa Kupro na alikuwa amekuwa muumini kwa siku nyingi.
17 Tulipofika Yerusalemu ndugu wakatukaribisha kwa furaha.
Tulipofika Yerusalemu, ndugu waumini walitupokea vizuri sana.
18 Kesho yake Paulo pamoja na wengine wetu tulikwenda kumwona Yakobo, na wazee wote walikuwepo.
Kesho yake Paulo alikwenda pamoja nasi kumwamkia Yakobo, na wazee wote wa kanisa walikuwako pia.
19 Baada ya kuwasalimu, Paulo akatoa taarifa kamili ya mambo yote ambayo Mungu alikuwa amefanya miongoni mwa watu wa Mataifa kupitia huduma yake.
Baada ya kuwasalimu, Paulo aliwapa taarifa kamili kuhusu yote Mungu aliyokuwa ametenda kati ya mataifa kwa njia ya utumishi wake.
20 Baada ya kusikia mambo haya wakamwadhimisha Mungu. Ndipo wakamwambia Paulo, “Ndugu, unaona kulivyo na maelfu ya Wayahudi walioamini, nao wote wana juhudi kwa ajili ya sheria.
Waliposikia hayo, walimtukuza Mungu. Kisha wakamwambia Paulo, “Ndugu, unaweza kuona kwamba kuna maelfu ya Wayahudi ambao sasa wamekuwa waumini na wote hao wanashika kwa makini Sheria ya Mose.
21 Lakini wameambiwa habari zako kwamba unafundisha Wayahudi wote waishio miongoni mwa watu wa Mataifa kumkataa Mose, na kwamba unawaambia wasiwatahiri watoto wao wala kufuata desturi zetu.
Wamepata habari zako kwamba umekuwa ukiwafundisha Wayahudi wanaoishi kati ya mataifa mengine kuwa wasiijali Sheria ya Mose, wasiwatahiri watoto wao na kwamba wasizifuate mila za Wayahudi.
22 Sasa tufanyeje? Bila shaka watasikia kwamba umekuja Yerusalemu.
Sasa, mambo yatakuwaje? Ni dhahiri kuwa watapata habari kwamba umekwisha wasili hapa.
23 Kwa hiyo fanya lile tunalokuambia. Tunao watu wanne hapa ambao wameweka nadhiri.
Basi, fanya kama tunavyokushauri. Tunao hapa watu wanne ambao wameweka nadhiri.
24 Jiunge na watu hawa, mfanye utaratibu wa ibada ya kujitakasa pamoja nao, na ulipe gharama ili wanyoe nywele zao. Kwa njia hii kila mtu atafahamu ya kuwa mambo waliyosikia si ya kweli na kwamba wewe unaishika sheria.
Jiunge nao katika ibada ya kujitakasa, ukalipe na gharama zinazohusika, kisha wanyolewe nywele zao. Hivyo watu wote watatambua kwamba habari zile walizoambiwa juu yako hazina msingi wowote, na kwamba wewe binafsi bado unaishi kufuatana na maagizo ya Sheria za Mose.
25 Lakini kuhusu wale watu wa Mataifa walioamini, tumewaandikia uamuzi wetu: kwamba wajitenge na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na wajiepushe na uasherati.”
Kuhusu wale watu wa mataifa mengine ambao wamekuwa waumini, tumekwisha wapelekea barua tukiwaambia mambo tuliyoamua: wasile chochote kilichotambikiwa miungu ya uongo, wasinywe damu, wasile nyama ya mnyama aliyenyongwa, na wajiepushe na uasherati.”
26 Ndipo kesho yake Paulo akawachukua wale watu na akajitakasa pamoja nao. Akaingia ndani ya hekalu ili atoe taarifa ya tarehe ambayo siku zao za utakaso zingemalizika na sadaka ingetolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.
Basi, kesho yake Paulo aliwachukua wale watu akafanya ibada ya kujitakasa pamoja nao. Kisha akaingia Hekaluni kutoa taarifa kuhusu mwisho wa siku za kujitakasa na kuhusu dhabihu itakayotolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.
27 Zile siku saba zilipokaribia kumalizika, baadhi ya Wayahudi kutoka sehemu za Asia waliokuwa wamemwona Paulo ndani ya Hekalu, wakachochea umati wote wa watu, nao wakamkamata.
Wakati siku hizo saba zilipokaribia kuisha, Wayahudi waliokuwa wametoka katika mkoa wa Asia walimwona Paulo Hekaluni. Wakachochea hasira kati ya kundi lote la watu, wakamtia nguvuni
28 Wakapiga kelele wakisema, “Waisraeli wenzetu, tusaidieni! Huyu ndiye yule mtu anayefundisha kila mtu na kila mahali, kinyume na watu wetu, sheria zetu na hata Hekalu hili. Zaidi ya hayo amewaleta Wayunani ndani ya Hekalu na kupanajisi mahali hapa patakatifu.”
wakipiga kelele: “Wananchi wa Israeli, msaada, msaada! Huyu ndiye yule mtu anayewafundisha watu kila mahali mambo yanayopinga watu wa Israeli, yanayopinga Sheria ya Mose na mahali hapa patakatifu. Hata sasa amewaingiza watu wa mataifa mengine Hekaluni na kupatia najisi mahali hapa patakatifu.”
29 (Walikuwa wamemwona Trofimo, mwenyeji wa Efeso, akiwa mjini pamoja na Paulo wakadhani kuwa Paulo alikuwa amemwingiza Hekaluni.)
Sababu ya kusema hivyo ni kwamba walikuwa wamemwona Trofimo mwenyeji, wa Efeso, akiwa pamoja na Paulo mjini, wakadhani kwamba Paulo alikuwa amemwingiza Hekaluni.
30 Mji wote ukataharuki, watu wakaja wakikimbia kutoka pande zote wakamkamata Paulo, wakamburuta kutoka Hekaluni. Milango ya Hekalu ikafungwa.
Mji wote ulienea ghasia; watu wakaja kutoka pande zote, wakamkamata Paulo, wakamburuta, wakamtoa nje ya Hekalu na papo hapo milango ya Hekalu ikafungwa.
31 Walipokuwa wakitaka kumuua, habari zikamfikia jemadari wa jeshi la askari wa Kirumi kwamba mji wa Yerusalemu wote ulikuwa katika machafuko.
Walikuwa tayari kumuua, lakini habari zilimfikia mkuu wa jeshi la Kiroma kuwa Yerusalemu yote ilikuwa imejaa ghasia.
32 Mara yule jemadari akachukua maafisa wengine wa jeshi pamoja na askari wakakimbilia kwenye ile ghasia, wale watu waliokuwa wakifanya ghasia walipomwona yule jemadari na askari wakija, wakaacha kumpiga Paulo.
Mara, mkuu wa jeshi akawachukua askari na jemadari, akalikabili lile kundi la watu. Nao walipomwona mkuu wa jeshi na askari, wakaacha kumpiga Paulo.
33 Yule jemadari akaja, akamkamata Paulo akaamuru afungwe kwa minyororo miwili. Akauliza yeye ni nani, na alikuwa amefanya nini.
Mkuu wa jeshi alimwendea Paulo, akamtia nguvuni na kuamuru afungwe minyororo miwili. Kisha akauliza, “Ni mtu gani huyu, na amefanya nini?”
34 Baadhi ya watu katika ule umati wakapiga kelele, hawa wakisema hili na wengine lile. Yule jemadari alipoona kuwa hawezi kupata hakika ya habari kwa sababu ya zile kelele, akaamuru Paulo apelekwe katika ngome ya jeshi.
Wengine katika lile kundi la watu walikuwa wanapayuka kitu hiki na wengine kitu kingine. Kwa sababu ya ghasia hiyo, mkuu wa jeshi hakufaulu kujua kisa kamili. Hivyo, aliamuru watu wake wampeleke Paulo ndani ya ngome.
35 Paulo alipofika penye ngazi, ilibidi askari wambebe juu juu kwa sababu fujo za ule umati wa watu zilikuwa kubwa.
Paulo alipofika kwenye ngazi, askari walilazimika kumbeba kwa sababu ya fujo za watu.
36 Umati wa watu ulikuwa ukifuata ukiendelea kupiga kelele ukisema, “Mwondoe huyu!”
Kwa maana kundi kubwa la watu walimfuata wakipiga kelele, “Muulie mbali!”
37 Mara tu Paulo alipokaribia kuingizwa kwenye ngome ya jeshi, akamwambia yule jemadari, “Je, naweza kukuambia jambo moja?” Yule jemadari akamjibu, “Je, unajua Kiyunani?
Walipokuwa wanamwingiza ndani ya ngome, Paulo alimwomba mkuu wa jeshi akisema, “Naweza kukwambia kitu?” Yule mkuu wa jeshi akamjibu, “Je unajua Kigiriki?
38 Je, wewe si yule Mmisri ambaye siku hizi za karibuni alianzisha uasi akaongoza kundi la magaidi 4,000 wenye silaha jangwani?”
Kwani wewe si yule Mmisri ambaye hivi majuzi alianzisha uasi na kuwaongoza majahili elfu nne hadi jangwani?”
39 Paulo akajibu, “Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso, huko Kilikia, raiya wa mji maarufu. Tafadhali niruhusu nizungumze na hawa watu.”
Paulo akajibu, “Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso katika Kilikia; mimi ni raia wa mji maarufu. Tafadhali, niruhusu niongee na watu.
40 Akiisha kupata ruhusa ya yule jemadari, Paulo akasimama penye ngazi akawapungia watu mkono ili wanyamaze. Wote waliponyamaza kimya, Paulo akazungumza nao kwa lugha ya Kiebrania, akasema:
Yule mkuu wa jeshi akamruhusu. Hivyo Paulo alisimama juu ya ngazi, akawapungia mkono wale watu na walipokaa kimya, akaanza kuongea nao kwa Kiebrania.

< Matendo 21 >