< Matendo 21 >
1 Tulipokwisha kujitenga nao, tukaanza safari kwa njia ya bahari moja kwa moja mpaka Kosi. Siku ya pili yake tukafika Rodo na kutoka huko tukaenda Patara.
Wakati tulipokua tumeachana nao, na tunasafiri baharini, tukafika moja kwa moja kwenye mji wa Kosi, na kesho yake tukafika mji wa Rodo, na kutoka huko tukafika mji wa Patara.
2 Hapo tukapata meli iliyokuwa inavuka kwenda Foinike tukapanda tukasafiri nayo.
Tulipopata meli inayovuka kwenda Foinike, tulipanda tukasafiri.
3 Tulipokiona kisiwa cha Kipro, tukakizunguka tukakiacha upande wetu wa kushoto, tukasafiri mpaka Shamu, tukatia nanga katika bandari ya Tiro ambapo meli yetu ilikuwa ipakue shehena yake.
Tulipofika mbele ya kisiwa cha Kipro, tukaiacha upande wa kushoto, tukasafiri hadi Siria, tukaweka nanga katika mji wa Tiro, kwa sababu huko ndiko meli ilikuwa ipakuliwe shehena yake.
4 Baada ya kuwatafuta wanafunzi wa huko, tukakaa nao kwa siku saba. Wale wanafunzi wakiongozwa na Roho wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu.
Baada ya kuwaona wanafunzi, tukakaa huko siku saba. Wanafunzi hawa wakamwambia Paulo kupitia kwa Roho kwamba yeye asikanyage Yerusalemu.
5 Lakini muda wetu ulipokwisha, tukaondoka tukaendelea na safari yetu. Wale wanafunzi pamoja na wake zao na watoto wakatusindikiza hadi nje ya mji. Wote tukapiga magoti pale pwani tukaomba.
Hata tulipotimiza siku zile, sisi tukaondoka tukaenda zetu. Wote pamoja, na wanawake zao na watoto wao, walitusindikiza katika njia zetu hadi tulipotoka nje ya mji. Kisha tukapiga magoti pwani, tukaomba, tukaagana kila mmoja.
6 Baada ya kuagana, tukapanda melini, nao wakarudi majumbani mwao.
Tukapanda meli, huku nao wakarudi nyumbani kwao tena.
7 Tukaendelea na safari yetu toka Tiro tukafika Tolemai, tukawasalimu ndugu wa huko, tukakaa nao kwa siku moja.
Hata tulipomaliza safari yetu kutoka Tiro, tukafika Tolemai. Pale tulisalimia ndugu, na kukakaa nao kwa siku moja.
8 Siku iliyofuata tukaondoka, tukafika Kaisaria. Huko tukaenda nyumbani kwa mwinjilisti mmoja jina lake Filipo, aliyekuwa mmoja wa wale Saba, tukakaa kwake.
Kesho yake tuliondoka tukaenda Kaisaria. Sisi tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa injili, aliyekuwa mmoja wa wale saba, nasi tukakaa pamoja naye.
9 Filipo alikuwa na binti wanne mabikira waliokuwa wanatoa unabii.
Mtu huyu alikuwa na mabinti wanne mabikira ambao walitabiri.
10 Baada ya kukaa kwa siku kadhaa, akateremka nabii mmoja kutoka Uyahudi jina lake Agabo.
Baada ya kukaa huko kwa siku kadhaa, akashuka kutoka Uyahudi nabii mmoja aitwaye Agabo.
11 Alipotufikia akachukua mshipi wa Paulo akajifunga, akautumia kufunga mikono na miguu yake mwenyewe akasema, “Roho Mtakatifu anasema: ‘Hivi ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mwenye mshipi huu na kumkabidhi kwa watu wa Mataifa.’”
Yeye alikuja kwetu na akautwaa mkanda wa Paulo. kwa huo alijifunga miguu na mikono yake mwenyewe na kusema, “Roho Mtakatifu asema hivi,” “Wayahudi wa Yerusalemu watamfunga mtu anayemiliki mkanda huu, nao watamkabidhi mikononi mwa watu wa mataifa.”
12 Tuliposikia maneno haya sisi na ndugu wengine tukamsihi Paulo asiende Yerusalemu.
Tuliposikia mambo hayo, sisi na watu waliokuwa wakiishi mahali pale tulimsihi Paulo asipande kwende Yerusalemu.
13 Lakini Paulo akajibu, “Kwa nini mnalia na kunivunja moyo? Mimi niko tayari si kufungwa tu, bali hata kufa huko Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana Yesu.”
Ndipo Paulo alijibu, “Mnafanya nini, mnalia na kunivunja moyo wangu? Kwa maana niko tayari, siyo tu kufungwa, lakini pia kufia huko Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana Yesu.”
14 Alipokuwa hashawishiki, tukaacha kumsihi, tukasema, “Mapenzi ya Bwana na yatendeke.”
Kwa vile Paulo hakutaka kushawishiwa, tuliacha na kusema, “Basi mapenzi ya Bwana yafanyike.”
15 Baada ya haya, tukajiandaa, tukaondoka kwenda Yerusalemu.
Baada ya siku hizi, tulichukua mifuko yetu na tukapanda Yerusalemu.
16 Baadhi ya wanafunzi kutoka Kaisaria wakafuatana nasi na kutupeleka nyumbani kwa Mnasoni, ambaye tungekaa kwake. Yeye alikuwa mtu wa Kipro, mmoja wa wanafunzi wa zamani.
Baadhi ya wanafunzi kutoka Kaisaria pia walifuatana nasi. Wakamleta mtu mmoja aitwaye Mnasoni, mtu wa Kipro, mwanafunzi wa zamani, ambaye tulikaa naye.
17 Tulipofika Yerusalemu ndugu wakatukaribisha kwa furaha.
Tulipofika Yerusalemu, ndugu walitukaribisha kwa furaha.
18 Kesho yake Paulo pamoja na wengine wetu tulikwenda kumwona Yakobo, na wazee wote walikuwepo.
Kesho yake Paulo alienda pamoja nasi kwa Yakobo, na wazee wote walikuwepo.
19 Baada ya kuwasalimu, Paulo akatoa taarifa kamili ya mambo yote ambayo Mungu alikuwa amefanya miongoni mwa watu wa Mataifa kupitia huduma yake.
Baada ya kuwasalimu, aliwapa taarifa moja baada ya nyingine ya mambo ambayo Mungu aliyotenda miongoni mwa mataifa kwa kupitia huduma yake.
20 Baada ya kusikia mambo haya wakamwadhimisha Mungu. Ndipo wakamwambia Paulo, “Ndugu, unaona kulivyo na maelfu ya Wayahudi walioamini, nao wote wana juhudi kwa ajili ya sheria.
Wakati waliposikia hayo, wakamsifu Mungu, na wakamwambia, “Unaona, ndugu, kuna maelfu wangapi wameamini miongoni mwa Wayahudi. Wao wote wana nia ya kushika sheria.
21 Lakini wameambiwa habari zako kwamba unafundisha Wayahudi wote waishio miongoni mwa watu wa Mataifa kumkataa Mose, na kwamba unawaambia wasiwatahiri watoto wao wala kufuata desturi zetu.
Wameambiwa kuhusu wewe, kwamba unafundisha Wayahudi wanaoishi kati ya mataifa kuachana na Musa, na kwamba unawaambia wasiwatahiri watoto wao, na wasifuate desturi za zamani.
22 Sasa tufanyeje? Bila shaka watasikia kwamba umekuja Yerusalemu.
Tunapaswa tufanye nini? Bila shaka watasikia kwamba wewe umekuja.
23 Kwa hiyo fanya lile tunalokuambia. Tunao watu wanne hapa ambao wameweka nadhiri.
Hivyo fanya kile sisi tunachokuambia sasa: tunao watu wanne ambao wameweka nadhiri.
24 Jiunge na watu hawa, mfanye utaratibu wa ibada ya kujitakasa pamoja nao, na ulipe gharama ili wanyoe nywele zao. Kwa njia hii kila mtu atafahamu ya kuwa mambo waliyosikia si ya kweli na kwamba wewe unaishika sheria.
Wachukue watu hawa na ujitakase mwenyewe pamoja nao, na uwalipie gharama zao, ili waweze kunyoa vichwa vyao. Hivyo kila mmoja apate kujua kwamba mambo waliyoambiwa kuhusu wewe ni ya uongo. Watajifunza kwamba wewe pia unafuata sheria.
25 Lakini kuhusu wale watu wa Mataifa walioamini, tumewaandikia uamuzi wetu: kwamba wajitenge na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na wajiepushe na uasherati.”
Lakini kwa habari za mataifa ambao wamekuwa waumini, tuliandika na kutoa maagizo kwamba wanapaswa kujiepusha na vitu vilivyotolewa dhabihu kwa sanamu, na damu, kutokana na kile kilichonyongwa, na wajiepushe na uasherati.”
26 Ndipo kesho yake Paulo akawachukua wale watu na akajitakasa pamoja nao. Akaingia ndani ya hekalu ili atoe taarifa ya tarehe ambayo siku zao za utakaso zingemalizika na sadaka ingetolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.
Ndipo, Paulo aliwatwaa wanaume, na siku ya pili, akajitakasa mwenyewe pamoja nao, akaingia Hekaluni, kutangaza kipindi cha siku za kujitakasa, hadi sadaka itolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.
27 Zile siku saba zilipokaribia kumalizika, baadhi ya Wayahudi kutoka sehemu za Asia waliokuwa wamemwona Paulo ndani ya Hekalu, wakachochea umati wote wa watu, nao wakamkamata.
Siku hizo saba zilipokaribia kumalizika, baadhi ya Wayahudi kutoka Asia wakamuona Paulo Hekaluni, na makutano wakakasirika, na wakamnyoshea mikono.
28 Wakapiga kelele wakisema, “Waisraeli wenzetu, tusaidieni! Huyu ndiye yule mtu anayefundisha kila mtu na kila mahali, kinyume na watu wetu, sheria zetu na hata Hekalu hili. Zaidi ya hayo amewaleta Wayunani ndani ya Hekalu na kupanajisi mahali hapa patakatifu.”
Walikuwa wanapiga kelele, “Watu wa Israeli, tusaidieni. Huyu ni yule mtu anayewafundisha watu kila mahali mambo ambayo ni kinyume na watu, sheria, na mahali hapa. Pia amewaleta Wayunani katika Hekalu na kupanajisi mahali hapa patakatifu.”
29 (Walikuwa wamemwona Trofimo, mwenyeji wa Efeso, akiwa mjini pamoja na Paulo wakadhani kuwa Paulo alikuwa amemwingiza Hekaluni.)
Kwa kuwa mwanzoni walikuwa wamemwona Trofimo Muefeso akiwa pamoja naye mjini, nao walidhani kwamba Paulo alimleta hekaluni.
30 Mji wote ukataharuki, watu wakaja wakikimbia kutoka pande zote wakamkamata Paulo, wakamburuta kutoka Hekaluni. Milango ya Hekalu ikafungwa.
Mji wote ulikuwa na taharuki, na watu wakakimbia pamoja na kumkamata Paulo. Wakamtoa nje ya Hekalu, na milango mara ikafungwa.
31 Walipokuwa wakitaka kumuua, habari zikamfikia jemadari wa jeshi la askari wa Kirumi kwamba mji wa Yerusalemu wote ulikuwa katika machafuko.
Walipokuwa wakijaribu kumuua, habari zilimfikia mkuu wa jeshi la walinzi kuwa Yerusalemu yote ilikuwa imejaa ghasia.
32 Mara yule jemadari akachukua maafisa wengine wa jeshi pamoja na askari wakakimbilia kwenye ile ghasia, wale watu waliokuwa wakifanya ghasia walipomwona yule jemadari na askari wakija, wakaacha kumpiga Paulo.
Mara hiyo akawachukua askari na jemadari akaukimbilia umati. Wakati Watu walipomwona mkuu wa jeshi na askari, wakaacha kumpiga Paulo.
33 Yule jemadari akaja, akamkamata Paulo akaamuru afungwe kwa minyororo miwili. Akauliza yeye ni nani, na alikuwa amefanya nini.
Kisha mkuu wa jeshi alimkaribia na akamshika Paulo, na akaamuru afungwe minyororo miwili. Akamuuliza yeye ni nani na amefanya nini.
34 Baadhi ya watu katika ule umati wakapiga kelele, hawa wakisema hili na wengine lile. Yule jemadari alipoona kuwa hawezi kupata hakika ya habari kwa sababu ya zile kelele, akaamuru Paulo apelekwe katika ngome ya jeshi.
Baadhi ya watu kwenye umati walikuwa wanapayuka kitu hiki na wengine kingine. Kwa kuwa jemadari hakuweza kuwaambia chochote kwa sababu ya zile kelele, akaamuru Paulo aletwe ndani ya ngome.
35 Paulo alipofika penye ngazi, ilibidi askari wambebe juu juu kwa sababu fujo za ule umati wa watu zilikuwa kubwa.
Basi alipofika kwenye ngazi, akachukuliwa na askari kwa sababu ya ghasia za umati.
36 Umati wa watu ulikuwa ukifuata ukiendelea kupiga kelele ukisema, “Mwondoe huyu!”
Maana umati wa watu walimfuata na waliendelea kupiga kelele, “Mwondoeni huyu!”
37 Mara tu Paulo alipokaribia kuingizwa kwenye ngome ya jeshi, akamwambia yule jemadari, “Je, naweza kukuambia jambo moja?” Yule jemadari akamjibu, “Je, unajua Kiyunani?
Paulo alipokuwa analetwa ndani ya ngome, alimwambia mkuu wa jeshi, “Naweza kukwambia kitu?” Yule mkuu wa jeshi akasema, “Je unaongea Kiyunani?
38 Je, wewe si yule Mmisri ambaye siku hizi za karibuni alianzisha uasi akaongoza kundi la magaidi 4,000 wenye silaha jangwani?”
Je, wewe si yule Mmisri ambaye awali aliongoza uasi na alichukua magaidi elfu nne nyikani?”
39 Paulo akajibu, “Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso, huko Kilikia, raiya wa mji maarufu. Tafadhali niruhusu nizungumze na hawa watu.”
Paulo akasema, “Mimi ni Myahudi, kutoka mji wa Tarso ya Kilikia. Mimi ni raia wa mji maarufu. Nawaomba, mniruhusu nizungumze na watu.”
40 Akiisha kupata ruhusa ya yule jemadari, Paulo akasimama penye ngazi akawapungia watu mkono ili wanyamaze. Wote waliponyamaza kimya, Paulo akazungumza nao kwa lugha ya Kiebrania, akasema:
Wakati jemadari alipompa ruhusa, Paulo akasimama penye ngazi na akatoa ishara kwa watu kwa mkono wake. Wakati kulipokuwa na ukimya sana, akaongea nao kwa Kihebrania. Akasema,