< Matendo 2 >

1 Siku ya Pentekoste ilipowadia, waamini wote walikuwa mahali pamoja.
Siku ya Pentekoste ilipofika, waumini wote walikuwa wamekusanyika pamoja.
2 Ghafula sauti kama mvumo mkubwa wa upepo mkali uliotoka mbinguni ukaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi.
Ghafla, sauti ikasikika kutoka angani; sauti iliyokuwa kama ya upepo mkali, ikajaza ile nyumba yote walimokuwa wamekaa.
3 Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kukaa juu ya kila mmoja wao.
Kisha, vikatokea vitu vilivyoonekana kama ndimi za moto, vikagawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao.
4 Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia.
Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha mbalimbali kadiri Roho alivyowawezesha.
5 Basi walikuwepo Yerusalemu Wayahudi wanaomcha Mungu kutoka kila taifa chini ya mbingu.
Na huko Yerusalemu walikuwako Wayahudi, watu wamchao Mungu, waliotoka katika kila nchi duniani.
6 Waliposikia sauti hii, umati wa watu ulikusanyika pamoja wakistaajabu, kwa sababu kila mmoja wao aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.
Waliposikia sauti hiyo, kundi kubwa la watu lilikusanyika. Wote walishtuka sana kwani kila mmoja wao aliwasikia hao waumini wakisema kwa lugha yake mwenyewe.
7 Wakiwa wameshangaa na kustaajabu wakauliza, “Je, hawa wote wanaozungumza si Wagalilaya?
Walistaajabu na kushangaa, wakisema, “Je, hawa wote tunaowasikia wakisema hivi, si wenyeji wa Galilaya?
8 Imekuwaje basi kila mmoja wetu anawasikia wakinena kwa lugha yake ya kuzaliwa?
Imekuwaje, basi, kwamba kila mmoja wetu anawasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe?
9 Wapathi, Wamedi, Waelami, wakazi wa Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto na Asia,
Baadhi yetu ni Waparthi, Wamedi na Waelami; wengine ni wenyeji wa Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na Asia,
10 Frigia, Pamfilia, Misri na pande za Libya karibu na Kirene na wageni kutoka Rumi,
Frugia na Pamfulia, Misri na sehemu za Libya karibu na Kurene; wengine wetu ni wageni kutoka Roma,
11 Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu, sote tunawasikia watu hawa wakisema mambo makuu ya ajabu ya Mungu katika lugha zetu wenyewe.”
Wayahudi na watu walioongokea dini ya Kiyahudi; wengine wametoka Krete na Arabia. Sisi sote tunasikia wakisema kwa lugha zetu wenyewe mambo makuu ya Mungu.”
12 Wakiwa wameshangaa na kufadhaika wakaulizana, “Ni nini maana ya mambo haya?”
Wote walishangaa na kufadhaika huku wakiulizana, “Hii ina maana gani?”
13 Lakini wengine wakawadhihaki wakasema, “Hawa wamelewa divai!”
Lakini wengine wakawadhihaki wakisema, “Watu hawa wamelewa divai mpya!”
14 Ndipo Petro akasimama pamoja na wale mitume kumi na mmoja, akainua sauti yake na kuhutubia ule umati wa watu, akasema: “Wayahudi wenzangu na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, jueni jambo hili mkanisikilize.
Lakini Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja akaanza kuwahutubia watu kwa sauti kubwa: “Ndugu Wayahudi nanyi nyote mnaokaa hapa Yerusalemu, sikilizeni kwa makini maneno yangu.
15 Hakika watu hawa hawakulewa kama mnavyodhania, kwa kuwa sasa ni saa tatu asubuhi!
Watu hawa hawakulewa kama mnavyodhani; mbona ni saa tatu tu asubuhi?
16 La, hili ni jambo lililotabiriwa na nabii Yoeli, akisema:
Ukweli ni kwamba jambo hili ni lile alilosema nabii Yoeli:
17 “‘Katika siku za mwisho, asema Mungu, nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili. Wana wenu na binti zenu watatabiri, vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto.
Katika siku zile za mwisho, asema Bwana, nitawamiminia binadamu wote Roho wangu. Watoto wenu, wanaume kwa wanawake, watautangaza ujumbe wangu; vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto.
18 Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile nitamimina Roho wangu, nao watatabiri.
Naam, hata watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, nitawamiminia Roho wangu, siku zile, nao watautangaza ujumbe wangu.
19 Nami nitaonyesha maajabu juu mbinguni, na ishara chini duniani: damu, moto, na mawimbi ya moshi.
Nitatenda miujiza juu angani, na ishara chini duniani; kutakuwa na damu, moto na moshi mzito;
20 Jua litakuwa giza na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kuja siku ile kuu ya Bwana iliyo tukufu.
jua litatiwa giza, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kutokea ile siku kuu na tukufu ya Bwana.
21 Na kila mtu atakayeliitia jina la Bwana, ataokolewa.’
Hapo, yeyote atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.
22 “Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Yesu wa Nazareti alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kupitia kwake, kama ninyi wenyewe mjuavyo.
“Wananchi wa Israeli, sikilizeni maneno haya! Yesu wa Nazareti alikuwa mtu ambaye mamlaka yake ya kimungu yalithibitishwa kwenu kwa miujiza, maajabu na ishara Mungu alizofanya kati yenu kwa njia yake, kama mnavyojua.
23 Huyu mtu akiisha kutolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa kwa kujua kwake Mungu tangu zamani, ninyi, kwa mikono ya watu wabaya, mlimuua kwa kumgongomea msalabani.
Kufuatana na mpango wake mwenyewe Mungu alikwisha amua kwamba Yesu angetiwa mikononi mwenu; nanyi mkamuua kwa kuwaachia watu wabaya wamsulubishe.
24 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu akamwondolea uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana yeye kushikiliwa na nguvu za mauti.
Lakini Mungu alimfufua kutoka wafu akamwokoa katika maumivu ya kifo kwa maana haingewezekana kabisa kifo kimfunge.
25 Kwa maana Daudi asema kumhusu yeye: “‘Nalimwona Bwana mbele yangu daima. Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume, sitatikisika.
Maana Daudi alisema juu yake hivi: Nilimwona Bwana mbele yangu daima; yuko nami upande wangu wa kulia, na hivyo sitatikisika.
26 Kwa hiyo moyo wangu unafurahia, na ulimi wangu unashangilia; mwili wangu nao utapumzika kwa tumaini.
Kwa hiyo, moyo wangu ulifurahi; tena nilipiga vigelegele vya furaha. Mwili wangu utakaa katika tumaini;
27 Kwa maana hutaniacha kaburini, wala hutamwacha Aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu. (Hadēs g86)
kwa kuwa hutaiacha roho yangu katika kuzimu, wala kumruhusu mtakatifu wako aoze. (Hadēs g86)
28 Umenionyesha njia za uzima, utanijaza na furaha mbele zako.’
Umenionyesha njia za kuufikia uzima, kuwako kwako kwanijaza furaha!
29 “Ndugu zangu Waisraeli, nataka niwaambie kwa uhakika kwamba baba yetu Daudi alikufa na kuzikwa, nalo kaburi lake lipo hapa mpaka leo.
“Ndugu zangu, napenda kuwaambieni waziwazi juu ya mambo yaliyompata Daudi, babu yetu. Yeye alikufa, akazikwa, tena kaburi lake liko papa hapa petu mpaka leo.
30 Lakini alikuwa nabii na alijua ya kuwa Mungu alikuwa amemwahidi kwa kiapo kwamba angemweka mmoja wa wazao wake penye kiti chake cha enzi.
Lakini kwa vile Daudi alikuwa nabii, alijua kuwa Mungu alimwapia kiapo kwamba atamtawaza mmoja wa uzawa wake kuwa mfalme mahali pake.
31 Daudi, akiona mambo yaliyoko mbele, akanena juu ya kufufuka kwa Kristo, kwamba hakuachwa kaburini, wala mwili wake haukuona uharibifu. (Hadēs g86)
Daudi aliona kabla mambo yatakayofanywa na Mungu na hivyo akasema juu ya ufufuo wa Kristo wakati aliposema: Hakuachwa kuzimu, mwili wake haukuoza. (Hadēs g86)
32 Mungu alimfufua huyu Yesu na sisi sote ni mashahidi wa jambo hilo.
Basi, Mungu alimfufua huyo Yesu na sisi sote ni mashahidi wa tukio hilo.
33 Basi ikiwa yeye ametukuzwa kwa mkono wa kuume wa Mungu, amepokea kutoka kwa Baba ahadi ya Roho Mtakatifu, naye amemimina kile mnachoona sasa na kusikia.
Yesu aliinuliwa juu mpaka upande wa kulia wa Mungu, akapokea kutoka kwa Baba ile zawadi aliyoahidi yaani Roho Mtakatifu; na mnachoona sasa na kusikia ni mmiminiko wa huyo Roho.
34 Kwa kuwa Daudi hakupaa kwenda mbinguni, lakini anasema, “‘Bwana alimwambia Bwana wangu: “Keti mkono wangu wa kuume,
Maana Daudi mwenyewe, hakupanda mpaka mbinguni; ila yeye alisema: Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia,
35 hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.”’
hadi nitakapowafanya adui zako kibao cha kukanyagia miguu yako.
36 “Kwa hiyo Israeli wote na wajue jambo hili kwa uhakika kwamba: Mungu amemfanya huyu Yesu, ambaye ninyi mlimsulubisha, kuwa Bwana na Kristo.”
“Watu wote wa Israeli wanapaswa kufahamu kwa hakika kwamba huyo Yesu mliyemsulubisha ninyi, ndiye huyo ambaye Mungu amemfanya kuwa Bwana na Kristo.”
37 Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?”
Basi, watu waliposikia hayo, walichomwa moyo, wakawauliza Petro na wale mitume wenzake: “Ndugu zetu, tufanye nini?”
38 Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
Petro akajibu, “Tubuni na kila mmoja wenu abatizwe kwa jina la Yesu Kristo ili mpate kuondolewa dhambi zenu na kupokea ile zawadi ya Roho Mtakatifu.
39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu, na kwa wote walio mbali, na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.”
Maana, ahadi ile ilikuwa kwa ajili yenu, kwa ajili ya watoto wenu, kwa ajili ya wote wanaokaa mbali; na kwa ajili ya kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita kwake.”
40 Petro akawaonya kwa maneno mengine mengi na kuwasihi akisema, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka.”
Kwa maneno mengine mengi, Petro alisisitiza na kuwahimiza watu akisema, “Jiokoeni katika kizazi hiki kiovu.”
41 Wale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa na siku ile waliongezeka watu wapatao 3,000.
Wengi waliyakubali maneno yake, wakabatizwa. Watu wapatao elfu tatu wakaongezeka katika kile kikundi siku hiyo.
42 Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali.
Hawa wote waliendelea kujifunza kutoka kwa mitume, kuishi pamoja kidugu, kumega mkate na kusali.
43 Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume.
Miujiza na maajabu mengi yalifanyika kwa njia ya mitume hata kila mtu akajawa na hofu.
44 Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika.
Waumini wote waliendelea kuwa kitu kimoja na mali zao waligawana pamoja.
45 Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.
Walikuwa wakiuza mali na vitu vyao kisha wakagawana fedha kadiri ya mahitaji ya kila mmoja.
46 Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe,
Waliendelea kukutana pamoja kila siku Hekaluni. Lakini wakati wa kumega mkate, walikutana katika nyumba zao na wakakishiriki chakula hicho kwa furaha na moyo mkunjufu.
47 wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa wale waliokuwa wakiokolewa.
Walimtukuza Mungu, wakapendwa na watu wote. Kila siku Bwana aliwaongezea idadi ya watu waliokuwa wakiokolewa.

< Matendo 2 >