< Matendo 17 >

1 Wakasafiri kupitia Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambako kulikuwa na sinagogi la Wayahudi.
Na walipopita katika miji ya Amfipoli na Apolonia, walikuja mpaka mji wa Thesalonike ambao kulikuwa na sinagogi la Wayahudi.
2 Kama desturi yake, Paulo aliingia ndani ya sinagogi, na kwa muda wa Sabato tatu akawa anahojiana nao kutoka kwenye Maandiko,
Kama ilivyo kawaida ya Paulo, alienda kwao, na kwa muda wa siku tatu za Sabato alijadiliana nao juu ya maandiko.
3 akidhihirisha wazi na kuthibitisha kwamba ilikuwa lazima Kristo ateswe na afufuke kutoka kwa wafu. Akasema, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake, ndiye Kristo.”
Alikuwa akiwafungulia maandiko na kuwaeleza kuwa, ilimpasa Kristo ateseke na kisha kufufuka tena kutoka kwa wafu. Aliwaambia, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake ndiye Kristo”
4 Baadhi ya Wayahudi wakasadiki, wakaungana na Paulo na Sila, wakiwepo idadi kubwa ya Wayunani waliomcha Mungu na wanawake wengi mashuhuri.
Baadhi ya Wayahudi walishawishika na kuungana na Paulo na Sila, pamoja na Wagiriki wachamungu, akinamama wengi waongofu na kundi kubwa la watu.
5 Lakini Wayahudi ambao hawakuwa wameamini wakawa na wivu, wakawakodi watu waovu kutoka sokoni, wakakutanisha umati wa watu, wakaanzisha ghasia mjini. Wakaenda mbio nyumbani kwa Yasoni wakiwatafuta Paulo na Sila ili kuwaleta nje penye ule umati wa watu.
Lakini baadhi ya Wayahudi wasioamini, waliojawa na wivu, walienda sokoni na kuwachukuwa baadhi ya watu waovu, wakakusanya umati wa watu pamoja, na kusababisha ghasia mjini, kisha wakaivamia nyumba ya Jason, wakitaka kuwakamata Paulo na Sila ilikuwaleta mbele za watu.
6 Lakini walipowakosa wakamburuta Yasoni na ndugu wengine mbele ya maafisa wa mji, wakipiga kelele: “Watu hawa ni wale walioupindua ulimwengu wamekuja huku,
Lakini walipowakosa, walimkamata Yasoni na baadhi ya ndugu wengine na kuwapeleka mbele ya maofisa wa mji, wakipiga kelele, “Hawa wanaume walioupindua ulimwengu wamefika mpaka huku pia,
7 naye Yasoni amewakaribisha nyumbani mwake. Hawa wote wanaasi amri za Kaisari wakisema yuko mfalme mwingine aitwaye Yesu.”
Wanaume hawa waliokaribishwa na Yasoni wanaihalifu sheria ya Kaisari, wanasema kuna mfalme mwingine anayeitwa Yesu”
8 Waliposikia haya, ule umati wa watu na maafisa wa mji wakaongeza ghasia.
Umati na maofisa wa mji waliposikia mambo hayo, waliingiwa na wasiwasi.
9 Nao baada ya kuchukua dhamana kwa ajili ya Yasoni na wenzake wakawaacha waende zao.
Baada ya kuwa wamekwisha kuchukua fedha ya thamani ya ulinzi kutoka kwa Yason na wengine, waliwaachia waende.
10 Usiku ule ule, wale ndugu walioamini wakawapeleka Paulo na Sila waende zao Beroya. Walipowasili huko wakaenda kwenye sinagogi la Wayahudi.
Usiku ule ndugu walimtuma Paulo na Sila Beroya. Na walipofika kule walikwenda katika sinagogi la Wayahudi.
11 Hawa Waberoya walikuwa waungwana zaidi kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa waliupokea ule ujumbe kwa shauku kubwa na kuyachunguza Maandiko kila siku ili kuona kama yale Paulo aliyosema yalikuwa kweli.
Watu wale walikuwa wenye werevu mkubwa kuliko wale watu wa Thesalonike, kwa sababu walikuwa na utayari wa kulipokea neno kwa akili zao, na kuchunguza maandiko kila siku ili kuona kama maneno yaliyonenwa ndivyo yalivyo.
12 Wayahudi wengi wakaamini pamoja na wanawake na wanaume wa Kiyunani wa tabaka la juu.
Kwa hiyo wengi wao waliamini, wakiwemo wanawake wenye ushawishi mkubwa wa Kigiriki na wanaume wengi.
13 Lakini wale Wayahudi wa Thesalonike waliposikia kuwa Paulo anahubiri neno la Mungu huko Beroya, wakaenda huko ili kuwashawishi watu na kuwachochea.
Lakini Wayahudi wa Thesalonike walipogundua kwamba Paulo anatangaza neno la Mungu huko Beroya, walienda huko na kuchochea na kisha kuanzisha ghasia kwa watu.
14 Mara hiyo, wale ndugu wakamsafirisha Paulo hadi pwani, lakini Sila na Timotheo wakabaki Beroya.
Kwa haraka, ndugu wakampeleka Paulo kwa njia ya ziwa, lakini Sila na Timotheo wakabaki pale.
15 Wale waliomsindikiza Paulo wakaenda naye mpaka Athene, kisha wakarudi Beroya wakiwa na maagizo kutoka kwa Paulo kuhusu Sila na Timotheo kwamba wamfuate upesi iwezekanavyo.
Wale ndugu waliompeleka Paulo walienda naye hadi Athene, walipomwacha Paulo huko, walipokea maagizo kutoka kwake kuwa, Sila na Timotheo waje kwake kwa haraka iwezeanavyo.
16 Paulo alipokuwa akiwasubiri huko Athene, alisumbuka sana moyoni mwake kuona vile mji huo ulivyojaa sanamu.
Na wakati akiwasubiri huko Athene, roho yake ilikasirishwa ndani yake kwa jinsi alivyouona mji ulivyojaa sanamu nyingi.
17 Hivyo akahojiana kwenye sinagogi na Wayahudi pamoja na Wayunani waliomcha Mungu, na pia sokoni kila siku na watu aliopatana nao huko.
Hivyo akajadiliana katika sinagogi na wayahudi wale waliomcha Mungu na kwa wale wote aliokutana nao kila siku sokoni.
18 Kisha baadhi ya Waepikureo na Wastoiko wenye falsafa wakakutana naye. Baadhi yao wakasema, “Je, huyu mpayukaji anajaribu kusema nini?” Wengine wakasema, “Inaonekana anasema habari za miungu ya kigeni.” Walisema haya kwa sababu Paulo alikuwa anahubiri habari njema kuhusu Yesu na ufufuo wa wafu.
Lakini baathi ya Wanafalsafa wa Waepikureo na Wastoiko wakamkabili. Na wengine wakasema, “Ni nini anachokisema huyu mwongeaji mchanga? Wengine wakasema, “inaonekana anahubiri habari ya mungu mgeni,” kwasababu anahubiri habari ya Yesu na ufufuo.
19 Hivyo wakamchukua na kumleta kwenye mkutano wa Areopago, walikomwambia, “Je, tunaweza kujua mafundisho haya mapya unayofundisha ni nini?
Wakamchukua Paulo na kumleta Areopago, wakisema, “Twaweza kujua haya mafundisho mapya unayoyaongea?
20 Wewe unaleta mambo mapya masikioni mwetu, hivyo tungetaka kujua maana yake ni nini.”
Kwasababu unaleta mambo mapya katika masikio yetu. Kwahivyo tunataka kujua haya mambo yana maana gani?”
21 (Waathene na wageni wote walioishi humo hawakutumia muda wao kufanya chochote kingine isipokuwa kueleza au kusikia mambo mapya).
(Na watu wote wa Athene pamoja na wageni waliopo kwao, hutumia muda wao aidha katika kuongea na kusikiliza juu ya jambo jipya.)
22 Ndipo Paulo akasimama katikati ya Areopago akasema, “Enyi watu wa Athene! Ninaona kwamba katika kila jambo ninyi ni watu wa dini sana.
Kwa hiyo Paulo akasimama katikati ya watu wa Areopago na kusema, “Enyi watu wa Athene, naona kuwa ninyi ni watu wa dini kwa kila namna,
23 Kwa kuwa nilipokuwa nikitembea mjini na kuangalia kwa bidii vitu vyenu vya kuabudiwa, niliona huko madhabahu moja iliyoandikwa: Kwa Mungu Asiyejulikana. Basi sasa kile ambacho mmekuwa mkikiabudu kama kisichojulikana, ndicho ninachowahubiria.
Kwani katika kupita kwangu na kuangalia vitu vyenu vya kuabudu, nimeona maneno yalioandikwa kwenye moja ya madhabahu yenu, ikisema “KWA MUNGU ASIYEJULIKANA”. Hivyo basi, huyo mnayemwabudu pasipokujua, ndiye ninayewajulisha ninyi.
24 “Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, yeye ndiye Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu.
Mungu aliyeumba dunia na kila kitu kilichoko ndani, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hawezi kukaa katika mahekalu yaliyotengenezwa na mikono.
25 Wala hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji chochote, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye awapaye watu wote uhai na pumzi na vitu vyote.
Na pia hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu kwao, kwani yeye mwenyewe huwapa watu uzima na pumzi na vitu vingine vyote.
26 Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi.
Kupitia mtu mmoja, alifanya mataifa yote ya watu waishio juu ya uso wa dunia, na akawawekea nyakati na mipaka katika maeneo wanaoishi.
27 Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu.
Kwa hiyo, wanatakiwa kumtafuta Mungu, na yamkini wamfikie na kumpata, na kwa uhakika hayupo mbali na kila mmoja wetu.
28 ‘Kwa kuwa katika yeye tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni watoto wake.’
Kwake tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu, kama vile mtunzi wenu mmoja wa shairi aliposema 'tu wazaliwa wake.'
29 “Kwa kuwa sisi ni watoto wa Mungu, haitupasi kudhani kuwa uungu ni kama sanamu ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe, mfano uliotengenezwa kwa ubunifu na ustadi wa mwanadamu.
Kwa hiyo, ikiwa sisi ni wazaliwa wa Mungu, hatupaswi kufikiri kuwa uungu ni kama dhahabu, au shaba, au mawe, sanamu iliyochongwa kwa ustadi na mawazo ya watu.
30 Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu.
Kwa hiyo, Mungu alinyamazia nyakati zile za ujinga, lakini sasa anaamuru watu wote kila mahali wapate kutubu.
31 Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua. Amewahakikishia watu wote mambo haya kwa kumfufua Kristo kutoka kwa wafu.”
Hii ni kwa sababu ameweka siku atakayo ihukumu dunia kwa haki kwa mtu ambaye alimchagua. Mungu alitoa uhakika wa mtu huyu kwa kila mtu pale alipomfufua katoka kwa wafu.
32 Waliposikia habari za ufufuo wa wafu, baadhi yao wakadhihaki, lakini wengine wakasema, “Tunataka kukusikia tena ukizungumza juu ya jambo hili.”
Na watu wa Athene waliposikia habari ya kufufuliwa kwa wafu, baadhi yao wakamdhihaki Paulo, ila wengine wakasema “Tutakusikiliza tena kwa habari ya jambo hili”
33 Kwa hiyo Paulo akaondoka katikati yao.
Baada ya hapo, Paulo akawaacha.
34 Lakini baadhi yao wakaungana naye wakaamini. Kati yao alikuwepo Dionisio, Mwareopago na mwanamke mmoja aliyeitwa Damari na wengine wengi.
Lakini baadhi ya watu waliungana naye wakaamini, akiwemo Dionisio Mwareopago, na Mwanamke anaitwa Damari na wengine pamoja nao.

< Matendo 17 >