< Matendo 16 >
1 Paulo akafika Derbe na kisha Listra, ambako kulikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, ambaye mama yake alikuwa Myahudi aliyeamini, lakini baba yake alikuwa Myunani.
Paulo pia alipokuja Derbe na Lystra; na tazama, pale palikuwepo na mwanafunzi aitwaye Timotheo, ni Kijana aliyezaliwa na mama wa Kiyahudi ambaye ni muumini na baba yake ni Mgiriki.
2 Alikuwa amesifiwa sana na wale ndugu waliokuwa wameamini huko Listra na Ikonio
Watu wa Listra na Ikonia walimshudia vizuri.
3 Paulo alitaka Timotheo afuatane naye, hivyo akamchukua na kumtahiri kwa sababu ya Wayahudi waliokuwa wanaishi eneo lile kwa maana wote walimjua baba yake ni Myunani.
Paulo alimtaka ili asafiri naye, hivyo akamchukua na kumtahiri kwa sababu ya Wayahudi waliokuwako huko kwani wote walimjua kuwa baba yake ni Mgiriki.
4 Walipokuwa wakienda mji kwa mji, wakawa wanawapa maamuzi yaliyotolewa na mitume na wazee huko Yerusalemu ili wayafuate.
Walipokuwa wakienda walipita kwenye miji na kutoa maagizo kwa makanisa ili kuyatii maagizo hayo yaliandikwa na mitume na wazee huko Yerusalemu.
5 Hivyo makanisa yakawa imara katika imani na kuongezeka kiidadi kila siku.
Hivyo makanisa yakaimarishwa katika imani na walioamini wakaongezeka kwa idadi kila siku.
6 Paulo pamoja na wenzake wakasafiri sehemu za Frigia na Galatia, kwa kuwa Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kulihubiri neno huko Asia.
Paulo na mwenzake wakaenda Firigia na Galatia, kwani Roho wa Mungu aliwakataza kuhubiri neno huko kwenye jimbo la Asia.
7 Walipofika mpaka wa Misia, wakajaribu kuingia Bithinia lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu.
Walipokaribia Misia, walijaribu kwenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu akawakataza.
8 Kwa hiyo wakapita Misia, wakafika Troa.
Kwa hiyo wakapita Misia wakaja mpaka Mji wa Troa.
9 Wakati wa usiku Paulo akaona maono, mtu wa Makedonia amesimama akimsihi, “Vuka uje huku Makedonia utusaidie.”
Maono yalimtokea Paulo usiku, kulikuwa na mtu wa Makedonia amesimama, akimwita na kusema “Njoni mtusaidie huku Makedonia”.
10 Baada ya Paulo kuona maono haya, tulijiandaa kwa haraka kuondoka kwenda Makedonia tukiwa tumesadiki kuwa Mungu alikuwa ametuita kuhubiri habari njema huko.
Paulo alipoona maono, mara tukajiandaa kwenda Makedonia, akijua kwamba Mungu alituita kwenda kuwahubiria injili.
11 Tukasafiri kwa njia ya bahari kutoka Troa na kwenda moja kwa moja hadi Samothrake, kesho yake tukafika Neapoli.
Hivyo tukaondoka kutoka Troa, tukaenda moja kwa moja Samothrake, na siku iliyofuata tukafika mji wa Neapoli.
12 Kutoka huko tukasafiri hadi Filipi, mji mkuu wa jimbo hilo la Makedonia, uliokuwa koloni ya Warumi. Nasi tukakaa huko siku kadhaa.
Kutoka hapo tukaenda Filipi ambao ni moja ya mji wa Makedonia, mji muhimu katika wilaya na utawala wa Kirumi na tukakaa siku kadhaa.
13 Siku ya Sabato tukaenda nje ya lango la mji kando ya mto, mahali ambapo tulitarajia tungepata mahali pa kufanyia maombi. Tukaketi, tukaanza kuongea na baadhi ya wanawake waliokuwa wamekusanyika huko.
Siku ya Sabato, tulikwenda nje ya lango kwa njia ya mto, sehemu ambayo tulidhania kutakuwa na mahali pa kufanyia maombi. Tulikaa chini na kuongea na akinamama waliokuja pamoja.
14 Mmoja wa wale wanawake waliotusikiliza aliitwa Lidia, mfanyabiashara wa nguo za zambarau, mwenyeji wa mji wa Thiatira, aliyekuwa mcha Mungu. Bwana akaufungua moyo wake akaupokea ujumbe wa Paulo.
Mwanamke mmoja aitwaye Lidia, muuzaji wa zambarau, kutoka katika mji wa Tiatira, mwenye kumwabudu Mungu, alitusikiliza. Bwana alimfungua moyo wake na kuweka maanani maneno yaliyosemwa na Paulo.
15 Basi alipokwisha kubatizwa yeye na watu wa nyumba yake, alitukaribisha nyumbani kwake akisema, “Kama mmeona kweli mimi nimemwamini Bwana, karibuni mkae nyumbani mwangu.” Naye akatushawishi.
Baada ya kubatizwa, yeye na nyumba yake yote, alitusihi akisema “kama mmeniona kuwa mimi ni mwaminifu katika Bwana, basi nawasihi muingie na kukaa kwangu”. Akatusihi sana.
16 Siku moja, tulipokuwa tukienda mahali pa kusali, tulikutana na mtumwa mmoja wa kike ambaye alikuwa na pepo wa uaguzi. Naye alikuwa amewapa mabwana zake mapato makubwa ya fedha kwa ubashiri.
Ikawa kwamba, tulipokuwa tunaenda mahali pa kuomba, msichana mmoja aliyekuwa na pepo la utambuzi akakutana nasi. Alimletea bwana wake faida nyingi kwa kubashiri.
17 Huyu msichana alikuwa akimfuata Paulo na sisi akipiga kelele, “Watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, wao wanawatangazieni njia ya wokovu.”
Mwanamke huyu alimfuata Paulo pamoja na sisi, akipiga kelele na kusema “Hawa wanaume ni watumishi wa Mungu aliye Mkuu, wanaowatangazia ninyi habari ya wokovu”.
18 Akaendelea kufanya hivi kwa siku nyingi, lakini Paulo akiwa ameudhika sana, akageuka na kumwambia yule pepo mchafu, “Ninakuamuru katika jina la Yesu Kristo, umtoke!” Yule pepo mchafu akamtoka saa ile ile.
Alifanya hivyo kwa siku nyingi, lakini Paulo akiwa amekasirishwa na tendo hilo, aligeuka nyuma na kumwambia pepo, “Nakuamuru kwa Jina la Yesu umtoke ndani yake.” Naye akatoka na kumwacha mara moja.
19 Basi mabwana wa yule mtumwa wa kike walipoona kuwa tumaini lao la kuendelea kujipatia fedha limetoweka, wakawakamata Paulo na Sila wakawaburuta mpaka sokoni mbele ya viongozi wa mji.
Mabwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limeondoka, waliwakamata Paulo na Sila na kuwaburuza sokoni mbele ya wenye mamlaka.
20 Baada ya kuwafikisha mbele ya mahakimu wakawashtaki wakisema, “Hawa watu wanaleta ghasia katika mji wetu, nao ni Wayahudi.
Walipowafikisha kwa mahakimu, walisema, “Hawa wanaume ni Wayahudi na wanasababisha ghasia kubwa katika mji wetu.
21 Wanafundisha desturi ambazo sisi raiya wa Kirumi hatuwezi kuzikubali au kuzitimiza.”
Wanafundisha mambo ambayo siyo sheria sisi kuyapokea wala kuyafuata kama Warumi.”
22 Umati wa watu waliokuwepo wakajiunga katika kuwashambulia Paulo na Sila na wale mahakimu wakaamuru wavuliwe nguo zao na wachapwe viboko.
Umati ukawainukia kinyume Paulo na Sila, mahakimu wakararua nguo zao na kuwavua na kuamuru wachapwe viboko
23 Baada ya kuwachapa sana, wakawatupa gerezani na kumwagiza mkuu wa gereza awalinde kikamilifu.
Baada ya kuwachapa viboko vingi, waliwatupa gerezani na kumuamuru askari wa gereza kuwalinda vyema.
24 Kufuata maelekezo haya, yule mkuu wa gereza akawaweka katika chumba cha ndani sana mle gerezani, na akawafunga miguu yao kwa minyororo.
Baada ya kupokea amri hiyo, askari wa gereza aliwatupa katika chumba cha ndani ya gereza na kuwafunga miguu yao kwenye sehemu alipowahifadhi.
25 Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.
Wakati wa usiku wa manane, Paulo na Sila wakawa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, huku wafungwa wengine wakiwasikiliza,
26 Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka.
Ghafla kukatokea tetemeko kuu na misingi ya gereza ikatikiswa, milango ya gereza ikafunguka, na minyororo ya wafungwa wote ikalegezwa.
27 Yule mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza iko wazi, akachomoa upanga wake akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wote wametoroka.
Mlinzi wa Gereza aliamka kutoka usingizini na akaona milango yote ya gereza imefunguliwa; hivyo akachukua upanga wake maana alitaka kujiua kwa sababu alifikiri wafungwa wote walikwishatoroka,
28 Lakini Paulo akapiga kelele kwa sauti kubwa, akasema, “Usijidhuru kwa maana sisi sote tuko hapa!”
Lakini, Paulo akapiga kelele kwa sauti kuu, akisema “usijidhuru kwa sababu wote tuko mahali hapa”.
29 Yule askari wa gereza akaagiza taa ziletwe, akaingia ndani ya kile chumba cha gereza, akapiga magoti akitetemeka mbele ya Paulo na Sila.
Mlinzi wa gereza aliomba taa ziletwe na akaingia ndani ya gereza kwa haraka, akitetemeka na kuogopa, akawaangukia Paulo na Sila,
30 Kisha akawaleta nje akisema, “Bwana zangu, nifanye nini nipate kuokoka?”
na kuwatoa nje ya gereza na kusema, “Waheshimiwa, nifanye nini ili nipate kuokoka?”
31 Wakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu Kristo, nawe utaokoka, pamoja na watu wa nyumbani mwako.”
Nao wakamwambia, “Mwamini Bwana Yesu nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.”
32 Wakamwambia neno la Bwana yeye pamoja na wote waliokuwako nyumbani mwake.
Walinena neno la Bwana kwake, pamoja na watu wote wa nyumbani kwake,
33 Wakati ule ule, yule mkuu wa gereza akawachukua, akawaosha majeraha yao, kisha akabatizwa yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake bila kuchelewa.
Mlinzi wa gereza aliwachukua usiku ule na kuwaosha sehemu walizoumia, yeye pamoja na watu wa nyumbani mwake wakabatizwa mara.
34 Akawapandisha nyumbani mwake akawaandalia chakula, yeye pamoja na nyumba yake yote wakafurahi sana kwa kuwa sasa walikuwa wamemwamini Mungu.
Akawaleta Paulo na Sila nyumbani kwake na kuwatengea chakula. Naye akawa na furaha kuu pamoja na watu wa nyumbani mwake kwa sababu walimwamini Mungu.
35 Kulipopambazuka wale mahakimu wakawatuma maafisa wao kwa mkuu wa gereza wakiwa na agizo linalosema, “Wafungue wale watu, waache waende zao.”
Ilipokuwa mchana, mahakimu walituma ujumbe kwa yule mlinzi wa gereza wakisema, “Waruhusu wale watu waende”,
36 Mkuu wa gereza akamwambia Paulo “Mahakimu wameagiza niwaache huru, kwa hiyo tokeni na mwende zenu kwa amani.”
Mlinzi wa gereza akamjulisha Paulo juu ya maneno hayo ya kuwa, “Mahakimu walituma ujumbe niruhusu mwondoke: hivyo tokeni nje na mwende kwa amani.”
37 Lakini Paulo akawaambia wale maafisa, “Wametupiga hadharani bila kutufanyia mashtaka na kutuhoji, nao wakatutupa gerezani, hata ingawa sisi ni raiya wa Rumi. Nao sasa wanataka kututoa gerezani kwa siri? Hapana! Wao na waje wenyewe watutoe humu gerezani.”
Lakini Paulo akawaambia, “Walitupiga hadharani, watu ambao ni Warumi bila kutuhukumu na waliamua kututupa gerezani; halafu sasa wanataka kututoa kwa siri? Hapana, haitawezekana, wao wenyewe waje kututoa mahali hapa”.
38 Wale maafisa wakarudi na kuwaambia wale mahakimu maneno haya, wakaogopa sana walipofahamu kuwa Paulo na Sila ni raiya wa Rumi.
Walinzi wakawajulisha mahakimu juu ya maneno hayo, mahakimu wakaogopa sana pale walipojua kuwa Paulo na Sila ni Warumi.
39 Kwa hiyo wakaja wakawaomba msamaha, wakawatoa gerezani, wakawaomba waondoke katika ule mji.
Mahakimu wakaja na kuwasihi watoke, na walipowatoa nje ya gereza, waliwaomba Paulo na Sila watoke nje ya mji wao.
40 Baada ya Paulo na Sila kutoka gerezani walikwenda nyumbani kwa Lidia, ambapo walikutana na wale ndugu walioamini, wakawatia moyo, ndipo wakaondoka.
Kwa hiyo Paulo na Sila wakatoka nje ya gereza wakaja nyumbani kwa Lidia. Paulo na Sila walipowaona ndugu, waliwatia moyo na kisha kuondoka katika mji huo.