< Matendo 10 >

1 Katika mji wa Kaisaria palikuwa na mtu jina lake Kornelio, ambaye alikuwa jemadari wa kile kilichojulikana kama kikosi cha Kiitalia.
Kulikuwa na mtu fulani katika mji wa kaisaria, jina lake aliitwa Kornelio, alikuwa mkuu wa kikosi cha Kiitalia.
2 Yeye alikuwa mcha Mungu pamoja na wote wa nyumbani mwake. Aliwapa watu sadaka nyingi na kumwomba Mungu daima.
Alikuwa mchamungu na alimwabudu Mungu na nyumba yake yote; alitoa pesa nyingi kwa wayahudi na aliomba kwa Mungu siku zote.
3 Siku moja alasiri, yapata saa tisa, aliona maono waziwazi, malaika wa Mungu akimjia na kumwambia, “Kornelio!”
Muda wa saa tisa za mchana, akaona maono Malaika wa Mungu anakuja kwake. Malaika akamwambia “Kornelio!
4 Kornelio akamkazia macho kwa hofu akasema, “Kuna nini, Bwana?” Malaika akamwambia, “Sala zako na sadaka zako kwa maskini zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.
Kornelio akamwangalia malaika na alikuwa na hofu kubwa sana akasema “Hii ni nini mkuu?” Malaika akamwambia “Maombi yako na zawadi zako kwa masikini zimepanda juu kama kumbukumbu kwenye uwepo wa Mungu”.
5 Sasa tuma watu waende Yafa wakamwite mtu mmoja jina lake Simoni aitwaye Petro.
Sasa tuma watu kwenda mji wa Yafa kumleta mtu mmoja anayeitwa Simoni ambaye pia huitwa Petro.
6 Yeye anaishi na Simoni mtengenezaji ngozi ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.”
Anakaa na mtengenezaji wa Ngozi aitwaye Simoni ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.”
7 Yule malaika aliyekuwa akizungumza naye alipoondoka, Kornelio akawaita watumishi wake wawili pamoja na askari mmoja mcha Mungu aliyekuwa miongoni mwa wale waliomtumikia.
Baada ya Malaika aliyekuwa akisema naye kuondoka, Kornelio akawaita watumishi wa nyumbani kwake wawili, na askari aliyekuwa akimwabudu Mungu kati ya maaskari waliokuwa wanamtumikia.
8 Akawaambia mambo yote yaliyotukia, kisha akawatuma waende Yafa.
Kornelio aliwaambia yote yaliyotokea na akawatuma Yafa.
9 Siku ya pili yake, walipokuwa wameukaribia mji, wakati wa adhuhuri, Petro alipanda juu ya nyumba kuomba.
Siku iliyofuata muda wa saa sita wakiwa njiani na wamekaribia mjini, Petro akapanda juu darini kuomba.
10 Alipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walikuwa wakiandaa chakula, akalala usingizi mzito sana.
Na pia akawa na njaa na alihitaji kitu cha kula, lakini wakati watu wanapika chakula, akaonyeshwa maono,
11 Akaona mbingu zimefunguka na kitu kama nguo kubwa kikishushwa duniani kwa ncha zake nne.
akaona anga limefuguka na chombo kinashuka na kitu fulani kama nguo kubwa ikishuka chini kwenye ardhi katika kona zake zote nne.
12 Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao nchini, na ndege wa angani.
Ndani yake kulikuwa na aina zote za wanyama wenye miguu minne na watambaao juu ya ardhi, na ndege wa angani.
13 Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.”
Tena sauti ikasema kwake “Amka, Petro chinja na ule”.
14 Petro akajibu, “La hasha Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu chochote kilicho najisi.”
Lakini Petro akasema “Siyo hivyo, Bwana kwa sababu sijawahi kula kitu chochote najisi na kichafu.
15 Ile sauti ikasema naye mara ya pili, “Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.”
Lakini sauti ikaja kwake tena kwa mara ya pili “Alichokitakasa Mungu usikiite najisi wala kichafu”.
16 Jambo hili lilitokea mara tatu na ghafula ile nguo ikarudishwa mbinguni.
Hii ilitokea mara tatu, na kile chombo kikawa kimechukuliwa tena angani.
17 Wakati Petro akiwa bado anajiuliza kuhusu maana ya maono haya, wale watu waliokuwa wametumwa na Kornelio wakaipata nyumba ya Simoni mtengenezaji wa ngozi wakawa wamesimama mbele ya lango.
Na wakati Petro akiwa katika hali ya kuchanganyikiwa juu ya hayo maono yanamaanisha nini, Tazama, watu waliokuwa wametumwa na Kornelio wakasimama mbele ya lango, wakiuliza njia ya kwenda kwenye nyumba.
18 Wakabisha hodi na kuuliza kama Simoni aliyeitwa Petro alikuwa anaishi hapo.
Na wakaita na kuuliza kama Simoni ambaye pia aliitwa Petro kama alikuwa anakaa pale.
19 Wakati Petro akiwa anafikiria juu ya yale maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Simoni, wako watu watatu wanaokutafuta.
Wakati huo Petro alipokuwa akiwaza juu ya hayo maono, Roho akasema naye, “Tazama watu watatu wanakutafuta.
20 Inuka na ushuke, usisite kwenda nao kwa kuwa mimi nimewatuma.”
Amka na ushuke chini na uende nao. Usiogope kwenda nao, kwa sababu nimewatuma.”
21 Petro akashuka na kuwaambia wale watu waliokuwa wametumwa kutoka kwa Kornelio, “Mimi ndiye mnayenitafuta. Mmekuja kwa sababu gani?”
Petro akashuka chini kwao na kusema “Mimi ni yule mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja?”
22 Wale watu wakamjibu, “Tumetumwa na Kornelio yule jemadari. Yeye ni mtu mwema anayemcha Mungu, na anaheshimiwa na Wayahudi wote. Yeye ameagizwa na malaika mtakatifu akukaribishe nyumbani kwake, ili asikilize maneno utakayomwambia.”
Wakasema, “Akida mmoja jina lake Kornelio, mtu wa haki na hupenda kumwabudu Mungu, na watu humsema vyema katika taifa lote la kiyahudi, ameambiwa na malaika wa Mungu kukutuma ili kwenda kwenye nyumba yake, ili asikie ujumbe kutoka kwako.”
23 Basi Petro akawakaribisha wakafuatana naye ndani, akawapa pa kulala. Kesho yake akaondoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu kutoka Yafa wakafuatana naye.
Petro akawakaribisha kuingia ndani na kukaa pamoja naye. Asubuhi iliyofuata akaamka akaenda pamoja naye, na ndugu wachache kutoka Yafa wakaambatana naye.
24 Siku iliyofuata wakawasili Kaisaria. Kornelio alikuwa akiwangoja pamoja na jamaa yake na marafiki zake wa karibu.
Siku iliyofuata walikuja Kaisaria. Na Kornelio alikuwa akiwasubiri; na alikuwa amewaita pamoja ndugu zake na marafiki zake wa karibu.
25 Petro alipokuwa akiingia ndani, Kornelio alikuja kumlaki, akaanguka miguuni pake kwa heshima.
Wakati Petro akiingia ndani, Kornelio akamlaki na kuinama hadi chini kwenye miguu yake kwa kumheshimu.
26 Lakini Petro akamwinua akamwambia, “Simama, mimi ni mwanadamu tu.”
Lakini Petro akamwinua na kusema “Simama; mimi mwenyewe pia ni mwanadamu.”
27 Petro alipokuwa akizungumza naye akaingia ndani na kukuta watu wengi wamekusanyika.
Wakati Petro akiwa anaongea naye, alienda ndani akakuta watu wamekusanyika pamoja.
28 Akawaambia, “Mnajua kabisa kwamba ni kinyume cha sheria yetu Myahudi kuchangamana na mtu wa Mataifa au kumtembelea. Lakini Mungu amenionyesha kwamba nisimwite mtu yeyote kuwa najisi au asiye safi.
Akawaambia, “Ninyi wenyewe mnajua kuwa siyo sheria ya kiyahudi kushirikiana au kutembelewa na mtu ambaye si wa taifa hili. Lakini Mungu amenionesha mimi kuwa sipaswi kumwita mtu yeyote ni najisi au mchafu.
29 Ndiyo sababu ulipotuma niitwe nilikuja bila kupinga lolote. Basi sasa naomba unieleze kwa nini umeniita?”
Na ndiyo maana nimekuja bila kubisha, nilipotumwa kwa ajili ya hiyo. Kwa hiyo niwaulize kwa nini mlitumwa kwa ajili yangu.”
30 Kornelio akajibu, “Siku nne zilizopita, nilikuwa nyumbani nikisali saa kama hii, saa tisa alasiri. Ghafula mtu aliyevaa nguo zilizongʼaa akasimama mbele yangu,
Kornelio akasema, “Siku nne zilizopita, wakati kama huu nilikuwa naomba muda wa saa tisa mchana ndani ya nyumba yangu; Nikaona mbele yangu mtu amesimama akiwa na mavazi meupe,
31 akasema, ‘Kornelio, maombi yako yamesikiwa na sadaka zako kwa maskini zimekumbukwa mbele za Mungu.
Akaniambia “Kornelio maombi yako yamesikiwa na Mungu, na zawadi zako kwa masikini zimekuwa ukumbusho mbele za Mungu.
32 Basi tuma watu waende Yafa wakaulize mtu mmoja Simoni aitwaye Petro, yeye ni mgeni katika nyumba ya Simoni mtengenezaji ngozi, ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.’
Kwa hiyo tuma mtu Yafa na akamwite mtu mmoja anayeitwa Simoni aje kwako, ambaye pia huitwa Petro. ambaye anaishi kwa mtengenezaji wa Ngozi mmoja aitwaye Simoni ambaye nyumba yake iko pembeni mwa bahari.
33 Nilituma watu kwako mara moja, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tuko hapa mbele za Mungu kuyasikiliza yote ambayo Bwana amekuamuru kutuambia.”
Zingatia: Msatri huu, “Naya atakapokuja atasema nanyi,” haumo kwenye maandiko ya kale.
34 Ndipo Petro akafungua kinywa chake akasema, “Mungu hana upendeleo,
Ndipo Petro akafungua mdomo wake na kusema “Kweli, nimeamini kuwa Mungu hawezi kuwa na upendeleo.
35 Lakini katika kila taifa, kila mtu amchaye na kutenda yaliyo haki hukubaliwa naye.
Badala yake, kila taifa mtu yeyote anayemwabudu na kufanya matendo ya haki anakubalika kwake.
36 Ninyi mnajua ule ujumbe uliotumwa kwa Israeli, ukitangaza habari njema za amani kwa Yesu Kristo. Yeye ni Bwana wa wote.
Unajua ujumbe alioutoa kwa watu wa Israel, alipokuwa akitangaza habari njema ya amani kupitia Yesu Kristo ambaye ni Bwana wa wote-
37 Mnajua yale yaliyotukia katika Uyahudi wote kuanzia Galilaya baada ya mahubiri ya Yohana Mbatizaji:
ninyi wenyewe mnajua tukio lililotokea, ambalo limetokea Yudea yote na lilianzia Galilaya, baada ya ubatizo ambao Yohana alitangaza.
38 Jinsi Mungu alivyomtia Yesu wa Nazareti mafuta katika Roho Mtakatifu na jinsi alivyokwenda huku na huko akitenda mema na kuponya wote waliokuwa wameonewa na nguvu za ibilisi, kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye.
tukio lililokuwa linamhusu Yesu Kristo jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na kwa nguvu. Alienda akifanya mema na kuponya wote walioteswa na ibilsi, kwa kuwa Mungu alikuwa pamoja naye.
39 “Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyoyafanya katika Uyahudi na Yerusalemu. Wakamuua kwa kumtundika msalabani.
Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyoyafanya katika nchi za Uyahudi na katika Yerusalemu- huyu ni Yesu waliyemuua na kumtundika mtini.
40 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu siku ya tatu na akamwezesha kuonekana na watu.
Huyu mtu Mungu alimfufua siku ya tatu na kumpa kujulikana,
41 Hakuonekana kwa watu wote, lakini kwetu sisi tuliochaguliwa na Mungu kuwa mashahidi, ambao tulikula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu.
si kwa watu wote, lakini kwa mashahidi waliochaguliwa kabla na Mungu. - sisi wenyewe, tulio kula naye na kunywa naye baada ya kufufuka kutoka kwa wafu.
42 Naye alituamuru kuhubiri kwa watu wote na kushuhudia kwamba ndiye alitiwa mafuta na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu.
Ametuagiza kuhubiri kwa watu na kushuhudia kuwa huyu ndiye ambaye Mungu alimchagua kuwa mwamuzi wa walio hai na waliokufa.
43 Manabii wote walishuhudia juu yake kwamba kila mtu amwaminiye hupokea msamaha wa dhambi katika Jina lake.”
Katika yeye manabii wote washuhudie, ili kwamba kila anayeamini katika yeye atapokea msamaha wa dhambi kupitia jina lake.”
44 Wakati Petro alikuwa akisema maneno haya, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wakisikiliza ule ujumbe.
Wakati Petro akiendelea kusema haya, Roho Mtakatifu akawajaza wote waliokuwa wakisikiliza ujumbe wake.
45 Wale wa tohara walioamini waliokuja na Petro walishangaa kwa kuona kuwa kipawa cha Roho Mtakatifu kimemwagwa juu ya watu wa Mataifa.
Watu wale wanaohusika na kikundi cha waamini waliotahiriwa- wale wote waliokuja na Petro- walishangazwa, kwa sababu ya karama ya Roho Mtakatifu aliyemwagwa pia kwa wamataifa.
46 Kwa kuwa waliwasikia wakinena kwa lugha mpya na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akasema,
Kwa kuwa walisikia hawa wamataifa wanaongea kwa lugha zingine na kumwabudu Mungu. Petro akajibu,
47 “Je, kuna mtu yeyote anayeweza kuzuia watu hawa wasibatizwe kwa maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea.”
“Kuna mtu yeyote anaweza kuzuia maji ili watu wasibatizwe, Watu hawa wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi?”
48 Kwa hiyo akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Wakamsihi Petro akae nao kwa siku chache.
Ndipo akawaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Baadaye wakamwomba akae nao kwa siku kadhaa.

< Matendo 10 >