< 2 Timotheo 4 >
1 Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja kwake na ufalme wake, kwamba:
2 Hubiri Neno; kuwa tayari wakati ufaao na wakati usiofaa; karipia, kemea na utie moyo kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri.
3 Maana wakati utakuja watu watakapokataa kuyakubali mafundisho yenye uzima. Badala yake, ili kutimiza tamaa zao wenyewe, watajikusanyia idadi kubwa ya walimu wapate kuwaambia yale ambayo masikio yao yanayowasha yanatamani kuyasikia.
4 Watakataa kusikiliza kweli na kuzigeukia hadithi za uongo.
5 Kwa habari yako wewe, vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiza wajibu wote wa huduma yako.
6 Kwa maana mimi sasa ni tayari kumiminwa kama sadaka ya kinywaji, nayo saa yangu ya kuondoka imetimia.
7 Nimevipiga vita vizuri, mashindano nimeyamaliza, imani nimeilinda.
8 Sasa nimewekewa taji ya haki ambayo Bwana, mwamuzi wa haki, atanitunukia siku ile: wala si mimi tu, bali pia wote ambao wamengoja kwa shauku kudhihirishwa kwake.
9 Jitahidi kuja kwangu upesi
10 kwa sababu Dema, kwa kuupenda ulimwengu, ameniacha na amekwenda Thesalonike. Kreske amekwenda Galatia na Tito amekwenda Dalmatia. (aiōn )
11 Ni Luka peke yake aliye hapa pamoja nami. Mtafute Marko uje naye kwa sababu ananifaa sana katika huduma yangu.
12 Nimemtuma Tikiko huko Efeso.
13 Utakapokuja, niletee lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa na vile vitabu vyangu, hasa vile vya ngozi.
14 Aleksanda yule mfua chuma alinitendea ubaya mkubwa. Bwana atamlipa kwa ajili ya yale aliyotenda.
15 Wewe pia ujihadhari naye kwa sababu aliyapinga sana maneno yetu.
16 Katika utetezi wangu wa mara ya kwanza, hakuna hata mmoja aliyeniunga mkono, bali kila mmoja aliniacha. Namwomba Mungu wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo.
17 Lakini Bwana alisimama upande wangu akanitia nguvu, ili kupitia kwangu lile Neno lihubiriwe kwa ukamilifu, watu wote Mataifa wapate kulisikia. Mimi niliokolewa kutoka kinywa cha simba.
18 Bwana ataniokoa katika kila shambulio baya na kunileta salama katika Ufalme wake wa mbinguni. Atukuzwe yeye milele na milele. Amen. (aiōn )
19 Wasalimu Prisila na Akila, na wote wa nyumbani kwa Onesiforo.
20 Erasto alibaki Korintho. Nami nikamwacha Trofimo huko Mileto akiwa mgonjwa.
21 Jitahidi ufike huku kabla ya majira ya baridi. Eubulo anakusalimu, vivyo hivyo Pude, Lino, Klaudia na ndugu wote.
22 Bwana awe pamoja na roho yako. Neema iwe pamoja nanyi. Amen.