< 2 Timotheo 4 >

1 Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja kwake na ufalme wake, kwamba:
Ninakupa agizo hili lenye uzito mbele za Mungu na Kristo Yesu, atakaye wahukumu walio hai na wafu, na kwa sababu ya kufunuliwa kwake na Ufalme wake:
2 Hubiri Neno; kuwa tayari wakati ufaao na wakati usiofaa; karipia, kemea na utie moyo kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri.
Hubiri Neno. Uwe tayari kwa wakati ufaao na usiofaa. Waambie watu dhambi zao, kemea, himiza, kwa uvumilivu wote na mafundisho.
3 Maana wakati utakuja watu watakapokataa kuyakubali mafundisho yenye uzima. Badala yake, ili kutimiza tamaa zao wenyewe, watajikusanyia idadi kubwa ya walimu wapate kuwaambia yale ambayo masikio yao yanayowasha yanatamani kuyasikia.
Kwa maana wakati utakuja ambao watu hawatachukuliana na mafundisho ya kweli. Badala yake, watajitafutia walimu wa kufundisha kulingana na tamaa zao. kwa njia hii masikio yao yatakuwa yametekenywa.
4 Watakataa kusikiliza kweli na kuzigeukia hadithi za uongo.
Wataacha kusikiliza mafundisho ya kweli, na kugeukia hadithi.
5 Kwa habari yako wewe, vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiza wajibu wote wa huduma yako.
Lakini wewe uwe mwaminifu katika mambo yote, vumilia magumu, fanya kazi ya mwinjilisti; timiza huduma yako.
6 Kwa maana mimi sasa ni tayari kumiminwa kama sadaka ya kinywaji, nayo saa yangu ya kuondoka imetimia.
Kwa maana mimi tayari nimekwisha kumiminwa. Muda wa kuondoka kwangu umewadia.
7 Nimevipiga vita vizuri, mashindano nimeyamaliza, imani nimeilinda.
Nimeshindana katika haki, Mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda.
8 Sasa nimewekewa taji ya haki ambayo Bwana, mwamuzi wa haki, atanitunukia siku ile: wala si mimi tu, bali pia wote ambao wamengoja kwa shauku kudhihirishwa kwake.
Taji ya haki imewekwa kwa ajili yangu, ambayo Bwana, anayehukumu kwa haki, atanipa siku ile. Na siyo kwangu tu bali pia kwa wote wanaongojea kwa shauku kuonekana kwake.
9 Jitahidi kuja kwangu upesi
Jitahidi kuja kwagu haraka.
10 kwa sababu Dema, kwa kuupenda ulimwengu, ameniacha na amekwenda Thesalonike. Kreske amekwenda Galatia na Tito amekwenda Dalmatia. (aiōn g165)
Kwa kuwa Dema ameniacha. Anaupenda ulimwengu wa sasa na amekwenda Thesalonike, Kreseni alikwenda Galatia, na Tito alikwenda Dalmatia. (aiōn g165)
11 Ni Luka peke yake aliye hapa pamoja nami. Mtafute Marko uje naye kwa sababu ananifaa sana katika huduma yangu.
Luka tu ndiye yuko pamoja nami. Umchukue Marko uje naye kwani yeye ni muhimu kwangu katika huduma.
12 Nimemtuma Tikiko huko Efeso.
Nimemtuma Tikiko Efeso.
13 Utakapokuja, niletee lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa na vile vitabu vyangu, hasa vile vya ngozi.
Lile joho ambalo nililiacha Troa kwa Karpo, utakapokuja lilete, pamoja na vile vitabu hasa vile vya ngozi.
14 Aleksanda yule mfua chuma alinitendea ubaya mkubwa. Bwana atamlipa kwa ajili ya yale aliyotenda.
Alekizanda mfua chuma alinitendea maovu mengi. Bwana atamlipa kulingana na matendo yake.
15 Wewe pia ujihadhari naye kwa sababu aliyapinga sana maneno yetu.
Nawe pia jihadhari naye, kwani aliyapinga sana maneno yetu.
16 Katika utetezi wangu wa mara ya kwanza, hakuna hata mmoja aliyeniunga mkono, bali kila mmoja aliniacha. Namwomba Mungu wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo.
Katika utetezi wangu wa kwanza, hakuna mtu yeyote aliyesimama pamoja nami, badala yake, kila mmoja aliniacha. Mungu asiwahesabie hatia.
17 Lakini Bwana alisimama upande wangu akanitia nguvu, ili kupitia kwangu lile Neno lihubiriwe kwa ukamilifu, watu wote Mataifa wapate kulisikia. Mimi niliokolewa kutoka kinywa cha simba.
Lakini Bwana alisimama pamoja nami, akanitia nguvu ili kwamba kupitia kwangu, neno linenwe kwa ukamilifu na mataifa wapate kusikia. Niliokolewa katika kinywa cha Simba.
18 Bwana ataniokoa katika kila shambulio baya na kunileta salama katika Ufalme wake wa mbinguni. Atukuzwe yeye milele na milele. Amen. (aiōn g165)
Bwana ataniepusha na matendo yote maovu na kuniokoa kwa ajili ya ufalme wake wa mbinguni. Utukufu uwe kwake milele na milele. Amen (aiōn g165)
19 Wasalimu Prisila na Akila, na wote wa nyumbani kwa Onesiforo.
Msalimie Priska, Akila na nyumba ya Onesiforo.
20 Erasto alibaki Korintho. Nami nikamwacha Trofimo huko Mileto akiwa mgonjwa.
Erasto alibaki huko Korintho, lakini Trifimo nilimuacha Mileto akiwa mgonjwa.
21 Jitahidi ufike huku kabla ya majira ya baridi. Eubulo anakusalimu, vivyo hivyo Pude, Lino, Klaudia na ndugu wote.
Fanya hima uje kabla ya kipindi cha baridi. Eubulo anakusalimu, pia Pude, Lino, Claudia na ndugu wote.
22 Bwana awe pamoja na roho yako. Neema iwe pamoja nanyi. Amen.
Mungu awe pamoja na roho yako, Neema iwe nawe.

< 2 Timotheo 4 >