< 2 Wathesalonike 3 >

1 Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili Neno la Bwana lipate kuenea kwa haraka na kuheshimiwa kila mahali, kama vile ilivyokuwa kwenu.
Na sasa, ndugu, tuombeeni, kwamba neno la Bwana liweze kuenea na kutukuzwa, kama ilivyo pia kwenu.
2 Ombeni pia ili tupate kuokolewa kutokana na watu waovu na wabaya, kwa maana si wote wanaoamini.
Ombeni kwamba tuweze kuokolewa kutoka katika uovu na watu waasi, kwa kuwa si wote wana imani.
3 Lakini Bwana ni mwaminifu, naye atawaimarisha ninyi na kuwalinda kutokana na yule mwovu.
Lakini Bwana ni mwaminifu, ambaye atawaimarisha ninyi na kuwalinda kutoka kwa yule mwovu.
4 Nasi tuna tumaini katika Bwana ya kuwa mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaagiza.
Tunaujasiri katika Bwana kwa ajili yenu, kwamba mnatenda na mtaendelea kutenda mambo ambayo tunawaagiza.
5 Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika saburi ya Kristo.
Bwana aweze kuongoza mioyo yenu katika upendo na katika uvumilivu wa Kristo.
6 Ndugu, tunawaagiza katika Jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni na kila ndugu ambaye ni mvivu na ambaye haishi kufuatana na maagizo tuliyowapa.
Sasa tunawaagiza, ndugu, katika jina la Bwana Yesu Kristo, kwamba mwepuke kila ndugu ambaye anaishi maisha ya uvivu na siyo kwa kutokana na desturi ambazo mlipokea kutoka kwetu.
7 Maana ninyi wenyewe mnajua jinsi iwapasavyo kufuata mfano wetu. Sisi hatukuwa wavivu tulipokuwa pamoja nanyi,
Kwa kuwa ninyi wenyewe mnajua ni sawa kwenu kutuiga sisi. Hatukuishi miongoni mwenu kama wale ambao hawakuwa na nidhamu.
8 wala hatukula chakula cha mtu yeyote pasipo kukilipia. Badala yake tulifanya kazi kwa bidii usiku na mchana, ili tusimlemee mtu yeyote miongoni mwenu.
Na hatukula chakula cha mtu yeyote bila kukilipia. Badala yake, tulifanya kazi usiku na mchana kwa kazi ngumu na kwa shida, ili tusiweze kuwa mzigo kwa yeyote katika ninyi.
9 Tulifanya hivi, si kwa sababu hatukuwa na haki ya kupata msaada kama huo, bali ndio sisi wenyewe tuwe kielelezo.
Tulifanya hivi si kwa sababu hatuna mamlaka. Badala yake, tulifanya hivi ili tuwe mfano kwenu, ili kwamba mweze kutuiga sisi.
10 Kwa maana hata tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwapa amri kwamba: “Mtu yeyote asiyetaka kufanya kazi, hata kula asile.”
Wakati tulipokuwa pamoja nanyi tuliwaagiza, “Ikiwa mmoja wenu hataki kufanya kazi, na asile.”
11 Kwa kuwa tunasikia kwamba baadhi ya watu miongoni mwenu ni wavivu. Hawafanyi kazi bali hujishughulisha na mambo ya wengine.
Kwa kuwa tunasikia kwamba baadhi wanaenenda kwa uvivu miongoni mwenu. Hawafanyi kazi lakini badala yake ni watu wasio na utaratibu.
12 Basi watu kama hao tunawaagiza na kuwahimiza katika Bwana Yesu Kristo, kwamba wafanye kazi kwa utulivu kwa ajili ya chakula chao wenyewe.
Sasa hao nao tunaagiza na kuwaasa katika Bwana Yesu Kristo, kwamba lazima wafanye kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe.
13 Kwa upande wenu, ndugu, ninyi kamwe msichoke katika kutenda mema.
Lakini ninyi, ndugu, msizimie roho katika kufanya yaliyo sahihi.
14 Ikiwa mtu yeyote hayatii maagizo yetu yaliyoko katika barua hii, mwangalieni sana mtu huyo. Msishirikiane naye, ili apate kuona aibu.
Ikiwa mtu yeyote hataki kutii neno letu katika waraka huu, mwe makini naye na msiwe na ushirika pamoja naye, ili kwamba aweze kuaibika.
15 Lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu.
Msimchukulie kama adui, lakini mwonyeni kama ndugu.
16 Basi, Bwana wa amani mwenyewe awapeni amani nyakati zote na kwa kila njia. Bwana awe nanyi nyote.
Bwana wa amani mwenyewe awape amani wakati wowote katika njia zote. Bwana awe nanyi nyote.
17 Mimi, Paulo, ninaandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Hii ndio alama ya utambulisho katika barua zangu zote. Hivi ndivyo niandikavyo.
Hii ni salam yangu, Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe, ambayo ni alama katika kila waraka. Hivi ndivyo niandikavyo.
18 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote. Amen.
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iweze kuwa nanyi nyote.

< 2 Wathesalonike 3 >