< 2 Samweli 9 >

1 Daudi akauliza, “Je, hakuna mtu hata mmoja wa nyumba ya Sauli aliyebaki ambaye naweza kumtendea wema kwa ajili ya Yonathani?”
Daudi akasema, “Je kuna yeyote aliyesalia wa familia ya Sauli ambaye naweza kumwonyesha kwa fadhiri kwa ajili ya Yonathani?
2 Basi palikuwepo mtumishi wa nyumba ya Sauli aliyeitwa Siba. Wakamwita aje mbele ya Daudi, naye mfalme akamwambia, “Wewe ndiwe Siba?” Akamjibu, “Naam, mimi ndiye mtumishi wako.”
Alikuwepo mtumishi katika familia ya Sauli jina lake Siba, akaitwa kwa Daudi. Mfalme akamuuliza, “Je wewe ndiye Siba?” Akajibu, “Mimi ni mtumishi wako, ndiye.”
3 Mfalme akauliza, “Je, hakuna yeyote ambaye amebaki wa nyumba ya Sauli ninayeweza kumwonyesha wema wa Mungu?” Siba akamjibu mfalme, “Bado yupo mwana wa Yonathani, yeye ni kiwete miguu yote.”
Hivyo mfalme akasema, “Je hakuna aliyesalia wa familia ya Sauli ambaye naweza kumuonesha wema wa Mungu?” Siba akamjibu mfalme, “Yonathani ana mwana, ambaye ni mlemavu wa miguu.
4 Mfalme akauliza, “Yuko wapi?” Siba akajibu, “Yuko nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli huko Lo-Debari.”
Mfalme akamwambia, “Yupo wapi?” Siba akamjibu mfalme, “Tazama, yupo katika nyumba ya Makiri mwana wa Amieli huko Lo Debari.
5 Basi Mfalme Daudi akamtaka aletwe kutoka Lo-Debari, kutoka nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli.
Ndipo mfalme Daudi akatuma watu na kumtoa katika nyumba ya Makiri mwana wa Amieli huko Lo Debari.
6 Mefiboshethi mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, alipofika kwa Daudi, akainama kumpa mfalme heshima. Daudi akamwita, “Mefiboshethi!” Mefiboshethi akajibu, “Ndimi mtumishi wako.”
Hivyo Mefiboshethi mwana wa Yonathani mwana wa Sauli, akaja kwa Daudi naye akainama uso wake hadi katika sakafu kwa kumheshimu Daudi. Daudi akasema, “Mefiboshethi.” Naye akajibu, “Angalia, mimi ni mtumishi wako!
7 Daudi akamwambia, “Usiogope, kwa maana hakika nitakutendea wema kwa ajili ya baba yako Yonathani. Nitakurudishia ardhi yote iliyokuwa mali ya Sauli baba yako, nawe daima utakula chakula mezani pangu.”
Daudi akamwambia, “Usiogope, maana hakika nitakufadhiri kwa ajili ya Yonathani baba yako, nami nitakurudishia ardhi yote ya Sauli babu yako, nawe utakula katika meza yangu daima.”
8 Mefiboshethi akasujudu akasema, “Mimi mtumishi wako ni nini hata uangalie mbwa mfu kama mimi?”
Mefiboshethi akainama na kusema, “Mtumishi wako ni nani, hata ukamwangalia kwa fadhiri mbwa mfu kama nilivyo?”
9 Ndipo mfalme akamwita Siba mtumishi wa Sauli na kumwambia, “Nimempa mwana wa bwana wako kila kitu kilichokuwa mali ya Sauli na jamaa yake.
Kisha mfalme akamwita Siba, mtumishi wa Sauli, na kumwambia, “Yote yaliyo ya Sauli na familia yake nimempa mjukuu wa bwana wako.
10 Wewe, wanao na watumishi wako mtamlimia mashamba Mefiboshethi na kumletea mavuno, ili kwamba mwana wa bwana wako apate mahitaji yake. Naye Mefiboshethi mwana wa bwana wako atakula chakula mezani pangu daima.” (Siba alikuwa na wana kumi na watano, na watumishi ishirini.)
Wewe, wanao, na watumishi wako mtalima mashamba kwa ajili yake nanyi mtavuna mazao ili kwamba mjukuu wa bwana wako apate chakula. Kwa maana Mefiboshethi, mjukuu wa bwana wako, atakula katika meza yangu daima.” Basi Siba alikuwa na wana kumi na watano na watumishi ishirini.
11 Ndipo Siba akamwambia mfalme, “Mtumishi wako atafanya chochote bwana wangu mfalme atakachoagiza mtumishi wake kufanya.” Basi Mefiboshethi akala chakula mezani pa Daudi kama mmoja wa wana wa mfalme.
Kisha Siba akamwambia mfalme, “Mtumishi wako atafanya yote ambayo bwana wangu mfalme amemwamuru mtumishi wake.” Mfalme akaongeza kusema, kwa Mefiboshethi yeye atakula katika meza yangu, kama mmojawapo ya wana wa mfalme.”
12 Mefiboshethi alikuwa na mwanawe mdogo aliyeitwa Mika, nao watu wote wa nyumba ya Siba walikuwa watumishi wa Mefiboshethi.
Mefiboshethi alikuwa na mwana mdogo jina lake Mika. Na wote waliokuwa wanaishi katika nyumba ya Siba walikuwa watumishi wa Mefiboshethi.
13 Naye Mefiboshethi akaishi huko Yerusalemu, kwa sababu daima alikula mezani pa mfalme, naye alikuwa kiwete miguu yote.
Hivyo Mefiboshethi akaishi Yerusalemu, naye akala chakula cha daima katika meza ya mfalme, japokuwa alikuwa mlemavu wa miguu yote.

< 2 Samweli 9 >