< 2 Samweli 7 >
1 Baada ya mfalme kuingia rasmi katika jumba lake la kifalme, naye Bwana akiwa amemstarehesha pande zote mbali na adui zake,
Ikawa mfalme alipokuwa amekwisha kukaa katika nyumba yake, na baada ya Yahwe kuwa amemstarehesha kutokana na adui zake wate waliomzunguka,
2 akamwambia nabii Nathani, “Mimi hapa, ninaishi katika jumba la kifalme la mierezi, wakati Sanduku la Mungu limebaki katika hema.”
mfalme akamwambia nabii Nathani, “Tazama, mimi ninaishi katika nyumba ya mierezi, lakini sanduku la Mungu lipo hemani.
3 Nathani akamjibu mfalme, “Lolote ulilo nalo moyoni, endelea ukalifanye, kwa maana Bwana yu pamoja nawe.”
Basi Nathani akamwambia mfalme, “Nenda, fanya lililo moyoni mwako, kwa maana Yahwe yupo nawe.”
4 Usiku ule neno la Bwana likamjia Nathani, kusema:
Lakini usiku usiku uleule neno la Yahwe lilimjia Nathani kusema,
5 “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Je, ewe ndiwe wa kunijengea mimi nyumba ili nikae ndani yake?
“Nenda na umwambie mtumishi wangu Daudi, 'Hivi ndivyo asemavyo Yahwe: Je utanijengea nyumba ya kuishi?”
6 Sijakaa ndani ya nyumba tangu siku niliyowaleta Waisraeli kutoka Misri hadi leo. Nimekuwa nikitembea kutoka mahali pamoja hadi mahali pengine ndani ya hema kama makao yangu.
Kwa maana sijawai kuishi katika nyumba tangu siku ile nilipowaleta wana wa Israeli kutoka Misri hata leo; badala yake nimekuwa nikitembea katika hema, hema la kukutania.
7 Popote nilipotembea pamoja na Waisraeli wote, je, nimewahi kumwambia kiongozi wao yeyote niliyemwamuru kuwachunga watu wangu Israeli, “Kwa nini hujanijengea nyumba ya mierezi?”’
Mahali pote ambapo nimekuwa nikihama miongoni mwa wana wote wa Israeli, Je niliwai kusema lolote na viongozi wa Israeli niliowaweka kuwachunga watu wangu Israeli, kusema, “Kwa nini hamjanijengea nyumba ya mierezi?”
8 “Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: Nilikutoa wewe kutoka machungani na kutoka kuandama kundi la kondoo na mbuzi ili kuwaongoza watu wangu Israeli.
Sasa basi, mwambie Daudi, mtumishi wangu, “Hiki ndicho asemacho Yahwe wa majeshi: 'Nilikutwaa kutoka machungani, kutoka katika kuwafuata kondoo, ili uwe mtawala juu ya watu wangu Israeli.
9 Nimekuwa pamoja nawe popote ulipokwenda, nami nimekuondolea mbali adui zako wote mbele yako. Basi nitalifanya jina lako kuwa kuu kama majina ya watu walio wakuu sana duniani.
Nimekuwa pamoja nawe popote ulipokwenda na nimewakatilia mbali adui zako wote mbele yako. Na nitakutengenezea jina kubwa, kama jina la mojawapo ya wakuu walio juu ya nchi.
10 Nami nitawapatia watu wangu Israeli mahali niwapande humo ili kwamba wawe na nyumbani kwao wenyewe wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawaonea tena, kama walivyofanya mwanzoni,
Nitatenga mahali kwa ajili ya watu wangu Israeli nami nitawapanda pale, ili kwamba waweze kuishi mahali pao wenyewe na wasisumbuliwe tena. Waovu hawatawatesa tena, kama walivyofanya mwanzo.
11 na kama walivyofanya tangu mwanzo wakati nilipowaweka viongozi juu ya watu wangu Israeli. Pia nitawapa raha mbele ya adui zenu wote. “‘Bwana akuambia kwamba Bwana mwenyewe atakujengea nyumba.
Kama walivyofanya tangu siku ile nilipoamuru waamuzi juu ya watu wangu Israeli. Nami nitakustarehesha kutokana na adui zako wote. Zaidi ya hayo, Mimi, Yahwe, nakutamkia kwamba nitakutengenezea nyumba.
12 Siku zako zitakapokwisha nawe ulale pamoja na baba zako, nitainua mzao wako aingie mahali pako, ambaye atatoka viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake.
Siku zako zitakapokwisha na ukalala pamoja na baba zako, nitainua mzao baada yako, atokaye katika mwili wako mwenyewe, nitauimalisha ufalme wake.
13 Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu, nami nitaimarisha kiti cha enzi cha ufalme wake milele.
Naye atajenga nyumba kwa jina langu, nami nitakiimalisha kiti chake cha enzi daima.
14 Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Atakapokosea nitamwadhibu kwa fimbo ya wanadamu, kwa adhabu ya kupigwa na wanadamu.
Nitakuwa baba kwake, naye atakuwa mwanangu. Atakapotenda dhambi, nitamwadhibu kwa fimbo ya wanadamu na kwa mapigo ya wana wa watu.
15 Lakini upendo wangu kamwe hautaondolewa kwake, kama nilivyouondoa kwa Sauli, niliyemwondoa atoke mbele yako.
Lakini uaminifu wa agano langu hautamwondokea, kama nilivyouondoa kutoka kwa Sauli, niliyemwondoa mbele yako.
16 Nyumba yako na ufalme wako utadumu milele mbele zangu, kiti chako cha enzi kitafanywa imara milele.’”
Nyumba yako na ufalme wako utathibitiswa mbele yako daima. Kiti chako cha enzi kitakuwa imara daima.”
17 Nathani akamwarifu Daudi maneno yote ya maono haya.
Nathani akamwambia Daudi na kumtaarifu maneno haya yote, na akamwambia kuhusu ono lote.
18 Ndipo Mfalme Daudi akaingia ndani, akaketi mbele za Bwana, akasema: “Ee Bwana Mwenyezi, mimi ni nani, na jamaa yangu ni nini, hata umenileta mpaka hapa nilipo?
Kisha mfalme Daudi akaingia ndani na kuketi mbele ya Yahwe; akasema, “Mimi ni nani, Yahwe Mungu, na familia yangu ni nini hata umenileta hapa nilipo?
19 Naam, kana kwamba hili halitoshi machoni pako, Ee Bwana Mwenyezi, wewe umenena pia kuhusu siku zijazo za nyumba ya mtumishi wako. Je, hii ndiyo njia yako ya kawaida ya kushughulika na mwanadamu, Ee Bwana Mwenyezi?
Na hili lilikuwa jambo dogo mbele yako, Bwana Yahwe. Hata ukasema kuhusu familia ya mtumishi wako wakati mkuu ujao, nawe umenionesha vizazi vijavyo, Bwana Yahwe!
20 “Je, Daudi aweza kukuambia nini zaidi? Kwa maana unamjua mtumishi wako, Ee Bwana Mwenyezi.
Mimi Daudi, niseme nini zaidi kwako? Umemweshimu mtumishi wako, Bwana Yahwe.
21 Kwa ajili ya neno lako na kwa mapenzi yako, umefanya jambo hili kubwa na kulifanya lijulikane na lifahamike kwa mtumishi wako.
Kwa ajili ya neno lako, na kwa ajili ya kutimiza kusudi lako mwenyewe, umefanya jambo kubwa namna hii na kulidhihirisha kwa mtumishi wako.
22 “Tazama jinsi ulivyo mkuu, Ee Bwana Mwenyezi! Hakuna mwingine kama wewe, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe,
Kwa hiyo wewe ni mkuu, Bwana Yahwe. Kwa maana hakuna mwingine aliye kama wewe, na hakuna Mungu mwingine badala yako, kama jinsi ambayo tumesikia kwa masikio yetu wenyewe.
23 Naye ni nani aliye kama watu wako Israeli, taifa pekee duniani ambalo Mungu alitoka kwenda kulikomboa kwa ajili yake mwenyewe, na kujifanyia jina mwenyewe, kwa kufanya maajabu makubwa na ya kutisha kwa kuwafukuza mataifa na miungu yao mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri?
Kwani kuna taifa lipi lililo kama watu wako Israeli, taifa moja juu ya nchi ambalo wewe, Mungu, ulikwenda na kuwakomboa kwa ajili yako wewe mwenyewe? Ulifanya hivi ili kwamba wawe watu kwa ajili yako mwenyewe, kujifanyia jina kwa ajili yako mwenyewe, na kufanya matendo makuu na ya kuogofya kwa ajili ya nchi yako. Uliyaondoa mataifa na miungu yao kutoka mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri.
24 Umeimarisha watu wako Israeli hasa kama watu wako mwenyewe milele, nawe, Ee Bwana, umekuwa Mungu wao.
Umeiimarisha Israel kama watu wako daima, na wewe, Yahwe, kuwa Mungu wao.
25 “Basi sasa, Bwana, ukaitimize ahadi uliyosema kuhusu mtumishi wako na nyumba yake milele. Fanya kama ulivyoahidi,
Basi sasa, Yahwe Mungu, ahadi uliyofanya kuhusu mtumishi wako na familia yake iwe imara daima. Ufanye kame uilivyo sema.
26 ili kwamba jina lako litukuke milele. Ndipo watu watasema, ‘Bwana Mwenye Nguvu Zote ni Mungu juu ya Israeli!’ Nayo nyumba ya mtumishi wako Daudi itakuwa imara mbele zako.
Na jina lako liwe kuu daima, ili watu waseme, 'Yahwe wa majeshi ni Mungu wa Israeli,' wakati nyumba yangu, Daudi, mtumishi wako itakapokaa imara mbele zako daima.
27 “Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, umelifunua hili kwa mtumishi wako, ukisema, ‘Nitakujengea nyumba.’ Hivyo mtumishi wako amepata ujasiri kukuletea dua hii.
Kwa maana wewe, Yahwe wa majeshi, Mungu wa Israeli, umedhihirisha kwa mtumishi wako kwamba utamjengea nyumba. Ndiyo maana mimi, mtumishi wako, nimepata ujasiri kuomba kwako.
28 Ee Bwana Mwenyezi, wewe ndiwe Mungu! Maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidi mtumishi wako mambo haya mazuri.
Sasa, Bwana Yahwe, wewe ni Mungu, na maneno yako ni amini, na umefanya ahadi hii njema kwa mtumishi wako.
29 Sasa naomba uwe radhi kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili idumu mbele zako milele, kwa maana wewe, Ee Bwana Mwenyezi, umesema, na kwa baraka zako nyumba ya mtumishi wako itaendelea kubarikiwa milele.”
Sasa basi, na ikupendeze kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili iendelee mbele yako daima. Kwa maana wewe, Bwana Yahwe, umeyasema mambo haya, na kwa ahadi yako nyumba ya mtumishi wako itabarikiwa daima.