< 2 Samweli 5 >

1 Makabila yote ya Israeli yakamjia Daudi huko Hebroni na kumwambia, “Sisi tu nyama yako na damu yako hasa.
Kisha kabila zote za Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni nao wakasema, “Tazama, sisi ni nyama na mifupa yako.
2 Zamani, wakati Sauli alikuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyeiongoza Israeli vitani. Naye Bwana alikuambia, ‘Wewe utawachunga watu wangu Israeli, na utakuwa mtawala wao.’”
Kipindi kilichopita, Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, ni wewe uliyeliongoza jeshi la Waisraeli. Yahwe akakwambia, 'Utawachunga watu wangu Israeli, na utakuwa mtawala juu ya Israeli.”
3 Wazee wote wa Israeli wakamwendea Mfalme Daudi huko Hebroni, mfalme akafanya mapatano nao huko Hebroni mbele za Bwana, nao wakamtia Daudi mafuta kuwa mfalme wa Israeli.
Hivyo wazee wote wa Israeli wakaja kwa mfalme huko Hebron na mfalme Daudi akafanya nao agano mbele ya Yahweh. Wakamtawaza Daudi kuwa mfalme wa Israeli.
4 Daudi alikuwa na miaka thelathini alipoanza kutawala, naye akatawala Israeli miaka arobaini.
Daudi alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kutawala, naye akatawala miaka arobaini.
5 Huko Hebroni alitawala Yuda kwa miaka saba na miezi sita, na katika Yerusalemu alitawala Israeli yote na Yuda kwa miaka thelathini na mitatu.
Alitawala juu ya Yuda miaka saba na miezi sit a huko Hebroni, na huko Yerusalemu akatawala miaka thelathini na mitatu juu ya Israeli yote na Yuda.
6 Mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu kuwashambulia Wayebusi walioishi humo. Wayebusi wakamwambia Daudi, “Wewe hutaingia humu, kwani hata vipofu na viwete wanaweza kukufukuza.” Walidhani, “Daudi hawezi kuingia humu.”
Mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu kupigana na wayebusi, waliokuwa wenyeji wa nchi. Wakamwambia Daudi, “Hautaweza kuja hapa kwani hata wipofu na vilema waweza kukudhuia kuingia. Daudi haweze kuja hapa.”
7 Hata hivyo, Daudi akaiteka ngome ya Sayuni, Mji wa Daudi.
Lakini, Daudi akaiteka ngome ya Sayuni, ambayo sasa ni mji wa Daudi.
8 Siku ile, Daudi akasema, “Yeyote ambaye atawashinda Wayebusi, atatumia huo mfereji kuwafikia hao ‘viwete na vipofu’ ambao ni adui za Daudi.” Ndiyo sababu wanasema, “‘Vipofu na viwete’ hawataingia kwenye jumba la ufalme.”
Wakati huo Daudi akasema, “Waliowashambulia wayebusi watapaswa kupita katika mfereji wa maji ili wawafikie virema na vipofu ambao ni adui wa Daudi.” Hii ndiyo maana watu husema, “Vipofu na virema wasingie katika kasri.”
9 Ndipo Daudi akafanya makao ndani ya ngome na kuiita Mji wa Daudi. Akajenga eneo linalozunguka kuanzia Milo kuelekea ndani.
Hivyo Daudi akaishi ngemeni naye akaiita mji wa Daudi. Akaizungushia ukuta, kuanzia barazani kuelekea ndani.
10 Daudi akazidi kuwa na nguvu zaidi na zaidi, kwa sababu Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote alikuwa pamoja naye.
Daudi akawa na nguvu sana kwa maana Yahwe, Mungu wa utukufu, alikuwa pamoja naye.
11 Basi Hiramu mfalme wa Tiro akawatuma wajumbe kwa Daudi, wakiwa na magogo ya mierezi, maseremala na waashi, nao wakajenga jumba la kifalme kwa ajili ya Daudi.
Kisha Hiramu mfalme wa Tiro akatuma wajumbe kwa Daudi, na miti ya mierezi, mafundi seremala na wajenzi. Wakamjengea Daudi nyumba.
12 Naye Daudi akafahamu kuwa Bwana amemwimarisha kuwa mfalme juu ya Israeli na ameinua ufalme wake kwa ajili ya Israeli, watu wake.
Daudi akatambua kuwa Yahwe alikuwa amemweka ili awe mfalme juu ya Israeli, na kwamba alikuwa ameutukuza ufalme wake kwa ajili ya Israeli watu wake.
13 Baada ya Daudi kuondoka Hebroni, akajitwalia masuria zaidi na wake huko Yerusalemu, nao wana na binti wengi walizaliwa kwake.
Baada ya Daudi kuondoka Hebroni na kwenda Yerusalemu, akajitwalia wake na masuria wengi huko Yerusalemu, na wana na binti wengi walizaliwa kwake.
14 Haya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko: Shamua, Shobabu, Nathani, Solomoni,
Haya ndiyo majina ya wanawe waliozaliwa kwake huko Yerusalemu: Shamua, Shobabu, Nathani, Selemani,
15 Ibihari, Elishua, Nefegi, Yafia,
Ibhari, Elishua, Nefegi, Yafia,
16 Elishama, Eliada na Elifeleti.
Elishama, Eliada na Elifeleti.
17 Wafilisti waliposikia kuwa Daudi ametiwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli, wakapanda na jeshi lao lote kwenda kumsaka, lakini Daudi akapata habari hizo, naye akateremka kwenye ngome.
Basi wafilisti waliposikia kwamba Daudi ametiwa mafuta kuwa mfalme juu ya Israeli, wakaenda wote kumtafuta. Daudi aliposikia hilo akashuka ngomeni.
18 Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kusambaa kwenye Bonde la Warefai,
Basi Wafilisiti walikuwa wamekuja na kuenea katika bonde la Mrefai.
19 kwa hiyo Daudi akamuuliza Bwana, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?” Bwana akamjibu, “Nenda, kwa maana hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.”
Kisha Daudi akaomba msaada kutoka kwa Yahwe. Akasema, “Je niwashambulie wafilisti? Je utanipa ushindi juu yao?” Yahwe akamwambia Daudi, “Washambulia, kwa hakika nitakupa ushindi juu ya wafilisti.”
20 Ndipo Daudi akaenda mpaka Baal-Perasimu, na huko akawashinda Wafilisti. Akasema, “Kama mafuriko yafurikavyo, Bwana amewafurikia adui zangu mbele yangu.” Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Baal-Perasimu.
Hivyo Daudi akawashambulia huko Baali Perasimu, naye akawashinda. Akasema, Yahwe amewafurikia adui zangu mbele yangu kama mafuriko ya maji. Kwa hiyo jina la mahali pale likawa Baali Perasimu.
21 Wafilisti wakaiacha miungu yao huko, naye Daudi na watu wake wakaichukua.
Wafilisiti wakaacha vinyago vyao pale, na Daudi na watu wake wakaviondoa.
22 Wafilisti walikwea kwa mara nyingine na kusambaa katika Bonde la Warefai.
Kisha wafilisiti wakaja kwa mara nyingine tena na kujieneza zaidi katika bonde la Mrefai.
23 Kwa hiyo Daudi akamuuliza Bwana, naye akamjibu, “Usipande moja kwa moja, bali wazungukie kwa nyuma na uwashambulie mbele ya miti ya miforosadi.
Hivyo Daudi akatafuta msaada tena kutoka kwa Yahweh, naye Yahweh akamwambia, “Usiwashambulie kwa mbele, lakini uwazunguke kwa nyuma na uwaendee kupitia miti ya miforosadi.
24 Mara utakaposikia sauti ya kutembea kutoka kwenye vilele vya miti ya miforosadi, nenda haraka, kwa sababu hiyo itamaanisha kuwa Bwana ametangulia mbele yako kupiga jeshi la Wafilisti.”
Wakati utakaposikia sauti za mwendo katika upepo uvumao juu ya miti ya miforosadi, hapo ushambulie kwa nguvu. Fanya hivi kwa kuwa Yahwe atatangulia mbele yako kulishambulia jeshi la Wafilisiti.”
25 Basi Daudi akafanya kama Bwana alivyomwagiza, naye akawaangusha Wafilisti njia yote kuanzia Geba hadi Gezeri.
Hivyo Daudi akafanya kama Yahwe alivyomwamuru. Akawaua wafilisti njiani mwote toka Geba hadi Gezeri.

< 2 Samweli 5 >