< 2 Samweli 4 >
1 Ish-Boshethi mwana wa Sauli aliposikia kwamba Abneri amekufa huko Hebroni, akakosa ujasiri, nayo Israeli yote wakatiwa hofu kuu.
Ikawa Ishboshethi, mwana wa Sauli, aliposikia kwamba Abneri amekufa huko Hebroni, mikono yake ikadhoofika, na Israeli yote ikataabika.
2 Basi mwana wa Sauli alikuwa na watu wawili waliokuwa viongozi wa vikundi vya uvamizi. Mmoja aliitwa Baana na mwingine Rekabu, waliokuwa wana wa Rimoni, Mbeerothi, kutoka kabila la Benyamini. Beerothi alihesabiwa kuwa sehemu ya Benyamini,
Basi mwana wa Sauli alikuwa na watu wawili waliokuwa wakuu wa vikosi vya askari. Mmoja wao alikuwa Baana na mwingine alikuwa Rekabu, wana wa Rimoni Mbeerothi wa wana wa Benjamini(kwa maana Berothi ilihesabiwa kuwa sehemu ya Benjamini,
3 kwa sababu watu wa Beerothi walikimbilia huko Gitaimu na wameishi huko kama wageni mpaka siku hii ya leo.
na Waberothi walikimbilia Gitaimu na wamekuwa wakiishi pale hadi sasa).
4 (Yonathani mwana wa Sauli alikuwa na mwana aliyekuwa mlemavu miguu yote miwili. Alikuwa na miaka mitano wakati habari kuhusu Sauli na Yonathani zilipofika kutoka Yezreeli. Yaya wake akambeba ili kukimbia, lakini yaya alipokuwa anaharakisha kuondoka, mtoto alianguka akawa kiwete. Jina lake aliitwa Mefiboshethi.)
Basi Yonathani, mwana wa Sauli, alikuwa na mwana mlemavu wa miguu. Alikuwa na umri wa miaka mitano habari kuhusu Sauli na Yonathani ilipofika Yezreeli. Yaya wake akamchukua ili akimbie. Lakini wakati anakimbia, mwana wa Yonathani alianguka na akawa kirema. Jina lake aliitwa Mefiboshethi.
5 Basi Rekabu na Baana, wana wa Rimoni Mbeerothi wakaenda nyumbani kwa Ish-Boshethi, nao walifika huko wakati alipokuwa kwenye mapumziko yake ya mchana.
Hivyo wana wa Rimoni mbeerothi, Rekabu na Baana, wakasafiri mchana wakati wa jua kali mpaka nyumbani mwa Ishbothethi, yeye alikuwa amepumzika mchana.
6 Wakaingia kwenye chumba cha ndani kana kwamba wanachukua ngano, wakamchoma Ish-Boshethi mkuki wa tumboni. Ndipo Rekabu na Baana nduguye wakatoroka.
Mwanamke aliyekuwa akililinda lango alisinzia wakati akipepeta ngano, Rekabu na Baana waliingia ndani polepole na wakampita.
7 Walikuwa wameingia ndani ya nyumba wakati alipokuwa amelala kitandani chumbani kwake. Baada ya kumchoma mkuki na kumuua, walikata kichwa chake. Wakiwa wamekichukua, walitembea usiku kucha kwa njia ya Araba.
Hivyo walipoingia ndani ya nyumba, walimpiga na kumuua wakati amelala chumbani mwake. Kisha wakakata kichwa chake na wakaondoka nacho, wakasafiri njiani usiku kucha mpaka Araba.
8 Wakamletea Daudi kichwa cha Ish-Boshethi huko Hebroni, wakamwambia mfalme, “Hiki hapa kichwa cha Ish-Boshethi mwana wa Sauli, adui yako, aliyejaribu kuondoa uhai wako. Siku hii ya leo Bwana amemlipia kisasi mfalme bwana wangu dhidi ya Sauli na mzao wake.”
Wakaleta kichwa cha Ishboshethi kwa Daudi huko Hebroni, nao wakamwambia mfalme, “Tazama, hiki ni kichwa cha Ishboshethi mwana wa Sauli, adui yako, aliyekuwa akiutafuta uhai wako. Leo Yahwe amemlipia kisasi bwana wetu mfalme dhidi ya Sauli na uzao wake.”
9 Daudi akawajibu Rekabu na Baana nduguye, wana wa Rimoni, Mbeerothi, akasema, “Hakika kama Bwana aishivyo, ambaye ameniokoa kutoka taabu zote,
Daudi akawajibu Rekabu na Baana nduguye, wana wa Rimoni mbeerothi, akawambia, “Kama Yahwe aishivyo, aliyeuokoa uhai wangu na kila shida,
10 yule mtu aliponiambia, ‘Sauli amekufa,’ akadhani ananiletea habari njema, nilimkamata, nikamuua huko Siklagi. Hiyo ndiyo zawadi niliyompa kwa ajili ya taarifa yake!
mtu mmoja aliponiambia, 'Tazama, Sauli amekufa,' akifikiri alileta habari njema, nilimkamata na kumwua huko Siklagi. Huo ndio ujira niliompa kwa habari yake.
11 Je, ni mara ngapi zaidi wakati watu waovu wamemuua mtu asiye na hatia akiwa ndani ya nyumba yake mwenyewe na kwenye kitanda chake mwenyewe? Je, sasa nisidai damu yake mikononi mwenu na kuwaondoa duniani?”
Namna gani, mtu mwovu anapomwua mwenye haki kitandi mwake ndani ya nyumba, Je nisiitake damu yake kutoka katika mikono yenu, na kuwaondoa duniani?”
12 Kwa hiyo Daudi akawaamuru watu wake, wakawaua. Wakakata mikono yao na miguu, na kutundika viwiliwili vyao kando ya dimbwi huko Hebroni. Lakini wakakichukua kichwa cha Ish-Boshethi na kukizika katika kaburi la Abneri huko Hebroni.
Kisha Daudi akawaagiza vijana, nao wakawaua wakakata mikono na miguu yao na kuwatundika kando ya bwawa huko Hebroni. Lakini wakakichukua kichwa cha Ishboshethi na kukizika katika kaburi la Abneri katika Hebroni.