< 2 Samweli 24 >

1 Hasira ya Bwana ikawaka tena dhidi ya Israeli, naye akamchochea Daudi dhidi yao, akisema, “Nenda ukawahesabu Israeli na Yuda.”
Kisha hasira ya Yahwe ikawaka dhidi ya Israeli, naye akamchochea Daudi kinyume chao kusema, “Nenda, ukawahesabu Israeli na Yuda.”
2 Kwa hiyo mfalme akamwambia Yoabu, pamoja na majemadari wa jeshi aliokuwa nao, “Nendeni kwa makabila yote ya Israeli kuanzia Dani hadi Beer-Sheba na mwandikishe watu wapiganaji, ili niweze kujua idadi yao.”
Mfalme akamwambia Yoabu, jemedari wa jeshi, aliyekuwa pamoja naye, “Nenda upite katika kabila zote za Israeli, toka Dani mpaka Beersheba, uwahesabu watu wote, ili niweze kujua idadi kamili ya watu wanaofaa kwa vita.”
3 Lakini Yoabu akamjibu mfalme, “Bwana Mungu wako na azidishe jeshi mara mia, nayo macho ya bwana wangu mfalme na yaone hili. Lakini kwa nini bwana wangu mfalme anataka kufanya kitu cha namna hii?”
Yoabu akamwambia mfalme, “Yahwe Mungu wako na aizidishe hesabu ya watu mara mia, na macho ya bwana wangu mfalme yaone ikifanyika. Lakini kwa nini bwana wangu mfalme analitaka jambo hili?
4 Hata hivyo, neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu pamoja na majemadari wa jeshi, kwa hiyo wakaondoka mbele ya mfalme kuandikisha wapiganaji wa Israeli.
Walakini neno la mfalme lilikuwa la mwisho dhidi ya Yoabu na dhidhi ya majemedari wa jeshi. Hivyo Yoabu na majemedari wakatoka mbele ya mfalme kuwahesabu watu wa Israeli.
5 Baada ya kuvuka Yordani, walipiga kambi karibu na Aroeri, kusini ya mji ulioko kwenye bonde jembamba, ndipo wakipitia Gadi, wakaenda hadi Yazeri.
Wakavuka Yordani na kupiga kambi karibu na Aroeri, kusini mwa mji bondeni. Kisha wakasafiri kupitia Gadi mpaka Yazeri.
6 Walikwenda hadi Gileadi na pia eneo la Tahtimu-Hodshi, wakaendelea hadi Dani-Yaani na kuzunguka kuelekea Sidoni.
Wakaja Gileadi na nchi ya Tahtimu Hodshi, kisha Dani, Jaani na karibu kuelekea Sidoni.
7 Kisha wakaenda kuelekea ngome ya Tiro pamoja na miji yote ya Wahivi na ya Wakanaani. Mwishoni, walikwenda mpaka Beer-Sheba katika Negebu ya Yuda.
Wakafika ngome ya Tiro na miji yote ya Wahivi na Wakanaani. Kisha wakaenda Negebu katika Yuda huko Beersheba.
8 Baada ya kupita katika nchi nzima, walirudi Yerusalemu baada ya miezi tisa na siku ishirini.
Walipokuwa wamepita katika nchi yote, wakarejea Yerusalemu mwishoni mwa miezi tisa na siku ishirini.
9 Yoabu akatoa hesabu ya wapiganaji kwa mfalme: Katika Israeli kulikuwako watu 800,000 wenye uwezo wa kupigana, na katika Yuda watu 500,000.
Ndipo Yoabu alipotoa taarifa ya hesabu kamili kwa mfalme kuhusu watu wawezao kupigana vita. Katika Israeli kulikuwa na watu 800, 000 jasiri wawezao kutoa upanga, na wale wa Yuda walikuwa watu 500, 000.
10 Dhamiri ya Daudi ilishtuka baada ya kuwahesabu wapiganaji, naye akamwambia Bwana, “Nimefanya dhambi kubwa kwa kufanya jambo hili. Ee Bwana, sasa ninakusihi, ondoa hatia ya mtumishi wako. Nimefanya jambo la kipumbavu sana.”
Ndipo moyo wa Daudi ukamchoma alipokuwa amewahesabu watu. Hivyo akamwambia Yahwe, “Kwa kufanya hivi nimetenda dhambi sana. Sasa, Yahwe, uiondoe hatia ya mtumishi wako, kwani nimetenda kwa upumbavu.”
11 Kabla Daudi hajaamka kesho yake asubuhi, neno la Bwana lilikuwa limemjia Gadi nabii, aliyekuwa mwonaji wa Daudi, kusema:
Daudi alipoinuka asubuhi, neno la Yahwe likamjia nabii Gadi, mwonaji wa Daudi, kusema,
12 “Nenda ukamwambie Daudi, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Ninakupa wewe uchaguzi wa mambo matatu. Nichagulie mojawapo nitakalotenda dhidi yako.’”
Nenda umwambie Daudi; 'Hivi ndivyo asemavyo Yahwe: “Ninakupa mambo matatu. Uchague mojawapo.”
13 Basi Gadi akaenda kwa Daudi na kumwambia, “Je, ije njaa ya miaka mitatu katika nchi yako? Au miezi mitatu ya kukimbia adui zako wakikufuatia? Au siku tatu za tauni katika nchi yako? Basi sasa, fikiri juu ya hilo na uamue jinsi nitakavyomjibu huyo aliyenituma.”
Hivyo Gadi akaenda kwa Daudi na kumwambia, “Je miaka mitatu ya njaa ije katika nchi yako? au miezi mitatu ukimbie kutoka kwa adui zako huku wakikufuatia? au kuwe na tauni ya siku tatu katika nchi yako? Amua sasa jibu gani nimrudishie aliyenituma.”
14 Daudi akamjibu Gadi, “Nitataabika sana. Afadhali tuangukie mikononi mwa Bwana, kwa maana rehema zake ni kuu, lakini usiniache nianguke mikononi mwa wanadamu.”
Ndipo Daudi alipomwambia Gadi, “Nipo katika shida kubwa. Haya na tuanguke katika mikono ya Yahwe kuliko kuanguka katika mikono ya mwanadamu, kwani matendo yake ya rehema ni makuu sana.”
15 Basi Bwana akatuma tauni katika Israeli kuanzia asubuhi mpaka mwisho wa muda ulioamriwa, wakafa watu 70,000 kuanzia Dani hadi Beer-Sheba.
Hivyo akatuma tauni juu ya Israeli kuanzia asubuhi kwa muda ulioamriwa, na watu sabini na tano elfu kutoka Dani mpaka Beersheba wakafa.
16 Malaika aliponyoosha mkono wake ili kuangamiza Yerusalemu, Bwana akahuzunika kwa sababu ya maafa, akamwambia yule malaika aliyekuwa anawadhuru watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako.” Wakati huo malaika wa Bwana alikuwa kwenye sakafu ya kupuria ya Arauna, Myebusi.
Malaika aliponyosha mkono wake kuelekea Yerusalemu ili kuuharibu, Yahwe akabadili nia yake kuhusu madhara, na akamwambia malaika aliyekuwa tiyari kuwaangamiza watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako sasa.” Wakati huo malaika wa Yahwe alikuwa amesimama katika kiwanja cha kupuria cha Arauna Myebusi.
17 Ikawa Daudi alipomwona huyo malaika aliyekuwa akiwaua watu, akamwambia Bwana, “Mimi ndiye niliyetenda dhambi na kukosa. Hawa ni kondoo tu. Wamefanya nini? Mkono wako uwe juu yangu na nyumba yangu.”
Daudi alipomwona malaika aliyekuwa amewapiga watu, akamwambia Yahwe kusema, “Nimetenda dhambi, na nimetenda kwa upumbavu. Lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Tafadhari, mkono wako na uniadhibu mimi na familia ya baba yangu!”
18 Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi na kumwambia, “Panda ukamjengee Bwana madhabahu kwenye sakafu ya kupuria ya Arauna Myebusi.”
Kisha Gadi akaja siku hiyo kwa Daudi na kumwambia, “Kwea na ujenge madhabahu kwa ajili ya Yahwe katika kiwanja cha kupuria cha Arauna Myebusi.”
19 Kwa hiyo Daudi akakwea kama vile Bwana alivyokuwa ameamuru kwa kinywa cha Gadi.
Hivyo Daudi akakwea kama Gadi alivyomwelekeza kufanya, kama Yahwe alivyokuwa ameagiza.
20 Arauna alipotazama na kumwona mfalme na watu wake wakija kumwelekea, alitoka nje na kusujudu mbele ya mfalme kifudifudi, akiuinamisha uso wake ardhini.
Arauna akatazama na kumwona mfalme na watumishi wake wakikaribia. Ndipo Arauna akaondoka na kumsujudia mfalme uso wake mpaka juu ya ardhi.
21 Arauna akasema, “Mbona bwana wangu mfalme amekuja kwa mtumishi wake?” Daudi akajibu, “Kununua sakafu yako ya kupuria, ili niweze kumjengea Bwana madhabahu, ili tauni iliyo katika watu iondolewe.”
Kisha Arauna akasema, “Kwa nini bwana wangu mfalme amekuja kwangu, mtumishi wake? Daudi akajibu, “Kununua uwanja wako wa kupuria, ili nimjengee Yahwe madhabahu, ili kwamba tauni iondolewe kwa watu.”
22 Arauna akamwambia Daudi, “Bwana wangu mfalme na achukue chochote kinachompendeza na akitoe sadaka. Hapa kuna maksai kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, pia kuna miti ya kupuria na nira za ngʼombe kwa ajili ya kuni.
Arauna akamwambia Daudi, “Chukua liwe lako, bwana wangu mfalme. Ulifanyie lolote lolote lililojema machoni pako. Tazama, ng'ombe kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa na miganda ya kupuria na nira kwa kuni.
23 Ee mfalme, Arauna anatoa vyote hivi kwa mfalme.” Pia Arauna akamwambia mfalme, “Bwana Mungu wako na akukubali.”
Haya yote bwana wangu mfalme, mimi Arauna nakupa.” Kisha akamwambia mfalme, “Yahwe Mungu wako na awe nawe.”
24 Lakini mfalme akamjibu Arauna, “La hasha, nasisitiza kuvilipia. Sitatoa sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana Mungu wangu isiyonigharimu chochote.” Kwa hiyo Daudi akanunua ile sakafu ya kupuria nafaka na maksai, akazilipia shekeli hamsini za fedha.
Mfalme akamwambia Arauna, “Hapana, nahimiza kukinunua kwa thamani yake. Sitatoa kama sadaka ya kuteketezwa kwa Yahwe chochote nisichokigharimia.” Hivyo Daudi akakinunua kiwanja cha kupuria na ng'ombe kwa shekeli hamsini za fedha.
25 Kisha Daudi akamjengea Bwana madhabahu mahali hapo, na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha Bwana akajibu kwa ajili ya nchi, nayo tauni ikakoma katika Israeli.
Daudi akajenga madhabahu kwa Yahwe pale na kutoa juu yake sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Hivyo wakamsihi Yahwe kwa niaba ya nchi, hivyo akaizuia tauni katika katika Israeli yote.

< 2 Samweli 24 >