< 2 Samweli 23 >

1 Haya ni maneno ya mwisho ya Daudi: “Neno la Daudi mwana wa Yese, neno la mtu aliyeinuliwa na Aliye Juu Sana, mtu aliyepakwa mafuta na Mungu wa Yakobo, mwimbaji wa nyimbo wa Israeli:
Haya ni maneno ya mwisho ya Daudi-Daudi mwana wa Yese, mtu aliyeheshimiwa sana, aliyetiwa mafuta na Mungu wa Yakobo, mwandishi mzuri wa zaburi wa Israeli.
2 “Roho wa Bwana alinena kupitia kwangu, neno lake lilikuwa ulimini mwangu.
“Roho ya Yahwe alisema nami, na neno lake lilikuwa ulimini mwangu.
3 Mungu wa Israeli alinena, mwamba wa Israeli akaniambia: ‘Mtu anatawala watu kwa haki, wakati anapotawala akiwa na hofu ya Mungu,
Mungu wa Israeli alinena, Mwamba wa Israeli aliniambia, “Atawalaye kwa haki juu yangu, atawalaye katika hofu ya Mungu.
4 yeye ni kama mwanga wa asubuhi jua lichomozapo asubuhi isiyo na mawingu, kama mwanga baada ya mvua uchipuzao majani kutoka ardhini.’
Atakuwa kama nuru ya asubuhi jua linapochomoza, asubuhi isiyo na mawingu, wakati mche mwororo unapochipua kutoka ardhini kupitia mwangaza wa mng'ao wa jua baada ya mvua.
5 “Je, si hivyo ilivyo nyumba yangu mbele za Mungu? Je, hajafanya Agano la milele nami, lililopangwa na kuimarishwa kila sehemu? Je, hatanifanya niufurahie wokovu wangu na kunijalia matakwa yangu yote?
Hakika, je familia yangu haiko hivi mbele za Mungu? Je hajafanya nami agano la milele, taratibu la uhakika kwa kila njia? Je yeye haongezi wokovu wangu na kutimiza kila hitaji langu?
6 Lakini watu waovu wote watatupwa kando kama miiba, ambayo haikusanywi kwa mkono.
Lakini yasiyofaa yote yatakuwa kama miiba na kutupwa mbali, kwa maana haiwezekani kukusanywa kwa mikono.
7 Yeyote agusaye miiba hutumia chombo cha chuma au mpini wa mkuki, nayo huchomwa pale ilipo.”
Ayagusaye ni lazima atumie chombo cha chuma au au fumo la mkuki. Ni lazima yachomwe mahali yalipo.
8 Haya ndiyo majina ya mashujaa wa Daudi: Yosheb-Bashebethi, Mtahkemoni, alikuwa kiongozi wa wale Watatu; yeye aliinua mkuki wake dhidi ya watu 800, ambao aliwaua katika pambano moja.
Haya ni majina ya askari wa Daudi: Yashobeamu Mhakmoni alikuwa kiongozi wa mashujaa. Aliua watu mia nne wakati mmoja.
9 Wa pili wake alikuwa Eleazari mwana wa Dodai, Mwahohi. Akiwa mmojawapo wa wale mashujaa watatu, alikuwa pamoja na Daudi wakati waliwadhihaki Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko Pas-Damimu kwa ajili ya vita. Kisha watu wa Israeli wakarudi nyuma,
Baada yake alikuwa Elieza mwana wa Dodo, mwana wa mwahohi, mmoja wa mashujaa watatu wa Daudi. Alikuwepo walipowashinda Wafilisti waliokuwa wamekusanyika kwa vita, na wakati watu wa Israeli walipokuwa wamekimbia.
10 lakini yeye alisimama imara akawaua Wafilisti hadi mkono wake ukachoka na ukagandamana na upanga. Bwana akawapa ushindi mkubwa siku ile. Vikosi vikarudi kwa Eleazari, kuteka tu nyara za waliokufa.
Elieza akasimama na kuwapiga Wafilisti mpaka mkono wake ukachoka, mpaka mkono wake ukang'ang'ania mpini wa upanga wake. Siku hiyo Yahwe akatoa ushindi mkuu. Jeshi likarejea kwa ajili ya kuteka tu nyara za waliouawa na Elieza.
11 Aliyefuata alikuwa Shama mwana wa Agee, Mharari. Wafilisti walipokusanyika pamoja mahali palipokuwa shamba lililojaa dengu, vikosi vya Israeli viliwakimbia.
Baada yake alikuwa Shama mwana wa Agee, Mharari. Wafilisti wakajikusanya pamoja palipokuwa na shamba la dengu, na jeshi likawakimbia.
12 Lakini Shama akasimama imara katikati ya lile shamba. Akalitetea na kuwaua Wafilisti, naye Bwana akawapa ushindi mkubwa.
Lakini Shama akasimama katikati ya shamba na kulitetea. Aliwauwa Wafilisti, na Yahwe akaleta ushindi mkuu.
13 Wakati wa mavuno, viongozi watatu kati ya viongozi thelathini walishuka, wakamwendea Daudi katika pango la Adulamu, wakati kikundi cha Wafilisti kilikuwa kimepiga kambi katika Bonde la Warefai.
Watatu kati ya askari thelathini walishuka kwa Daudi nyakati za mavuno, katika pango la Adulamu. Jeshi la Wafilisti lilikuwa limepiga kambi katika bonde la Mrefai.
14 Wakati huo Daudi alikuwa katika ngome, na kambi ya Wafilisti ilikuwa huko Bethlehemu.
Wakati huo Daudi alikuwa katika ngome yake, pangoni, wakati Wafilisti walikuwa wanaimilk Bethlehemu.
15 Daudi akatamani maji, akasema, “Laiti mtu angenipatia maji ya kunywa kutoka kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu!”
Daudi alitamani maji na akasema, “Kama ingekuwa mtu mmoja angenipa maji ya kunywa kutoka kisima kilichopo Bethlehemu, kisima kilichopo langoni!”
16 Basi mashujaa hao watatu wakapenya katikati ya Wafilisti, wakaenda kuchota maji kutoka kwa kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu, wakamletea Daudi. Lakini Daudi akakataa kuyanywa. Badala yake, aliyamimina mbele za Bwana.
Hivyo mashujaa hawa watatu wakapita kati ya jeshi la Wafilisti na kuchota maji katika kisima cha Bethlehemu, kilichopo langoni. Wakachukua maji na kuyaleta kwa Daudi, lakini yeye akakataa kuyanywa. Badala yake akayamwaga mbele za Yahwe.
17 Akasema, “Iwe mbali nami, Ee Bwana, kufanya kitu hiki. Je, hii si damu ya watu ambao walikwenda kwa kuhatarisha maisha yao?” Naye Daudi hakuyanywa. Haya yalifanywa na hao mashujaa watatu.
Kisha akasema, “Iwe mbali nami, Yahwe, kwamba niyanywe haya. Je ninywe damu ya watu waliohatarisha maisha yao?” Hivyo akakataa kuyanywa. Haya ni mambo yaliyofanywa na mashujaa watatu.
18 Abishai ndugu yake Yoabu mwana wa Seruya ndiye alikuwa kiongozi wa hao Watatu. Aliinua mkuki wake dhidi ya watu 300 ambao aliwaua, kwa hiyo naye akawa na sifa kama hao Watatu.
Abishai, nduguye Yoabu na mwana wa Seruya, alikuwa akida wa watatu. Alipigana kwa mkuki wake na watu mia tatu na akawauwa wote mara. Mara kwa mara alitajwa kati ya mashujaa watatu.
19 Je, hakupata heshima kubwa zaidi kuliko hao Watatu? Alikuwa jemadari wao, ingawa hakuhesabiwa miongoni mwao.
Hakuwa maarufu kuliko wale watatu? Alifanywa akida wao. Lakini, umaarufu wake haukulingana na umaarufu wa wale mashujaa watatu.
20 Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa mpiganaji hodari kutoka Kabseeli ambaye alifanya mambo makubwa ya ujasiri. Aliwaua mashujaa wawili waliokuwa hodari kuliko wote wa Moabu. Pia alishuka shimoni kulipokuwa na theluji na kumuua simba.
Benaya kutoka Kabseeli mwana wa Yehoyada; alikuwa mtu hodari aliyefanya matendo makuu. Aliwauwa wana wawili wa Arieli wa Moabu. Pia alishuka shimoni na kuuwa simba wakati wa theruji.
21 Pia alimuua Mmisri mrefu mkubwa. Ingawa Mmisri alikuwa na mkuki mkononi mwake, Benaya alimwendea akiwa na rungu. Alipokonya mkuki kutoka mkononi mwa Mmisri na kumuua kwa mkuki wake mwenyewe.
Na alimwua Mmisri aliyekuwa mtu mnene sana. Mmisri alikuwa na mkuki mkononi, lakini Benaya alipigana naye kwa fimbo tu. Aliuchukua mkuki mkononi mwa Mmisri na kisha kumwua nao.
22 Haya yalikuwa mambo ya ushujaa ya Benaya mwana wa Yehoyada; naye pia alikuwa maarufu kama wale mashujaa watatu.
Benaya mwana wa Yehoyada alifanya matendo haya, naye alitajwa kati ya mashujaa watatu.
23 Yeye aliheshimiwa zaidi ya wale Thelathini, lakini hakujumuishwa miongoni mwa wale Watatu. Daudi akamweka kuwa kiongozi wa walinzi wake.
Alikuwa na heshima kuliko mashujaa thelathini kwa ujumla wao, lakini hakuwa na heshima kama wale mashujaa watatu. Hata hivyo Daudi alimweka kuwa mlinzi wake.
24 Miongoni mwa wale Thelathini walikuwepo: Asaheli ndugu wa Yoabu; Elhanani mwana wa Dodo kutoka Bethlehemu;
Wafuatao ni wale watu thelathini: Asaheli nduguye Yoabu, Elhanani mwana wa Dodo kutoka Bethlehemu,
25 Shama, Mharodi; Elika, Mharodi;
Shama Mharodi, Elika Mharodi,
26 Helesi, Mpalti; Ira mwana wa Ikeshi kutoka Tekoa;
Helesi Mpeloni, Ira mwana wa Ikeshi Mtekoi,
27 Abiezeri kutoka Anathothi; Mebunai, Mhushathi;
Abi Ezeri Mwanathothi, Mebunai Mhushathi,
28 Salmoni, Mwahohi; Maharai, Mnetofathi;
Salmoni Mhahoi, Maharai Mnetofathi;
29 Heledi mwana wa Baana, Mnetofathi; Itai mwana wa Ribai kutoka Gibea ya Benyamini;
Helebu mwana wa Baana, Mnetofathi, Itai mwana wa Rabai kutoka Gibea ya Wabenjamini,
30 Benaya Mpirathoni; Hidai kutoka mabonde ya Gaashi;
Benaya Mpirathoni, Hidai wa mabonde ya Gaashi.
31 Abi-Alboni, Mwaribathi; Azmawethi, Mbarhumi;
Abieliboni Mwarbathi, Azmawethi Mbarhumi,
32 Eliaba, Mshaalboni; wana wa Yasheni; Yonathani
Eliaba Mshalboni, wana wa Yasheni, Yonathani mwana wa Shama Mharari;
33 mwana wa Shama, Mharari; Ahiamu mwana wa Sharari, Mharari;
Ahiamu mwana wa Sharari Mharari,
34 Elifeleti mwana wa Ahasbai, Mmaakathi; Eliamu mwana wa Ahithofeli, Mgiloni;
Elifeleti mwana wa Ahasbai Mmaakathi, Eliamu mwana wa Ahithofeli Mgiloni,
35 Hezro, Mkarmeli; Paarai, Mwarbi;
Hezro Mkarmeli, Parai Mwarbi,
36 Igali mwana wa Nathani kutoka Soba; Bani, Mgadi;
Igali mwana wa Nathani kutoka Soba, Bani kutoka kabila la Gadi,
37 Seleki, Mwamoni; Naharai, Mbeerothi, aliyekuwa mbeba silaha za Yoabu mwana wa Seruya;
Zeleki Mwamoni, Naharai Mbeerothi, mbeba silaha wa Yoabu mwana wa Seruya,
38 Ira, Mwithiri; Garebu, Mwithiri;
Ira Mwithri, Garebu Mwithri,
39 na Uria, Mhiti. Jumla yao wote walikuwa watu thelathini na saba.
Uria Mhiti - jumla yao thelathini na wanane.

< 2 Samweli 23 >