< 2 Samweli 23 >
1 Haya ni maneno ya mwisho ya Daudi: “Neno la Daudi mwana wa Yese, neno la mtu aliyeinuliwa na Aliye Juu Sana, mtu aliyepakwa mafuta na Mungu wa Yakobo, mwimbaji wa nyimbo wa Israeli:
2 “Roho wa Bwana alinena kupitia kwangu, neno lake lilikuwa ulimini mwangu.
3 Mungu wa Israeli alinena, mwamba wa Israeli akaniambia: ‘Mtu anatawala watu kwa haki, wakati anapotawala akiwa na hofu ya Mungu,
4 yeye ni kama mwanga wa asubuhi jua lichomozapo asubuhi isiyo na mawingu, kama mwanga baada ya mvua uchipuzao majani kutoka ardhini.’
5 “Je, si hivyo ilivyo nyumba yangu mbele za Mungu? Je, hajafanya Agano la milele nami, lililopangwa na kuimarishwa kila sehemu? Je, hatanifanya niufurahie wokovu wangu na kunijalia matakwa yangu yote?
6 Lakini watu waovu wote watatupwa kando kama miiba, ambayo haikusanywi kwa mkono.
7 Yeyote agusaye miiba hutumia chombo cha chuma au mpini wa mkuki, nayo huchomwa pale ilipo.”
8 Haya ndiyo majina ya mashujaa wa Daudi: Yosheb-Bashebethi, Mtahkemoni, alikuwa kiongozi wa wale Watatu; yeye aliinua mkuki wake dhidi ya watu 800, ambao aliwaua katika pambano moja.
9 Wa pili wake alikuwa Eleazari mwana wa Dodai, Mwahohi. Akiwa mmojawapo wa wale mashujaa watatu, alikuwa pamoja na Daudi wakati waliwadhihaki Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko Pas-Damimu kwa ajili ya vita. Kisha watu wa Israeli wakarudi nyuma,
10 lakini yeye alisimama imara akawaua Wafilisti hadi mkono wake ukachoka na ukagandamana na upanga. Bwana akawapa ushindi mkubwa siku ile. Vikosi vikarudi kwa Eleazari, kuteka tu nyara za waliokufa.
11 Aliyefuata alikuwa Shama mwana wa Agee, Mharari. Wafilisti walipokusanyika pamoja mahali palipokuwa shamba lililojaa dengu, vikosi vya Israeli viliwakimbia.
12 Lakini Shama akasimama imara katikati ya lile shamba. Akalitetea na kuwaua Wafilisti, naye Bwana akawapa ushindi mkubwa.
13 Wakati wa mavuno, viongozi watatu kati ya viongozi thelathini walishuka, wakamwendea Daudi katika pango la Adulamu, wakati kikundi cha Wafilisti kilikuwa kimepiga kambi katika Bonde la Warefai.
14 Wakati huo Daudi alikuwa katika ngome, na kambi ya Wafilisti ilikuwa huko Bethlehemu.
15 Daudi akatamani maji, akasema, “Laiti mtu angenipatia maji ya kunywa kutoka kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu!”
16 Basi mashujaa hao watatu wakapenya katikati ya Wafilisti, wakaenda kuchota maji kutoka kwa kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu, wakamletea Daudi. Lakini Daudi akakataa kuyanywa. Badala yake, aliyamimina mbele za Bwana.
17 Akasema, “Iwe mbali nami, Ee Bwana, kufanya kitu hiki. Je, hii si damu ya watu ambao walikwenda kwa kuhatarisha maisha yao?” Naye Daudi hakuyanywa. Haya yalifanywa na hao mashujaa watatu.
18 Abishai ndugu yake Yoabu mwana wa Seruya ndiye alikuwa kiongozi wa hao Watatu. Aliinua mkuki wake dhidi ya watu 300 ambao aliwaua, kwa hiyo naye akawa na sifa kama hao Watatu.
19 Je, hakupata heshima kubwa zaidi kuliko hao Watatu? Alikuwa jemadari wao, ingawa hakuhesabiwa miongoni mwao.
20 Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa mpiganaji hodari kutoka Kabseeli ambaye alifanya mambo makubwa ya ujasiri. Aliwaua mashujaa wawili waliokuwa hodari kuliko wote wa Moabu. Pia alishuka shimoni kulipokuwa na theluji na kumuua simba.
21 Pia alimuua Mmisri mrefu mkubwa. Ingawa Mmisri alikuwa na mkuki mkononi mwake, Benaya alimwendea akiwa na rungu. Alipokonya mkuki kutoka mkononi mwa Mmisri na kumuua kwa mkuki wake mwenyewe.
22 Haya yalikuwa mambo ya ushujaa ya Benaya mwana wa Yehoyada; naye pia alikuwa maarufu kama wale mashujaa watatu.
23 Yeye aliheshimiwa zaidi ya wale Thelathini, lakini hakujumuishwa miongoni mwa wale Watatu. Daudi akamweka kuwa kiongozi wa walinzi wake.
24 Miongoni mwa wale Thelathini walikuwepo: Asaheli ndugu wa Yoabu; Elhanani mwana wa Dodo kutoka Bethlehemu;
25 Shama, Mharodi; Elika, Mharodi;
26 Helesi, Mpalti; Ira mwana wa Ikeshi kutoka Tekoa;
27 Abiezeri kutoka Anathothi; Mebunai, Mhushathi;
28 Salmoni, Mwahohi; Maharai, Mnetofathi;
29 Heledi mwana wa Baana, Mnetofathi; Itai mwana wa Ribai kutoka Gibea ya Benyamini;
30 Benaya Mpirathoni; Hidai kutoka mabonde ya Gaashi;
31 Abi-Alboni, Mwaribathi; Azmawethi, Mbarhumi;
32 Eliaba, Mshaalboni; wana wa Yasheni; Yonathani
33 mwana wa Shama, Mharari; Ahiamu mwana wa Sharari, Mharari;
34 Elifeleti mwana wa Ahasbai, Mmaakathi; Eliamu mwana wa Ahithofeli, Mgiloni;
35 Hezro, Mkarmeli; Paarai, Mwarbi;
36 Igali mwana wa Nathani kutoka Soba; Bani, Mgadi;
37 Seleki, Mwamoni; Naharai, Mbeerothi, aliyekuwa mbeba silaha za Yoabu mwana wa Seruya;
38 Ira, Mwithiri; Garebu, Mwithiri;
39 na Uria, Mhiti. Jumla yao wote walikuwa watu thelathini na saba.