< 2 Samweli 20 >

1 Basi, kulikuwa na mtu mbaya sana aliyeitwa Sheba mwana wa Bikri, Mbenyamini, aliyekuwako huko. Akapiga tarumbeta na kupaza sauti, “Hatuna fungu katika Daudi, wala hatuna sehemu katika mwana wa Yese! Kila mtu aende hemani mwake, enyi Israeli!”
Ikatukia pia kuwa katika eneo lilelile kulikuwa mfanya fujo jina lake Sheba mwana wa Bikri Mbenjamini. Akapiga tarumbeta na kusema, “Sisi hatuna sehemu katika Daudi, wala hatuna urithi katika mwana wa Yese. Haya kila mtu na aende nyumbani kwake, Israeli.”
2 Kwa hiyo watu wote wa Israeli wakamwacha Daudi na kumfuata Sheba mwana Bikri. Lakini watu wa Yuda wakawa karibu na mfalme wao katika safari yote kutoka Yordani mpaka Yerusalemu.
Hivyo watu wote wa Israeli wakamwacha Daudi na kumfuata Sheba mwana wa Bikri. Lakini watu wa Yuda wakamfuata mfalme wao kwa karibu sana, kutoka Yordani njia yote hadi Yerusalemu.
3 Daudi aliporudi katika jumba lake la kifalme huko Yerusalemu, aliwachukua wale masuria kumi aliokuwa amewaacha ili kuangalia jumba la kifalme na kuwaweka ndani ya nyumba chini ya ulinzi. Akawapa mahitaji yao lakini hakukutana nao kimwili. Waliwekwa kifungoni wakaishi kama wajane mpaka kifo chao.
Daudi alipofika katika kasri lake huko Yerusalemu, akawachukua masuria aliokuwa amewaacha kulitunza kasri, na akawaweka katika nyumba chini ya uangalizi. Aliwaandalia mahitaji yao lakini hakulala nao tena. Hivyo walikuwa wametengwa hadi siku ya kufa kwao, waliishi kama wajane.
4 Ndipo mfalme akamwambia Amasa, “Waite watu wa Yuda waje kwangu katika muda wa siku tatu, nawe mwenyewe uwepo hapa.”
Kisha mfalme akamwambia Amasa, “Uwaite watu wa Yuda ndani ya siku hizi tatu; wewe pia uwepo hapa.”
5 Lakini Amasa alipokwenda kuwaita Yuda, alichukua muda mrefu zaidi ya ule mfalme aliokuwa amemwekea.
Hivyo Amasa akaenda kuwaalika watu wote wa Yuda kwa pamoja, lakini akatumia muda mrefu kulika mfalme alivyokuwa amemwamuru.
6 Daudi akamwambia Abishai, “Sasa Sheba mwana wa Bikri atatuletea madhara zaidi kuliko alivyofanya Absalomu. Wachukue watu wa bwana wako na umfuatie, la sivyo atapata mji wenye ngome na kututoroka.”
Hivyo Daudi akamwambia Abishai, “Sasa Sheba mwana wa Bikri atatufanyia madhara zaidi ya Absalomu. Chukua watumishi wa bwana wako, askari wangu, na umfuatie asije akaingia katika mji wenye ngome na kututoroka.”
7 Hivyo watu wa Yoabu, na Wakerethi na Wapelethi, pamoja na wapiganaji mashujaa wote wakaondoka chini ya uongozi wa Abishai. Wakatoka Yerusalemu ili kumfuata Sheba mwana wa Bikri.
Ndipo watu wa Yoabu wakamfuatia, pamoja na Wakerethi na Wapelethi na mashujaa wote. Wakatoka Yerusalemu ili kumfuatia Sheba mwana wa Bikri.
8 Wakati walikuwa kwenye mwamba mkubwa huko Gibeoni, Amasa alikuja kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa mavazi yake ya kijeshi; juu yake alifunga mkanda kwenye kiuno wenye upanga ndani ya ala. Alipokuwa akienda mbele, ule upanga ukaanguka kutoka kwenye ala.
Walipokuwa katika jiwe kubwa lililoko Gibeoni, Amasa akaja kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa silaha ya vita aliyokuwa ameivaa, alikuwa pia na upanga uliokuwa umefungwa na mkanda katika kiuno chake. Kadili alivyoendelea mbele upanga ukadondoka.
9 Yoabu akamwambia Amasa, “U hali gani, ndugu yangu?” Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wake wa kuume ili ambusu.
Hivyo Yoabu akamwambia Amasa, “Haujambo binamu yangu?” Kwa utaratibu Yoabu akakishika kidevu cha Amasa kwa mkono wake wa kulia ili ambusu.
10 Amasa hakuona upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu, naye Yoabu akamchoma nao tumboni, nayo matumbo yake yakamwagika chini. Pasipo kuchomwa mara ya pili, Amasa akafa. Basi Yoabu na Abishai nduguye wakamfuatia Sheba mwana wa Bikri.
Amasa hakutambua kwamba kulikuwa na jambia katika mkono wa kushoto wa Yoabu. Yoabu akamchoma Amasa tumboni na matumbo yake yakadondoka chini. Wala Yoabu hakumpiga tena, na Amasa akafa. Hivyo Yoabu na Abishai nduguye wakamfuatia Sheba mwana wa Bikri.
11 Mmoja wa watu wa Yoabu akasimama kando ya Amasa, akasema, “Yeyote ampendaye Yoabu na yeyote aliye upande wa Daudi, na amfuate Yoabu!”
Kisha mmoja wa watu wa Yoabu akasimama kando ya Amasa naye akasema, “Aliye upande wa Yoabu na aliyeupande wa Daudi na amfuate Yoabu.”
12 Amasa alikuwa akigaagaa katika damu yake katikati ya barabara; mtu mmoja akaona kwamba vikosi vyote vilikuwa vinasimama pale. Huyo mtu alipotambua kwamba kila aliyefika pale Amasa alipokuwa alisimama, alimburuta Amasa kutoka barabarani mpaka kwenye shamba na kutupia nguo juu yake.
Amasa akawa anagalagala katika damu yake katikati ya njia. Mtu yule alipoona kwamba watu wote wamesimama, akambeba Amasa na kumweka shambani kando ya njia. Akatupa vazi juu yake kwa maana aliona kila mmoja aliyekuja alisimamaa pale.
13 Baada ya Amasa kuondolewa kutoka barabarani, watu wote walienda pamoja na Yoabu kumfuatia Sheba mwana wa Bikri.
Baada ya Amasa kuondolewa njiani watu wote wakamfuata Yoabu katika kumfuatia Sheba mwana wa Bikri.
14 Sheba akapita katika makabila yote ya Israeli hadi Abel-Beth-Maaka na kupitia eneo lote la Waberi ambao walijikusanya pamoja na kumfuata.
Sheba akazipita kabila zote za Israeli mpaka Abeli wa Beth Maaka, na katika nchi yote ya Berite ambao pia walijikusanya pamoja pia na kumfuatia Sheba.
15 Vikosi vyote vya Yoabu vikaja na kumhusuru Sheba mwana wa Bikri huko Abel-Beth-Maaka. Wakauzingira mji kwa kuweka vikosi vya askari, ili kukabiliana na ngome ya mji. Walipokuwa wanagongagonga ukuta ili kuubomoa na kuuangusha chini,
Walimpata na kumzingira huko Abeli wa Bethi Maaka. Wakajenga buruji ya kuhusuru mji nyuma ya ukuta. Jeshi lote lilokuwa pamoja na Yoabu likaugongagonga ukuta ili uanguke.
16 mwanamke mmoja mwenye busara akaita kutoka ndani ya mji, akisema, “Sikilizeni! Sikilizeni! Mwambieni Yoabu aje hapa ili niweze kuzungumza naye.”
Ndipo mwanamke mwerevu akapiga kelele kutoka ndani ya mji, “Sikiliza, Yoabu, tafadhari sikiliza! Sogea karibu nami ili niongee nawe.”
17 Yoabu alikwenda mbele yake, akamuuliza, “Wewe ni Yoabu?” Akamjibu, “Ndiye mimi.” Yule mwanamke akamwambia, “Sikiliza kile mtumishi wako atakachokuambia.” Akamwambia, “Ninasikiliza.”
Hivyo Yoabu akakaribia, mwanamke akamwambia, “Je wewe ni Yoabu? Akajibu, “ni mimi.” mwanamke akamwambia, “Sikiliza maneno ya mtumishi wako.” Akajibu, “Nasikiliza.”
18 Huyo mwanamke akaendelea kusema, “Zamani za kale walikuwa wakisema, ‘Wakaulize ushauri huko Abeli,’ hivyo kulimaliza lile shauri.
Ndipo aliposema,”Hapo zamani ilisemwa, 'Bila shaka tafuteni ushauri huko Abeli,' na kwamba ushauri huo utakata maneno.
19 Sisi ni watu wa amani na waaminifu katika Israeli. Wewe unajaribu kuharibu mji ambao ni mama katika Israeli. Kwa nini unataka kumeza urithi wa Bwana?”
Sisi ni mji ulio miongoni mwa miji yenye nguvu na aminifu sana katika Israeli. Mnataka kuharibu mji ambao ni mama katika Israeli. Kwa nini unataka kuumeza urithi wa Yahwe?”
20 Yoabu akajibu, “Hilo liwe mbali nami. Hilo liwe mbali nami kumeza au kuharibu.
Ndipo Yoabu alipojibu na kusema, “Iwe mbali, iwe mbali nami, hata nikameze au kuharibu.
21 Hivyo sivyo ilivyo. Mtu mmoja jina lake Sheba mwana wa Bikri, kutoka nchi ya vilima vya Efraimu, ameinua mkono wake dhidi ya mfalme, dhidi ya Daudi. Nikabidhini mtu huyu mmoja, nami nitajiondoa katika mji huu.” Huyu mwanamke akamwambia Yoabu, “Kichwa chake mtatupiwa kupitia juu ya ukuta.”
Hiyo si kweli. Lakini mtu kutoka katika nchi ya milima ya Efraimu, aitwaye Sheba mwana wa Bikri, ameinua mkono wake kinyume cha mfalme, kinyume cha Daudi. Mtoeni yeye nami nitauacha mji.” Mwanamke akamwambia Yoabu, “Utarushiwa kichwa chake kutoka juu ya ukuta.”
22 Ndipo huyo mwanamke akaenda kwa watu wote akiwa na ushauri wake wa busara, nao wakakata kichwa cha Sheba mwana wa Bikri na kumtupia Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akapiga tarumbeta, na watu wake wakatawanyika kutoka mjini, kila mmoja akirejea nyumbani kwake. Naye Yoabu akarudi kwa mfalme huko Yerusalemu.
Kisha mwanamke akawaendea watu wote wa mji kwa hekima yake. Wakakiondoa kichwa cha Sheba mwana wa Bikri na kumrushia Yoabu. Ndipo alipopiga tarumbeta na watu wa Yoabu wakauacha mji kila mtu nyumbani kwake. Na Yoabu akarejea Yerusalemu kwa mfalme.
23 Yoabu alikuwa jemadari wa jeshi lote la Israeli; Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi;
Yoabu alikuwa juu ya jeshi lote la Israeli na Benaya mwana wa Yehoiada alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi.
24 Adoramu alikuwa kiongozi wa wale waliofanya kazi ya kulazimishwa; Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mweka kumbukumbu;
Adoramu alikuwa juu ya watu waliofanya kazi ya shokoa na Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mkumbushaji.
25 Sheva alikuwa mwandishi; Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani;
Sheva alikuwa mwandishi, na Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani.
26 na Ira, Myairi, alikuwa kuhani wa Daudi.
Ira wa Yairi alikuwa mhudumu mkuu wa Daudi.

< 2 Samweli 20 >