< 2 Samweli 2 >
1 Ikawa baada ya mambo haya, Daudi akamuuliza Bwana, “Je, nipande kwenda katika mojawapo ya miji ya Yuda?” Bwana akasema, “Panda.” Daudi akauliza, “Je, niende wapi?” Bwana akajibu, “Nenda Hebroni.”
Ikawa baada ya haya Daudi akamuuliza Yahwe, “Je naweza kuupandia mmojawapo wa miji ya Yuda?” Yahweh akamjibu, “Panda.” Daudi akauliza, “Niuendee mji upi? Yahwe akajibu, “Hebroni”
2 Basi Daudi akakwea kwenda huko pamoja na wake zake wawili, Ahinoamu wa Yezreeli na Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli.
Hivyo Daudi akakwea pamoja na wake zake wawili, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili wa Karmeli, mjane wa Nabali.
3 Pia Daudi akawachukua watu waliokuwa pamoja naye, kila mmoja na jamaa yake, nao wakaishi huko Hebroni na miji yake.
Daudi akawaleta watu waliokuwa pamoja naye, na kila mmoja akaleta familia yake katika mji wa Hebroni walipoanza kuishi.
4 Ndipo watu wa Yuda wakaja Hebroni, huko wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya nyumba ya Yuda. Daudi alipoambiwa kuwa ni watu wa Yabeshi-Gileadi waliomzika Sauli,
Kisha watu wa Yuda wakaja na kumtia Daudi mafuta kuwa mfalme juu ya nyumba ya Yuda. Wakamwambia Daudi, “Watu wa Yabeshi Gileadi wamemzika Sauli.”
5 akatuma wajumbe kwa watu wa Yabeshi-Gileadi kuwaambia, “Bwana awabariki kwa kuonyesha wema huu kwa kumzika Sauli bwana wenu.
Hivyo Daudi akatuma wajumbe kwa watu wa Yabeshi Gileadi akawambia, “Mbarikiwe na Yahwe, kwa kuwa mmeonesha utiifu huu kwa bwana wenu Sauli mliyemzika.
6 Sasa Bwana na awaonyeshe wema na uaminifu, nami pia nitawaonyesha wema ule ule kwa kuwa mmefanya jambo hili.
Sasa Yahwe awadhihirishie utiifu na uaminifu wa kiagano. Nami pia nitawaonesha wema kwa sababu ya yale mliyoyafanya.
7 Sasa basi, kuweni hodari na mashujaa, kwa maana bwana wenu Sauli amekufa, nayo nyumba ya Yuda imenitia mafuta niwe mfalme juu yao.”
Sasa basi, mikono yenu itiwe nguvu; mwe jasiri kwa maana Sauli bwana wenu amekufa, na nyumba yote ya Yuda imenitia mafuta niwe mfalime wao.
8 Wakati huo Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Sauli, alikuwa amemchukua Ish-Boshethi mwana wa Sauli na kumleta hadi Mahanaimu.
Lakini Abneri mwana wa Neri, mkuu wa jeshi la Sauli, akamchukuwa Ishboshethi mwana wa Sauli akamleta Mahanaimu.
9 Akamweka awe mfalme juu ya nchi ya Gileadi, Waasheri, Yezreeli, Efraimu, Benyamini na Israeli yote.
Akamfanya Ishboshethi mfalme juu ya Gileadi, Asheri, Yezreeli, Efraimu, Benjamini na juu ya Israeli yote.
10 Ish-Boshethi mwana wa Sauli alikuwa na umri wa miaka arobaini alipoanza kutawala Israeli, naye akatawala miaka miwili. Hata hivyo, nyumba ya Yuda ikamfuata Daudi.
Ishiboshethi mwana wa Sauli alikuwa na umri wa miaka arobaini alipoanza kutawala juu ya Israeli, akatawala miaka miwili. Lakini nyumba ya Yuda ikaambatana na Daudi.
11 Muda ambao Daudi alikuwa mfalme juu ya nyumba ya Yuda huko Hebroni ilikuwa miaka saba na miezi sita.
Muda ambao Daudi alikuwa mfalme juu ya nyumba ya Yuda huko Hebroni ni miaka saba na miezi sita.
12 Abneri mwana wa Neri, pamoja na watu wa Ish-Boshethi mwana wa Sauli, wakatoka Mahanaimu kwenda Gibeoni.
Abneri mwana wa Neri na watumishi wa Ishboshethi mwana wa Sauli walitoka Mahanaimu kwenda Gibeoni.
13 Yoabu mwana wa Seruya na watu wa Daudi wakatoka na kukutana nao kwenye bwawa la Gibeoni. Kikundi kimoja kiliketi upande mmoja wa bwawa, na kikundi kingine upande wa pili.
Yoabu mwana wa Seruya na watumishi wa Daudi wakatoka na kukutana nao katika bwawa la Gibeoni. Wakakaa pale, kundi moja upande huu wa bwawa na kundi lingine upande wa pili.
14 Ndipo Abneri akamwambia Yoabu, “Tuwaweke baadhi ya vijana wasimame na wapigane ana kwa ana mbele yetu.” Yoabu akasema, “Sawa, na wafanye hivyo.”
Abneri akamwambia Yoabu, “haya, vijana na wainuke na kushindana mbele yetu.” Yoabu akajibu, “haya na wainuke.”
15 Kwa hiyo vijana wakasimama, wakahesabiwa: watu wa Benyamini na wa Ish-Boshethi mwana wa Sauli kumi na wawili, na upande wa Daudi kumi na wawili.
Ndipo vijana walipoinuka na kukutana, kumi na wawili kwa ajili ya Banjamini na Ishboshethi mwana wa Sauli, na kumi na wawili kutoka kwa watumishi wa Daudi.
16 Kisha kila mtu akakamatana na mpinzani wake kichwani na kuchomana kwa upanga, nao wakaanguka chini pamoja. Kwa hiyo mahali pale katika Gibeoni pakaitwa Helkath-Hasurimu.
Kila mtu akakamata kichwa cha adui yake na kupiga upanga wake katika ubavu wa adui yake, wakaanguka chini pamoja. Kwa hiyo mahali pale pakaitwa kwa Kiebrania, “Helkath Hazzurim,” yaani “konde la upanga,” lililopo Gibeoni.
17 Siku hiyo vita vilikuwa vikali sana, naye Abneri na watu wa Israeli wakashindwa na watu wa Daudi.
Vita ikawa kali sana siku ile na Abneri na watu wa Israeli wakashindwa na watumishi wa Daudi.
18 Wana watatu wa Seruya walikuwako huko: nao ni Yoabu, Abishai na Asaheli. Basi huyo Asaheli alikuwa na mbio kama paa.
Wana watatu wa Seruya walikuwepo pale: Yoabu, Abishai na Asaheli.
19 Asaheli akamfukuza Abneri, pasipo kugeuka kulia wala kushoto wakati akimfuata.
Asaheli alikuwa mwepesi miguuni kama paa. Akamfuatilia Abneri kwa karibu bila kugeuka upande wowote.
20 Abneri akaangalia nyuma na kumuuliza, “Ni wewe, Asaheli?” Akamjibu, “Ndiyo.”
Abneri akaangalia nyuma yake na kusema, “Ni wewe Asaheli?” Akajibu, “ni mimi.”
21 Ndipo Abneri akamwambia, “Geuka upande wa kulia au kushoto. Mchukue mmoja wa vijana wa kiume na umvue silaha zake.” Lakini Asaheli hakuacha kumfukuza.
Abneri akamwambia, “Geuka upande wako wa kuria au kushoto umshike mmojawapo wa vijana na kuchukua silaha yake.” Lakini Asaheli hakugeuka.
22 Abneri akamwonya tena Asaheli akimwambia, “Acha kunifukuza! Kwa nini nikuue? Je, nitawezaje kumtazama ndugu yako Yoabu usoni?”
Ndipo Abneri alipomwambia tena Asaheli, “Simama usinifuate. Kwa nini nikupige hata chini? Nitautazamaje uso wa Yoabu ndugu yako?”
23 Lakini Asaheli alikataa kuacha kumfuatia, kwa hiyo Abneri akamchoma Asaheli tumboni kwa ncha butu ya mkuki wake, mkuki ukamtoboa ukatokea mgongoni mwake. Akaanguka na kufa papo hapo. Ikawa kila mtu alisimama alipofika mahali pale Asaheli alipoanguka na kufa.
Lakini Asaheli hakukubari kugeuka. na hivyo Abneri akamchoma kwa nchi ya mkuki wake, hata ukatokea upande wa pili. Asaheli akaanguka chini akafa. Hata ikawa kila mmoja aliyefika mahali pale Asaheli alipoanguka na kufa, alisimama hapo hapo.
24 Lakini Yoabu na Abishai walimfuata Abneri, na jua lilipokuwa linatua, wakafika kwenye kilima cha Ama, karibu na Gia kwenye njia ya kuelekea kwenye nyika ya Gibeoni.
Lakini Yoabu na Abishai wakamfuatilia Abneri. Wakati jua linazama walikuwa wamefika mlima wa Amma, uliopo karibu na Gia katika njia ielekeayo nyika ya Gibeoni.
25 Ndipo watu wa kabila la Benyamini wakakusanyika tena nyuma ya Abneri. Wakaunda kikosi na kujiimarisha juu ya kilima.
Wabenjamini wakajikusanya nyuma ya Abneri na kusimama juu ya kilima.
26 Abneri akamwita Yoabu, akamwambia, “Je, ni lazima upanga uendelee kuangamiza milele? Hutambui kwamba jambo hili litaishia katika uchungu? Utaacha kuwaagiza watu wako waache kuwafuatilia ndugu zao hata lini?”
Kisha Abneri akamwita Yoabu na kusema, “Je ni lazima upanga uendelee kurarua daima? Je haujui kwamba mwisho wake utakuwa mchungu? Hata line ndipo uwaambie watu wako waache kuwafuatia ndugu zao?”
27 Yoabu akajibu, “Hakika kama aishivyo Mungu, kama hukusema, hawa watu wangeendelea kuwafuatia ndugu zao mpaka asubuhi.”
Yoabu akajibu, “Kama Mungu aishivyo, usingesema hivyo, askari wangu wangewafuatia ndugu zao hata asubuhi!”
28 Basi Yoabu akapiga tarumbeta, nao watu wote wakasimama, hawakuwafuata Israeli tena, wala hawakuwapiga tena.
Ndipo Yoabu akapiga tarumbeta, na watu wake wote wakasimama na hawakuendelea kuwafuata Israeli tena wala hawakupigana tena.
29 Usiku ule wote Abneri na watu wake wakatembea kupitia Araba. Wakavuka Mto Yordani, wakaendelea wakipitia nchi yote ya Bithroni wakafika Mahanaimu.
Abneri na watu wake wakasafiri usiku wote kupitia Araba. Wakavuka Yordani, wakatembea asubuhi yote iliyofuata, na hata wakafika Mahanaimu.
30 Basi Yoabu akarudi kutoka kumfuatia Abneri, na kuwakusanya watu wake wote. Pamoja na Asaheli, watu kumi na tisa wa Daudi walikuwa wamepotea.
Yoabu akarudi kutoka katika kumfuatia Abneri. Akawakusanya watu wake wote, ambopo Asahali na askari wengine kumi na tisa wa Daudi walipungua.
31 Lakini watu wa Daudi walikuwa wamewaua watu wa kabila la Benyamini 360 waliokuwa pamoja na Abneri.
Lakini watu wa Daudi walikuwa wameua watu 360 wa Benjamini na Abneri.
32 Wakamchukua Asaheli, wakamzika katika kaburi la baba yake huko Bethlehemu. Kisha Yoabu na watu wake wakatembea usiku kucha na kufika huko Hebroni wakati wa mapambazuko.
Kisha wakamchukua Asahali na kumzika katika kaburi la baba yake, lililokuwapo Bethlehemu. Yoabu na watu wake wakasafiri usiku wote, kukacha wakati wanafika Hebroni.