< 2 Samweli 14 >

1 Yoabu mwana wa Seruya akafahamu kuwa moyo wa mfalme ulikuwa na shauku ya kumwona Absalomu.
Yoabu mwana wa Seruya akatambua kwamba moyo wa mfalme ulitamani kumwona Absalomu.
2 Kwa hiyo Yoabu akamtuma mtu fulani kwenda Tekoa na kumleta mwanamke mwenye hekima kutoka huko. Akamwambia huyo mwanamke, “Jifanye uko katika maombolezo. Vaa nguo za kuomboleza, nawe usitumie mafuta yoyote ya uzuri, jifanye kama mwanamke ambaye amekuwa na huzuni kwa siku nyingi kwa ajili ya kufiwa.
Hivyo Yoabu akatuma neno huko Tekoa kumleta kwake mwanamke mwelevu. Akamwambia, “Tafadhari, vaa mavazi ya uombolezaji ujifanye kuwa mwombolezaji. Usijipake mafuta, lakini uwe kama mwanamke ambaye ameomboleza kwa muda mrefu kwa ajili yake aliyekufa.
3 Kisha nenda kwa mfalme ukazungumze maneno haya.” Naye Yoabu akaweka maneno kinywani mwa yule mwanamke.
Kisha ingia kwa mfalme na umwambiye maneno nitakayokueleza.” Hivyo Yoabu akamwambia maneno ambayo angeyasema kwa mfalme.
4 Huyo huyo mwanamke kutoka Tekoa alipofika kwa mfalme, akaanguka kifudifudi kumpa mfalme heshima, akasema, “Ee mfalme, nisaidie!”
Wakati mwanamke kutoka Tekoa alipoongea na mfalme, aliinamisha uso wake chini na kusema,
5 Mfalme akamuuliza, “Una shida gani?” Akamwambia, “Mimi ni mjane hasa, mume wangu amekufa.
“Mfalme, anisaidie.” Mfalme akamwambia, “Shida yako ni nini?” Akajibu, Ukweli ni kwamba mimi ni mjane, mme wangu alikufa.
6 Mimi mtumishi wako nilikuwa na wana wawili. Wakapigana wao kwa wao huko shambani wala huko hapakuwa na mtu hata mmoja wa kuwaamua. Mmoja akampiga mwenzake na kumuua.
Mimi, mtumishi wako, nilikuwa na wana wawili, wakagombana shambani, na hakukuwa na wa kuwaachanisha. Mmoja wao akampiga mwenziwe na kumwua.
7 Sasa ukoo wote umeinuka dhidi ya mtumishi wako, wakisema, ‘Utukabidhi huyo aliyemuua ndugu yake, ili tumuue kwa ajili ya uhai wa ndugu yake ambaye alimuua, nasi hapo tutakuwa tumekatilia mbali na mrithi pia.’ Wakifanya hivyo, watakuwa wamezima tumaini langu lililobaki, mume wangu hataachiwa jina wala mzao katika uso wa dunia.”
Na sasa ukoo wote umeinuka juu ya mtumishi wako, wanasema, 'Mtoe aliyempiga nduguye, ili tumwue kulipe uhai wa nduguye aliyeuawa.' Na hivyo watamwangamiza mrithi. Hivyo watalizima kaa liwakalo nililobakiwa, hata kumwondolea mme wangu jina na mzao juu ya uso wa nchi.”
8 Mfalme akamwambia huyo mwanamke, “Nenda nyumbani, nami nitatoa agizo kwa ajili yako.”
Hivyo mfalme akamwambia mwanamke, “Nenda nyumbani kwako, nami nitaagiza jambo la kukufanyia.”
9 Lakini huyo mwanamke kutoka Tekoa akamwambia, “Mfalme bwana wangu, lawama na iwe juu yangu na juu ya nyumba ya baba yangu, naye mfalme na kiti chake cha enzi na asiwe na hatia.”
Mwanamke kutoka Tekoa akamjibu mfalme, “Bwana wangu mfalme, hatia na iwe juu yangu na juu ya familia ya baba yangu. Mfalme na kiti chake cha enzi hawana hatia.”
10 Mfalme akajibu, “Ikiwa mtu yeyote atakusemesha lolote, mlete kwangu, naye hatakusumbua tena.”
Mfalme akasema, “Yeyote atakayekwambia neno umlete kwangu, naye hatakugusa tena.”
11 Huyo mwanamke akasema, “Basi mfalme na amwombe Bwana Mungu wake ili kuzuia mlipiza kisasi cha damu kuongeza juu ya uharibifu, ili kwamba mwanangu asije akaangamizwa.” Mfalme akasema, “Hakika kama aishivyo Bwana, hakuna unywele mmoja wa kichwa cha mwanao utakaoanguka chini.”
Kisha mwanamke akasema, “Tafadhari mfalme amkumbuke Yahwe Mungu wake, ili kwamba mlipa kisasi cha damu asiaribu zaidi, ili kwamba wasimwangamize mwanangu.” Mfalme akajibu, “Kama Mungu aishivyo, hakuna hata unywele mmoja wa mwanao utaanguka chini.”
12 Ndipo huyo mwanamke akasema, “Mruhusu mtumishi wako aseme neno kwa mfalme bwana wangu.” Mfalme akajibu, “Sema.”
Kisha mwanamke akasema, “Tafadhari acha mtumishi wako anene neno moja zaidi kwa bwana wangu mfalme.” Akasema, “Sema.”
13 Huyo mwanamke akasema, “Mbona basi wewe umewaza jambo kama hili dhidi ya watu wa Mungu? Je, mfalme asemapo hili, hajitii hatiani mwenyewe, kwa maana mfalme hajamrudisha mwanawe aliyefukuziwa mbali?
Hivyo mwanamke akasema, “Kwa nini basi umetenda kwa hila dhidi ya watu Mungu? Maana kwa kusema hivi, mfalme ni kama mtu mwenye hatia, kwa kuwa mfalme hamjamrudisha tena mwanaye aliyeondoka.
14 Kama vile maji yaliyomwagika ardhini, yasivyoweza kuzoleka tena, hivyo sisi kufa ni lazima. Lakini Mungu haondoi uhai, badala yake, yeye hufanya njia ili kwamba aliyefukuzwa asibaki akiwa amefarikishwa naye.
Kwa maana sisi sote tutakufa, kwa kuwa tu kama maji yamwagwayo juu ya ardhi na kwamba hayawezi kukusanywa tena. Lakini Mungu hatachukua uhai; badala yake, utafuta njia kwa walio mbali kurejeshwa.
15 “Nami sasa nimekuja kusema hili kwa bwana wangu mfalme kwa sababu watu wameniogopesha. Mtumishi wako alifikiri, ‘Nitanena na mfalme, labda mfalme atamfanyia mtumishi wake kile anachoomba.
Sasa basi, nimesema jambo hili kwa bwana wangu mfalme, kwa sababu watu wamenitisha. Hivyo mtumishi wako akajinenea nafsini mwake, 'Sasa nitaongea na mfalme. Huenda mfalme akampa mtumishi wake haja yake.
16 Labda mfalme atakubali kumwokoa mtumishi wake kutoka mkononi mwa mtu anayejaribu kunikatilia mbali, mimi na mwanangu, kutoka kwenye urithi Mungu aliotupatia.’
Kwa maana mfalme atanisikiliza, ili kwamba kumtoa mtumishi wake katika mikono ya mtu ambaye angeniangamiza mimi na mwanangu pamoja, tutoke katika urithi wa Mungu.
17 “Basi sasa mtumishi wako anasema, ‘Neno la bwana wangu mfalme na linipatie pumziko, kwa maana bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu katika kutambua jema na baya. Bwana Mungu wako na awe pamoja nawe.’”
Kisha mtumishi wako akaomba, 'Yahwe, tafadhari ruhusu neno la bwana wangu mfalme linipe msaada, kwa maana bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu kwa kutofautisha wema na ubaya.' Yahwe, Mungu na awe pamoja nawe.”
18 Basi mfalme akamwambia huyo mwanamke, “Usinifiche jibu kuhusu hilo nitakalokuuliza.” Huyo mwanamke akasema, “Mfalme bwana wangu na aseme.”
Ndipo mfalme akajibu na kumwambia yule mwanamke, Tafadhari usinifiche neno lolote nikuulizalo.” Mwanamke akajibu, “Basi bwana wangu mfalme na aseme sasa.
19 Mfalme akauliza, “Je, mkono wa Yoabu haupo pamoja nawe katika jambo hilo lote?” Huyo mwanamke akajibu, “Hakika kama uishivyo, bwana wangu mfalme, hakuna yeyote anayeweza kugeuka kulia wala kushoto kutokana na chochote anachosema bwana wangu mfalme. Naam, ni mtumishi wako Yoabu ndiye alinifundisha kufanya hivi, naye ndiye aliweka maneno haya yote kinywani mwa mtumishi wako.
Mfalme akasema, Je siyo mkono wa Yoabu ulio pamoja nawe katika haya yote? Mwanamke akajibu na kusema, “Kama uishivyo bwana wangu mfalme, hakuna awezae kuelekea mkono wa kulia wala wa kushoto kwa yale bwana wangu mfalme aliyosema. Ni mtumishi wako Yoabu aliyeniambia na kuniagiza kusema kile mtumishi wako alichokisema.
20 Mtumishi wako Yoabu amefanya hivi ili kubadili hali iliyopo. Bwana wangu ana hekima kama ile ya malaika wa Mungu, hufahamu kila kitu kinachotokea katika nchi.”
Mtumishi wako Yoabu amefanya hivi ili kubadilisha hali ya kile kinachotendeka. Bwana wangu ni mwenye akili kama hekima ya malaika wa Mungu, ajuaye yote yatendekayo ndani ya nchi.”
21 Mfalme akamwambia Yoabu, “Vyema sana, nitalifanya jambo hili. Nenda, ukamlete kijana Absalomu.”
Hivyo mfalme akamwambia Yoabu, “Tazama, nitatenda jambo hili. Nenda na umrudishe huyo kijana Absalomu.”
22 Yoabu akaanguka kifudifudi mpaka ardhini kumpa mfalme heshima, naye akambariki mfalme. Yoabu akasema, “Leo mtumishi wako anajua kuwa amepata kibali machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa sababu mfalme amemjalia mtumishi wake ombi lake.”
HivyoYoabu akainamisha uso wake chini juu ya ardhi katika heshima na shukurani kwa mfalme. Yoabu akasema, “Mtumishi wako amejua kwamba amepata neema mbele zako, bwana wangu, mfalme, kwa vile mfalme amempa mtumishi wake haja ya moyo wake.
23 Ndipo Yoabu akaenda hadi Geshuri akamrudisha Absalomu Yerusalemu.
Hivyo Yoabu akainuka na kwenda Geshuri, akamrejesha Absalomu Yerusalemu tena.
24 Lakini mfalme akasema, “Lazima Absalomu aende kwenye nyumba yake mwenyewe; kamwe asiuone uso wangu.” Kwa hiyo Absalomu akaenda kwenye nyumba yake na hakuuona uso wa mfalme.
Mfalme akasema, “Na arudi nyumbani kwake, lakini hasinione uso wangu.” Hivyo Absalomu akarudi katika nyumba yake mwenyewe, na hakuweza kuuona uso wa mfalme.
25 Katika Israeli yote hakuna mtu yeyote aliyesifiwa kwa uzuri wa sura kama Absalomu. Kuanzia utosi wa kichwa chake hadi wayo wa mguu wake hapakuwa na kasoro.
Hakukuwa na mtu katika Israeli aliyesifiwa kwa uzuri kama Absalomu. Kutoka katika wayo wa mguu wake hadi katika utosi wake hakuwa na waa lolote.
26 Kila mara aliponyoa nywele za kichwa chake, kwa kuwa alikuwa akinyoa mara kwa mara zilipokuwa zinamwia nzito, alizipima uzito wake ulikuwa shekeli mia mbili kwa kipimo cha kifalme.
Alipokata nywele za kichwa chake mwishoni mwa kila mwaka, kwa sababu zilikuwa nzito juu yake, alipima nywele zake zaidi ya shekeli mia mbili, kwa kiwango cha kipimo cha mfalme.
27 Walizaliwa wana watatu na binti mmoja kwa Absalomu. Jina la binti yake aliitwa Tamari, naye akawa mwanamke mzuri wa sura.
Kwake Absalomu walizaliwa wana watatu na binti mmoja, jina lake Tamari. Alikuwa mwanamke mzuri.
28 Absalomu akaishi miaka miwili huko Yerusalemu pasipo kuuona uso wa mfalme.
Absalomu akaishi Yerusalem miaka miwili pasipo kuona uso wa mfalme.
29 Basi Absalomu akamwita Yoabu kwa kusudi la kumtuma kwa mfalme, lakini Yoabu akakataa kuja kwa Absalomu. Ndipo akamwita tena mara ya pili, lakini pia akakataa kuja.
Kisha Absalome akatuma neno kwa Yoabu ili ampeleke kwa mfalme, lakini Yoabu hakwenda kwake. Hivyo Absalomu akatuma neno mara ya pili, lakini Yoabu hakuja bado.
30 Ndipo akawaambia watumishi wake, “Tazama, shamba la Yoabu liko jirani na langu, naye ana shayiri humo. Nendeni mkalitie moto.” Kisha watumishi wa Absalomu wakalitia moto shamba hilo.
Hivyo Absalomu akawambia watumishi wake, “Tazameni, shamba la Yoabu lipo karibu na langu, naye ana shayiri kule. Nendeni mkalichome moto” Hivyo watumishi wa Absalome wakalichoma moto lile shamba.
31 Basi Yoabu akaenda nyumbani kwa Absalomu, akamwambia, “Kwa nini watumishi wako wametia moto shamba langu?”
Kisha Yoabu akainuka na kwenda nyumbani kwa Absalomu akamwambia, “Kwa nini watumishi wako wamelichoma moto shamba langu?
32 Absalomu akamwambia Yoabu, “Tazama, nilikutumia ujumbe na kusema, ‘Njoo ili niweze kukutuma kwa mfalme kuuliza, “Kwa nini nimekuja kutoka Geshuri? Ingekuwa bora zaidi kwangu kama ningebaki huko!”’ Sasa basi, nataka kuuona uso wa mfalme, na ikiwa nina hatia ya jambo lolote, basi na aniue.”
Absalomu akamjibu Yoabu, “Tazama nilituma neno kwako kusema, 'Njoo ili nikutume kwa mfalme kusema, “Kwa nini nilikuja kutoka Geshuri? Ingekuwa heri kwangu kama ningesalia huko. Kwa hiyo sasa niache niuone uso wa mfalme na kama nina hatia basi na aniue.”
33 Basi Yoabu akaenda kwa mfalme na kumwambia jambo hili. Kisha mfalme akamwita Absalomu, naye akaingia ndani akasujudu uso wake mpaka ardhini mbele ya mfalme. Naye mfalme akambusu Absalomu.
Hivyo Yoabu akaenda kwa mfalme na kumwambia. Mfalme alipomwita, Absalomu alikuja kwa mfalme na akainama hadi juu ya uso nchi mbele ya mfalme na mfalme akambusu Absalomu.

< 2 Samweli 14 >