< 2 Samweli 14 >
1 Yoabu mwana wa Seruya akafahamu kuwa moyo wa mfalme ulikuwa na shauku ya kumwona Absalomu.
2 Kwa hiyo Yoabu akamtuma mtu fulani kwenda Tekoa na kumleta mwanamke mwenye hekima kutoka huko. Akamwambia huyo mwanamke, “Jifanye uko katika maombolezo. Vaa nguo za kuomboleza, nawe usitumie mafuta yoyote ya uzuri, jifanye kama mwanamke ambaye amekuwa na huzuni kwa siku nyingi kwa ajili ya kufiwa.
3 Kisha nenda kwa mfalme ukazungumze maneno haya.” Naye Yoabu akaweka maneno kinywani mwa yule mwanamke.
4 Huyo huyo mwanamke kutoka Tekoa alipofika kwa mfalme, akaanguka kifudifudi kumpa mfalme heshima, akasema, “Ee mfalme, nisaidie!”
5 Mfalme akamuuliza, “Una shida gani?” Akamwambia, “Mimi ni mjane hasa, mume wangu amekufa.
6 Mimi mtumishi wako nilikuwa na wana wawili. Wakapigana wao kwa wao huko shambani wala huko hapakuwa na mtu hata mmoja wa kuwaamua. Mmoja akampiga mwenzake na kumuua.
7 Sasa ukoo wote umeinuka dhidi ya mtumishi wako, wakisema, ‘Utukabidhi huyo aliyemuua ndugu yake, ili tumuue kwa ajili ya uhai wa ndugu yake ambaye alimuua, nasi hapo tutakuwa tumekatilia mbali na mrithi pia.’ Wakifanya hivyo, watakuwa wamezima tumaini langu lililobaki, mume wangu hataachiwa jina wala mzao katika uso wa dunia.”
8 Mfalme akamwambia huyo mwanamke, “Nenda nyumbani, nami nitatoa agizo kwa ajili yako.”
9 Lakini huyo mwanamke kutoka Tekoa akamwambia, “Mfalme bwana wangu, lawama na iwe juu yangu na juu ya nyumba ya baba yangu, naye mfalme na kiti chake cha enzi na asiwe na hatia.”
10 Mfalme akajibu, “Ikiwa mtu yeyote atakusemesha lolote, mlete kwangu, naye hatakusumbua tena.”
11 Huyo mwanamke akasema, “Basi mfalme na amwombe Bwana Mungu wake ili kuzuia mlipiza kisasi cha damu kuongeza juu ya uharibifu, ili kwamba mwanangu asije akaangamizwa.” Mfalme akasema, “Hakika kama aishivyo Bwana, hakuna unywele mmoja wa kichwa cha mwanao utakaoanguka chini.”
12 Ndipo huyo mwanamke akasema, “Mruhusu mtumishi wako aseme neno kwa mfalme bwana wangu.” Mfalme akajibu, “Sema.”
13 Huyo mwanamke akasema, “Mbona basi wewe umewaza jambo kama hili dhidi ya watu wa Mungu? Je, mfalme asemapo hili, hajitii hatiani mwenyewe, kwa maana mfalme hajamrudisha mwanawe aliyefukuziwa mbali?
14 Kama vile maji yaliyomwagika ardhini, yasivyoweza kuzoleka tena, hivyo sisi kufa ni lazima. Lakini Mungu haondoi uhai, badala yake, yeye hufanya njia ili kwamba aliyefukuzwa asibaki akiwa amefarikishwa naye.
15 “Nami sasa nimekuja kusema hili kwa bwana wangu mfalme kwa sababu watu wameniogopesha. Mtumishi wako alifikiri, ‘Nitanena na mfalme, labda mfalme atamfanyia mtumishi wake kile anachoomba.
16 Labda mfalme atakubali kumwokoa mtumishi wake kutoka mkononi mwa mtu anayejaribu kunikatilia mbali, mimi na mwanangu, kutoka kwenye urithi Mungu aliotupatia.’
17 “Basi sasa mtumishi wako anasema, ‘Neno la bwana wangu mfalme na linipatie pumziko, kwa maana bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu katika kutambua jema na baya. Bwana Mungu wako na awe pamoja nawe.’”
18 Basi mfalme akamwambia huyo mwanamke, “Usinifiche jibu kuhusu hilo nitakalokuuliza.” Huyo mwanamke akasema, “Mfalme bwana wangu na aseme.”
19 Mfalme akauliza, “Je, mkono wa Yoabu haupo pamoja nawe katika jambo hilo lote?” Huyo mwanamke akajibu, “Hakika kama uishivyo, bwana wangu mfalme, hakuna yeyote anayeweza kugeuka kulia wala kushoto kutokana na chochote anachosema bwana wangu mfalme. Naam, ni mtumishi wako Yoabu ndiye alinifundisha kufanya hivi, naye ndiye aliweka maneno haya yote kinywani mwa mtumishi wako.
20 Mtumishi wako Yoabu amefanya hivi ili kubadili hali iliyopo. Bwana wangu ana hekima kama ile ya malaika wa Mungu, hufahamu kila kitu kinachotokea katika nchi.”
21 Mfalme akamwambia Yoabu, “Vyema sana, nitalifanya jambo hili. Nenda, ukamlete kijana Absalomu.”
22 Yoabu akaanguka kifudifudi mpaka ardhini kumpa mfalme heshima, naye akambariki mfalme. Yoabu akasema, “Leo mtumishi wako anajua kuwa amepata kibali machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa sababu mfalme amemjalia mtumishi wake ombi lake.”
23 Ndipo Yoabu akaenda hadi Geshuri akamrudisha Absalomu Yerusalemu.
24 Lakini mfalme akasema, “Lazima Absalomu aende kwenye nyumba yake mwenyewe; kamwe asiuone uso wangu.” Kwa hiyo Absalomu akaenda kwenye nyumba yake na hakuuona uso wa mfalme.
25 Katika Israeli yote hakuna mtu yeyote aliyesifiwa kwa uzuri wa sura kama Absalomu. Kuanzia utosi wa kichwa chake hadi wayo wa mguu wake hapakuwa na kasoro.
26 Kila mara aliponyoa nywele za kichwa chake, kwa kuwa alikuwa akinyoa mara kwa mara zilipokuwa zinamwia nzito, alizipima uzito wake ulikuwa shekeli mia mbili kwa kipimo cha kifalme.
27 Walizaliwa wana watatu na binti mmoja kwa Absalomu. Jina la binti yake aliitwa Tamari, naye akawa mwanamke mzuri wa sura.
28 Absalomu akaishi miaka miwili huko Yerusalemu pasipo kuuona uso wa mfalme.
29 Basi Absalomu akamwita Yoabu kwa kusudi la kumtuma kwa mfalme, lakini Yoabu akakataa kuja kwa Absalomu. Ndipo akamwita tena mara ya pili, lakini pia akakataa kuja.
30 Ndipo akawaambia watumishi wake, “Tazama, shamba la Yoabu liko jirani na langu, naye ana shayiri humo. Nendeni mkalitie moto.” Kisha watumishi wa Absalomu wakalitia moto shamba hilo.
31 Basi Yoabu akaenda nyumbani kwa Absalomu, akamwambia, “Kwa nini watumishi wako wametia moto shamba langu?”
32 Absalomu akamwambia Yoabu, “Tazama, nilikutumia ujumbe na kusema, ‘Njoo ili niweze kukutuma kwa mfalme kuuliza, “Kwa nini nimekuja kutoka Geshuri? Ingekuwa bora zaidi kwangu kama ningebaki huko!”’ Sasa basi, nataka kuuona uso wa mfalme, na ikiwa nina hatia ya jambo lolote, basi na aniue.”
33 Basi Yoabu akaenda kwa mfalme na kumwambia jambo hili. Kisha mfalme akamwita Absalomu, naye akaingia ndani akasujudu uso wake mpaka ardhini mbele ya mfalme. Naye mfalme akambusu Absalomu.