< 2 Samweli 13 >

1 Ikawa baada ya hayo, Amnoni mwana wa Daudi akampenda Tamari, umbu lake Absalomu mwana wa Daudi, ambaye alikuwa mzuri wa sura.
Ikawa baada ya hayo kwamba Amnoni mwana wa Daudi, akamtamani sana Tamari dada yake wa kambo aliyekuwa mzuri, alikuwa tumbo moja na Absalome, mwana wingine wa Daudi.
2 Amnoni akasumbuka sana kuhusu Tamari hata akaugua, kwa kuwa Tamari alikuwa bikira, na ilionekana kwamba haiwezekani Amnoni kumfanyia jambo lolote.
Amnoni akasononeka sana kiasi cha kuugua kwa ajili ya Tamari dada yake. Tamari alikuwa bikra, na hivyo ilionekana haiwezekani Amnoni kufanya neno lolote kwake.
3 Basi Amnoni alikuwa na rafiki jina lake Yonadabu mwana wa Shimea, nduguye Daudi. Yonadabu alikuwa mtu wa hila nyingi sana.
Lakini Amnoni alikuwa na rafiki jina lake Yehonadabu mwana wa Shama, nduguye Daudi.
4 Akamuuliza Amnoni, “Wewe ni mtoto wa mfalme; kwa nini siku baada ya siku unaonekana kukonda? Hutaniambia?” Amnoni akamwambia, “Ninampenda Tamari, dada yake Absalomu ndugu yangu.”
Yehonadabu alikuwa mtu mwelevu sana. Akamwambia Amnoni, “Kwa nini, mwana wa mfalme, unadhoofika kila siku? Kwa nini uniambii? Ndipo Amnoni akamjibu, “Nampenda Tamari, dada yake Absalome ndugu yangu.”
5 Yonadabu akamwambia, “Nenda ukalale kitandani na ujifanye kuwa mgonjwa. Baba yako atakapokuja kukuona mwambie, ‘Ningependa Tamari dada yangu aje kunipatia chochote ili nile. Tafadhali mruhusu aje na kuniandalia chakula mbele yangu ningali ninamwona, ili nipate kula kutoka mkononi mwake.’”
Ndipo Yehonadabu akamwambia, “Lala kitandani mwako na ujifanye kuwa mgonjwa. Wakati baba yako atakapo kuja kukuona, mwambie, Tafadhari mtume dada yangu Tamari aandaye chakula mbele yangu, ili kwamba nikione na kula kutoka mkononi mwake?”
6 Kwa hiyo Amnoni akalala kitandani kujifanya mgonjwa. Mfalme alipokuja kumwona, Amnoni akamwambia, “Ningependa dada yangu Tamari aje na kuniandalia mikate maalum mbele yangu, ili nipate kula toka mkononi mwake.”
Hivyo Amnoni akalala na kujifanya kuwa mgonjwa. Mfalme alipokuja kumwona, Amnoni akamwambia mfalme, “Tafadhari mtume Tamari dada yangu aandaye chakula kwa ajili ya ugonjwa wangu mbele yangu ili kwamba nikile kutoka mkononi mwake.
7 Daudi akampelekea Tamari ujumbe huko kwenye jumba la kifalme, kusema: “Nenda katika nyumba ya ndugu yako Amnoni ukamwandalie chakula.”
Ndipo Daudi katika kasri lake akatuma neno kwa Tamari, kusema, “Nenda katika nyumba ya nduguyo Amnoni na umwandalie chakula. Hivyo
8 Kwa hiyo Tamari akaenda nyumbani kwa nduguye Amnoni, ndugu ambaye alikuwa amelala. Tamari akachukua unga uliotiwa chachu akaukanda, akaiandaa mikate mbele yake na kuioka.
Tamari akaenda katika nyumba ya Amnoni nduguye alipokuwa amelala. Akachukua donge na kulifinyanga na kuandaa mkate mbele zake, kisha akauoka.
9 Tamari akaondoa mikate kwenye kikaango ili ampatie Amnoni, lakini akakataa kula. Amnoni akamwambia, “Mtoe nje kila mtu aliyeko hapa.” Kwa hiyo kila mmoja akaondoka.
Akachukua kikaangio na kumpa mkate, lakini akakataa kula. Kisha Amnoni akawambia waliokuwepo, “Kila mtu na aondoke.” Hivyo kila mmoja akaondoka.
10 Ndipo Amnoni akamwambia Tamari, “Leta mkate hapa ndani ya chumba changu ili nipate kula kutoka mkononi mwako.” Basi Tamari akachukua mikate aliyoiandaa na kumletea Amnoni ndugu yake ndani ya chumba chake.
Amnoni akamwambia Tamari, “Lete chakula chumbani kwangu nikile katika mkono wako.” Tamari akachukua mkate aliokuwa ameuandaa, na kuuleta katika chumba cha Amnoni kaka yake.
11 Lakini alipompelekea ili ale, akamkamata kwa nguvu na kumwambia, “Njoo ulale nami, dada yangu.”
Alipoleta chakula kwake, Amnoni akamshikilia na kumwambia, “Njoo, ulale nami, dada yangu.”
12 Akamwambia, “Usifanye hivyo, ndugu yangu! Usinitende jeuri! Jambo la namna hii halistahili kufanyika katika Israeli! Usitende jambo hili ovu.
Yeye akamjibu, “Hapana, kaka yangu, usinilazimishe, kwani hakuna jambo kama hili linapaswa kufanyika katika Israeli. Usifanye jambo la aibu kiasi hiki!
13 Kwa upande wangu je, itakuwaje? Nitaipeleka wapi aibu yangu? Pia kwa upande wako, itakuwaje? Utakuwa kama mmoja wa wapumbavu waovu katika Israeli. Tafadhali zungumza na mfalme; hatakukatalia wewe kunioa,”
Nitakwenda wapi ili nijiepushe na aibu ambayo jambo hili litaileta juu ya maisha yangu? Na tendo hili litakuonesha kuwa mpumbavu usiye na aibu katika Israeli yote. Tafadhari, ninakuomba uongee na mfalme. Yeye atakuruhusu unioe.”
14 Lakini Amnoni akakataa kumsikiliza, na kwa kuwa alikuwa na nguvu kuliko Tamari, akamtenda jeuri.
Lakini Amnoni hakuweza kumsikiliza. Kwa kuwa alikuwa zaidi akamkamata na akalala naye.
15 Kisha Amnoni akamchukia Tamari, kwa machukio makuu sana. Kwa kweli, Amnoni alimchukia kuliko alivyokuwa amempenda. Amnoni akamwambia, “Inuka na utoke nje!”
Kisha Amnoni akamchukia Tamari kwa chuki kuu. Akamchukia zaidi ya jinsi alivyokuwa amemtamani. Amnoni akamwambia, “Inuka na uondoke.”
16 Tamari akamwambia, “Hapana! Kunifukuza itakuwa vibaya zaidi kuliko yale uliyonitendea.” Lakini Amnoni akakataa kumsikiliza.
Lakini yeye akamjibu, “Hapana! kwa maana uovu wa kunifanya ni uondoke ni mbaya zaidi ya kile ulichonitenda!” Lakini Amnoni hakumsikiliza.
17 Akamwita mtumishi wake mahsusi na kumwambia, “Mtoe huyu mwanamke hapa na ufunge mlango nyuma yake.”
Badala yake, akamwita mtumishi wake na akasema, “Mwondoe mwanamke huyu mbele yangu, na uufunge mlango nyuma yake.”
18 Kwa hiyo, mtumishi wake akamtoa nje na kufunga mlango nyuma yake. Tamari alikuwa amevaa joho lililopambwa vizuri, kwa maana lilikuwa aina ya mavazi yaliyovaliwa na binti za mfalme waliokuwa mabikira.
Hivyo mtumishi wake akamtoa na kufunga mlango. Tamari alikuwa amevaa vazi lilinakishiwa kwani ndivyo binti za wafalme waliobikra valivyokuwa wakivaa.
19 Tamari akajitia majivu kichwani mwake na kurarua lile joho alilokuwa amevaa. Akaweka mkono wake kichwani, akaenda zake akilia kwa sauti.
Tamari akaweka majivu juu ya kichwa chake na akalirarua vazi lake
20 Absalomu nduguye akamuuliza, “Je, huyo Amnoni ndugu yako, amekutana nawe kimwili? Sasa nyamaza umbu langu, yeye ni ndugu yako. Usilitie jambo hili moyoni.” Naye Tamari akaishi nyumbani kwa Absalomu nduguye, akiwa mwanamke mwenye huzuni.
Absalome, kaka yake, akamwambia, “Amnoni, kaka yako, amekuwa nawe? Lakini sasa nyamaza, dada yangu. Yeye ni kaka yako. Usiliweke hili moyoni.” Hivyo Tamari akakaa peke yake katika nyumba ya Absalomu kaka yake.
21 Mfalme Daudi aliposikia mambo haya yote, akakasirika sana.
Mfalme Daudi aliposikia haya yote, alikasirika sana.
22 Absalomu hakusema neno lolote na Amnoni, likiwa zuri au baya, kwa kuwa alimchukia Amnoni kwa sababu alikuwa amemtia aibu Tamari, dada yake.
Absalome hakusema chochote kwa Amnoni, kwa maana Absalome alimchukia kwa kile alichokifanya, kumdhalilisha Tamari, dada yake.
23 Miaka miwili baadaye, wakati wakata manyoya ya kondoo wa Absalomu walipokuwa huko Baal-Hasori karibu na mpaka wa Efraimu, alialika wana wote wa mfalme kuja huko.
Ikawa baada ya miaka miwili mizima Absalomu akawa na wakatao kondoo manyoya wakifanya kazi huko Baali Hazori, ulioko karibu na Efraim, naye Absalomu akawaarika wana wote wa mfalme kufika huko.
24 Absalomu akaenda kwa mfalme na kumwambia, “Mtumishi wako ninao wakata manyoya ya kondoo waliokuja. Tafadhali, je, mfalme na maafisa wake wanaweza kuungana nami?”
Absalomu akamwendea mfalme na kusema, “Tazama sasa, mtumishi wako anao wakatao kondoo manyoya. Tafadhari, naomba mfalme na watumishi wake waende nami, mtumishi wako.”
25 Mfalme akajibu, “La hasha, mwanangu si lazima sisi sote tuje, tutakuwa tu mzigo kwako.” Ingawa Absalomu alimsihi sana, mfalme alikataa kwenda, lakini alimbariki.
Mfalme akamjibu Absalomu, “hapana mwanangu, tusiende sisi yote kwani tutakuwa mzigo kwako.” Absalomu akamhakikishia mfalme, lakini yeye asikubali kwenda, ila alimbariki Absalomu.
26 Basi Absalomu akasema, “Kama hutakuja, tafadhali mruhusu ndugu yangu Amnoni twende pamoja naye.” Mfalme akamuuliza, “Kwa nini aende pamoja nawe?”
Kisha Absalomu akasema, “kama sivyo, basi tafadhari mwache ndugu yangu Amnoni aende nasi.” Mfalme akamuliza, “Kwa nini Amnoni aende nanyi?”
27 Lakini Absalomu alimsihi, kwa hiyo mfalme akamtuma Amnoni pamoja na wana wengine wa mfalme waliobaki.
Absalomu akamsihi Daudi, hivyo akamruhusu Amnoni na wana wengine wa mfalme kwenda naye.
28 Absalomu aliagiza watu wake, “Sikilizeni! Wakati Amnoni atakapokuwa amekunywa mvinyo na kulewa sana nami nikiwaambia, ‘Mpigeni Amnoni,’ basi muueni. Msiogope. Je, si mimi niliyewapa amri hii? Kuweni hodari na wenye ushujaa.”
Absalomu akawaamuru watumishi wake kusema, “Sikilizeni kwa makini. Amnoni atakapokuwa amelewa mvinyo, na nitakapowambia, 'Mpigeni Amnoni,' msiogope mwueni. Je siyo mimi niliyewamru? Mwe jasiri na hodari.”
29 Kwa hiyo watu wa Absalomu wakamtendea Amnoni kama vile Absalomu alivyokuwa amewaagiza. Ndipo wana wote wa mfalme wakainuka, wakapanda nyumbu zao, wakakimbia.
Hivyo watumishi wa Absalome wakamtendea Amnoni kama walivyoamriwa. Kisha wana wote wa mfalme wakainuka na kila mmoja akapanda nyumbu wake akakimbia.
30 Wakati wakiwa njiani, taarifa ilimjia Daudi, kusema: “Absalomu amewaua wana wote wa mfalme; hakuna hata mmoja aliyesalia.”
Hata ikawa wakati wakiwa njiani habari zikafika kwa Daudi kusema, “Absalomu ameua wana wote wa mfalme na hakuna hata mmoja aliyesalia.”
31 Mfalme akasimama, akararua nguo zake, akalala chini ardhini; nao watumishi wake wote wakasimama kando yake na nguo zao zikiwa zimeraruliwa.
Kisha mfalme akainuka na kurarua mavazi yake na kujilaza juu ya sakafu; watumishi wake wote wakasimama karibu naye mavazi yao yameraruriwa.
32 Lakini Yonadabu mwana wa Shimea, nduguye Daudi, akasema, “Bwana wangu asifikiri kwamba wamewaua wana wote wa mfalme; ni Amnoni peke yake ndiye alikufa. Hili limekuwa kusudi la moyo wa Absalomu tangu siku ile Amnoni alipomtendea jeuri Tamari, dada yake.
Yehonadabu mwana wa Shama, nduguye Daudi, akajibu na kusema, “Bwana wangu asidhani kuwa vijana wote ambao ni wana wa mfalme wameuawa, kwa maana ni Amnoni pekee ndiye aliyeuawa. Absalomu alilipanga jambo hili tangu siku ile Amnoni alivyomwaribu Tamari, dada yake.
33 Mfalme bwana wangu asisumbuliwe na taarifa kwamba wamewaua wana wote wa mfalme. Ni Amnoni peke yake aliyekufa.”
Kwa hiyo basi, bwana wangu mfalme asiiweke taarifa hii moyoni, kudhani kwamba wana wote wa mfalme wameuawa, kwani aliyeuawa ni Amnoni peke yake.”
34 Wakati huo, Absalomu akawa amekimbia. Basi mlinzi akaangalia, naye akaona watu wengi barabarani magharibi yake, wakishuka kutoka upande wa kilima. Mlinzi akaenda akamwambia mfalme, “Naona watu wakitokea upande wa Horonaimu, huko upande wa kilimani.”
Absalomu akakimbia. Mtumishi aliyekuwa akiangalia akainua macho yake na kuona watu wengi wakija njiani kando ya kilima upande wake wa magharibi.
35 Yonadabu akamwambia mfalme, “Tazama, wana wa mfalme wako hapa; imekuwa kama vile mtumishi wako alivyosema.”
Kisha Yehonadabu akamwambia mfalme, “Tazama, wana wa mfalme wanakuja. kama mtumishi wako alivyosema.”
36 Mara alipomaliza kusema, wana wa mfalme wakaingia ndani wakiomboleza kwa makelele. Pia mfalme na watumishi wake wote wakalia sana kwa uchungu.
Ikawa mara alipomaliza kusema wana wa mfalme wakafika, wakainua sauti zao na kulia. Na mfalme pamoja na watumishi wake wote pia wakalia kwa uchungu.
37 Absalomu akakimbia na kwenda kwa Talmai mwana wa Amihudi, mfalme wa Geshuri. Lakini Mfalme Daudi akaomboleza kwa ajili ya mwanawe kila siku.
Lakini Absalomu akakimbia na kwenda kwa Talmai mwana wa Amihudi, mfalme wa Geshuri. Mfalme akaomboleza kila siku kwa ajili ya mwanaye.
38 Baada ya Absalomu kukimbia na kwenda Geshuri, akakaa huko miaka mitatu.
Hivyo Absalomu akakimbia na kwenda Geshuri na akakaa huko kwa miaka mitatu.
39 Roho ya Mfalme Daudi ikatamani kumwendea Absalomu, kwa maana mfalme alikuwa amefarijika kuhusu kifo cha Amnoni.
Moyo wa mfalme Daudi ukatamani kwenda kumwona Absalomu, kwa maana alikuwa amefarijika kwa habari ya kifo cha Amnoni.

< 2 Samweli 13 >