< 2 Samweli 1 >
1 Baada ya kifo cha Sauli, Daudi alipokuwa amerudi kutoka kuwashinda Waamaleki, Daudi alikaa siku mbili huko Siklagi.
Baada ya kifo cha Sauli, Daud alirudi kutoka kuwashambulia Waamaleki na akakaa Siklagi kwa siku mbili.
2 Siku ya tatu akaja mtu mwenye nguo zilizoraruka na mavumbi kichwani mwake kutoka kwenye kambi ya Sauli. Alipomjia Daudi, akajitupa chini ili kumpa heshima.
Siku ya tatu, mtu mmoja alikuja kutoka kambi ya Sauli nguo zake zikiwa zimeraruliwa na akiwa na vumbi juu ya kichwa chake. Alipofika kwa Daudi alinamisha uso wake chini akajifanya yeye mwenyewe kuwa si kitu.
3 Daudi akamuuliza, “Wewe umetoka wapi?” Akamjibu, “Nimetoroka kutoka kambi ya Waisraeli.”
Daudi akamuliza, “Unatoka wapi?” Yeye akajibu, “Nimeponyoka kutoka kambi ya Israeli.”
4 Daudi akamuuliza, “Ni nini kilichotokea? Niambie.” Akasema, “Watu walikimbia kutoka vitani. Wengi wao walianguka na kufa. Naye Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa.”
Daudi akamwambia, “Tafadhari nieleze jinsi mambo yalivyokuwa.” Akajibu, “Watu walikimbia kutoka vitani. Wengi wameanguka, na wengi wao wameuawa. Sauli na Yonathani mwanawe pia wameuawa.”
5 Ndipo Daudi akamwambia huyo kijana aliyemletea taarifa, “Je, umefahamuje kwamba Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa?”
Daudi akamwuliza kijana, “unajuaje kuwa Sauli na Yonathani mwanawe wameuawa?”
6 Yule kijana akasema, “Nilijipata huko Mlima Gilboa, naye Sauli alikuwa huko akiegemea mkuki wake, na magari ya vita na wapanda farasi wa upande wa adui wakawa wamemkaribia sana.
Yule kijana akajibu, “Kwa bahati nilikuwa juu ya Mlima Gilboa, na pale alikuwepo Sauli ameegemea mkuki wake, na magari ya farasi na waongozaji walikuwa karibu kumkamata.
7 Alipogeuka na kuniona, akaniita, nami nikasema, ‘Je, nifanye nini?’
Sauli alipogeuka aliniona na akaniita. Nikajibu, 'Mimi hapa.'
8 “Akaniuliza, ‘Wewe ni nani?’ “Nikamjibu, ‘Mimi ni Mwamaleki.’
Akaniuliza, 'Wewe ni nani?' Nikamjibu, 'Mimi ni Mwamaleki,'
9 “Kisha akaniambia, ‘Nikaribie mimi na uniue! Niko katika maumivu makali ya kifo, lakini bado ningali hai.’
Akaniambia, Tafadhari simama juu yangu uniuwe, kwa kuwa shida kubwa imenipata, lakini uhai ungalimo ndani yangu.'
10 “Kwa hiyo nikamkaribia nikamuua, kwa sababu nilijua kwamba baada ya kuanguka hangeweza kupona. Nami nikachukua lile taji lililokuwa kichwani mwake na utepe uliokuwa mkononi mwake nami nimevileta hapa kwa bwana wangu.”
Hivyo nilisimama juu yake nikamuuwa, kwa maana nilijua kwamba asingeweza kuishi baada ya kuwa ameanguka. Ndipo nikachukuwa taji iliyokuwa juu ya kichwa chake na kikuku kilichokuwa mkononi mwake, na nimevileta hapa kwako, bwana wangu.”
11 Ndipo Daudi pamoja na watu wote waliokuwa pamoja naye wakazishika nguo zao na kuzirarua.
Kisha Daudi akararua mavazi yake, na watu wote waliokuwa pamoja naye wakafanya vilevile.
12 Wakaomboleza, wakalia pia na kufunga mpaka jioni kwa ajili ya Sauli na Yonathani mwanawe, kwa ajili ya jeshi la Bwana na nyumba ya Israeli, kwa sababu wameanguka kwa upanga.
Walilia, wakaomboleza na kufunga mpaka jioni kwa ajili ya Sauli, Yonathani mwanawe, watu wa Yahwe, na kwa ajili ya nyumba ya Israeli kwa maana wameanguka kwa upanga.
13 Daudi akamwambia yule kijana aliyemletea taarifa, “Wewe ni mwenyeji wa wapi?” Akamjibu, “Mimi ni mwana wa mgeni, Mwamaleki.”
Daudi akamwambia yule kijana, “Unatokea wapi?” Akajibu, mimi ni kijana wa mgeni Mwamaleki.”
14 Daudi akamuuliza, “Kwa nini hukuogopa kuinua mkono wako ili kumwangamiza mpakwa mafuta wa Bwana?”
Daudi akamwambia, “Kwa nini haukuogopa kumwua mfalme, mtiwa mafuta wa Yahwe kwa mkono wako?”
15 Kisha Daudi akamwita mmoja wa watu wake na kumwambia, “Nenda ukamuue!” Kwa hiyo akampiga, naye akafa.
Daudi akamwita mmojawapo wa vijana na akamwambia, “Nenda ukamuue.” Hivyo kijana huyo akaenda na kumpiga hata ata chini, Mwamaleki akafa.
16 Kwa maana Daudi alikuwa amemwambia, “Damu yako iwe juu ya kichwa chako mwenyewe. Kinywa chako mwenyewe kimeshuhudia dhidi yako uliposema, ‘Nilimuua mpakwa mafuta wa Bwana.’”
Ndipo Daudi akamwambia Mwamaleke aliyekufa, “Damu yako iwe juu ya kichwa chako kwa kuwa kinywa chako kimeshuhudia dhidi yako kusema, Nimemuua mfalme mtiwa mafuta wa Yahwe.
17 Daudi akafanya maombolezo haya kuhusu Sauli na Yonathani mwanawe,
Ndipo Daudi akaimba wimbo wa maombolezo juu ya Sauli na Yonathani mwanawe.
18 naye akaagiza kwamba watu wa Yuda wafundishwe ombolezo hili la upinde (ambalo limeandikwa katika Kitabu cha Yashari):
Akawaamuru watu kuufundisha wimbo wa Bow kwa wana wa Yuda, ambao umeandikwa katika Kitabu cha Yashari.
19 “Walio fahari yako, ee Israeli, wameuawa juu ya mahali pako palipoinuka. Jinsi wenye nguvu walivyoanguka!
“Utukufu wako, Israel, umeondolewa, umeondolewa juu ya mahali pako pa juu! Jinsi mwenye nguvu alivyoanguka!
20 “Msilisimulie hili katika Gathi, msilitangaze hili katika barabara za Ashkeloni, binti za Wafilisti wasije wakafurahia, binti za hao wasiotahiriwa wasije wakashangilia.
Msiiseme katika Gathi, msiitangaze katika mitaa ya Ashikeloni, ili binti za wafilisti wasifurahi, ili binti za wasiotailiwa wasisherehekee.
21 “Enyi milima ya Gilboa, msipate umande wala mvua, wala mashamba yazaayo sadaka ya nafaka. Kwa maana huko ndiko ngao ya mwenye nguvu iliponajisiwa, ngao ya Sauli haitapakwa tena mafuta.
Milima ya Gilboa, kusiwe na umande au mvua juu yenu. wala mashamba yasitoe nafaka kwa ajili ya sadaka, kwa maana hapo ngao ya mwenye nguvu imeharibiwa. Ngao ya Sauli haiwezi tena kutiwa mafuta.
22 Kutokana na damu ya waliouawa, kutokana na miili ya wenye nguvu, ule upinde wa Yonathani haukugeuka nyuma. Upanga wa Sauli haukurudi bure.
Kutoka katika damu ya waliouawa, kutoka katika miili ya wenye nguvu, upinde wa Yonathani haukurudi nyuma, na upanga wa Sauli haukurudi patupu.
23 “Sauli na Yonathani, maishani walipendwa na kuneemeka, na katika kifo hawakutengana. Walikuwa wepesi kuliko tai, walikuwa na nguvu kuliko simba.
Sauli na Yonathani walikuwa wakipendwa na walikuwa wenye neema maishani, hata wakati wa mauti yao walikuwa pamoja. Walikuwa na kasi kuliko tai, walikuwa na nguvu kuliko simba.
24 “Enyi binti za Israeli, lieni kwa ajili ya Sauli, ambaye aliwavika nguo nyekundu na maridadi, ambaye aliremba mavazi yenu kwa mapambo ya dhahabu.
Enyi binti wa Israeli lieni juu ya Sauli, aliyewavika mavazi ya thamani pamoja na vito vya thamani, na aliyetia mapambo ya dhahabu katika mavazi yenu.
25 “Tazama jinsi mashujaa walivyoanguka vitani! Yonathani ameuawa mahali pako palipoinuka.
Jinsi wenye nguvu walivyoanguka vitani! Yonathani ameuawa juu ya mahali pako pa juu.
26 Nahuzunika kwa ajili yako, Yonathani ndugu yangu, kwangu ulikuwa mpendwa sana. Upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, wa ajabu zaidi kuliko ule wa wanawake.
Nimesikitishwa sana kwa ajili yako, Yonathani ndugu yangu. Ulikuwa mpendwa wangu sana. Upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, ukipita upendo wa wanawake.
27 “Tazama jinsi mashujaa walivyoanguka! Silaha za vita zimeangamia!”
Jinsi wenye nguvu walivyoanguka na silaha za vita zimeteketea!”