< 2 Petro 1 >
1 Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Yesu Kristo: Kwa wale ambao kwa njia ya haki ya Mungu na Mwokozi wetu Yesu Kristo mmepokea imani iliyo na thamani kama yetu:
2 Neema na amani iwe kwenu kwa wingi katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu.
3 Uweza wake wa uungu umetupatia mambo yote tunayohitaji kwa ajili ya uzima na uchaji wa Mungu, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe.
4 Kwa sababu hiyo, ametukirimia ahadi zake kuu na za thamani kupitia mambo haya, ili kupitia hayo mpate kuwa washiriki wa asili ya uungu, na kuokoka kutoka upotovu ulioko duniani unaosababishwa na tamaa mbaya.
5 Kwa sababu hii hasa, jitahidini sana katika imani yenu kuongeza wema; na katika wema, maarifa;
6 katika maarifa, kiasi; katika kiasi, saburi; katika saburi, utauwa;
7 katika utauwa, upendano wa ndugu; na katika upendano wa ndugu, upendo.
8 Kwa maana haya yakiwa ndani yenu kwa wingi na kuzidi kuongezeka, yanawasaidia msikose bidii wala kutozaa matunda katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.
9 Lakini mtu yeyote asipokuwa na mambo haya haoni mbali, na ni kipofu, naye amesahau kule kutakaswa kutoka dhambi zake za zamani.
10 Kwa hiyo, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuuthibitisha wito wenu na uteule wenu. Kwa maana mkifanya hivyo, hamtajikwaa kamwe,
11 na mtajaliwa kwa ukarimu mwingi kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. (aiōnios )
12 Hivyo nitawakumbusha mambo haya siku zote, hata ingawa mnayajua na mmethibitishwa katika kweli mliyo nayo.
13 Naona ni vyema kuwakumbusha mambo haya wakati wote niwapo katika hema hili ambalo ni mwili wangu,
14 kwa sababu najua ya kwamba hivi karibuni nitaliweka kando, kama vile Bwana wetu Yesu Kristo alivyoliweka wazi kwangu.
15 Nami nitafanya kila juhudi kuona kwamba baada ya kuondoka kwangu mtaweza kuyakumbuka mambo haya siku zote.
16 Tulipowafahamisha juu ya uweza na kuja kwa Bwana wetu Yesu Kristo, hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, bali tulishuhudia kwa macho yetu ukuu wake.
17 Alipewa heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba, sauti ilipomjia katika Utukufu Mkuu, ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa naye sana.”
18 Sisi wenyewe tuliisikia sauti hii ambayo ilitoka mbinguni, wakati tulipokuwa pamoja naye kwenye ule mlima mtakatifu.
19 Nasi tunalo pia neno la hakika zaidi la unabii, ambalo mtafanya vyema mkiliangalia kwa bidii, kama vile nuru inavyongʼaa gizani, hadi kupambazuka na nyota ya asubuhi izuke mioyoni mwenu.
20 Zaidi ya yote, yawapasa mjue kwamba hakuna unabii katika Maandiko uliofasiriwa kama alivyopenda nabii mwenyewe.
21 Kwa maana unabii haukuja kamwe kwa mapenzi ya mwanadamu, bali watu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.