< 2 Petro 2 >

1 Lakini pia waliinuka manabii wa uongo miongoni mwa watu, kama vile watakavyokuwako walimu wa uongo miongoni mwenu. Wataingiza mafundisho yasiyopatana na kweli kwa siri, hata kumkana Bwana wa pekee aliyewanunua, na hivyo kujiletea wenyewe maangamizi ya haraka.
Palitokea manabii wa uongo kati ya watu, na vivyo hivyo walimu wa uongo watatokea kati yenu. Watu hao wataingiza mafundisho maharibifu na kumkana Bwana aliyewakomboa, na kwa njia hiyo watasababisha ghafla maangamizi yao wenyewe.
2 Hata hivyo, wengi watafuata njia zao za ufisadi, na kwa ajili yao njia ya kweli itatukanwa.
Tena watu wengi watazifuata hizo njia zao mbaya, kwa sababu yao, wengine wataipuuza Njia ya ukweli.
3 Nao katika tamaa zao mbaya, walimu hawa watajipatia faida kwenu kwa hadithi walizotunga wenyewe. Lakini hukumu imekwisha kutangazwa dhidi yao tangu zamani, wala uangamivu wao haujalala usingizi.
Kwa tamaa yao mbaya watajipatia faida kwa kuwaambieni hadithi za uongo. Lakini kwa muda mrefu sasa Hakimu wao yu tayari, na Mwangamizi wao yu macho!
4 Kwa maana, kama Mungu hakuwasamehe malaika walipotenda dhambi, bali aliwatupa kuzimu katika vifungo vya giza wakae humo mpaka ije hukumu; (Tartaroō g5020)
Malaika walipotenda dhambi, Mungu hakuwahurumia, bali aliwatupa katika moto wa Jehanamu ambako wamefungwa wakingojea Siku ile ya Hukumu. (Tartaroō g5020)
5 kama hakuusamehe ulimwengu wa kale alipoleta gharika juu ya watu wale wasiomcha Mungu, bali akamhifadhi Noa, mhubiri wa haki, pamoja na watu wengine saba;
Mungu hakuihurumia dunia ya hapo kale, bali alileta gharika kuu juu ya nchi ile ya watu wasiomcha Mungu; lakini Noa ambaye alihubiri uadilifu, Mungu alimwokoa pamoja na watu wengine saba.
6 kama aliihukumu miji ya Sodoma na Gomora kwa kuiteketeza kwa moto ikawa majivu, na kuifanya kuwa kielelezo kwa yale yatakayowapata wale wasiomcha Mungu;
Mungu aliadhibu miji ya Sodoma na Gomora, akaiteketeza kwa moto, akaifanya iwe mfano wa mambo yatakayowapata watu wasiomcha Mungu.
7 na kama alimwokoa Loti, mtu mwenye haki, ambaye alihuzunishwa na maisha machafu ya watu wapotovu
Alimwokoa Loti, mtu mwema, ambaye alisikitishwa sana na mwenendo mbaya wa watu hao waasi.
8 (kwa sababu yale matendo mapotovu aliyoyaona na kuyasikia huyo mtu mwenye haki alipoishi miongoni mwao yalimhuzunisha siku baada ya siku):
Loti aliishi miongoni mwa watu hao, na kwa siku nyingi moyo wake ulikuwa katika wasiwasi mkuu aliposikia matendo yao maovu.
9 ikiwa hivyo ndivyo, basi Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa wamchao Mungu kutoka majaribu, na kuwaweka waasi katika adhabu hadi siku ya hukumu.
Kwa hiyo, basi, Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa katika majaribu watu wanaomcha Mungu, na jinsi ya kuwaweka waovu katika adhabu hadi Siku ile ya hukumu,
10 Hii ni hakika hasa kwa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kudharau mamlaka. Kwa ushupavu na kwa kiburi, watu hawa hawaogopi kunena mabaya dhidi ya viumbe vya mbinguni.
hasa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kupuuza mamlaka. Watu hao ni washupavu na wenye majivuno, huvitukana na hawaviheshimu viumbe vitukufu vya juu.
11 Lakini hata malaika, ingawa wana nguvu na uwezo zaidi, hawaleti mashtaka mabaya dhidi ya viumbe kama hao mbele za Bwana.
Lakini malaika, ambao wana uwezo na nguvu zaidi kuliko hao walimu wa uongo, hawawashtaki na kuwatukana hao mbele ya Bwana.
12 Lakini watu hawa hukufuru katika mambo wasiyoyafahamu. Wao ni kama wanyama wasio na akili, viumbe wanaotawaliwa na hisia za mwili, waliozaliwa ili wakamatwe na kuchinjwa. Hawa nao kama wanyama wataangamizwa pia.
Watu hao ambao hutukana chochote kile wasichoelewa, ni sawa na wanyama wasio na akili, ambao huzaliwa na baadaye hukamatwa na kuchinjwa! Wataangamizwa kutokana na uharibifu wao wenyewe,
13 Watalipwa madhara kwa ajili ya madhara waliyowatendea wengine. Huhesabu kuwa ni fahari kufanya karamu za ulevi na ulafi mchana peupe. Wao ni mawaa na dosari, wakijifurahisha katika anasa zao wanaposhiriki katika karamu zenu.
na watalipwa mateso kwa mateso ambayo wameyasababisha. Furaha yao ni kufanya, tena mchana kabisa, chochote kinachotosheleza anasa zao za mwili. Hao ni fedheha na aibu tupu kwa jumuiya yenu wakati wanapojiunga nanyi katika karamu zenu, bali wakifurahia njia zao za udanganyifu.
14 Wakiwa na macho yaliyojaa uzinzi, kamwe hawaachi kutenda dhambi. Huwashawishi wale wasio imara. Wao ni hodari kwa kutamani; ni wana wa laana!
Macho yao yamejaa uzinzi na uwezo wao wa kutenda dhambi hauna kikomo. Huwaongoza watu walio dhaifu mpaka mitegoni. Mioyo yao imezoea kuwa na tamaa ya mali. Wapo chini ya laana ya Mungu!
15 Wameiacha njia iliyonyooka, wakapotoka na kuifuata njia ya Balaamu mwana wa Beori aliyependa mshahara wa uovu.
Wameiacha njia iliyonyoka, wakapotoka na kuifuata njia aliyofuata Balaamu, mwana wa Beori, ambaye alipendelea kupata faida kwa kufanya udanganyifu,
16 Lakini kwa ajili ya uovu wake, alikemewa na punda, mnyama asiyejua kusema, akaongea akitumia sauti ya mwanadamu na kuzuia wazimu wa huyo nabii.
akakaripiwa kwa ajili ya uovu wake. Punda ambaye hasemi alinena kwa sauti ya binadamu, akaukomesha wazimu wa huyo nabii.
17 Watu hawa ni chemchemi zisizo na maji, na ukungu upeperushwao na tufani. Giza nene limewekwa tayari kwa ajili yao.
Watu hao ni kama chemchemi zilizokauka, kama mawingu yanayopeperushwa na tufani; makao yao waliyowekewa ni mahali pa giza kuu.
18 Kwa maana wao hunena maneno makuu mno ya kiburi cha bure, na kwa kuvutia tamaa mbaya za asili ya mwili, huwashawishi watu ambao ndipo tu wamejiondoa miongoni mwa wale wanaoishi katika ufisadi.
Husema maneno ya majivuno na yasiyo na maana, na kutumia tamaa zao mbaya za kimwili kuwatega wale ambao wamejitenga hivi karibuni na watu waishio katika udanganyifu.
19 Huwaahidi uhuru hao waliowanasa, wakati wao wenyewe ni watumwa wa ufisadi: kwa maana mtu ni mtumwa wa kitu chochote kinachomtawala.
Huwaahidi watu wengine eti watakuwa huru, kumbe wao wenyewe ni watumwa wa upotovu—maana mtu ni mtumwa wa chochote kile kinachomtawala.
20 Kama wameukimbia upotovu wa dunia kwa kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo, kisha wakanaswa tena humo na kushindwa, hali yao ya mwisho ni mbaya zaidi kuliko ile ya kwanza.
Watu waliokwisha ponyoka katika upotovu wa ulimwengu kwa kupata kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, kisha wakakubali kunaswa na kutawaliwa tena na upotovu huo, hali yao itakuwa mbaya zaidi kuliko awali.
21 Ingelikuwa afadhali kwao kama wasingeliijua kamwe njia ya haki, kuliko kuijua kisha wakaiacha ile amri takatifu waliyokabidhiwa.
Ingalikuwa afadhali kwao kama wasingalijua kamwe njia hiyo ya uadilifu kuliko kujua na kisha kuiacha na kupoteza amri takatifu waliyopokea.
22 Imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli isemayo: “Mbwa huyarudia matapiko yake mwenyewe,” tena, “Nguruwe aliyeoshwa hurudi kugaagaa matopeni.”
Ipo mithali isemayo: “Mbwa huyarudia matapishi yake mwenyewe,” na nyingine isemayo: “Nguruwe aliyekwisha oshwa hugaagaa tena katika matope!” Ndivyo ilivyo kwao sasa.

< 2 Petro 2 >