< 2 Wafalme 1 >
1 Baada ya kifo cha Mfalme Ahabu, nchi ya Moabu iliasi dhidi ya Israeli.
Moabu aliasi dhidi ya Israeli baada ya kifo cha Ahabu.
2 Basi Ahazia alikuwa ameanguka huko Samaria kutoka baraza ya chumba chake cha juu, akaumia. Hivyo akatuma wajumbe, akiwaambia, “Nendeni mkaulize kwa Baal-Zebubu, mungu wa Ekroni, mkaone kama nitapona kutokana na kuumia huku.”
Baada hapo Ahazi akaanguka chini ya dirisha lenye waya zinazikinzana kwenye chumba chake juu katika Samaria, na alikuwa amejeruhiwa. Kwa hiyo alituma wajumbe na kuwaambia, “Nendeni, muulizeni Baal Zebubu, mungu wa Ekroni, kama nitapona hili jeraha.”
3 Lakini malaika wa Bwana akamwambia Eliya, Mtishbi, “Panda ukakutane na wajumbe wa mfalme wa Samaria, uwaulize, ‘Je, ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli ndiyo maana mnakwenda kumuuliza Baal-Zebubu, mungu wa Ekroni?’
Lakini malaika wa Yahwe wakamwambia Eliya Mtishbi, “Inuka, nenda ukaonane na wajumbe wa mfalme wa Samaria, na uwaulize, 'Je ni kwasababu hakuna Mungu katika israeli ambaye mnayekwenda kuuliza pamoja na Zebebu, mungu wa Ekroni?
4 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana, ‘Hutaondoka kwenye kitanda unachokilalia. Hakika utakufa!’” Hivyo Eliya akaenda.
Kwa hiyo Yahwe anasema, “Hutaweza kushuka chini kutoka kwenye kitanda ambacho ulichokipanda; badala yake, utakufa hakika."”” Baada ya hapo Eliya akaondoka.
5 Wajumbe waliporudi kwa mfalme, akawauliza, “Kwa nini mmerudi?”
wakati wale wajumbe waliporudi kwa Ahazia, akawaambia, “Kwa nini mmerudi?”
6 Wakamjibu, “Mtu fulani alikuja kukutana nasi, naye akatuambia, ‘Rudini kwa mfalme aliyewatuma na mkamwambie, “Hili ndilo asemalo Bwana: Je, ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli ndiyo maana unawatuma watu kwenda kuuliza kwa Baal-Zebubu, mungu wa Ekroni? Kwa hiyo hutaondoka kwenye kitanda unachokilalia. Hakika utakufa!”’”
Wakamwambia, “mtu amekuja kuonana na sisi ambaye ametuambia, 'Turudi kwa mfalme ambaye aliyewatuma, na mkamwambie, Yahwe amesema hivi: 'Je ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli mpaka mmewatuma watu kwenda kumuuliza kwa Baal Zabubu, mungu wa Ekron? Kwa hiyo hutashuka kutoka kitanda ulichokipanda; badala yake, utakufa hakika."””
7 Mfalme akawauliza, “Alikuwa mtu wa namna gani ambaye mlikutana naye, akawaambia hili?”
Ahazi akawaambia wajumbe wake, “'Alikuwa mtu wa aina gani, yule ambaye alikuja kuonana na ninyi na akasema haya maneno kwenu?”
8 Wakamjibu, “Alikuwa mtu aliyekuwa na vazi la manyoya na mkanda wa ngozi kiunoni mwake.” Mfalme akasema, “Huyo alikuwa ni Eliya, Mtishbi.”
Wakamjibu, “Alikuwa amevaa kanzu yenye manyaya na alikuwa na mkanda wa ngozi kiunanoni kwake.'” Hivyo mfalme akajibu, '“Yule alikuwa Eliya Mtishbi.”
9 Ndipo mfalme akamtuma mkuu mmoja wa kikosi pamoja na kikosi chake cha askari hamsini kwa nabii Eliya. Yule mkuu wa kikosi akamwendea Eliya, aliyekuwa ameketi juu ya kilima, na kumwambia, “Mtu wa Mungu, mfalme anasema, ‘Shuka chini!’”
Ndipo mfalme akatuma nahodha wa askari hamsini kwa Elya. Nahodha akaenda mpaka kwa Eliya ambapo alipokuwa amekaa juu ya mlima. Nahodha akamwambia Eliya, “Wewe, mtu wa Mungu, mfalme amesema, 'shuka chini.'”
10 Eliya akamjibu yule mkuu wa kikosi, “Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni ukuteketeze wewe na watu wako hamsini!” Ndipo moto ukashuka kutoka mbinguni na kuwateketeza yule mkuu wa kikosi pamoja na watu wake.
Eliya akajibu na kusema kwa nahodha, “Kama mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke chini kutoka mbinguni na kukula wewe na watu wako hamsini.” Kisha moto ukashuka chini kutoka mbinguni na kumla yeye na watu wake hamsini.
11 Aliposikia hili, mfalme akatuma kwa Eliya mkuu wa kikosi mwingine na askari wake hamsini. Yule mkuu wa kikosi akamwambia Eliya, “Mtu wa Mungu, hili ndilo asemalo mfalme, ‘Shuka chini mara moja!’”
Tena Mfalme Ahazi akamtuma nahodha mwingine pamoja na maaskari wengine hamsini. Huyu nahodha pia akasema kwa Eliya, “Wewe, mtu wa Mungu, mfalme anasema, teremka chini haraka.”'
12 Eliya akajibu, “Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni ukuteketeze wewe na watu wako hamsini!” Ndipo moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza yeye na watu wake hamsini.
Eliya akajibu na kuwaambia, “Kama mimi ni mtu wa Mungu, ngoja moto ushuke kutoka mbinguni na ukule wewe na watu wako hamsini.” Moto wa Mungu ukashuka chini tena kutoka mbinguni na kumla yeye na watu wake hamsini.
13 Hivyo mfalme akatuma mkuu wa kikosi wa tatu na watu wake hamsini. Huyu mkuu wa kikosi wa tatu akapanda na kupiga magoti mbele ya Eliya, akiomba, “Mtu wa Mungu, tafadhali niachie uhai wangu na uhai wa hawa watu hamsini, watumishi wako!
Bado tena mfalme alituma kundi la tatu la wapiganaji hamsini. Huyu nahodha akaenda, akaanguka mbele ya miguu ya Eliya, na kumsihi na kumwambia, “Wewe, mtu wa Mungu, Nakuomba, acha uzima wangu na uzima wa hawa watumishi wako hamsini uwe na thamani machoni kwako.
14 Tazama, moto umeshuka kutoka mbinguni na kuwateketeza wale wakuu wa vikosi viwili vya kwanza pamoja na watu wao. Lakini sasa niachie uhai wangu!”
Ndipo, moto ukashuka chini kutoka mbinguni na kuwala wale manahodha wawili wa kwanza pamoja na watu wao, bali sasa acha uzima wangu uwe na thamani machoni kwako.”
15 Malaika wa Bwana akamwambia Eliya, “Shuka pamoja naye, usimwogope.” Hivyo Eliya akainuka na kushuka pamoja naye kwa mfalme.
Malaika wa Yahwe akamwambia Eliya, “'Nenda chini pamoja naye. Usimwogope.”' Hivyo Eliya akainuka na kwenda chini pamoja naye kwenda kwa mfalme.
16 Akamwambia mfalme, “Hili ndilo asemalo Bwana: Je, ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli wa kumuuliza habari, ndiyo maana ukatuma wajumbe kuuliza Baal-Zebubu, mungu wa Ekroni? Kwa sababu umefanya hili, kamwe hutaondoka kwenye kitanda unachokilalia. Hakika utakufa!”
Baadye Eliya akamwambia Ahazia, '“Hivi ndivyo Yahwe asemavyo, Umewatuma wajumbe kuzungumza pamoja na Baal-Zebubu, mungu wa Ekron. Je ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli ambaye unayeweza kumuuliza habari? Kwa hiyo sasa, hutaweza kushuka chini kutoka kwenye kitanda ulichokipanda; utakufa hakika.'”
17 Hivyo akafa, sawasawa na lile neno la Bwana ambalo Eliya alikuwa amesema. Kwa kuwa Ahazia hakuwa na mwana, Yoramu akawa mfalme baada yake katika mwaka wa pili wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda.
Hivyo Mfalme Ahazia alikufa kulingana na neno la Yahwe ambalo Eliya alilisema. Yoramu alianza kutawala katika eneo lake, katika mwaka wa pili Yoramu mwana wa Yohoshafati mfalme wa Yuda, kwa sababu Ahazia hakuwa na mtoto.
18 Kwa matukio mengine ya utawala wa Ahazia na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
Kama mambo mengine yanayomuhusu Ahazia, je hayakuandikwa katika kitabu cha matukio ya wafalme wa Israeli?