< 2 Wafalme 7 >
1 Elisha akasema, “Sikiliza neno la Bwana. Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Wakati kama huu kesho, kipimo kimoja cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli moja ya fedha, na vibaba viwili vya shayiri kwa shekeli moja ya fedha katika lango la Samaria.”
Elisha akasema, “Sikiliza neno la Yahwe. Hivi ndivyo Yahwe asemavyo: “Kesho mda kama huu kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, kwenye lango la Samaria.””
2 Yule afisa ambaye mfalme alikuwa anauegemea mkono wake akamwambia yule mtu wa Mungu, “Tazama, hata kama Bwana atafungua madirisha ya mbinguni, je, jambo hili litawezekana?” Elisha akajibu, “Utaona kwa macho yako mwenyewe, lakini wewe hutakula chochote kati ya hivyo!”
Basi yule nahodha ambaye alikuwa akitegemea mkono wake amemjibu mtu wa Mungu, na kusema, “Ona, hata kama Yahwe ataweka madirisha mbinguni, je jambo hili linawezekana?” Elisha akajibu, “Ona, utaona ikitokea kwa macho yako mwenyewe, lakini hutakula chochote katika hilo.”
3 Basi kulikuwepo na watu wanne wenye ukoma katika ingilio la lango la mji. Wakaambiana, “Kwa nini tukae hapa mpaka tufe?
Basi, kulikuwa na watu wanne wenye ukoma upande wa nje wa lango la mji. Wakaambizana kila mmoja, “Kwa nini tukae hapa hadi hapo tutakapokufa?
4 Kama tukisema, ‘Tutaingia mjini,’ mjini kuna njaa, nasi tutakufa humo. Kama tukikaa hapa, tutakufa. Kwa hiyo twende kwenye kambi ya Waaramu na tujisalimishe. Kama wakituacha hai, tutaishi; kama wakituua, basi na tufe.”
Kama tukisema kwamba tutaenda kwenye ule mji, maana mjini kuna njaa, na tutakufa hapo. Lakini kama tukiendelea kukaa hapa, bado tutakufa. Sawa, njoni, twendeni kwenye lile jeshi la Washami. Kama wakitupa uhai, tutakuwa hai, na kama wakituua, tutakufa tu.”
5 Wakati wa giza la jioni, wakaondoka na kwenda kwenye kambi ya Waaramu. Walipofika mwanzo wa kambi, hapakuwa na mtu,
Hivyo wakaamka asubuhi kabla giza halijaisha kwenda kwenye kambi ya Washami; Wakati walipofika sehemu ya mwanzo wa kambi, hapakuwa na mtu hapo.
6 kwa kuwa Bwana alilifanya jeshi la Waaramu lisikie sauti kama ya magari ya vita, farasi na jeshi kubwa, kiasi kwamba waliambiana, “Tazama, mfalme wa Israeli ameajiri mfalme wa Wahiti na mfalme wa Wamisri kuja kutushambulia sisi!”
Kwa kuwa Bwana alikuwa ameunda jeshi la Washami kusikia sauti ya magari ya farasi, na sauti za farasi-sauti za jeshi jingine kubwa, ndipo wakaambizana kila mmoja wao, “Yule mfalme wa Israeli amekodisha wafalme wa Wahiti na Wamisri waje wapigane dhidi yetu.”
7 Kwa hiyo wakaondoka na kukimbia wakati wa giza la jioni na kuacha mahema yao, farasi wao na punda wao. Wakakimbia kuokoa maisha yao na kuacha kila kitu ndani ya kambi kama kilivyokuwa.
Hivyo wale maaskari wakaondoka kungali giza; waliacha mahema yao, punda zao, na kambi kama ilivyokuwa, na kukimbia kwa ajili ya maisha yao.
8 Wale watu wenye ukoma walipofika mwanzoni mwa kambi, wakaingia kwenye mojawapo ya mahema. Wakala na kunywa, na kuchukua fedha, dhahabu na nguo, wakaenda kuvificha. Wakarudi na kuingia katika hema jingine, na kuchukua baadhi ya vitu kutoka ndani yake na kuvificha pia.
Wakati wale watu wenye ukoma walipokuja sehemu ya mwisho wa kambi, wakaenda kwenye hema moja na kula na kunywa, na kubeba fedha na dhahabu na nguo, na kwenda na kuzificha. Wakarudi na kuingia kwenye hema nyingine na kubeba kutoka pale pia, na kwenda kuvificha.
9 Kisha wakaambiana, “Hili tunalolifanya sio jema. Hii ni siku ya habari njema, nasi tunakaa kimya. Kama tukisubiri mpaka mapambazuko, maafa yatatupata. Twendeni mara moja tukatoe habari hizi katika jumba la mfalme.”
Basi, wakaambizana kila mmoja, “Hatufanyi sahihi. Siku hii ni siku ya habari njema, lakini tunanyamaza kimya kuhusu hili. Kama tukisubiri mpaka kutakapopambazuka, adhabu itakuwa juu yetu. Basi, njoni, twendeni na kuwaambia nyumba ya mfalme.”
10 Hivyo wakaenda mjini na kuwaita walinzi wa langoni, wakawaambia, “Tulikwenda katika kambi ya Waaramu lakini hapakuwepo na mtu huko, hata sauti ya mtu yeyote, ila farasi na punda waliofungwa na mahema yaliyoachwa kama yalivyokuwa.”
Kwa hiyo wakaenda na kuwaita mabawabu wa mji. Wakawaambia, wakisema, “Tumeenda kambi ya Washami, lakini hapakuwa na mtu pale, hakuna sauti ya mtu yeyote, lakini kulikuwa na farasi wamefungwa, na punda wamefungwa, na zile hema kama zilivyokuwa.”
11 Walinzi wa langoni wakatangaza habari ile kwa sauti kuu, na taarifa hii ikatolewa ndani ya jumba la mfalme.
Ndipo mabawabu wakatoa habari, ndipo wakaambiwa ndani ya nyumba ya mfalme.
12 Mfalme akaamka usiku na kuwaambia maafisa wake, “Nitawaambia kile Waaramu walichotufanyia. Wanajua kwamba tuna njaa, hivyo wameacha kambi yao ili kujificha mashambani, wakifikiri, ‘Kwa hakika watatoka nje ya mji, nasi tutawakamata wakiwa hai na kuingia ndani ya mji.’”
Basi yule mfalme akainuka usiku nakusema kwa watumishi wake, “Nitawaambia sasa kile ambacho Washami walichotufanyia. Wanajua kwamba tunanjaa, hivyo wameondoka kwenye kambi kwenda kujificha kwenye mashamba. Wanasema, 'Wakati watakapotoka mjini, tutawakamata wakiwa hai, na kuingia mjini.”
13 Mmoja wa maafisa wake akajibu, “Waamuru watu wachache wakawachukue farasi watano kati ya wale waliobaki katika mji. Hatima yao itakuwa kama ya Waisraeli wote walio hapa. Watakuwa tu kama Waisraeli hawa ambao wanangoja kifo. Hivyo tuwatumeni wajue kumetendeka nini.”
Mmoja wa wale watumishi wa mfalme akajibu na kusema, “Nakuomba, ngoja baadhi ya watu wachukue farasi watano wale waliosalia, ambao wamebaki kwenye mji. Wako kama mkutano wote wa Israeli waliobaki-wengi wamekufa; ngoja tuwatume na tuone.”
14 Ndipo wakachagua magari mawili ya vita pamoja na farasi wake, naye mfalme akawatuma wafuatilie jeshi la Waaramu. Akawaamuru waendeshaji akisema, “Nendeni mkaone ni nini kilichotokea.”
Hivyo wakachukua magari mawili ya farasi pamoja na farasi, na mfalme akawatuma baada ya jeshi la Washami, akisema, “Enendeni mkaone.”
15 Wakawafuatia hadi Yordani, nao wakakuta barabara yote ikiwa imetapakaa nguo na vyombo vya Waaramu walivyokuwa wamevitupa walipokuwa wanatoroka. Basi wale wajumbe wakarudi na kutoa taarifa kwa mfalme.
Wakawafuata kwenda Yordani, na barabara zote zilikuwa zimejaa na vifaa ambavyo Washami walivitupa wapate kukimbia haraka. Kwa hiyo wale wajumbe wakarudi na kumwambia mfalme.
16 Kisha watu wakatoka na kuteka nyara kambi ya Waaramu. Kwa hiyo kipimo cha unga mzuri kikauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, kama vile Bwana alivyokuwa amesema.
Wale watu wakatoka nje na wakaziteka nyara zile kambi za Washami. Hivyo kipimo cha unga mzuri uliuzwa kwa shekeli moja, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli moja, kama vile ambavyo neno la Yahwe lilivyosema.
17 Basi mfalme alikuwa amemweka yule afisa ambaye mfalme alikuwa anauegemea mkono wake awe msimamizi wa lango. Nao watu wakamkanyaga walipoingia langoni, naye akafa, kama vile mtu wa Mungu alivyokuwa ametangulia kusema wakati mfalme alipofika nyumbani kwake.
Naye mfalme alimwagiza yule nahodha ambaye alitegemea mkono wake kuwa mkuu wa lango, na watu wakamkanyaga chini langoni. Alikufa kama mtu wa Mungu alivyosema, ambaye ameongea wakati yule mfalme alipomshukia.
18 Ikatokea kama vile mtu wa Mungu alivyokuwa amemwambia mfalme: “Wakati kama huu kesho, kipimo kimoja cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli moja ya fedha, na vibaba viwili vya shayiri kwa shekeli moja ya fedha katika lango la Samaria.”
Basi ikatokea kama yule mtu wa Mungu alivyosema kwa mfalme akisema, “Mda kama huu kwenye lango la Samaria, vipimo viwili vya shayiri vitapatikana kwa shekeli, na kipimo cha unga mzuri kwa shekeli.”
19 Yule afisa alikuwa amemwambia yule mtu wa Mungu, “Tazama, hata kama Bwana atafungua madirisha ya mbinguni, je, jambo hili litawezekana?” Naye yule mtu wa Mungu alikuwa amemjibu, “Utaona kwa macho yako mwenyewe, lakini wewe hutakula chochote kati ya hivyo!”
Yule nahodha alimjibu yule mtu wa Mungu na kusema, “Tazama, hata kama Yahwe angefanya madirisha mbinguni, je hiki kitu kingeweza kutokea” Elisha akasema, “Tazama, utaona kikitokea kwa macho yako mwenyewe, lakini hutakula chochote katika hicho.”
20 Ndivyo hasa ilivyotokea kwake, kwa kuwa watu walimkanyaga langoni, naye akafa.
Hivyo ndivyo haswa kilichompata, kwa kuwa watu wakamkanyaga kwenye lango, na kufa.