< 2 Wafalme 4 >

1 Mke wa mmoja wa wana wa manabii akamlilia Elisha, akamwambia, “Mtumishi wako, mume wangu, amekufa, nawe unajua alikuwa anamcha Bwana. Lakini sasa yule anayemdai anakuja kuchukua wanangu wawili kama watumwa wake.”
Ndipo mke wa mmoja wa watoto wa manbii alipokuja kwa Elisha akilia, akisema, “Mtumishi wako mme wangu amukufa, na unajua kwamba mtumishi wako alikuwa anamcha Yahwe. Basi aliyemuwia amekuja kuwachukua watoto wangu wawili kwenda kuwa watumwa.”
2 Elisha akamjibu, “Nitawezaje kukusaidia? Niambie, una nini ndani ya nyumba yako?” Akasema, “Mtumishi wako hana kitu chochote kabisa, isipokuwa mafuta kidogo.”
Hivyo Elisha akamwambia, “Nikusaidie nini? Niambie una nini kwenye nyumba yako?” Akamwambia “Mtumishi wako hana kitu kwenye nyumba, isipokuwa chupa ya mafuta.”
3 Elisha akasema, “Zunguka kwa majirani zako wote ukaombe vyombo vitupu. Usiombe vichache.
Kisha Elisha akasema, “Nenda kaazime vyombo kwa majirani zako, vyombo vitupu. Azima vyombo vingi uwezavyo.
4 Kisha ingia ndani na ujifungie mlango, wewe na wanao. Mimina mafuta kwenye vyombo vyote, na kila kimoja kinapojaa, kiweke kando.”
Kisha lazima uende ndani na kujifungia mlango wewe na watoto wako, na kumiminia mafuta vyombo vyote; vile vilivyojaa ukavitenge.”
5 Yule mjane akaondoka na kujifungia ndani, yeye na wanawe. Wao wakamletea vyombo, naye akaendelea kumimina mafuta.
Basi akamuacha Elisha na kujifungia mlango yeye na watoto wake. Wakavileta vile vyombo kwake, na akivijaza kwa mafuta.
6 Vyombo vyote vilipojaa, akamwambia mwanawe, “Niletee chombo kingine.” Lakini mwanawe akajibu, “Hakuna chombo kingine kilichobaki.” Basi mafuta yakakoma kutiririka.
Ikawa vyombo vilipojaa, akamwambia mtoto wake, “Niletee chombo kingine.” Ila akamwambia, “Hakuna vyombo vingine.” Kisha mafuta yakakoma kutoka.
7 Yule mwanamke akaenda akamwambia yule mtu wa Mungu, naye mtu wa Mungu akasema, “Nenda ukayauze hayo mafuta ulipe madeni yako. Wewe na wanao mnaweza kuishi kwa kile kinachosalia.”
Ndipo akaja na kumwambia mtu wa Mungu. Akasema, “Nenda kauze mafuta; lipa deni lako, na yatakayobaki waachie watoto wako.”
8 Siku moja Elisha akaenda Shunemu. Huko kulikuwa na mwanamke mmoja mwenye cheo, ambaye alimsisitiza Elisha aje kula chakula. Kwa hiyo kila mara alipitia pale, akaingia humo ili ale.
Siku moja Elisha alitembea Shunemu ambapo mwanamke muhimu aliishi; alimsihi ale chakula pamoja naye. Ikawa alipopita mara nyingi, angeweza kusimama pale na kula.
9 Akamwambia mumewe, “Ninajua kwamba huyu mtu ambaye anakuja kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu.
Huyo mwanamke akamwambia mme wake, “Ona, sasa nadhani kwamba huyu ni mtu mtakatifu wa Mungu ambaye hupita siku zote.
10 Tutengeneze chumba kidogo juu darini na tuweke ndani yake kitanda na meza, kiti na taa kwa ajili yake. Kisha anaweza kukaa humo kila mara akija kwetu.”
Ngoja tutengeneze chumba kidogo kwenye paa kwa ajili ya Elisha, na tuweke kitanda juu ya hicho chumba, meza, na taa. Kisha atakapokuwa anakuja kwetu, atakuwa anakaa hapo.”
11 Siku moja Elisha alipofika, akapanda chumbani kwake na kulala humo.
Ikawa siku moja akaja tena kwamba Elisha akasimama pale, akakaa kwenye hicho chumba na kupumzika hapo.
12 Akamwambia mtumishi wake Gehazi, “Mwite huyo Mshunami.” Hivyo akamwita, naye akaja akasimama mbele yake.
Elisha akamwambia Gehazi mtumishi wake, “Mwite huyu Mshunami.” Wakati alipomuita, alisimama mbele yake.
13 Elisha akamwambia mtumishi wake, “Mwambie huyu mwanamke, ‘Umetaabika sana kwa ajili yetu. Sasa utendewe nini? Je, tunaweza kuzungumza na mfalme au jemadari wa jeshi kwa niaba yako?’” Akajibu, “Mimi ninaishi kwangu miongoni mwa watu wangu.”
Elisha akamwambia, “Mwambie, 'Umetusumbukia kwa kutujali. Nini kifanyike kwa ajili yako? Tunaweza kukuombea kwa mfalme au amri jeshi?”” Akajibu, “Ninaishi miongoni mwa watu wangu.”
14 Elisha akamwambia mtumishi wake, “Je, ni nini kinachoweza kufanyika kwa ajili yake?” Gehazi akasema, “Hakika, hana mwana, na mume wake ni mzee.”
Kisha Elisha akajibu, “Tumfanyie nini kwa ajili yake, sasa?” Gehazi akajibu, “Kweli hana mtoto, na mume wake ni
15 Ndipo Elisha akasema, “Mwite huyo mwanamke.” Kwa hiyo akamwita, naye akaja akasimama mlangoni.
mzee.” Hivyo Elisha akajibu, “Mwite.” Wakati alipomuita, akasimama kwenye mlango.
16 Elisha akamwambia, “Mwaka ujao, wakati kama huu utabeba mwana mikononi mwako.” Yule mama akapinga, akasema, “La hasha, bwana wangu, usimpotoshe mtumishi wako, ee mtu wa Mungu!”
Elisha akasema, “Katika kipindi kama hiki mwakani, katika kipindi cha mwaka mmoja, utakuwa ukimkumbatia mtoto.” Akasema “Hapana, bwana wangu na mtu wa Mungu, usidanganye kwa mtumishi wako.”
17 Lakini yule mwanamke akapata mimba, na mwaka uliofuata wakati kama ule ule akamzaa mwana, kama vile Elisha alivyokuwa amemwambia.
Lakini yule mwanamke akabeba mimba na kujifungua mtoto wakume kipindi hicho hicho katika mwaka uliofuata, kama Elisha alivyokuwa amemwambia.
18 Mtoto akakua, naye siku moja akamwendea baba yake, ambaye alikuwa pamoja na wavunaji.
Wakati mtoto alipokuwa mkubwa, akaenda kwa baba yake siku moja, ambaye alikuwa na watu wanaovuna.
19 Akamwambia baba yake, “Kichwa changu! Kichwa changu!” Baba yake akamwambia mtumishi, “Mchukue umpeleke kwa mama yake.”
Akamwambia baba yake, “Kichwa changu, kichwa changu.” Baba yake akamwambia mtumishi wake, “Mbebe mpeleke kwa mama yake.”
20 Baada ya mtumishi kumbeba na kumpeleka kwa mama yake, mtoto akaketi mapajani mwa mama yake mpaka adhuhuri, kisha akafa.
Wakati mtumishi alipombeba kumrudisha kwa mama yake, yule mtoto alikaa kwenye magoti yake hadi mchana na baada ya hapo mtoto alikufa.
21 Mama akampandisha na kumlaza juu ya kitanda cha yule mtu wa Mungu, kisha akafunga mlango, akatoka nje.
Hivyo yule mwanamke akambeba na kumlaza kwenye kile kitanda cha mtu wa Mungu, akafunga mlango, na kutoka nje.
22 Akamwita mume wake na kusema, “Tafadhali mtume mmoja miongoni mwa mtumishi pamoja na punda ili niweze kwenda kwa mtu wa Mungu haraka na kurudi.”
Akamwita mume wake, na kusema, “Tafadhali nitumie mmoja wa watumishi wako na moja ya punda wako ili niweze kuwahi kwa mtu wa Mungu ili niweze kurudi.”
23 Mume wake akamuuliza, “Kwa nini uende kwake leo? Leo si mwandamo wa mwezi, wala si Sabato.” Mwanamke akasema, “Yote ni sawa.”
Mume wake akasema, “Kwa nini unataka kwenda kwake leo? Sio mwezi mpya wala Sabato.” alijibu, “Itakuwa sawa.”
24 Akatandika punda na kumwambia mtumishi wake, “Mwongoze huyo punda. Usinipunguzie mwendo mpaka nikuambie.”
Ndipo akatandika kwenye punda na kumwambia mtumishi wake, “Mwendeshe haraka; usinipunguzie mwendo hadi nitakapokwambia ufanye hivyo.”
25 Kwa hiyo akaenda na kumfikia huyo mtu wa Mungu katika Mlima Karmeli. Alipomwona kwa mbali, huyo mtu wa Mungu akamwambia mtumishi wake Gehazi, “Tazama, yule Mshunami!
Hivyo alienda na kuja na mtu wa Mungu katika mlima Karmeli. Basi wakati mtu wa Mungu alipomuona kwa mbali, akamwambia Gehazi mtumishi wake, “Tazama, mwanamke Mshunami anakuja.
26 Kimbia ukamlaki, umuulize, ‘Je, wewe hujambo? Mume wako hajambo? Mtoto wako ni mzima?’” Akasema, “Kila kitu ni sawasawa.”
Tafadhali mkimbilie na umwambie, 'Hamjambo kwako pamoja na mume wako na mtoto wako?” Akajibu, “Hawajambo.”
27 Alipomfikia huyo mtu wa Mungu pale mlimani, akashika miguu yake. Gehazi akaja ili amwondoe, lakini yule mtu wa Mungu akasema, “Mwache! Yuko katika uchungu mkubwa, lakini Bwana amenificha jambo hili na hajaniambia kwa nini.”
Baada ya kufika kwa huyo mtu wa Mungu katika mlima, alimkumbatia miguu yake. Gehazi akaja karibu ili kumuondoa lakini mtu wa Mungu akasema, “Muache, kwa kuwa amefadhaika sana. na Yahwe amenificha tatizo kwangu, na hajanambia kitu.”
28 Yule mwanamke akasema, “Je, bwana wangu, mimi nilikuomba mwana? Je, sikukuambia, ‘Usiamshe matumaini yangu’?”
Ndipo aksema, “Nilikuuliza mtoto wako, bwana wangu? Sikusema, 'Usinifiche'?
29 Elisha akamwambia Gehazi, “Jikaze viuno, chukua fimbo yangu mkononi mwako na ukimbie. Ikiwa utakutana na mtu yeyote, usimsalimie, na mtu yeyote akikusalimu, usimjibu. Ilaze fimbo yangu juu ya uso wa mtoto.”
Ndipo Elisha akamwambia Geahazi, “Vaa kwa ajili ya safari na uchukue fimbo yangu mkononi mwako. Nenda kwake. Kama ukimkuta mtu yeyote, usimsalimie, na kama mtu yeyote akikusalimia, usimjibu. Laza fimbo yangu kwenye uso wa mtoto.
30 Lakini mama mtoto akasema, “Hakika kama Bwana aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Kwa hiyo Elisha akainuka, akafuatana naye.
Lakini mama yake na huyo mtoto akasema, “Kama Yahwe aishivyo, na kama uishivyo, sintokuacha.” Hivyo Elisha akainuka na kumfuata.
31 Gehazi akatangulia mbele na kuilaza fimbo juu ya uso wa mtoto, lakini hapakuwa na sauti wala itikio. Hivyo Gehazi akarudi kukutana na Elisha, na kumwambia, “Mtoto hajaamka.”
Gehazi akawatangulia na kulaza ile fimbo kwneye uso wa yule mtoto, lakini yule mtoto hakuongea wala kusikia. Hivyo baada ya hapo Gehazi akarudi kuonana na Elisha na kumwambia akisema, “Mtoto hakuamka.”
32 Elisha alipofika kwenye ile nyumba, mtoto alikuwa amelala juu ya kitanda chake angali amekufa.
Ndipo Elisha alipofika kwenye ile nyumba, yule mtoto alikuwa amekufa na alikuwa bado yupo kwenye kitanda.
33 Akaingia ndani, akajifungia yeye na yule mtoto, akamwomba Bwana.
Hivyo Elisha aliingia ndani na kufunga malango yeye mwenyewe na yule mtoto na kuomba kwa Yahwe.
34 Kisha akapanda kitandani, akalala juu ya yule mtoto, mdomo wake juu ya mdomo wa mtoto, macho yake juu ya macho ya mtoto, mikono yake juu ya mikono ya mtoto. Naye alipojinyoosha juu yake, mwili wa mtoto ukapata joto.
Alipanda juu na kulala juu ya yule mtoto; aliweka mdomo wake kwenye mdomo wake, macho yake kweneye macho yake, na mikono yake kwenye mikono yake. Akajinyoosha yeye mwenyewe kwa yule kijna, na mwili wa yule mtoto ukaanza kupata joto.
35 Elisha akajiondoa juu yake na kuanza kutembeatembea ndani ya chumba, kisha akarudi tena kitandani na kujinyoosha tena juu ya mtoto mara nyingine. Mtoto akapiga chafya mara saba, akafungua macho yake.
Baada ya hapo Elisha aliinuka na kuanza kutembea kuzunguka kile chumba na kurudi tena juu na kujinyoosha mwenyewe kwa yule kijana. Yule kijana alipiga chafya mara saba na kisha akafungua macho yake!
36 Elisha akamwita Gehazi na kumwambia, “Mwite huyo Mshunami.” Naye akafanya hivyo. Yule Mshunami alipokuja, Elisha akasema, “Mchukue mwanao.”
Hivyo Elisha akamwita Gehazi na kumwambia, “Mwite yule Mshunami!” Hivyo akamwita, na wakati alipofika kwenye kile chumba, Elisha akasema, “Mchukue mtoto wako.”
37 Akaingia ndani, akaanguka miguuni pa Elisha na kusujudu hadi nchi. Kisha akamchukua mwanawe na kutoka nje.
Kisha akainamisha uso wake chini kwenye miguu yake na kusujudu, na kisha kumchukua mtoto wake na kuondoka.
38 Elisha akarudi Gilgali, nako huko kulikuwa na njaa katika eneo lile. Wakati wana wa kundi la manabii walipokuwa wanakutana naye, akamwambia mtumishi wake, “Teleka chungu kikubwa jikoni uwapikie manabii.”
Kisha Elisha akarudi tena Gilgali. Kulikuwa na njaa katika nchi, na wana wa manabii walikuwa wamekaa mbele yake. Akamwambia mtumishi wake, “Weka sufuria kubwa kwenye moto na pika kwa ajili ya watoto wa manabii.”
39 Mmoja wao akatoka kwenda mashambani kuchuma mboga na akapata mtango mwitu. Akachuma matango na kujaza nguo yake aliyoikunja ili kubebea. Aliporudi, akayakatakata na kuyatumbukiza ndani ya chungu, ingawa hakuna aliyejua ni nini.
Mmoja wao akaenda kwenye shamba kukusanya mboga mboga. Alikuta matango ya porini na kukusanya ya kutosha hadi alipojaza kwenye nguo yake. Walizikata na kuziweka kwenye sufuria, lakini hakujua zilikuwa za aina gani.
40 Mchuzi ukagawiwa watu, lakini walipoanza kula, wakalia, “Ee mtu wa Mungu, kuna mauti ndani ya chungu.” Nao hawakuweza kula.
Basi, wakawapakulia na kusambaziwa kwa watu kwa ajili ya kula. Baadae, kadiri walivyokuwa wakiendelea kula, walipiga kelele na kusema, “Mtu wa Mungu, kuna kifo kwenye sufuria!” Hivyo wasingeweza kula tena.
41 Elisha akasema, “Leteni unga.” Akauweka ndani ya chungu na kusema, “Wagawie watu ili wale.” Wala hapakuwa na kitu chochote chenye madhara ndani ya chungu.
Lakini Elisha akasema, “Late unga.” Alitupia kwenye sufuria na kusema, “Pakua kwa watu kwa ajili ya kula, kwa hiyo wanaweza kula.” Kisha hapakuwa kitu chochote kibaya kwenye ile sufuria.
42 Akaja mtu kutoka Baal-Shalisha, akimletea mtu wa Mungu mikate ishirini ya shayiri iliyookwa kutokana na nafaka ya kwanza, pamoja na masuke ya nafaka mpya. Elisha akasema, “Wape watu ili wale.”
Akaja mtu kutoka Baal Shalisha kwa mtu wa Mungu na kumletea chakula cha kwanza cha mavuno yake mikate shirirni ya shayiri, na masuke mabichi kwenye gunia. Akasema, “Wape haya watu ili waweze kula.”
43 Mtumishi wake akamuuliza, “Nitawezaje kuandaa hii mbele ya watu mia?” Lakini Elisha akajibu, “Wape watu ili wale. Kwa maana hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Watakula na kusaza.’”
Mtumishi wake akasema, “Je, niandae hii mbele ya watu mia moja?” Lakini Elisha akasema, “Wapeni hawa watu, ili waweze kula, kwa sabau Yahwe anasema, 'Watakula na kingine kitabaki.”'
44 Basi akaiandaa mbele yao ile mikate, wakala na baadhi yake wakasaza, sawasawa na neno la Bwana.
Basi mtumishi wake akawaandalia mbele yao; wakala, na kuacha kingine kimebaki, kama neno la Yahwe lilivyokuwa limesema.

< 2 Wafalme 4 >