< 2 Wafalme 23 >
1 Kisha mfalme akawaita pamoja wazee wote wa Yuda na Yerusalemu.
Hivyo mfalme akawatuma wajumbe waliokuwa wamemzunguka wazee wote wa Yuda na wa Yerusalemu.
2 Akapanda kwenda hekaluni mwa Bwana pamoja na watu wa Yuda, watu wa Yerusalemu, makuhani na manabii, watu wote wakubwa kwa wadogo. Akasoma wakiwa wanasikia maneno yote ya Kitabu cha Agano, ambacho kilikuwa kimepatikana katika Hekalu la Bwana.
Kisha mfalme akapanda hadi kwenye nyumba ya Yahwe, na watu wote wa Yuda na wenyeji wote wa Yerusalemu pamoja naye, na makuhani, manabii, na watu wote, kuanzia mdogo hadi mkubwa. Kisha akasoma katika masikioni kwao maneno yote ya kitabu cha agano ambalo lililokuwa limepatikana kwenye nyumba ya Yahwe.
3 Mfalme akasimama karibu na nguzo, na kufanya upya agano mbele za Bwana: yaani kumfuata Bwana na kuzishika amri zake, maagizo na sheria kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, hivyo kuyathibitisha maneno ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Kisha watu wote wakajifunga wenyewe kwa kiapo katika agano.
Mfalme akasimama karibu na nguzo na kufanya agano mbele ya Yahwe, kutembea pamoja na Yahwe na kukumbuka maagizo yake, kanuni zake, na sheria zake, kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, kuthibitisha maneno ya hili agano ambalo lililokuwa limeandikwa kwenye hiki kitabu. Hivyo watu wote wakakubaliana kusimama kwenye agano
4 Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani mkuu, makuhani waliomfuata kwa cheo, na mabawabu kuondoa kutoka kwenye Hekalu la Bwana vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali na Ashera na jeshi lote la mianga ya angani! Akavichoma nje ya Yerusalemu katika mashamba ya Bonde la Kidroni, na kuyachukua hayo majivu mpaka Betheli.
Mfalme akamwamuru Hilkia yule kuhani mkuu, makuhani chini yake, na walinzi wa lango watoe kwenye hekalu vyombo vilivyokuwa vimetengenezwa kwa ajili ya Baali na Ashera, na kwa ajili ya nyota zote za mbinguni. Akivichoma moto Yerusalimu kwenye mashamba ya bonde la Kidroni na kubeba majivu yake kwenda Betheli.
5 Akawafukuza makuhani wa kipagani waliokuwa wameteuliwa na wafalme wa Yuda kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji ya Yuda na ile iliyozunguka Yerusalemu, yaani wale waliofukiza uvumba kwa Baali, kwa jua na mwezi, kwa makundi ya nyota, na jeshi lote la angani.
Akawaondoa makuhani waliokuwa wanaabudu miungu ambao wafalme wa Yuda waliwachagua ili kwa ajili ya kufukiza ubani katika mahali pa juu kwenye miji ya Yuda na sehemu zinazoizunguka Yerusalemu-wale waliokuwa wanchoma ubani kwa Baali, kwa juana kwa mwezi, kwa sayari, na kwa nyota zote za mbinguni.
6 Akaiondoa nguzo ya Ashera kutoka kwenye Hekalu la Bwana, na kuipeleka kwenye Bonde la Kidroni nje ya Yerusalemu, akaiteketeza huko. Akaisaga hadi ikawa unga na kusambaza hilo vumbi juu ya makaburi ya watu wa kawaida.
Akaiondoa Ashera kutoka kwenye hekalu la Yahwe, nje ya Yerusalemu hata bonde la Kidroni na kuichoma hapo. Akaipiga kwenye mavumbi na kuiyatupa yale mavumbi kwenye makaburi ya watu wa kawaida.
7 Akabomoa pia nyumba za mahanithi wa mahali pa ibada za miungu, zilizokuwa ndani ya Hekalu la Bwana na mahali wanawake walipofuma kwa ajili ya Ashera.
Akavisafisha vyumba vya makahaba ambao walikuwa kwenye hekalu la Yahwe, ambako wanawake waliposhonea nguo kwa ajili ya Ashera
8 Yosia akawaleta makuhani wote wa Bwana kutoka miji yote ya Yuda, na kunajisi mahali pa juu pa kuabudia miungu, kuanzia Geba hadi Beer-Sheba, mahali pote ambapo hao makuhani wa miungu walifukiza uvumba. Akabomoa mahali pa kuwekea vitu vya ibada za miungu palipokuwa katika malango, kwenye ingilio la Lango la Yoshua, mtawala wa mji, lililoko upande wa kushoto wa lango la mji.
Yosia akawaleta makuhani wote nje ya miji ya Yuda na kupanajisi mahali pa juu ambako makuhani walipokuwa wakichomea ubani, kutoka Geba hata Bersheba. Akapaharibu mahala pa juu kwenye malango ambayo yaliyokuwa ya kuingilia kwenda kwenye lango la Yoshua (liwali wa mji), upande wa kushoto wa lango la mji.
9 Ingawa makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia miungu hawakuhudumu katika madhabahu ya Bwana katika Yerusalemu, walikula mikate isiyotiwa chachu miongoni mwa ndugu zao.
Ingawa makuhani wa mahali pa juu hawakuruhusiwa kuhudumu kwenye madhabahu ya Yahwe katika Yerusalemu, wakala mikate isiyotiwa chachu miongoni mwa ndugu zao.
10 Kisha mfalme akanajisi Tofethi, palipokuwa katika Bonde la Ben-Hinomu, ili mtu yeyote asiweze kupatumia kumtoa kafara mwanawe au binti yake katika moto kwa mungu Moleki.
Yosia akainajisi Tofethi, ambayo ipo kwenye bonde la Ben Hinomu, ili kwamba mtu yeyote asimuweke mtoto wake wa kiume au binti yake kwenye moto kama sadaka kwa Molaki.
11 Akaondoa kutoka kwenye ingilio la Hekalu la Bwana wale farasi ambao wafalme wa Yuda walikuwa wamewaweka wakfu kwa ajili ya jua. Walikuwa kwenye ua karibu na chumba cha afisa aliyeitwa Nathan-Meleki. Basi Yosia akayachoma moto yale magari yaliyokuwa yamewekwa wakfu kwa jua.
Akawachukua farasi ambao wafalme wa Yuda waliokuwa wametolewa kwa ajili ya jua. Walikuwa kwenye eneo la lango la uingilia kwenye hekalu la Yahwe, karibu na chumba cha Nathani Meleki, msimamizi mkuu wa nyumba ya mfalme. Yosia akayachoma yale magari ya farasi ya jua
12 Alizivunja madhabahu ambazo wafalme wa Yuda walikuwa wamezijenga kwenye paa la ghorofa ya Ahazi, pia madhabahu alizokuwa amezijenga Manase katika nyua mbili za Hekalu la Bwana. Akaziondoa huko, akazivunja vipande vipande, na kutupa hicho kifusi katika Bonde la Kidroni.
Yosia mfalme akayaharibu madhabahu yaliyokuwa kwenye dari ya juu ya chumba cha Ahazi, ambacho wafalme wa Yuda walikitengeneza, na madhabahu ambayo Manase aliyatengeneza kwenye behewa mbili za nyumba ya Yahwe. Yosia akazivunga vipande vipande na kuvitupa kwenye bonde la Kidroni.
13 Mfalme pia akanajisi mahali pa juu pa kuabudia miungu, palipokuwa mashariki ya Yerusalemu upande wa kusini wa Kilima cha Uharibifu, pale ambapo Solomoni mfalme wa Israeli alikuwa amejenga kwa ajili ya Ashtorethi mungu mke chukizo la Wasidoni, kwa ajili ya Kemoshi mungu chukizo la Wamoabu, na kwa ajili ya Moleki mungu chukizo la watu wa Amoni.
Mfalme akapaangamiza mahali pa juu magharibi mwa Yerusalemu, kusini mwa mlima wa uharibifu ambapo Sulemani mfalme wa Israeli alipajenga kwa ajili ya Ashtorithi, chukizo la Wamoabu; sanamu za karaha za Wasidoni; kwa Kemoshi, sanamu za karaha wa Moabu; na kwa Moleki, sanamu wa karaha wa watu wa Amoni.
14 Yosia akapasua yale mawe ya kuabudiwa na kuzikatakata nguzo za Ashera. Kisha akafunika hayo maeneo kwa mifupa ya wanadamu.
Akazivunja nguzo za jiwe kuwa vipande vipande na kuziangusha chini nguzo za Ashera na kuzijaza zile sehemu kwa mifupa ya watu.
15 Hata madhabahu yaliyokuwa huko Betheli, mahali pa juu pa kuabudia miungu palipokuwa pamejengwa na Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye aliwafanya Israeli watende dhambi, alibomoa hata hayo madhabahu na mahali pa juu pa kuabudia miungu. Alipateketeza kwa moto hapo mahali pa juu pa kuabudia miungu na kupasaga hadi pakawa vumbi, na kuichoma hiyo nguzo ya Ashera pia.
Yosia pia akaiteketeza kabisa madhabahu iliyokuwa Betheli na mahali pa juu ambako Yeroboamu mwana wa Nebati (ambaye aliwafanya Waisraeli kuasi) aliijenga. Pia aliichoma moto ile madhabahu na mahali pa juu na kupapiga hadi pakawa vumbi. Pia akaichoma moto nguzo ya Ashera.
16 Kisha Yosia akatazama huku na huko, naye alipoona makaburi yaliyokuwa huko kwenye kilima, akaamuru mifupa itolewe humo na akaichoma juu ya madhabahu ya Betheli ili kupanajisi. Hili lilitokea kulingana na neno la Bwana lililosemwa na mtu wa Mungu ambaye alitangulia kusema mambo haya.
Yosia alipotazama kwenye lile eneo, akagundua kwamba yale makaburi yalikuwa juu ya mlima. Akawatuma watu kuichukua mifupa kutoka kwenye yale makaburi; kisha akaichoma kwenye madhabahu, akainajisi. Hii ilitokana na neno la Yahwe ambalo mtu wa Mungu aliliongea, yule mtu aliyekuwa ameongea haya mambo kabla.
17 Mfalme akauliza, “Lile kaburi lenye mnara wa ukumbusho ninaloliona ni kwa ajili gani?” Watu wa mji wakasema, “Hii ni alama ya kaburi la mtu wa Mungu aliyekuja kutoka Yuda, naye akanena dhidi ya hii madhabahu ya Betheli mambo yale yale uliyoifanyia leo.”
Kisha akasema, “Ni ukumbusho wa nani ule ninao uona?” Mtu wa ule mji akamwambia, “Lile ni kaburi la mtu wa Mungu ambaye alikuja kutoka Yuda na kuongea kuhusu haya mambo ambayo ameyafanya dhidi ya madhabahu ya Betheli.”
18 Akasema, “Liacheni, msiliguse. Msimruhusu mtu yeyote kuiondoa mifupa yake.” Basi wakaiacha mifupa yake pamoja na ile ya yule nabii ambaye alikuwa amekuja kutoka Samaria.
Hivyo Yosia akasema, “Mwacheni. Mtu asihamishe mifupa yake.” Hivyo wakaacha mifupa yake, pamoja na mifupa ya nabii ambaye alikuja kutoka Samaria.
19 Kama alivyokuwa amefanya huko Betheli, Yosia akabomoa na kunajisi mahali pa kuabudia miungu kwenye mahali pa juu ambapo wafalme wa Israeli walikuwa wamejenga ndani ya miji ya Samaria, ambayo ilikuwa imemghadhibisha Bwana.
Kisha Yosia akahamisha nyumba zote za mahali pa juu ambazo zilikuwa katika mji wa Samaria, ambazo wafalme wa Israeli walizokuwa wamezitengeneza, na ambazo zilizokuwa zimemgadhabisha Yahwe kwa hasira.
20 Yosia akawachinja makuhani wote wa mahali pa juu pa kuabudia miungu katika madhabahu zao wenyewe, na kuchoma mifupa ya wanadamu juu yake. Kisha akarudi Yerusalemu.
Aliwafanyia kile ambacho kilikuwa kimefanyika katika Betheli. Aliwachinja makuhani wote wa mahali pa juu ya madhabahu na aliichoma mifupa ya watu juu yao. Kisha akarudi Yerusalemu.
21 Mfalme akatoa agizo hili kwa watu wote: “Adhimisheni Pasaka kwa Bwana Mungu wenu, kama ilivyoandikwa katika Kitabu hiki cha Agano.”
Kisha mfalme akawaamuru watu wote, akisema, “Itunzeni Pasaka ya Yahwe Mungu wenu, kama ilivyoandikwa kwenye hiki kitabu cha agano.”
22 Hapakuwahi kuwepo na adhimisho lingine la Pasaka kama hilo tangu nyakati za Waamuzi walioongoza Israeli, wala katika nyakati zote za wafalme wa Israeli na wafalme wa Yuda.
Hiyo Pasaka haijawahi kufanyika tangu siku za waamuzi ambao waliiongoza Israeli, wala katika siku zote za wafalme wa Israeli au Yuda.
23 Lakini katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Mfalme Yosia, Pasaka hii iliadhimishwa kwa Bwana huko Yerusalemu.
Lakini katika mwaka wa kumi na nane wa Mfalme Yosia hii Pasaka ya Yahwe ilisheherekewa katika Yerusalemu.
24 Zaidi ya hayo, Yosia akawaondoa waaguzi, wanaoabudu mizimu, sanamu za kuagulia, sanamu za kuabudiwa, na vitu vingine vyote vya machukizo vilivyoonekana huko Yuda na Yerusalemu. Aliyafanya haya ili kutimiza matakwa ya sheria iliyoandikwa ndani ya kile kitabu ambacho Hilkia kuhani alikipata ndani ya Hekalu la Bwana.
Yosia pia akawafukuza wale ambao waliokuwa wameongea na wafu au na roho. Pia aliifukuza miungu ya sananmu, sanamu, na vitu vyote ambavyo ni chukizo vilivyokuwa vinaonekana katika nchi ya Yuda na katika Yerusalemu, hivyo kwa kuthibitisha yale maneno ya sheria ambayo iliyokuwa imeandikwa kwenye kitabu cha Hilkia yule kuhani aliyekuwa amepatikana kwenye nyumba ya Yahwe.
25 Kabla wala baada ya Mfalme Yosia hapakuwepo na mfalme mwingine yeyote ambaye alimpenda Bwana kwa moyo wake wote, kwa roho yake yote, na kwa nguvu zake zote, sawasawa na Sheria yote ya Mose.
Kabla ya Yosia, hapakuwa na mfalme kama yeye, aliyekuwa amemwelekea yahwe kwa moyo wake wote, roho yake yote, na nguvu zake zote, ambaye alifuata sheria zote za Musa. Hapakuwa na mfalme kama Yosia aliyeinuka baada ya yeye.
26 Hata hivyo, Bwana hakuacha ghadhabu yake iliyowaka dhidi ya Yuda kwa sababu ya yale yote ambayo Manase alikuwa amefanya kumghadhibisha.
Walakini, Yahwe hakugeuka kutoka kwenye ukali wa hasira yake, ambayo ilikuwa dhidi ya Yuda kwa waabudu wapagani wote pamoja ambao Manase aliokuwa amemgadhibisha.
27 Hivyo Bwana akasema, “Nitamwondoa Yuda mbele zangu kama nilivyomwondoa Israeli, nami nitaukataa Yerusalemu, mji niliouchagua, na Hekalu hili, ambalo nilisema, ‘Jina langu litakaa humo.’”
Hivyo Yahwe akasema, “Pia nitaiondoa Yuda usoni kwangu, kama nilivyoiondoa Israeli, na nitautupilia mbali huu mji ambao nilio uchagua, Yerusalemu, na ile nyumba ambayo niliyokuwa nimesema, 'Jina langu litakuwa humo.”'
28 Matukio mengine ya utawala wa Yosia na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
Kama kwa mambo mengine yanayo muhusu Yosia, kila kitu alichofanya, je vimeandikwa kwenye kitabu cha matukio ya wafalme wa Yuda?
29 Yosia alipokuwa mfalme, Farao Neko mfalme wa Misri akapanda mpaka Mto Frati kumsaidia mfalme wa Ashuru. Mfalme Yosia akatoka kwenda kupigana naye, lakini Neko akamkabili na kumuua huko Megido.
Katika siku zake, Farao Neko, mfalme wa Misri, alienda kupigana dhidi ya mfalme wa Ashuru huko mto Frati. Mfalme Yosia akaenda kuonana na Neco katika mapigano, na Neko akamuua huko Megido.
30 Watumishi wa Yosia wakauleta mwili wake katika gari la vita kutoka Megido hadi Yerusalemu, wakamzika kwenye kaburi lake mwenyewe. Nao watu wa nchi wakamchukua Yehoahazi mwana wa Yosia, wakamtia mafuta na kumfanya mfalme mahali pa baba yake.
Watumishi wa Yosia wakambeba kwenye gari la farasi akiwa amekufa kutoka Migido, kumleta Yerusalemu, na kumzika katika kaburi lake mwenyewe. Kisha watu wa nchi wakamchukua Yehoahazi mwana wa Yosia, wakamtia mafuta, na kumfanya kuwa mfalme katika mahali pake.
31 Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miezi mitatu. Jina la mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia kutoka Libna.
Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na tatu alipoanza kutawala, na alitawala miezi mitatu katika Yerusalemu. Mama yake alikuwa akiitwa Hamutali; alikuwa binti wa Yeremia wa Libana.
32 Akafanya maovu machoni mwa Bwana, kama baba zake walivyofanya.
Yehoahazi alifanya yaliyo maovu usoni kwa Yahwe, kama kila kitu ambacho babu zake walichokifanya.
33 Farao Neko akamfunga kwa minyororo huko Ribla katika nchi ya Hamathi ili asiweze kutawala huko Yerusalemu, naye akatoza kodi ya talanta mia moja za fedha, na talanta moja ya dhahabu katika Yuda.
Farao Neko akamfunga gerezani huko Ribla katika nchi ya Hamathi, hivyo asiweze kutawala katika Yerusalemu. Kisha Neko akaitoza Yuda talanta mia moja za fedha na talanta moja ya dhahabu.
34 Farao Neko akamfanya Eliakimu mwana wa Yosia kuwa mfalme mahali pa baba yake Yosia, na kulibadilisha jina la Eliakimu kuwa Yehoyakimu. Lakini akamchukua Yehoahazi na kumpeleka Misri, naye akafia huko.
Farao Neko akamfanya Eliakimu mwana wa Yosia mfalme katika mahali pa Yosia baba yake, na kubadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu. Lakini akamchukua mfalme Yehoahazi kwenda Misri, na Yehoahazi akafia huko.
35 Yehoyakimu akamlipa Farao Neko ile fedha na dhahabu aliyodai. Ili kuweza kufanya hivyo, Yehoyakimu akatoza nchi kodi na kulipiza fedha na dhahabu kutoka kwa watu wa nchi kulingana na makadrio ya mapato yao.
Yehoyakimu akalipa fedha na dhahabu kwa Farao. Ili akutane na amri ya Farao, Yehoyakimu akaitoza nchi na kulazimisha kila mtu miongoni mwa watu wa nchi wamlipe fedha na dhahabu kulingana na makadirio yao.
36 Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na mmoja. Jina la mama yake aliitwa Zebida binti Pedaya kutoka Ruma.
Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, na alitawala miaka kumi na moja katika Yerusalemu. Mama yake alikuwa akiitwa Zebida; alikuwa binti wa Pedaia wa Ruma.
37 Naye akafanya maovu machoni mwa Bwana, kama baba zake walivyokuwa wamefanya.
Yehoyakimu akafanya yale yaliyo maovu usoni kwa Yahwe, kama waliyoyafanya babu zake.