< 2 Wafalme 21 >
1 Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na mitano. Mama yake aliitwa Hefsiba.
Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na mbili wakati alipoanza kutawala; alitawala miaka hamsini na tano katika Yerusalemu. Mama yake alikuwa anaitwa Hefziba.
2 Akafanya maovu machoni pa Bwana, akafuata desturi za machukizo za mataifa ambayo Bwana aliyafukuza mbele ya Waisraeli.
Alifanya maovu usoni kwa Yahwe, kama machukizo ya mataifa ambayo Yahwe aliyafukuza nje mbele ya wana wa Israeli.
3 Akajenga upya mahali pa juu pa kuabudia miungu ambapo Hezekia baba yake alikuwa amepabomoa. Pia akasimamisha madhabahu za Baali na kutengeneza nguzo ya Ashera, kama Ahabu mfalme wa Israeli alivyofanya. Akalisujudia jeshi lote la angani na kuliabudu.
Kwa kupajenga tena mahala pa juu ambapo Hezekia baba yake alipaharibu, na akajenga madhabahu kwa ajili ya Baali, akafanya Ashera, kama Ahabu mfalme wa Israeli alivyofanya, akasujudu kwa nyota zote za mbinguni na kuwaabudu wao.
4 Akajenga madhabahu katika Hekalu la Bwana, ambamo Bwana alikuwa amesema, “Katika Yerusalemu nitaliweka Jina langu.”
Manase akajenga madhabahu za kipagani kwenye nyumba ya Yahwe, ingawaje Yahwe aliamuru, “Jina langu litakuwa Yerusalemu daima.”
5 Katika nyua zote mbili za Hekalu la Bwana, akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la angani.
Akajenga madhabahu kwa ajili ya nyota zote za mbinguni katika behewa mbili za nyumba ya Yahwe.
6 Akamtoa kafara mwanawe mwenyewe katika moto, akafanya uchawi na uaguzi, na akataka shauri kwa wapiga ramli na kwa mizimu. Akafanya maovu mengi sana machoni mwa Bwana na kumghadhibisha.
Akamuweka mtoto wake wa kiume kwenye moto; akatazama bao ushirikina na kujishuhulisha pamoja wale ambao wenye pepo wa utambuzi na wale wachawi. Akafanya maovu mengi usoni kwa Yahwe na kuchochea hasira kwa Mungu.
7 Akachukua nguzo ya Ashera aliyoichonga na kuiweka katika Hekalu, ambalo Bwana alikuwa amemwambia Daudi na mwanawe Solomoni, “Katika Hekalu hili na katika Yerusalemu niliouchagua kutoka kabila zote za Israeli, nitaliweka Jina langu milele.
Sanamu ya kuchongwa ya Ashera ambayo aliitnegeneza, akaiweka kwenye nyumba ya Yahwe. Nyumba hii ndiyo ambayo Yahwe alimwambia Daudi na Sulemani mwanawe; alisema: “Ni nyumba hii na katika Yerusalemu, ambayo nimeichagua kutoka makabila yote ya Isaraeli, ambako nitaliweka jina langu milele.
8 Sitaifanya tena miguu ya Waisraeli itangetange kutoka nchi niliyowapa baba zao, ikiwa watakuwa waangalifu kufanya kila kitu nilichowaamuru, na kuishika Sheria yote ambayo walipewa na Mose mtumishi wangu.”
Sintofanya miguu ya Israeli kushindwa tena nje ya nchi ambayo niliwapa babu zao, kama tu watakuwa makini kutii yale yote niliyowaamuru, na kufuata sheria zote ambazo mtumishi wangu Musa aliwaamuru.”
9 Lakini hawa watu hawakusikiliza. Manase akawapotosha, hivyo kwamba walifanya maovu mengi kuliko mataifa ambayo Bwana aliyaangamiza mbele ya Waisraeli.
Lakini watu hawakusikia, na Manase akawaongoza kufanya maovu zaidi kuliko yale ya mataifa ambayo Yahwe aliyaharibu mbele ya watu wa Israeli.
10 Bwana akasema kupitia watumishi wake manabii:
Basi Yahwe akaongea na watumishi wake manabii, akisema,
11 “Manase mfalme wa Yuda ametenda dhambi hizi za kuchukiza. Amefanya maovu mengi kuliko Waamori waliokuwepo kabla yake, na ameiongoza Yuda katika dhambi kwa sanamu zake.
Kwasababu Manase mfalme wa Yuda amefanya haya machukizo, na kutenda maovu zaidi kuliko yote waliyoyatenda Waamori ambao walikuwa mbele yake walikubali, na pia aliwafanya Yuda kuasi kwa sanamu zake,
12 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Nitaleta maafa makubwa juu ya Yerusalemu na Yuda, kiasi kwamba masikio ya kila mmoja atakayesikia habari zake yatawasha.
kwa hiyo Yahwe, Mungu wa Israeli, akasema hivi: Tazama, nakaribia kuleta uovu juu ya Yerusalemu na Yuda ambayo kila mtu asikiapo kuhusu hilo, masikio yake yote yatang'aa.
13 Nitanyoosha juu ya Yerusalemu kamba ya kupimia iliyotumika dhidi ya Samaria, na timazi iliyotumika dhidi ya nyumba ya Ahabu. Nitaifutilia mbali Yerusalemu kama mtu afutaye sahani, nikiifuta na kuifunikiza.
Nitanyoosha juu ya Yerusalemu kipimo kilichotumika dhidi ya Samaria, na kuangusha msatari utakaotumika dhidi ya nyumba ya Ahabu; Nitaifuta Yerusalemu safi, kama kufuta sahani, kuifuta na kuifunika juu chini.
14 Nitawakataa mabaki wa urithi wangu na kuwatia mikononi mwa adui zao. Watapokonywa mali zao na kutekwa nyara na adui zao wote,
Nitawatupa masalia ya urithi wangu na kuwaweka mikononi mwa maadui zao. Watakuwa nyara na mateka kwa maadui zao wote,
15 kwa sababu wametenda uovu machoni pangu na kunighadhibisha tangu siku baba zao walipotoka Misri mpaka siku ya leo.”
kwa sababu wamefanya yaliyo maovu usoni kwangu, na kunichochea hasira, tangu siku babu zao walipotoka Misri, hadi leo.”
16 Zaidi ya hayo, Manase pia alimwaga damu nyingi isiyo na hatia, hivi kwamba aliijaza Yerusalemu kutoka mwanzo hadi mwisho, mbali na dhambi ambayo alikuwa amesababisha Yuda kufanya, na hivyo wakatenda maovu machoni pa Bwana.
Aidha, Manase akazimwaga damu nyingi za wasio na hatia, hadi alipoijaza Yerusalemu kutoka upande huu kwenda mwingine kwa kifo. Hii ilikuwa ni kuongeza kwenye dhambi ambayo aliifanya Yuda kuasi, wakati walipofanya uovu mbele za Yahwe.
17 Matukio mengine ya utawala wa Manase, na yote aliyoyafanya, pamoja na dhambi alizotenda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
Kama kwa mambo mengine yamhusuyo Manase, yote aliyoyafanya, na dhambi ambayo aliyoifanya, je haya hayajaandikwa kwenye kitabu cha matukio cha wafalme wa Yuda?
18 Manase akalala pamoja na baba zake na akazikwa katika bustani ya jumba lake la kifalme, katika bustani ya Uza. Naye Amoni mwanawe akawa mfalme baada yake.
Manase akalala pamoja na babu zake na alizikwa kwenye bustani ya nyumba yake, katika bustani ya Uza. Amoni mwanawe akawa mfalme katika sehemu yake.
19 Amoni alikuwa na miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka miwili. Mamaye aliitwa Meshulemethi binti Haruzi, kutoka Yotba.
Amoni alikuwa na miaka kumi na mbili alipoanza kutawala; alitawala miaka miwili katika Yerusalemu. Mama yake alikuwa anaitwa Meshlemethi; alikuwa binti wa Haruzi wa Yotba.
20 Akatenda maovu machoni mwa Bwana, kama baba yake Manase alivyofanya.
Alifanya yaliyo maovu usoni mwa Yahwe, kama manase baba yake alivyofanya.
21 Akaenenda katika njia zote za baba yake, akaabudu sanamu ambazo baba yake aliziabudu na kuzisujudia.
Amoni alifuata njia zote ambazo baba yake alizotembelea na kuabudu sanamu ambazo baba yake aliziabudu, na kuzisujudia.
22 Akamwacha Bwana, Mungu wa baba zake, wala hakuenenda katika njia za Bwana.
Akajitenga na Yahwe, Mungu wa baba zake, na hakutembea katika njia ya Yahwe.
23 Watumishi wa Amoni wakafanya fitina juu yake, nao wakamuulia kwake nyumbani.
Watumishi wa Amoni wakafanya njama dhidi yake na kumuua mfalme kwenye nyumba yake mwenyewe.
24 Kisha watu wa nchi wakawaua wale wote waliokuwa wamefanya hila dhidi ya Mfalme Amoni. Wakamfanya Yosia mwanawe kuwa mfalme mahali pake.
Lakini watu wa nchi wakawaua watu wote waliofanya njama dhidi ya mfalme Amoni, na wakamfanya Yosia mtoto wake kuwa mfalme katika sehemu yake.
25 Matukio mengine ya utawala wa Amoni na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
Kama ilivyo kwa mambo mengine yamhusuyo Amoni yale aliyoyafanya, je hayajaandikwa kwenye kitabu cha matukio ya wafalme wa Yuda?
26 Akazikwa kwenye kaburi lake katika bustani ya Uza. Naye Yosia mwanawe akawa mfalme baada yake.
Watu wakamzika kwenye kaburi lake katika bustani ya Uza, na Yosia mwanawe akawa mfalme katika sehemu yake.