< 2 Wafalme 2 >
1 Wakati Bwana alipokuwa karibu kumchukua Eliya mbinguni kwa upepo wa kisulisuli, Eliya na Elisha walikuwa njiani wakitoka Gilgali.
2 Eliya akamwambia Elisha, “Kaa hapa. Bwana amenituma Betheli.” Lakini Elisha akasema, “Kwa hakika, kama Bwana aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Kwa hiyo wakaenda Betheli pamoja.
3 Wana wa manabii waliokuwako huko Betheli wakamjia Elisha na kumuuliza, “Je, unajua ya kwamba Bwana atakuondolea bwana wako leo?” Elisha akawajibu, “Ndiyo, najua, lakini msizungumze juu ya jambo hilo.”
4 Kisha Eliya akamwambia, “Baki hapa, Elisha. Bwana amenituma Yeriko.” Naye akajibu, “Kwa hakika kama Bwana aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wakaenda Yeriko.
5 Wana wa manabii waliokuwako huko Yeriko wakamwendea Elisha na kumuuliza, “Je, unajua ya kwamba Bwana atakuondolea bwana wako leo?” Akawajibu, “Ndiyo, najua, lakini msizungumze juu ya jambo hilo.”
6 Kisha Eliya akamwambia, “Kaa hapa. Bwana amenituma kwenda Yordani.” Naye akamjibu, “Kwa hakika kama Bwana aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wote wawili wakaendelea pamoja.
7 Wana hamsini wa manabii wakaenda na kusimama kwa mbali, kuelekea mahali ambapo Eliya na Elisha walikuwa wamesimama kando ya Mto Yordani.
8 Eliya akachukua vazi lake, akalisokota na kupiga nalo maji. Maji yakagawanyika upande wa kuume na upande wa kushoto, nao wawili wakavuka pakavu.
9 Walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, “Niambie, nikufanyie nini kabla sijaondolewa kutoka kwako?” Elisha akajibu, “Naomba nirithi sehemu maradufu ya roho yako.”
10 Eliya akasema, “Umeomba jambo gumu. Lakini kama utaniona wakati ninapoondolewa kutoka kwako litakuwa lako. La sivyo, hautalipata.”
11 Walipokuwa wakitembea pamoja na kuzungumza, ghafula gari la moto na farasi wa moto vilitokea na kuwatenganisha wao wawili, naye Eliya akapanda mbinguni katika upepo wa kisulisuli.
12 Elisha aliona hili, naye akapaza sauti, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya Israeli na wapanda farasi wake!” Naye Elisha hakumwona tena. Kisha akazishika nguo zake mwenyewe na kuzirarua.
13 Akaliokota lile vazi lililoanguka kutoka kwa Eliya, kisha akarudi na kusimama ukingoni mwa Yordani.
14 Ndipo akalichukua lile vazi ambalo lilikuwa limeanguka kutoka kwa Eliya, naye akayapiga yale maji nalo. Akauliza, “Yuko wapi sasa Bwana, Mungu wa Eliya?” Elisha alipoyapiga maji, yakagawanyika kulia na kushoto, naye akavuka.
15 Wale wana wa manabii kutoka Yeriko waliokuwa wakitazama wakasema, “Roho wa Eliya inamkalia Elisha.” Nao wakaenda kumlaki na kusujudu hadi nchi mbele yake.
16 Wakasema, “Tazama, sisi watumishi wako tunao watu hamsini wenye uwezo. Waruhusu waende kumtafuta bwana wako. Labda Roho wa Bwana amemtwaa na kumweka katika mlima fulani au bonde fulani.” Elisha akajibu, “Hapana, msiwatume.”
17 Lakini wakasisitiza, mpaka akaona aibu kuwakatalia. Hivyo akasema, “Watumeni.” Nao wakawatuma watu hamsini, wakamtafuta kwa siku tatu, lakini hawakumpata.
18 Walipomrudia Elisha, ambaye alikuwa akingojea huko Yeriko, akawaambia, “Je, sikuwaambia msiende?”
19 Watu wa mji wakamwambia Elisha, “Tazama, bwana wetu, mahali mji huu ulipojengwa ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo, lakini maji yake ni mabaya, na nchi haizai.”
20 Akasema, “Nileteeni bakuli mpya, mweke chumvi ndani yake.” Kwa hiyo wakamletea.
21 Kisha akaenda kwenye chemchemi na kuitupa ile chumvi ndani yake, akisema, “Hili ndilo asemalo Bwana: ‘Nimeyaponya maji haya. Kamwe hayatasababisha mauti tena wala kutozaa.’”
22 Nayo yale maji yakaponywa mpaka leo, sawasawa na neno la Elisha alilokuwa amesema.
23 Kutoka huko Elisha akakwea kwenda Betheli. Ikawa alipokuwa akitembea barabarani, baadhi ya vijana wakatoka mjini na kumfanyia mzaha. Wakasema, “Paa, wewe mwenye upaa! Paa, wewe mwenye upaa!”
24 Akageuka, akawatazama na kuwalaani kwa Jina la Bwana. Kisha dubu wawili wa kike wakatokea mwituni na kuwararua vijana arobaini na wawili miongoni mwao.
25 Naye akaondoka huko, akaenda Mlima Karmeli, na kutoka huko akarudi Samaria.