< 2 Wafalme 19 >

1 Mfalme Hezekia aliposikia haya, akararua nguo zake na kuvaa nguo ya gunia, naye akaenda katika Hekalu la Bwana.
Ikawa kuhusu kwamba wakati Mfalme Hezekia aliposikia taazrifa zao, akararua mavazi yake, akavaa nguo za magunia, na kwenda kwenye nyumba ya Yahwe.
2 Akawatuma Eliakimu msimamizi wa nyumba ya mfalme, Shebna mwandishi, na viongozi wa makuhani, wote wakiwa wamevaa nguo za magunia, waende kwa nabii Isaya mwana wa Amozi.
Akamtuma Elkana, ambaye alikua msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna yule mwandishi, na wazee wa makuhani, wote walikuwa wamefunikwa na nguo za magunia, kwenda kwa Isaya mwana wa Amozi, yule nabii.
3 Wakamwambia, “Hili ndilo asemalo Hezekia: Siku hii ni siku ya dhiki, ya kukaripiwa na ya aibu, kama wakati watoto wanapofikia karibu kuzaliwa na kumbe hakuna nguvu ya kuwazaa.
Wakamwambia, “Hezekia wakisema, 'siku hii ni siku ya mateso, shutuma, na fedheha, kwa kuwa wakati umewadia watoto kuzaliwa, lakini hakuna nguvu ili wazaliwe.
4 Yamkini Bwana, Mungu wako atayasikia maneno ya jemadari wa jeshi, ambaye bwana wake, mfalme wa Ashuru, amemtuma kumdhihaki Mungu aliye hai, tena kwamba atamkemea kwa maneno ambayo Bwana, Mungu wako ameyasikia. Kwa hiyo omba kwa ajili ya mabaki ambao bado wako.”
Inaweza kuwa Yahwe Mungu wako atasikia maneno yote ya amiri jeshi mkuu, ambaye mfalme wa Ashuru bwana wake amemtuma kumkaidi Mungu aliye hai, naye atayakemea yale maneno ambayo Yahwe Mungu wako aliyasikia. Sasa inua maombi yako juu kwa ajili ya mabaki yaliyo bakia hapo.”'
5 Maafisa wa Mfalme Hezekia walipofika kwa Isaya,
Hivyo watumishi wa mfalme Hezekia wakaja kwa Isaya,
6 Isaya akawaambia, “Mwambieni bwana wenu, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Usiogope kwa hayo uliyoyasikia, yale maneno ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana nayo.
na Isaya akawaambia, “Mwambieni bwana wenu: 'Yahwe asema hivi, “Usiyaogope maneno ambayo uliyoyasikia, pamoja na kwamba watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana.
7 Sikiliza! Nitatia roho fulani ndani yake ili atakaposikia taarifa fulani, atarudi nchi yake mwenyewe, nami huko nitafanya auawe kwa upanga.’”
Tazama, nitaweka roho ndani yake, na yamkini atasikia taarifa na kurudi kwenye nchi yake mwenyewe. Nitamfanya aanguke kwa upanga katika nchi yake mwenyewe."”'
8 Jemadari wa jeshi aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru ameondoka Lakishi, alirudi, akamkuta mfalme akipigana na Libna.
Kisha amiri jeshi mkuu akarudi na kumkuta mfalme wa Ashuru akipigana dhidi ya Libna, kwa kuwa alisikia kwamba mfalme alikuwa ameenda kutoka Lakishi.
9 Basi Senakeribu akapata taarifa kwamba Tirhaka, Mkushi mfalme wa Misri, alikuwa anaenda kupigana naye. Basi akatuma tena wajumbe kwa Hezekia na neno hili:
Kisha Senakeribu akasikia kwamba Tirhaka mfalme wa Kushi na Misri alihamasisha kupigana dhidi yake, hivyo akatuma wajumbe tena kwa Hezekia pamoja na ujumbe:
10 “Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda: Usikubali huyo Mungu unayemtumainia akudanganye wakati anaposema, ‘Yerusalemu haitatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.’
“Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda, 'Asikudanganye Mungu wako unayemwamini, kusema, “Yerusalemu haitawekwa kwenye mikono ya mikono ya mfalme wa Ashuru.”
11 Hakika umesikia yale ambayo wafalme wa Ashuru wametenda kwa nchi zote, wakiwaangamiza kabisa. Je, wewe utaokolewa?
Tazama, umesikia kwamba wafalme wa Ashuru wamemaliza nchi zote kwa kuziharibu kabisa. Kwa hiyo je utaokoka?
12 Je, miungu ya mataifa ambayo yaliangamizwa na baba zangu iliweza kuwaokoa, hiyo miungu ya Gozani, Harani, Resefu, na ya watu wa Edeni waliokuwa Telasari?
Je wale miungu wa mataifa wamewaokoa, mataifa ambao baba zangu waliyaharibu: Gozani, Harani, Resefu, na watu wa Edeni katika Telasari?
13 Yuko wapi mfalme wa Hamathi, mfalme wa Arpadi, mfalme wa mji wa Sefarvaimu, au wa Hena au wa Iva?”
Je yuko wapi mfalme wa Hamathi, mfalme Arpadi, mfalme wa miji ya Sefarvaimu, wa Hena, na Iva?”'
14 Hezekia akapokea barua kutoka kwa wale wajumbe, naye akaisoma. Kisha akapanda katika Hekalu la Bwana, akaikunjua mbele za Bwana.
Hezekia akapokea hii barua kutoka wale wajumbe na kuisoma. Kisha akapanda hata kwenye nyumba ya Yahwe na kuukunjua mbele yake.
15 Naye Hezekia akamwomba Bwana akisema: “Ee Bwana, Mungu wa Israeli, uketiye juu ya kiti cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Wewe umeumba mbingu na nchi.
Kisha Hezekia akaomba mbele ya Yahwe na kusema, “Yahwe wa majeshi, Mungu wa Israeli, uketiye juu ya makerubi, wewe ni Mungu wa pekee juu ya tawala zote za dunia. Uliyeziumba mbingu na nchi.
16 Tega sikio, Ee Bwana, usikie; fungua macho yako, Ee Bwana, uone; sikiliza maneno ambayo Senakeribu ametuma kumtukana Mungu aliye hai.
Tega sikio lako, Yahwe, na usikie. Fungua macho yako, Yahwe, na tazama, na sikia maneno ya Senakeribu, ambayo ameyatuma kumdhihaki Mungu aliye hai.
17 “Ni kweli, Ee Bwana, kwamba wafalme wa Ashuru wameyaangamiza mataifa haya na nchi zao.
Ni kweli, Yahwe, wafalme wa Ashuru ameyaharibu mataifa na nchi zao.
18 Wameitupa miungu yao kwenye moto na kuiangamiza, kwa kuwa haikuwa miungu, bali miti na mawe tu iliyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
Wameiweka miungu yao kwenye moto, kwa kuwa hawakuwa miungu lakini ilikuwa kazi ya mikono ya watu, ilikuwa miti na mawe. Hivyo Waashuru wamewaharibu.
19 Sasa basi, Ee Bwana Mungu wetu, tuokoe kutoka mkononi mwake, ili falme zote duniani zipate kujua kwamba wewe peke yako, Ee Bwana, ndiwe Mungu.”
Basi sasa, Yahwe Mungu wetu, tuokoe, nakusihi, kutoka kwenye nguvu zake, ili kwamba mamlaka zote za dunia zipate kujua yakwamba wewe, Yahwe, ndiye Mungu wa pekee.”
20 Kisha Isaya mwana wa Amozi akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akasema: “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Nimesikia maombi yako kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru.
Kisha Isaya mwana wa Amozi akatuma ujumbe kwa Hezekia, akisema, “Yahwe, Mungu wa Israeli asema, 'Kwasababu umeomba kwangu kuhusiana na Senakeribu mfalme wa Ashuru, nimekusikia.
21 Hili ndilo neno ambalo Bwana amelisema dhidi yake: “‘Bikira Binti Sayuni anakudharau na kukudhihaki. Binti Yerusalemu anatikisa kichwa chake unapokimbia.
Hili ndilo neno ambalo Yahwe ameliongea kuhusu yeye: “Bikira binti Sayuni amekudharau na kukucheka kwa dharau. Binti wa Yerusalemu akatikisa kichwa juu yako.
22 Ni nani uliyemtukana na kumkufuru? Ni nani uliyeinua sauti yako dhidi yake, na kumwinulia macho yako kwa kiburi? Ni dhidi ya yule Aliye Mtakatifu wa Israeli!
Je ni nani uliyemchokoza na kumtukana? Dhidi ya nani umeinua sauti yako na kuinua macho yako katika majivuno? Juu ya Mtakatifu wa Israeli!
23 Kupitia kwa wajumbe wako umelundika matukano juu ya Bwana. Nawe umesema, “Kwa magari yangu mengi ya vita, nimepanda juu ya vilele vya milima, vilele vya juu sana katika Lebanoni. Nami nimeiangusha mierezi yake mirefu, misunobari yake iliyo bora sana. Nimefikia sehemu zake zilizo mbali sana, misitu yake iliyo mizuri sana.
Kupitia wajumbe wako wamemdharau Bwana, na kusema, 'Pamoja na wingi wa magari yangu ya farasi nimeenda juu ya vilele ya milima, hata juu ya kilele cha Lebanoni. Nitaikata mierezi mirefu na kuchagua miti ya mivinje huko. Nitaingia sehemu za makazi yake yaliyo mbali, msitu wake uzaao sana.
24 Nimechimba visima katika nchi za kigeni na kunywa maji yake. Kwa nyayo za miguu yangu nimekausha vijito vyote vya Misri.”
Nimechimba visima na kunywa maji mageni. Nimekausha mito yote ya Misri chini ya soli ya miguu yangu.'
25 “‘Je, hujasikia? Zamani sana niliamuru hili. Siku za kale nilipanga hili; sasa nimelifanya litokee, kwamba umegeuza miji yenye ngome kuwa malundo ya mawe.
Je hukusikia jinsi nilivyoagiza tangu zamani, na kuyafanya tangu siku za zamani? Sasa ninalileta kupita. Uko hapa kupunguza miji isiyoingilika kwenye rundo la maangamizi.
26 Watu wa miji hiyo wameishiwa nguvu, wanavunjika mioyo na kuaibishwa. Wao ni kama mimea katika shamba, kama machipukizi mororo ya kijani, kama majani yachipuayo juu ya paa la nyumba, ambayo hukauka kabla ya kukua.
Makazi yao, ya nguvu kidogo, imevunjwa vunjwa na aibu. Wamekuwa mimea katika shamba, majani ya kijani, majani juu kwenye dari au kwenye shamba, lililochomwa kabla halijakua.
27 “‘Lakini ninajua mahali ukaapo, kutoka kwako na kuingia kwako, na jinsi unavyoghadhibika dhidi yangu.
Lakini najua kuketi kwako chini, na kutoka kwako, kuingia kwako dhidi yangu.
28 Kwa sababu unaghadhibika dhidi yangu, na ufidhuli wako umefika masikioni mwangu, nitaweka ndoana yangu puani mwako na hatamu yangu kinywani mwako, nami nitakufanya urudi kwa njia ile uliyoijia.’
Kwasababu kiburi chako kimeyafikia masikio yangu, Nitaweka kulabu yangu kwenye pua yako, na hatamu yangu kwenye mdomo wako; nitakurudisha nyuma kwa njia ile ile uliyoijia.”
29 “Hii ndiyo itakuwa ishara kwako, ee Hezekia: “Mwaka huu utakula kile kiotacho chenyewe, na mwaka wa pili utakula kutoka machipukizi yake. Lakini katika mwaka wa tatu, panda na uvune, panda mashamba ya mizabibu na ule matunda yake.
Hii ndiyo itakuwa ishara kwako: Mwaka huu mtakula vitu viotavyo porini, na katika mwaka wa pili vile vikuavyo katika huo. Lakini katika mwaka wa tatu ni lazima mpande na kuvuna, kupanda mashamba ya mizabibu na kula matunda yake.
30 Mara nyingine tena mabaki ya nyumba ya Yuda wataeneza mizizi chini na kuzaa matunda juu.
Mabaki ya nyumba ya Yuda ambayo yataokoka yatachukua tena mizizi na kuzaa matunda.
31 Kwa kuwa kutoka Yerusalemu watakuja mabaki, na kutoka Mlima Sayuni kundi la walionusurika. Wivu wa Bwana Mwenye Nguvu Zote ndio utatimiza jambo hili.
Kwa kuwa mabaki yatatoka Yerusalemu, kutoka Mlima Sayuni wenye kuokoka utakuja. Wivu wa Yahwe wa majeshi utafanya hivyo.
32 “Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana kuhusu mfalme wa Ashuru: “Hataingia katika mji huu wala hatapiga mshale hapa. Hatakuja mbele yake akiwa na ngao, wala kupanga majeshi kuuzingira.
Kwa hiyo Yahwe asema hivi kuhusu mfalme wa Ashuru: “Hatakuja kwenye huu mji wala kupiga mshale hapa. Wala hatakuja mbele yake na ngao au kujenga boma dhidi yake.
33 Kwa njia ile aliyoijia, ndiyo atakayorudi; hataingia katika mji huu, asema Bwana.
Njia ile ile aliyoijia ndiyo njia atakayoondokea; hatoingia mji huu - hivi ndivyo asemavyo Yahwe.”
34 Nitaulinda mji huu na kuuokoa, kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu.”
Kwa maana nitaulinda huu mji na kuuokoa, kwa ajili yangu mwenyewe na kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu.”'
35 Usiku ule, malaika wa Bwana akaenda, akawaua wanajeshi 185,000 katika kambi ya Waashuru. Wenzao walipoamka asubuhi yake, walikuta maiti kila mahali!
Ikawa kuhusu usiku huo ambao malaika wa Yahwe alitoka na kuvamia kambi ya Waashuru, akawaua maaskari 185, 000. Kisha watu wakaamka asubuhi na mapema, miili ya watu waliokuwa wamekufa ilikuwa imelala kila mahali.
36 Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akavunja kambi na kuondoka. Akarudi Ninawi na kukaa huko.
Hivyo Senakeribu mfalme wa Ashuru akaondoka Israeli na kwenda nyumbani na kuishi katika Ninawi.
37 Siku moja, alipokuwa akiabudu katika hekalu la mungu wake Nisroki, wanawe Adrameleki na Shareza wakamuua kwa upanga, nao wakakimbilia nchi ya Ararati. Naye Esar-Hadoni mwanawe akawa mfalme badala yake.
Baadaye, alipokuwa akiabudu kwenye nyumba ya Nisroki mungu wake, watoto wake Adramaleki na Shareza wakamuua kwa upanga. Kisha wakakimbilia kwenye nchi ya Ararati. Kisha Esarhodani mwanaye akawa mfalme katika mahali pake.

< 2 Wafalme 19 >