< 2 Wafalme 19 >
1 Mfalme Hezekia aliposikia haya, akararua nguo zake na kuvaa nguo ya gunia, naye akaenda katika Hekalu la Bwana.
2 Akawatuma Eliakimu msimamizi wa nyumba ya mfalme, Shebna mwandishi, na viongozi wa makuhani, wote wakiwa wamevaa nguo za magunia, waende kwa nabii Isaya mwana wa Amozi.
3 Wakamwambia, “Hili ndilo asemalo Hezekia: Siku hii ni siku ya dhiki, ya kukaripiwa na ya aibu, kama wakati watoto wanapofikia karibu kuzaliwa na kumbe hakuna nguvu ya kuwazaa.
4 Yamkini Bwana, Mungu wako atayasikia maneno ya jemadari wa jeshi, ambaye bwana wake, mfalme wa Ashuru, amemtuma kumdhihaki Mungu aliye hai, tena kwamba atamkemea kwa maneno ambayo Bwana, Mungu wako ameyasikia. Kwa hiyo omba kwa ajili ya mabaki ambao bado wako.”
5 Maafisa wa Mfalme Hezekia walipofika kwa Isaya,
6 Isaya akawaambia, “Mwambieni bwana wenu, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Usiogope kwa hayo uliyoyasikia, yale maneno ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana nayo.
7 Sikiliza! Nitatia roho fulani ndani yake ili atakaposikia taarifa fulani, atarudi nchi yake mwenyewe, nami huko nitafanya auawe kwa upanga.’”
8 Jemadari wa jeshi aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru ameondoka Lakishi, alirudi, akamkuta mfalme akipigana na Libna.
9 Basi Senakeribu akapata taarifa kwamba Tirhaka, Mkushi mfalme wa Misri, alikuwa anaenda kupigana naye. Basi akatuma tena wajumbe kwa Hezekia na neno hili:
10 “Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda: Usikubali huyo Mungu unayemtumainia akudanganye wakati anaposema, ‘Yerusalemu haitatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.’
11 Hakika umesikia yale ambayo wafalme wa Ashuru wametenda kwa nchi zote, wakiwaangamiza kabisa. Je, wewe utaokolewa?
12 Je, miungu ya mataifa ambayo yaliangamizwa na baba zangu iliweza kuwaokoa, hiyo miungu ya Gozani, Harani, Resefu, na ya watu wa Edeni waliokuwa Telasari?
13 Yuko wapi mfalme wa Hamathi, mfalme wa Arpadi, mfalme wa mji wa Sefarvaimu, au wa Hena au wa Iva?”
14 Hezekia akapokea barua kutoka kwa wale wajumbe, naye akaisoma. Kisha akapanda katika Hekalu la Bwana, akaikunjua mbele za Bwana.
15 Naye Hezekia akamwomba Bwana akisema: “Ee Bwana, Mungu wa Israeli, uketiye juu ya kiti cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Wewe umeumba mbingu na nchi.
16 Tega sikio, Ee Bwana, usikie; fungua macho yako, Ee Bwana, uone; sikiliza maneno ambayo Senakeribu ametuma kumtukana Mungu aliye hai.
17 “Ni kweli, Ee Bwana, kwamba wafalme wa Ashuru wameyaangamiza mataifa haya na nchi zao.
18 Wameitupa miungu yao kwenye moto na kuiangamiza, kwa kuwa haikuwa miungu, bali miti na mawe tu iliyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
19 Sasa basi, Ee Bwana Mungu wetu, tuokoe kutoka mkononi mwake, ili falme zote duniani zipate kujua kwamba wewe peke yako, Ee Bwana, ndiwe Mungu.”
20 Kisha Isaya mwana wa Amozi akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akasema: “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Nimesikia maombi yako kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru.
21 Hili ndilo neno ambalo Bwana amelisema dhidi yake: “‘Bikira Binti Sayuni anakudharau na kukudhihaki. Binti Yerusalemu anatikisa kichwa chake unapokimbia.
22 Ni nani uliyemtukana na kumkufuru? Ni nani uliyeinua sauti yako dhidi yake, na kumwinulia macho yako kwa kiburi? Ni dhidi ya yule Aliye Mtakatifu wa Israeli!
23 Kupitia kwa wajumbe wako umelundika matukano juu ya Bwana. Nawe umesema, “Kwa magari yangu mengi ya vita, nimepanda juu ya vilele vya milima, vilele vya juu sana katika Lebanoni. Nami nimeiangusha mierezi yake mirefu, misunobari yake iliyo bora sana. Nimefikia sehemu zake zilizo mbali sana, misitu yake iliyo mizuri sana.
24 Nimechimba visima katika nchi za kigeni na kunywa maji yake. Kwa nyayo za miguu yangu nimekausha vijito vyote vya Misri.”
25 “‘Je, hujasikia? Zamani sana niliamuru hili. Siku za kale nilipanga hili; sasa nimelifanya litokee, kwamba umegeuza miji yenye ngome kuwa malundo ya mawe.
26 Watu wa miji hiyo wameishiwa nguvu, wanavunjika mioyo na kuaibishwa. Wao ni kama mimea katika shamba, kama machipukizi mororo ya kijani, kama majani yachipuayo juu ya paa la nyumba, ambayo hukauka kabla ya kukua.
27 “‘Lakini ninajua mahali ukaapo, kutoka kwako na kuingia kwako, na jinsi unavyoghadhibika dhidi yangu.
28 Kwa sababu unaghadhibika dhidi yangu, na ufidhuli wako umefika masikioni mwangu, nitaweka ndoana yangu puani mwako na hatamu yangu kinywani mwako, nami nitakufanya urudi kwa njia ile uliyoijia.’
29 “Hii ndiyo itakuwa ishara kwako, ee Hezekia: “Mwaka huu utakula kile kiotacho chenyewe, na mwaka wa pili utakula kutoka machipukizi yake. Lakini katika mwaka wa tatu, panda na uvune, panda mashamba ya mizabibu na ule matunda yake.
30 Mara nyingine tena mabaki ya nyumba ya Yuda wataeneza mizizi chini na kuzaa matunda juu.
31 Kwa kuwa kutoka Yerusalemu watakuja mabaki, na kutoka Mlima Sayuni kundi la walionusurika. Wivu wa Bwana Mwenye Nguvu Zote ndio utatimiza jambo hili.
32 “Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana kuhusu mfalme wa Ashuru: “Hataingia katika mji huu wala hatapiga mshale hapa. Hatakuja mbele yake akiwa na ngao, wala kupanga majeshi kuuzingira.
33 Kwa njia ile aliyoijia, ndiyo atakayorudi; hataingia katika mji huu, asema Bwana.
34 Nitaulinda mji huu na kuuokoa, kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu.”
35 Usiku ule, malaika wa Bwana akaenda, akawaua wanajeshi 185,000 katika kambi ya Waashuru. Wenzao walipoamka asubuhi yake, walikuta maiti kila mahali!
36 Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akavunja kambi na kuondoka. Akarudi Ninawi na kukaa huko.
37 Siku moja, alipokuwa akiabudu katika hekalu la mungu wake Nisroki, wanawe Adrameleki na Shareza wakamuua kwa upanga, nao wakakimbilia nchi ya Ararati. Naye Esar-Hadoni mwanawe akawa mfalme badala yake.