< 2 Wafalme 18 >
1 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Hoshea mwana wa Ela mfalme wa Israeli, Hezekia mwana wa Ahazi mfalme wa Yuda alianza kutawala.
Ikawa katika mwaka wa tatu wa Hoshea mwana wa Ela, mfalme wa Israeli, Hezekia mwana wa Ahazi, mfalme wa Yuda akaanza kutawala.
2 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Abiya binti Zekaria.
Alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala; alitawala miaka ishirini na tisa katika Yerusalemu. Jina la mama yake alikuwa anaitwa Abija; alikuwa binti wa Zekaria.
3 Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana, kama Daudi baba yake alivyofanya.
Alifanya yaliyo mema usoni pa Yahwe, kufuata mfano wa yote ambayo Daudi, babu yake, aliyoyafanya.
4 Akapaondoa mahali pa juu pa kuabudia miungu, akazivunja sanamu, akakatakata nguzo za Ashera. Akavunja vipande vipande ile nyoka ya shaba Mose aliyotengeneza, kwa kuwa hadi siku hizo wana wa Israeli walikuwa wanaifukizia uvumba (ilikuwa ikiitwa Nehushtani).
Alipaondoa mahali pa juu, akaiharibu nguzo ya jiwe, akaikata hiyo nguzo ya Ashera. Akavunja vipande vipande ile nyoka ambayo Musa aliyokuwa ameifanya, kwa sababu siku zile wana wa Israeli walikuwa wakichoma ubani katika hiyo; ilikuwa inaitwa “Nehushtani.”
5 Hezekia aliweka tumaini lake kwa Bwana, Mungu wa Israeli. Hapakuwepo na mfalme mwingine wa kufanana naye miongoni mwa wafalme wa Yuda, kabla yake au baada yake.
Hezekia alimwamini Yahwe, Mungu wa Israeli, hivyo basi baada ya yeye hapakuwa kama yeye miongoni mwa wafalme wote wa Yuda, wala miongoni mwa wafalme ambao walikuwa kabla yake.
6 Alishikamana na Bwana kwa bidii wala hakuacha kumfuata; alishika amri ambazo Bwana alikuwa amempa Mose.
Aliambatana na Yahwe. Hakuacha kumfuata lakini alizifuata amri zake, ambazo Yahwe alimwamuru Musa.
7 Naye Bwana alikuwa pamoja naye, akafanikiwa katika kila alichokifanya. Aliasi dhidi ya mfalme wa Ashuru, wala hakumtumikia.
Hivyo Yahwe alikuwa na Hezekia, kila alipokwenda alifanikiwa. Akaasi dhidi ya mfalme wa Ashuru na hakumtumikia.
8 Kuanzia mnara wa ulinzi hadi kwenye mji wenye ngome, aliwashinda Wafilisti, hadi kufikia Gaza na himaya yake yote.
Akawashambulia Wafilisti hadi Gaza na mipaka inayoizunguka, kutoka mnara wa walinzi hadi hadi mji wenye ngome.
9 Mwaka wa nne wa Mfalme Hezekia, ambao ulikuwa mwaka wa saba wa Hoshea mwana wa Ela kutawala Israeli, Shalmanesa mfalme wa Ashuru alikwenda kuishambulia Samaria na kuuzunguka kwa majeshi.
Katika mwaka wa nne wa Mfalme Hezekia, ambao ulikuwa mwaka wa saba wa Hoshea mwana wa Ela mfalme wa Israeli, Shalmanesa mfalme wa Ashuru akapanda hadi Samaria na kuizunguka.
10 Baada ya miaka mitatu Waashuru wakautwaa. Kwa hiyo Samaria ulitekwa katika mwaka wa sita wa utawala wa Mfalme Hezekia, ambao ulikuwa mwaka wa tisa wa utawala wa Hoshea mfalme wa Israeli.
Mwishoni mwa miaka mitatu wakaichukua, katika mwaka wa sita wa Hezekia, ambao ulikuwa mwaka wa tisa wa Hoshea mfalme wa Israeli; hivi ndivyo Samaria ilivyotekwa.
11 Mfalme wa Ashuru akawahamishia Waisraeli huko Ashuru na akawaweka Hala, na Gozani karibu na Mto Habori, na katika miji ya Wamedi.
Basi mfalme wa Ashuru akawachukua Israeli kwenda Ashuru na kuwaweka kwenye Hala, na katika mto Habori katika Gozani, na katika mji wa Wamedi.
12 Hili lilitokea kwa sababu hawakumtii Bwana Mungu wao, lakini walikuwa wamevunja agano lake, yale yote ambayo Mose mtumishi wa Bwana aliwaamuru. Hawakuzisikiliza amri wala kuzitimiza.
Alifanya hivi kwasababu hakutii sauti ya Yahwe Mungu wao, lakini walikiuka makubaliano ya agano lake, yote yale ambayo Musa yule mtumishi wa Yahwe aliwaamuru. Walikataa kuyasikiliza au kuyafanya.
13 Katika mwaka wa kumi na nne wa utawala wa Mfalme Hezekia, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaishambulia miji yote ya Yuda yenye ngome na kuiteka.
Kisha katika mwaka wa kumi na nne wa mfalme Hezekia, Senakerebu mfalme wa Ashuru akaishambulia miji yote yenye boma na kuwateka mateka.
14 Basi Hezekia mfalme wa Yuda akamtumia ujumbe mfalme wa Ashuru huko Lakishi akisema: “Nimefanya makosa. Ondoka katika nchi yangu, nami nitakulipa chochote unachokitaka kwangu.” Mfalme wa Ashuru akamtoza Hezekia mfalme wa Yuda talanta 300 za fedha, na talanta thelathini za dhahabu.
Basi Hezekia mfalme wa Yuda akatuma neno kwenda kwa mfalalme wa Yuda akatuma neno kwa mfalme wa Ashuru, ambaye alikuwa Lachishi, akisema, “Nimekuudhi. Nichukue. Popote utakaponiweka nitavumulia”. Mfalme wa Ashuru akamtaka Hezekia mfalme wa Yuda kulipa talanta mia tatu za fedha na talanta thelathini za dhahabu.
15 Basi Hezekia akampa fedha yote iliyopatikana ndani ya Hekalu la Bwana na katika hazina ya jumba la mfalme.
Hivyo Hezekia akampatia fedha zote ambazo zilikuwa zimepatikana kwenye nyumba ya Yahwe na kawenye hazina nyumba ya mfalme.
16 Wakati huu Hezekia mfalme wa Yuda akabandua dhahabu yote iliyokuwa imefunika milango na miimo ya Hekalu la Bwana, akampa mfalme wa Ashuru.
Kisha Hezekia akaikata ile dhahabu kutoka kwenye milango ya hekalu la Yahwe na kutoka juu ya nguzo; akampatia dhahabu mfalme wa Ashuru.
17 Mfalme wa Ashuru akamtuma jemadari wake mkuu, na afisa wake mkuu, na jemadari wa jeshi, pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi hadi kwa Mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Wakaja Yerusalemu na kusimama kwenye mfereji wa Bwawa la Juu, lililojengwa katika barabara iendayo kwenye Uwanja wa Dobi.
Lakini mfalme wa Ashuru akalihamasisha jeshi lake kubwa, akawatuma Tartani na Rabsarisi na amiri jeshi mkuu kutoka Lakishi kwenda kwa Hezekia huko Yerusalemu. Wakasafiri hadi kwenye mabarabara na kufika nje ya Yerusalemu. Wakakaribia karibu na mfereji wa birika la juu, kwenye barabara kuu ya shamba la dobi, na kusimama hapo.
18 Wakaagiza mfalme aitwe. Eliakimu mwana wa Hilkia aliyekuwa msimamizi wa jumba la mfalme, Shebna aliyekuwa katibu, na Yoa mwana wa Asafu mwandishi wakawaendea.
Wakati walipokuwa wamemwita Mfalme Hezekia, Eliakimu mwana wa Hilkia, ambaye alikuwa kiongozi wa nyumba ya mfalme na Shebna mwandishi, na Joa mwana wa Asafu, anayeandika kumbukumbu, wakatoka nje kwenda kuwalaki
19 Yule jemadari wa jeshi akawaambia, “Mwambieni Hezekia: “‘Hili ndilo asemalo mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni wapi unapoweka hili tumaini lako?
Basi yule amiri jeshi mkuu akawaambia wamwambie Hezekia kile alichosema mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru, amesema: “Nini chanzo cha ujasiri wako?
20 Unasema mnayo mikakati na nguvu za kijeshi, lakini unasema maneno matupu tu. Je, wewe unamtegemea nani, hata ukaniasi mimi?
Unaongea maneno yasiyo na maana, kusema lipo neno na nguvu ya vita. Sasa unamtumainia nani? Nani anakupa ujasiri wa kuasi dhidi yangu?
21 Tazama sasa, unaitegemea Misri, fimbo ile ya mwanzi uliopasuka, ambayo huuchoma na kuujeruhi mkono wa mtu akiiegemea! Hivyo ndivyo alivyo Farao mfalme wa Misri, kwa wote wanaomtegemea.
Tazama, unatumainia kutembelea fimbo ya mwanzi huu uliopondeka wa Misri, lakini kama mtu akiutegemea, utamchapa kwenye mkono wake na kuutoboa. Hicho ndicho Farao mfalme wa Misri kwa ymtu yeyote ambaye anayemtumainia.
22 Nawe kama ukiniambia, “Tunamtumainia Bwana Mungu wetu”: je, siyo yeye ambaye Hezekia aliondoa mahali pake pa juu pa kuabudia miungu na madhabahu zake, akiwaambia Yuda na Yerusalemu, “Ni lazima mwabudu mbele ya madhabahu haya katika Yerusalemu”?
Lakini kama ukiniambia, 'Tunamwamini Yahwe Mungu watu; je si yeye ambaye mahali pa juu na madhabahu Hezekia amezichukua, na kumwambia Yuda na kwa Yerusalemu, 'Lazima uabudu mbele ya hii madhabahu katika Yerusalemu'?
23 “‘Njooni sasa, fanyeni mapatano na bwana wangu, mfalme wa Ashuru: Nitakupa farasi elfu mbili, kama unaweza kuwapandisha waendesha farasi juu yao!
Basi kwa hiyo, nataka kukufanyia ahadi nzuri kutoka kwa bwana wangu mfalme wa Ashuru. Nitakupatia farasi elfu mbili, kama unaweza kuwatafuta kuwaendesha kwa ajili yao.
24 Utawezaje kumzuia hata afisa mmoja aliye mdogo kati ya maafisa wa bwana wangu, ijapo unategemea Misri kwa magari ya vita na wapanda farasi?
Wanawezaje kumpinga hata nahodha mmoja wa watumishi walio wadogo? Mmeweka tumaini lenu katika Misri kwa magari ya farasi na waendesha farasi!
25 Zaidi ya hayo, je, nimekuja kushambulia na kuangamiza mahali hapa pasipo neno kutoka kwa Bwana? Bwana mwenyewe ndiye aliniambia niishambulie nchi hii na kuiangamiza.’”
Je nimesafiri kwenda huko juu bila Yahwe kupapigania hapa mahali na kupaharibu? Yahwe ameniambia, 'Ishambulie hii nchi na uiharibu.”'
26 Ndipo Eliakimu mwana wa Hilkia, Shebna na Yoa wakamwambia yule jemadari wa jeshi, “Tafadhali zungumza na watumishi wako kwa lugha ya Kiaramu, kwa kuwa tunaifahamu. Usiseme nasi kwa Kiebrania watu walioko juu ya ukuta wakiwa wanasikia.”
Kisha Elikana mwana wa Hilkia, na Shebna, na Joa wakamwambia amiri jeshi mkuu, “Tafadhali ongea na watumishi wako katika lugha ya Kiaramu, kwa kuwa tunaielewa. Usiongee nasi katika lugha ya Yuda katika masikio ya watu ambao wako ukutani.”
27 Lakini yule jemadari wa jeshi akajibu, “Je, bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu tu? Je, hakunituma pia kwa watu walioketi ukutani, ambao, kama ninyi, itawabidi kula mavi yao na kunywa mikojo yao wenyewe?”
Lakini yule amiri jeshi mkuu akawaambia, “Je bwana wangu amenituma kwa bwana wako na kuwachukua kuongea haya maneno? Je hajanituma kwa hawa watu ambao wameketi kwenye ukuta, ambao watakula kinyesi chao na kunywa mkojo wao wenyewe?”
28 Kisha yule jemadari wa jeshi akasimama na kuita kwa lugha ya Kiebrania, akasema: “Sikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru!
Kisha yule amiri jeshi mkuu akasimama na akapiga kelele kubwa kwa lugha ya Kiyahudi, akisema, “Sikilizeni neno la mfalme mkuu, mfale wa Ashuru.
29 Hili ndilo asemalo mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye. Hawezi kuwaokoa mkononi mwangu.
Mfalme asema, 'Msimwache Hezekia akawadanganya, kwa kuwa hataweza kuwaokoa kwenye nguvu yangu.
30 Msikubali Hezekia awashawishi kumtumaini Bwana kwa kuwaambia, ‘Hakika Bwana atatuokoa. Mji huu hautaangukia mikononi mwa mfalme wa Ashuru.’
Msimwache Hezekia akawatumainisha katika Yahwe, akisema, “Yahwe atatuokoa hakika, na huu mji hautawekwa kwenye mkono wa mfalme wa Ashuru.'”
31 “Msimsikilize Hezekia. Hili ndilo mfalme wa Ashuru asemalo: Fanyeni amani nami na mje kwangu. Kisha kila mmoja wenu atakula kutoka kwa mzabibu wake na mtini wake mwenyewe, na kunywa maji kutoka kisima chake mwenyewe,
Msikilize Hezekia, kwa kuwa hivi ndivyo mfalme wa Ashuru asemavyo: 'Fanyeni amani pamoja nami na njooni kwangu. Kisha kila mmoja wenu atakula kutoka kwenye mzabibu wake mwenyewe na kutoka kwenye mtini wake mwenyewe, na kunywa kutoka kwenye maji kwenye maji ya birika lake mwenyewe.
32 mpaka nije nikawapeleke katika nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai mpya, nchi ya mkate na mashamba ya mizabibu, nchi ya mizeituni na asali. Chagueni uzima, sio mauti! “Msimsikilize Hezekia, kwa kuwa anawapotosha asemapo, ‘Bwana atatuokoa.’
Mtafanya hivyo hadi nitakapokuja na kuwachukua kwenda kwenye nchi kama nchi yenu, nchi ya nafaka na divai, nchi ya mkate na mashamba ya mizabibu, nchi ya miti ya mizaituni na asali, ili muweze kuishi na sio kufa.' Msimsikilize Hezekia wakati atakapojaribu kuwashawishi, akisema, 'Yahwe atatuokoa.'
33 Je, yuko mungu wa taifa lolote aliyewahi kuokoa nchi yake kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru?
Je miungu yeyote ya watu inayewaokoa kutoka kwenye nchi ya mfalme wa Ashuru?
34 Iko wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, Hena na Iva? Je, imeokoa Samaria kutoka mkononi mwangu?
Iko wapi miungu ya Hamathi na Arpadi? iko wapi miungu ya Sefarvaimu, Hena, na Iva? Je imeiokoa Samaria kutoka mkono wangu?
35 Ni yupi miongoni mwa miungu yote ya nchi hizi ameweza kuokoa nchi yake mkononi mwangu? Inawezekanaje basi Bwana aiokoe Yerusalemu mkononi mwangu?”
Miongoni mwa miungu yote ya nchi, je kuna mungu ambaye ameiokoa nchi yake kutoka kwenye nguvu yangu? Inawezekanaje Yahwe akaiokoa Yerusalemu kutoka kwenye uwezo wangu?”
36 Lakini wale watu wakakaa kimya, wala hawakujibu lolote, kwa kuwa mfalme alikuwa amewaamuru, “Msimjibu lolote.”
Lakini watu wakabaki kimya na hawakujibu, kwa kuwa mfalme alikuwa ameamuru, “Msimjibu.”
37 Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna katibu, na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi wakamwendea Hezekia, nguo zao zikiwa zimeraruliwa, na kumwambia yale jemadari wa jeshi aliyoyasema.
Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia, ambaye alikuwa juu ya nyumba ya mfalme; Shebna yule mwandishi; na Joa mwana wa Asafu, mtunza kumbukumbu, akaja kwa Hezekia pamoja na nguo zao zilizoraruliwa, na kumpatia taarifa ya maneno ya yule amiri mkuu.