< 2 Wafalme 17 >

1 Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Ahazi mfalme wa Yuda, Hoshea mwana wa Ela akawa mfalme wa Israeli katika Samaria, akatawala kwa miaka tisa.
Katika mwaka wa kumi na moja wa Ahazi mfalme Yuda, utawala wa Hoshea mwana wa Elahi ulianza. Alitawala katika Samaria juu ya Israeli kwa muda wa miaka minane.
2 Akafanya maovu machoni pa Bwana, lakini si kama wafalme wengine wa Israeli waliomtangulia.
Alifanya yaliyo maovu usoni pa Yahwe, ila sio kama waflme wa Israeli ambao ulikuwa kabla yake.
3 Mfalme Shalmanesa wa Ashuru akainuka dhidi ya Mfalme Hoshea, ambaye hapo mbeleni alikuwa mtumwa wake na kumlipa ushuru.
Shalmanesa mfalme wa Ashuru akamshambulia, na Hoshea akawa mtumishi na kumletea kodi.
4 Lakini mfalme wa Ashuru akagundua kuwa Hoshea alikuwa msaliti, kwa kuwa alikuwa ametuma wajumbe kwa So mfalme wa Misri, naye hakuendelea kulipa ushuru kwa mfalme wa Ashuru tena kama alivyokuwa anafanya kila mwaka. Kwa hiyo Shalmanesa akamkamata na kumtia gerezani.
Kisha mfalme wa Ashuru akaona kwamba Hoshea alikuwa na njama dhidi ya yake, kwa kuwa Hoshea aliwatuma wajumbe kwa So mfalme wa Misri; pia, hakumpatia kodi mfalme wa Ashuru, kama alivyofanya mwaka hadi mwaka.
5 Mfalme wa Ashuru akaishambulia nchi yote, akapigana dhidi ya Samaria na kuizunguka kwa majeshi miaka mitatu.
Basi mfalme wa Ashuru akamfunga akamtia kifungoni. Kisha mfalme wa Ashuru akaishambulia nchi yote, akaishambulia Samaria na kuizunguka kwa miaka mitatu.
6 Katika mwaka wa tisa wa Hoshea, mfalme wa Ashuru akaiteka Samaria na kuwahamishia Waisraeli huko Ashuru. Akawaweka huko Hala, na Gozani karibu na Mto Habori, na katika miji ya Wamedi.
Katika mwaka wa tisa wa Hoshea, mfalme wa Ashuru akaichukua Samaria na akawapeleka Israeli hadi Ashuru. Akawaweka kwenye Hala, kwenye Habori Mto wa Gozani, na katika mji wa Wamedi.
7 Yote haya yalitokea kwa sababu Waisraeli walikuwa wametenda dhambi dhidi ya Bwana Mungu wao, ambaye alikuwa amewapandisha kutoka Misri akiwatoa chini ya utawala wa nguvu wa Farao mfalme wa Misri. Waliabudu miungu mingine
Utekwaji huu ulitokea kwa sababu wana wa Israeli walifanya dhambi dhidi ya Yahwe Mungu wao, ambaye aliwaleta kutoka nchi ya Misri, kutoka chini ya mkono wa Farao mfalme wa Misri. Watu walikuwa wakiabudu miungu mingine
8 na kufuata desturi za mataifa ambayo Bwana alikuwa ameyafukuza mbele yao, pamoja na desturi ambazo wafalme wa Israeli walizileta.
na kutembea katika matendo ya wamataifa ambao Yahwe aliwafukuza mbele ya watu wa Israeli, na katika matendo ya wafalme wa Israeli ambayo waliyokuwa wameyafanya.
9 Waisraeli wakafanya vitu kwa siri dhidi ya Bwana Mungu wao, ambavyo havikuwa sawa. Kuanzia kwenye mnara wa ulinzi hadi kwenye mji wenye maboma walijijengea wenyewe mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji yao yote.
Wana wa Israeli wakafanya kwa siri mambo mabaya dhidi ya Yahwe Mungu wao. Wakajijengea mahala pa juu katika miji yao yote, kutoka mnara wa walinzi hadi mji wenye boma.
10 Wakaweka mawe ya kuabudiwa na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti uliotanda.
Pia wakasimamisha nguzo za mawe na Ashera juu ya kila mlima chini ya kila mti mbichi.
11 Wakafukiza uvumba kila mahali palipoinuka, kama yalivyofanya yale mataifa ambayo Bwana alikuwa ameyafukuza mbele yao. Wakafanya mambo maovu ambayo yalimghadhibisha Bwana.
Huko wakafukiza ubani katika mahali pa juu pote, kama mataifa walivyokuwa wamefanya, ambao Yahwe aliwafukuza mbele yao. Waisraeli wakafanya mambo maovu ili kuchochea hasira ya Yahwe,
12 Wakaabudu sanamu, ingawa Bwana alikuwa amesema, “Msifanye mambo haya.”
wakaabudu sanamu, ambazo Yahwe alizokuwa amewaambia, “Msifanye jambo hili.”
13 Bwana akawaonya Israeli na Yuda kupitia kwa manabii na waonaji wake wote: “Acheni njia zenu mbaya. Shikeni amri na maagizo yangu, kufuatana na sheria yangu yote niliyowaagiza baba zenu kuitii ambayo niliileta kwenu kupitia kwa watumishi wangu manabii.”
Bado Yahwe aliwashuhudia Israeli na Yuda kwa kila nabii na kila muonaji, kusema, “Geukeni kutoka nija zenu mbaya na kuzishika amri zangu na hukumu zangu, na kuwa makini kufuata ile sheria yote niliyowaamuru baba zenu, na ambayo niliwapelekea kwa watumishi wangu manabii.”
14 Lakini hawakusikiliza, walikuwa na shingo ngumu kama baba zao, ambao hawakumtegemea Bwana Mungu wao.
Lakini hawakuweza kusikia; badala yake walikuwa wakaidi kama baba zao ambao hawakumwamini Yahwe Mungu wao.
15 Walizikataa amri zake, na agano alilokuwa amelifanya na baba zao, na maonyo aliyokuwa amewapa. Wakafuata sanamu zisizofaa, nao wenyewe wakawa hawafai. Wakayaiga mataifa yaliyowazunguka, ingawa Bwana alikuwa amewaonya akiwaambia, “Msifanye kama wanavyofanya,” nao wakafanya mambo ambayo Bwana alikuwa amewakataza wasifanye.
Walizikataa sheria zake na lile agano ambalo alilifanya pamoja na babu zao, na hilo agano wakakubaliana wapewe. Wakafuata mambo yao yasiyofaa na wakawa hawafai. Wakawafuata mataifa ya kipagani ambao waliwazunguka, ambao Yahwe alikuwa amewaamuru wasiige.
16 Wakayaacha maagizo yote ya Bwana Mungu wao na kujitengenezea sanamu mbili, walizozisubu katika sura ya ndama na nguzo ya Ashera. Wakasujudia mianga yote ya angani, na wakamtumikia Baali.
Wakazipuuza amri zote za Yahwe Mungu wao. Wakatengeneza sanamu za kusubu za ndama wawili kuziabudu. Wakatengeza nguzo ya Ashera, na wakaziabudu nyota zote za mbinguni na Baali.
17 Wakawatoa kafara wana wao na mabinti zao katika moto. Wakafanya uaguzi na uchawi, nao wakajiuza wenyewe katika kutenda uovu machoni pa Bwana, wakamghadhibisha.
Wakawatupia watoto wao wakike kwa wakiume kwenye moto, wakapiga ramli na uchawi, wakajiuza wenyewe kufanya yale ambayo yalikuwa maovu usoni pa Yahwe, na kuichochea hasira yake.
18 Basi Bwana akawakasirikia sana Israeli na kuwaondoa kwenye uwepo wake. Ni kabila la Yuda tu lililobaki;
Kwa hiyo Yahwe alikuwa na hasira na Israeli na kuwaondoa usoni mwake. Hakubakia mtu hata mmoja isipokuwa kabila la Yuda peke yake.
19 na hata hivyo nao Yuda hawakuzishika amri za Bwana Mungu wao. Wakafuata desturi ambazo Israeli walikuwa wamezianzisha.
Hata watu wa Yuda hawakushika amri za Yahwe Mungu wao, lakini badala yake walifuata mambo hayo hayo ya kipagani ambayo Israeli walifuata.
20 Kwa hiyo Bwana aliwakataa watu wote wa Israeli; akawatesa na kuwaachia katika mikono ya wateka nyara hadi alipowaondoa kutoka kwenye uwepo wake.
Hivyo Yahwe akawakataa vizazi vyote vya Israeli; akawatesa na kuwatia kwenye mkono wa wale wenye kuwateka nyara, hadi atakapokuwa amewatupa usoni mwake.
21 Alipokwisha kuwatenga Israeli mbali na nyumba ya Daudi, wakamfanya Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme wao. Yeroboamu akawashawishi Israeli waache kumfuata Bwana na akawasababisha kutenda dhambi kuu.
Akawatoa Israeli kutoka kwenye mstari wa kifalme wa Daudi, na wakamfanya Yeroboamu mwana wa Nabeti mfalme. Yeroboamu akawapeleka Israeli mbali kutoka kumfuata Yahwe na kuwafanya wafanye dhambi kubwa.
22 Nao Israeli wakadumu katika dhambi zote za Yeroboamu mwana wa Nebati, nao hawakuziacha
Wana wa Israeli wakafuata dhambi zote za Yeroboamu na hawakujiepusha nazo,
23 hadi Bwana alipowaondoa kutoka kwenye uwepo wake, kama vile alivyokuwa ameonya kupitia watumishi wake wote manabii. Hivyo watu wa Israeli wakaondolewa kutoka nchi yao kwenda uhamishoni Ashuru, nao wako huko mpaka sasa.
basi Yahwe akawaondoa Israeli kutoka usoni pake, kama alivyokuwa amesema kupitia watumishi wake wote manabii kwamba angeweza kufanya. Hivyo Israeli walichukuliwa kutoka nchi yao kwenda Ashuru, na iko hivyo hata leo.
24 Mfalme wa Ashuru akawaleta watu kutoka Babeli, Kutha, Ava, Hamathi na Sefarvaimu na kuwaweka katika miji ya Samaria badala ya Waisraeli. Wakaimiliki Samaria na kuishi katika miji yake.
Mfalme wa Ashuru akawaleta watu kutoka Babeli na kutoka Kutha, na kutoka Ava, na kutoka Hamathi na Sefarvaimu, na kuwaweka katika mji wa Samaria na kuishi katika huo mji wake.
25 Wakati walianza kuishi humo, hawakumwabudu Bwana, kwa hiyo akatuma simba miongoni mwao, wakawaua baadhi ya watu.
Ikatokea wakati walipoanza kuishi huko hawakumcha Yahwe. Hivyo Yahwe akatuma simba miongoni mwao ambao waliwaua baadhi yao.
26 Habari ikapelekwa kwa mfalme wa Ashuru, kusema: “Watu uliowahamisha na kuwaweka katika miji ya Samaria hawajui kile Mungu wa nchi hiyo anachokitaka. Ametuma simba miongoni mwao, ambao wanawaua, kwa sababu watu hawajui anachokitaka.”
Basi wakaongea na mfalme wa Ashuru, wakisema, “Wale mataifa uliowaamisha na kuwaweka kwenye miji ya Samaria hawayajui mambo wanayotakiwa kuyafanya kutokana na mungu wa nchi. Hivyo alikuwa amewatuma simba kwenda kwao, na, tazama, wale simba walikuwa wakiwauua watu huko kwa sababu hawakufahamu yale mambo waliyokuwa wanatakiwa kuyafanya kwa mungu wa nchi.”
27 Ndipo mfalme wa Ashuru akaamuru hivi: “Mtwae mmoja wa makuhani uliowachukua mateka kutoka Samaria ili arudi kuishi humo na awafundishe watu kile ambacho Mungu wa nchi anataka.”
Kisha mfalme wa Ashuru akatoa amri, akisema, “Mchukueni mmoja wa makuhani hapo ambaye mmemleta kutoka huko, na mumwache aende na kuishi huko, na mumwache awafundishe mambo yanayotakiwa kwa mungu wa nchi.”
28 Basi mmoja wa makuhani ambaye alikuwa amepelekwa uhamishoni kutoka Samaria akaja kuishi Betheli na kuwafundisha jinsi ya kumwabudu Bwana.
Hivyo mmoja wa makuhani ambaye walimchukua kutoka Samaria akaja na kuishi katika Betheli; akawafundisha jinsi wavyotakiwa mcha Yahwe.
29 Hata hivyo, kila kikundi cha taifa lililoletwa Samaria kilitengeneza miungu yao wenyewe katika miji kadhaa mahali walipoishi, nao wakaiweka mahali pa ibada za miungu ambapo watu wa Samaria walikuwa wametengeneza katika mahali pa juu.
Watu wa kila kabila wakajifanyia miungu yao wenyewe, na kuiweka mahala pa juu ambapo Wasamaria walifanya kila kabila katika mji ambako walipoishi.
30 Watu kutoka Babeli wakamtengeneza Sukoth-Benothi kuwa mungu wao, watu kutoka Kutha wakamtengeneza Nergali, na watu kutoka Hamathi wakamtengeneza Ashima;
Watu wa Babeli wakatengeneza Sakoth Benithi; watu wa Sakoth wakatengeneza Nergali; watu wa Hamathi wakatengeza Ashima;
31 Waavi wakatengeneza Nibhazi na Tartaki, nao Wasefarvi wakachoma watoto wao kama kafara kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu.
Waavi wakatengeneza Nibhazi na Tartaki. Nao Wasefarvi wakwachoma watoto wao kwenye moto kwa Adrameleki na Anameleki, wale miungu wa Sefarvaimu.
32 Walimwabudu Bwana, lakini pia waliteua aina zote za watu wao ili kuwawakilisha kama makuhani katika mahali pa kuabudia miungu kwenye mahali pa juu pa ibada.
Pia wakamcha Yahwe, na kuwateua kutoka miongoni mwao makuhani wa mahali pa juu, ambao waliteketeza kwa ajili yao kwenye hekalun mahali pa juu.
33 Walimwabudu Bwana, lakini pia waliitumikia miungu yao kulingana na desturi za mataifa walikotoka.
Wakamcha Yahwe na pia kuabudu miungu yao wenyewe, sawa sawa na tamaduni za mataifa kutoka miongoni mwao waliokuwa wamewachukua.
34 Mpaka leo wanashikilia desturi zao za zamani. Hawamwabudu Bwana wala kuzishika hukumu na maagizo, sheria na amri ambazo Bwana aliwapa uzao wa Yakobo, ambaye alimwita Israeli.
Hadi siku hii ya leo wameshikilia tamaduni zao za zamani. Wala hawamwogopi Yahwe, wala hawazifuati sheria zake, torati, au amri ambazo Yahwe aliwapa watu wa Yakobo ambaye alemwita jina Israeli
35 Wakati Bwana alipofanya Agano na Waisraeli, aliwaamuru akisema: “Msiiabudu miungu mingine yoyote wala kuisujudia, wala kuitumikia wala kuitolea dhabihu.
pamoja na ambao Yahwe alifanya agano nao na kuwaamuru, “Msiiche miungu mingine, wala kuisujudia, wala kuiabudu, wala kuitolea sadaka.
36 Bali imewapasa kumwabudu Bwana aliyewapandisha kutoka Misri kwa uwezo wake mkuu na kwa mkono wake ulionyooshwa. Kwake yeye mtasujudu na kwake yeye mtatoa dhabihu.
Lakini Yahwe, ambaye aliwatoa kutoka nchi ya Misri kwa nguvu kubwa na mkono ulionyooshwa, yeye ndiye mnayetakiwa kumwabudu, yeye ndiye manayetakiwa kumsujudia, na yeye ndiye mnayetakiwa kumtolea sadaka.
37 Imewapasa daima kuwa waangalifu kutunza hukumu na maagizo, sheria na amri alizowaandikia. Msiabudu miungu mingine.
Na sheria na hukumu, na torati na amri ambazo alizoziandika kwa ajili yenu, mtazishika milele. Hivyo msiiche miungu mingine,
38 Msisahau agano nililofanya nanyi, wala msiabudu miungu mingine.
na agano ambalo nimelifanya pamoja nanyi, hamtalisahau; wala kuicha miungu mingine.
39 Bali, mtamwabudu Bwana Mungu wenu, kwani yeye ndiye atakayewakomboa kutoka mikononi mwa adui zenu wote.”
Lakini Yahwe Mungu wenu, ndiye ambaye mtakayemcha. Atawalinda mbali na nguvu ya maadui zenu,”
40 Hata hivyo hawakusikiliza, lakini waliendelea na desturi zao za awali.
Hawatasikia, kwasababu waliendelea kufanya yale waliyokuwa wameyafanya nyuma.
41 Hata wakati watu hawa walipokuwa wanamwabudu Bwana, walikuwa bado wakitumikia sanamu zao. Mpaka leo watoto wao na watoto wa watoto wao wanaendelea kufanya kama baba zao walivyofanya.
Hivyo haya mataifa wakamcha Yahwe na pia wakaabudu sanamu zao za kuchonga, na watoto wao wakafanya hivyo hivyo na watoto wa watoto wao. Wakaendelea kufanya yale ambayo babu zao waliyoyafanya, hata leo.

< 2 Wafalme 17 >