< 2 Wafalme 13 >

1 Katika mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wa Yoashi mwana wa Ahazia mfalme wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala Israeli katika Samaria, naye akatawala miaka kumi na saba.
Katika mwaka wa ishirini na tatu wa Yoashi mwana wa Ahazia mfalme wa Yuda, Yehoazi mwana wa Yehu alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; alitawala miaka kumi na saba.
2 Akafanya maovu machoni pa Bwana kwa kufuata dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda, na wala hakuziacha.
Alifanya yaliyo maovu usoni mwa Yahwe na kufuata dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye alisababisha Israeli kuasi; na Yehoazi hakurudi kutoka kwao
3 Kwa hiyo hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Israeli na kwa muda mrefu akawaweka chini ya utawala wa Hazaeli mfalme wa Aramu, na Ben-Hadadi mwanawe.
Hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, na akaendelea kuwakabidhi kwenye mikono ya Hazaeli mfalme wa Shamu na kwenye mikono ya Ben Hadadi mwana wa Hazaeli.
4 Ndipo Yehoahazi akamsihi Bwana rehema, naye Bwana akamsikiliza, kwa maana aliona jinsi mfalme wa Aramu alivyokuwa akiwatesa Israeli vikali.
Hivyo Yehoazi akamsihi Yahwe, na Yahwe akamsikiliza kwa sababu aliona mateso ya Israeli, vile mfalme wa Shamu alivyokuwa akiwatesa.
5 Bwana akamtoa mwokozi kwa ajili ya Israeli, nao wakaokoka kutoka kwenye mamlaka ya Aramu. Hivyo Waisraeli wakaishi katika nyumba zao wenyewe kama ilivyokuwa hapo awali.
Basi Yahwe akawapa Israeli ulinzi, na wakakimbia kutoka kwenye mikono ya Washami, na watu wa Israeli wakaanza kuishi kwenye nyumba zao kama walivyokuwa kabla.
6 Lakini hawakuziacha dhambi za nyumba ya Yeroboamu, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda, bali wakaendelea kuzitenda. Nguzo ya Ashera pia iliendelea kusimama katika Samaria.
Hata hivyo, hawakuziacha dhambi za nyumba ya Yeroboamu, ambaye alisabisha Israeli kuasi, na wakaendelea katika hayo; na huyo Ashera akabaki hivyo katika Samaria.
7 Hapakubaki kitu chochote katika jeshi la Yehoahazi isipokuwa wapanda farasi hamsini, magari kumi ya vita na askari wa miguu elfu kumi, kwa kuwa mfalme wa Aramu alikuwa amewaangamiza hao wengine na kuwafanya kama mavumbi wakati wa kupura nafaka.
Washami wakamuacha Yehoazi pamoja na waendesha farasi hamsini tu, magari ya farasi kumi, na watembea kwa miguu elfu kumi, kwa ajili ya mfalme wa Shamu alikuwa ameiharibu na kuwafanya kama makapi yaliyopurwa.
8 Matukio mengine ya utawala wa Yehoahazi yote aliyoyafanya na mafanikio yake, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
Kama mambo mengine yanayomuhusu Yehoazi, na yote aliyoyafanya na nguvu zake, je hayakuandikwa kwenye kitabu cha matukio ya wafalme wa Israeli?
9 Yehoahazi akalala pamoja na baba zake, akazikwa huko Samaria. Naye Yehoashi mwanawe akawa mfalme baada yake.
Basi Yehoyazi akalala na mababu zake, na wakamzika katika samaria. Yohoashi mwanaye akawa mfalme katika sehemu yake.
10 Katika mwaka wa thelathini na saba wa utawala wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yehoashi mwana wa Yehoahazi alianza kutawala Israeli huko Samaria, naye akatawala miaka kumi na sita.
Katika mwaka wa thelathini na saba wa Yoashi mfalme wa Yuda, utawala wa Yehoashi mwana wa Yehoazi ulianza juu ya Israeli katika Samaria; alitawala miaka kumi na sita.
11 Alifanya maovu machoni pa Bwana, na hakuacha dhambi yoyote kati ya zile za Yeroboamu mwana wa Nebati ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda, bali aliendelea kuzitenda.
Akafanya yaliyo maovu kwenye uso wa Yahwe. Hakuacha nyuma dhambi zozote za Yeroboamu mwana wa Nebati, kwa kuwa aliwafanya Israeli kuasi, lakini alitembea pamoja nao.
12 Na kwa matukio mengine ya utawala wa Yehoashi, yote aliyoyafanya na mafanikio yake, pamoja na vita yake dhidi ya Amazia mfalme wa Yuda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
Kama kwa mambo mengine yanayomuhusu Yehoashi, na yote aliyoyafanya, na shujaa wake ambaye aliyepigana dhidi ya Amazia mfalme wa Yuda, je hayakuandikwa kwenye kitabu cha matukio ya wafalme wa Israeli?
13 Yehoashi akalala pamoja na baba zake, akazikwa Samaria pamoja na wafalme wa Israeli. Yeroboamu akawa mfalme baada yake.
Yehoashi akalala na mababu zake, na Yeroboamu akakalia kiti chake cha enzi cha kifalme. Yehoashi akazikwa katika Samaria pamoja na wafalme wa Israeli.
14 Wakati huu, Elisha alikuwa anaumwa na ugonjwa ambao baadaye ulimuua. Yehoashi mfalme wa Israeli akashuka kwenda kumwona na kumlilia. Akalia, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya vita ya Israeli na wapanda farasi wake!”
Basi Elisha akaugua ugonjwa ambao baadae ulimuua, hivyo Yehoashi yule mfalme wa Israeli akashuka chini kwake na kumlilia juu yake. Akasema, “Baba yangu, baba yangu, haya magari ya farasi ya Israeli na hawa waendesha farasi wanakuchukua!”
15 Elisha akasema, “Leta upinde na baadhi ya mishale,” naye mfalme akafanya hivyo.
Elisha akamwambia, “Chukua upinde na mishale,” basi Yoashi akachukua upinde na mishale.
16 Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, “Shika upinde mikononi mwako.” Alipokwisha kuichukua, Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme.
Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, “Weka mkono wako kwenye upinde,” basi akaweka mkono wake kwenye huo. Kisha Elisha akalaza mikono yake kwenye mikono ya mfalme.
17 Elisha akasema, “Fungua dirisha la mashariki,” naye akalifungua. Elisha akasema, “Piga mshale!” Naye akapiga mshale. Elisha akasema, “Mshale wa ushindi wa Bwana, mshale wa ushindi juu ya Aramu! Utawaangamiza Waaramu kabisa huko Afeki.”
Elisha akasema, “Fungua dirisha upande wa mashariki,” basi akalifungua. Kisha Elisha akasema, “Funga”, na akafunga. Elisha akasema, “Huu ndiyo mshale wa ushindi wa Yahwe, huu mshale wa ushindi juu ya Shamu, kwa kuwa utawapiga Washami katika Afeki hadi utakapowaangamiza.”
18 Kisha akasema, “Chukua mishale,” naye mfalme akaichukua. Elisha akamwambia, “Piga ardhi kwa hiyo mishale.” Akaipiga mara tatu, halafu akaacha.
Kisha Elisha aksema, “Chukua mishale,” basi Yoashi akaichukua. Akamwambia mfalme wa Israeli, “Piga chini pamoja nao,” na akapiga chini mara tatu, kisha akaacha.
19 Mtu wa Mungu akamkasirikia na akasema, “Ungepiga chini mara tano au sita, ndipo ungeishinda Aramu na kuiangamiza kabisa. Lakini sasa utaishinda mara tatu tu.”
Lakini mtu wa Mungu alikuwa na hasira naye na akasema, “Ungelipiga chini mara tano au mara sita. Ndipo ungeipiga Shamu hadi kuiangamiza, lakini sasa utaipiga Shamu mara tatu tu.”
20 Elisha akafa, nao wakamzika. Vikosi vya Wamoabu vilikuwa vinashambulia nchi kwa vita kila mwaka wakati wa vuli.
Kisha Elisha akafa, na wakamzika. Sasa vikundi vya Wamoabi wakaingia kwenye nchi mwanzoni mwa mwaka.
21 Ikawa Waisraeli fulani walipokuwa wanamzika mtu, ghafula wakaona kikosi cha washambuliaji, basi wakaitupa ile maiti ya yule mtu ndani ya kaburi la Elisha. Wakati ile maiti ilipogusa mifupa ya Elisha, yule mtu akafufuka na kusimama kwa miguu yake.
Ikawa walipokuwa wakimzika huyo mtu, wakaona kundi la Wamoabi, hivyo wakautupia ule mwili kwenye kaburi la Elisha. Mara yule mtu alipoigusa mifupa ya Elisha, alifufuka na kusimama kwa miguu yake.
22 Hazaeli mfalme wa Aramu aliwatesa Israeli wakati wote wa utawala wa Yehoahazi.
Hazaeli mfalme wa Shamu akawatesa Israeli siku zote za Yehoazi.
23 Lakini Bwana akawarehemu na akawahurumia, akaonyesha kujishughulisha nao kwa sababu ya Agano lake na Abrahamu, Isaki na Yakobo. Hadi leo, hajawaangamiza wala kuwafukuza mbele zake.
Lakini Yahwe aliwahurumia Israeli, na alikuwa na huruma juu yao na kushuhulika kwa ajili yao, kwa sababu ya agano lake na Ibrahimu, Isaka, na Yakobo. Hivyo Yahwe hakuwaangamiza, na bado hakuwatupa kutoka kwenye uwepo wake.
24 Hazaeli mfalme wa Shamu akafa, naye Ben-Hadadi mwanawe akawa mfalme baada yake.
Hazaeli mfalme wa Shamu akafa, na Ben Hadadi mtoto wake akawa mfalme katika sehemu yake.
25 Kisha Yehoashi mwana wa Yehoahazi akateka tena kutoka kwa Ben-Hadadi mwana wa Hazaeli ile miji aliyokuwa ameitwaa kwa vita kutoka kwa baba yake Yehoahazi. Yehoashi alimshinda mara tatu, hivyo akaweza kuiteka tena ile miji ya Waisraeli.
Yehoashi mwana wa Yehoazi akairudisha kutoka kwa Ben Hadadi mwana wa Hazaeli miji ambayo aliichukua kutoka Yehoazi baba yake kwa vita. Yehoashi akamshambulia mara tatu, na akaipata miji ya Israeli.

< 2 Wafalme 13 >