< 2 Wafalme 11 >
1 Wakati Athalia mamaye Ahazia alipoona kuwa mwanawe amekufa, akainuka na kuiangamiza jamaa yote ya mfalme.
2 Lakini Yehosheba, binti wa Mfalme Yehoramu, aliyekuwa pia dada yake Ahazia, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia kwa siri kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Akamweka Yoashi pamoja na yaya wake ndani ya chumba cha kulala na kumficha humo ili Athalia asimwone; kwa hiyo hakuuawa.
3 Alibaki amefichwa pamoja na yaya wake katika Hekalu la Bwana kwa muda wa miaka sita wakati Athalia alikuwa akitawala nchi.
4 Katika mwaka wa saba, Yehoyada akatumania wakuu wa vikundi vya mamia, na Wakari, na walinzi, nao wakaletwa kwake katika Hekalu la Bwana. Alifanya agano nao na kuwaapisha katika Hekalu la Bwana. Ndipo akawaonyesha mwana wa mfalme.
5 Akawaamuru akisema, “Hivi ndivyo iwapasavyo kufanya: Ninyi ambao mko makundi matatu mnaoingia zamu siku ya Sabato, theluthi yenu inayolinda jumba la kifalme,
6 theluthi nyingine Lango la Suri, na theluthi nyingine lango lililo nyuma ya walinzi, ambao hupeana zamu kulinda Hekalu,
7 nanyi ambao mko katika makundi mengine mawili ambao kwa kawaida hupumzika Sabato, wote mtalinda Hekalu kwa ajili ya mfalme.
8 Jipangeni kumzunguka mfalme, kila mtu akiwa na silaha yake mkononi. Yeyote anayesogelea safu zenu lazima auawe. Kaeni karibu na mfalme popote aendapo.”
9 Wakuu wa vikosi vya mamia wakafanya kama vile kuhani Yehoyada aliagiza. Kila mmoja akawachukua watu wake, wale waliokuwa wakiingia zamu siku ya Sabato na wale waliokuwa wakienda mapumziko, nao wakaja kwa kuhani Yehoyada.
10 Ndipo akawapa wale wakuu mikuki na ngao zilizokuwa za Mfalme Daudi, zilizokuwa ndani ya Hekalu la Bwana.
11 Wale walinzi, kila mmoja akiwa na silaha yake mkononi mwake, wakajipanga kumzunguka mfalme, karibu na madhabahu na Hekalu, kuanzia upande wa kusini hadi upande wa kaskazini mwa Hekalu.
12 Yehoyada akamtoa mwana wa mfalme na kumvika taji, akampa nakala ya agano, na kumtangaza kuwa mfalme. Wakamtia mafuta, nao watu wakapiga makofi na kupaza sauti, wakisema, “Mfalme aishi maisha marefu!”
13 Athalia aliposikia kelele iliyofanywa na walinzi pamoja na watu, akawaendea watu pale penye Hekalu la Bwana.
14 Akaangalia, na tazama alikuwako mfalme, akiwa amesimama karibu na nguzo, kama ilivyokuwa desturi. Maafisa na wapiga tarumbeta walikuwa pembeni mwa mfalme, nao watu wote wa nchi walikuwa wakifurahi na kupiga tarumbeta. Ndipo Athalia akararua mavazi yake na kulia, “Uhaini! Uhaini!”
15 Kuhani Yehoyada akawaagiza majemadari wa vikosi vya mamia, waliokuwa viongozi wa jeshi, “Mleteni nje kati ya safu, na mkamuue kwa upanga yeyote anayemfuata.” Kwa kuwa kuhani alikuwa amesema, “Hatauawa ndani ya Hekalu la Bwana.”
16 Basi wakamkamata Athalia, na alipofika mahali ambapo farasi huingilia katika viwanja vya jumba la mfalme, wakamuulia hapo.
17 Kisha Yehoyada akafanya agano kati ya Bwana na mfalme na watu kwamba watakuwa watu wa Bwana. Akafanya pia agano kati ya mfalme na watu.
18 Watu wote wa nchi wakaenda kwenye hekalu la Baali na kulibomoa. Wakavunjavunja madhabahu na sanamu, na kumuua Matani kuhani wa Baali mbele ya hayo madhabahu. Kisha Yehoyada kuhani akawaweka walinzi kwenye Hekalu la Bwana.
19 Pamoja naye akawachukua majemadari wa mamia, Wakari, walinzi na watu wote wa nchi, nao kwa pamoja wakamteremsha mfalme kutoka Hekalu la Bwana na kwenda kwenye jumba la mfalme, wakiingilia njia ya lango la walinzi. Ndipo mfalme akachukua nafasi yake kwenye kiti cha enzi,
20 nao watu wote wa nchi wakafurahi. Mji ukatulia, kwa sababu Athalia alikuwa ameuawa kwa upanga nyumbani kwa mfalme.
21 Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala.