< 2 Wafalme 11 >

1 Wakati Athalia mamaye Ahazia alipoona kuwa mwanawe amekufa, akainuka na kuiangamiza jamaa yote ya mfalme.
Basi Athalia, mama yake na Ahazia, alipoona kwamba mtoto wake amekufa, aliinuka na kuwaua watoto wote wa kifalme.
2 Lakini Yehosheba, binti wa Mfalme Yehoramu, aliyekuwa pia dada yake Ahazia, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia kwa siri kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Akamweka Yoashi pamoja na yaya wake ndani ya chumba cha kulala na kumficha humo ili Athalia asimwone; kwa hiyo hakuuawa.
Lakini Yehosheba, binti wa mfalme Yehoramu na dada wa Ahazia, akamchukua Yoashi mwana wa Ahazia, na kumficha mbali mwa miongoni mwa watoto wa mfalme waliokuwa wameuawa, wakati wote pamoja na mlezi wake; akawaweka kwenye chumba cha kulala. Wakamficha kutoka Athalia kwa hiyo hakuuawa.
3 Alibaki amefichwa pamoja na yaya wake katika Hekalu la Bwana kwa muda wa miaka sita wakati Athalia alikuwa akitawala nchi.
Alikuwa pamoja na Yehosheba, wamejificha kwenye nyumba ya Yahwe, kwa mda wa miaka sita, wakati Athalia alipotawala juu ya nchi.
4 Katika mwaka wa saba, Yehoyada akatumania wakuu wa vikundi vya mamia, na Wakari, na walinzi, nao wakaletwa kwake katika Hekalu la Bwana. Alifanya agano nao na kuwaapisha katika Hekalu la Bwana. Ndipo akawaonyesha mwana wa mfalme.
Katika mwaka wa saba, Yehoyada alituma ujumbe na kuleta maamiri jeshi mamia wa Wakari na wa walinzi, na kuwaleta kwake mwenyewe, ndani ya nyumba ya Yahwe. Akafanya agano pamoja nao, na kuwaapisha kiapo katika nyumba ya Yahwe. Kisha akawaonyesha mtoto wa mfalme.
5 Akawaamuru akisema, “Hivi ndivyo iwapasavyo kufanya: Ninyi ambao mko makundi matatu mnaoingia zamu siku ya Sabato, theluthi yenu inayolinda jumba la kifalme,
Akawaamuru, akisema, “Hivi ndivyo mnavyotakiwa kufanya. Theluthi yenu mtakaokuja kwenye Sabato mtakuwa mkiiangalia nyumba ya mfalme,
6 theluthi nyingine Lango la Suri, na theluthi nyingine lango lililo nyuma ya walinzi, ambao hupeana zamu kulinda Hekalu,
na theluthi mtakuwa langoni mwa Suri, na theluthi langoni nyuma ya walinzi.”
7 nanyi ambao mko katika makundi mengine mawili ambao kwa kawaida hupumzika Sabato, wote mtalinda Hekalu kwa ajili ya mfalme.
Makundi mengine mawili ambayo hayatumikii Sabato, Mtayalinda juu ya nyumba ya Yahwe kwa ajili ya mfalme.
8 Jipangeni kumzunguka mfalme, kila mtu akiwa na silaha yake mkononi. Yeyote anayesogelea safu zenu lazima auawe. Kaeni karibu na mfalme popote aendapo.”
Ni lazima mumzunguke mfalme, kila mmoja na silaha zake kwenye mkono wake. Yeyote aingiaye ndani ya safu, auwawe. Lazima mkae pamoja na mfalme kila atokapo na kila aingiapo.
9 Wakuu wa vikosi vya mamia wakafanya kama vile kuhani Yehoyada aliagiza. Kila mmoja akawachukua watu wake, wale waliokuwa wakiingia zamu siku ya Sabato na wale waliokuwa wakienda mapumziko, nao wakaja kwa kuhani Yehoyada.
Hivyo mamia ya maamri jeshi wakatii kila kitu Yehoyada kuhani alichokiamuru. Kila mmoja akachukua watu wake, wale ambao walitakiwa kuja kutumika siku ya hiyo Sabato, na wale ambao wataacha kuitumika kwenye hiyo Sabato; ndipo wakaja kwa Yehoyada kuhani.
10 Ndipo akawapa wale wakuu mikuki na ngao zilizokuwa za Mfalme Daudi, zilizokuwa ndani ya Hekalu la Bwana.
Kisha Yehoyada yule kuhani akawapa mikuki na ngao mamia wa maamri jeshi ambayo ilikuwa mali ya mfalme Daudi ambayo ilikuwa kwenye nyumba ya Yahwe.
11 Wale walinzi, kila mmoja akiwa na silaha yake mkononi mwake, wakajipanga kumzunguka mfalme, karibu na madhabahu na Hekalu, kuanzia upande wa kusini hadi upande wa kaskazini mwa Hekalu.
Basi walinzi wakasimama, kila mtu na silaha kwenye mkono wake, kutoka upande wa kuume wa hekalu, kwenda upande wa kushoto, karibu na madhabahu ya hekelu, wakimzunguka mfalme.
12 Yehoyada akamtoa mwana wa mfalme na kumvika taji, akampa nakala ya agano, na kumtangaza kuwa mfalme. Wakamtia mafuta, nao watu wakapiga makofi na kupaza sauti, wakisema, “Mfalme aishi maisha marefu!”
Kisha Yehoyada akamleta nje mtoto wa mfalme Yoashi, na kumvalisha taji la kifalme, na kumpatia mikataba ya agano. Kisha wakamfanya mfalme na kummiminia mafuta. Wakapiga makofi wakisema, “Mfalme na aishi!”
13 Athalia aliposikia kelele iliyofanywa na walinzi pamoja na watu, akawaendea watu pale penye Hekalu la Bwana.
Wakati Athalia aliposikia sauti za walinzi na za watu, alikuja kwa wale watu kwenye nyumba ya Yahwe.
14 Akaangalia, na tazama alikuwako mfalme, akiwa amesimama karibu na nguzo, kama ilivyokuwa desturi. Maafisa na wapiga tarumbeta walikuwa pembeni mwa mfalme, nao watu wote wa nchi walikuwa wakifurahi na kupiga tarumbeta. Ndipo Athalia akararua mavazi yake na kulia, “Uhaini! Uhaini!”
Akatazama, na, kisha, yule mfalme alikuwa amesimama kwenye nguzo, kama ilivyokuwa desturi, na manahodha na wapiga mabaragumu walikuwa karibu na mfalme. Watu wote wa nchi hiyo walikuwa wakifurahi na kupiga matarumbeta. Kisha Athalia akachana mavazi yake kwa hasira na kupiga kelele, “Uhaini! Uhaini!”
15 Kuhani Yehoyada akawaagiza majemadari wa vikosi vya mamia, waliokuwa viongozi wa jeshi, “Mleteni nje kati ya safu, na mkamuue kwa upanga yeyote anayemfuata.” Kwa kuwa kuhani alikuwa amesema, “Hatauawa ndani ya Hekalu la Bwana.”
Ndipo Yehoyada yule kuhani akawaagiza maamri jeshi wa mamia ambao waliokuwa juu ya jeshi, akisema, “Mtoeni kwenye safu.” Atakayemfuata, muueni kwa upanga.” Kwa kuwa kuhani alisema, “Msimwache auawe kwenye nyumba ya Yahwe.”
16 Basi wakamkamata Athalia, na alipofika mahali ambapo farasi huingilia katika viwanja vya jumba la mfalme, wakamuulia hapo.
Hivyo wakamtwaa kadiri walivyokuwa wakiikaribia hiyo sehemu iliyokuwa na farasi wakaingia chini, na akauawa huko.
17 Kisha Yehoyada akafanya agano kati ya Bwana na mfalme na watu kwamba watakuwa watu wa Bwana. Akafanya pia agano kati ya mfalme na watu.
Kisha Yehoyada akafanya agano kati ya Yahwe na mfalme na watu, ambao wangekuwa watu wa Yahwe, na pia kati ya mfalme na watu.
18 Watu wote wa nchi wakaenda kwenye hekalu la Baali na kulibomoa. Wakavunjavunja madhabahu na sanamu, na kumuua Matani kuhani wa Baali mbele ya hayo madhabahu. Kisha Yehoyada kuhani akawaweka walinzi kwenye Hekalu la Bwana.
Basi watu wote wa nchi wakaenda kwenye nyumba ya Baali na kuingusha chini. Wakaangusha madhabahu ya Baali na sanamu zake wakazivunja vipande vipande, na kumuua Matani, mfalme wa Baali, mbele ya haya madhabahu. Kisha Yehoyada kuhani akawachagua walinzi juu ya hekalu la Yahwe.
19 Pamoja naye akawachukua majemadari wa mamia, Wakari, walinzi na watu wote wa nchi, nao kwa pamoja wakamteremsha mfalme kutoka Hekalu la Bwana na kwenda kwenye jumba la mfalme, wakiingilia njia ya lango la walinzi. Ndipo mfalme akachukua nafasi yake kwenye kiti cha enzi,
Yehoyada akawachukua maamiri jeshi wa mamia, Wakari, walinzi, na watu wote wa nchi, na kwa pamoja wakamleta chini mfalme kutoka kwenye nyumba ya Yahwe na wakaenda kwenye nyumba ya mfalme, wakaingia kwa njia ya lango la walinzi. Yoashi akachukua nafasi yake kwenye kiti cha enzi cha mfalme.
20 nao watu wote wa nchi wakafurahi. Mji ukatulia, kwa sababu Athalia alikuwa ameuawa kwa upanga nyumbani kwa mfalme.
Hivyo watu wote wa nchi wakamsifu, na nchi ilikuwa kimya baada ya Athalia kuuawa kwa upanga kwenye nyumba ya mfalme.
21 Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala.
Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba tangu alipoanza kutawala.

< 2 Wafalme 11 >