< 2 Wafalme 10 >
1 Wakati huu katika Samaria walikuwepo wana sabini wa nyumba ya Ahabu. Kwa hiyo Yehu akaandika barua na kuzituma Samaria: kwa maafisa wa Yezreeli, kwa wazee, na kwa walezi wa watoto wa Ahabu. Akasema,
Basi Ahabu alikuwa na watoto sabini katika Samaria. Yehu akaandika barua na kuzituma kwenda Samaria, kwa watawala wa Yezreeli, pamoja na wazee na walinzi wa wana wa Ahabu akisema,
2 “Mara tu barua hii itakapokufikia, kwa kuwa wana wa bwana wako wapo pamoja nawe, nawe una magari ya vita na farasi, mji wenye ngome na silaha,
“Wana wa bwana wako wako pamoja na wewe, na wewe pia una magari ya farasi na farasi na kuimarisha mji dhidi ya maadui na silaha. Hivyo basi, haraka iwezekanavyo barua hii ikufikiapo,
3 mchague mwenye uwezo zaidi kati ya wana wa bwana wako, na umweke juu ya kiti cha enzi cha baba yake. Kisha upigane kwa ajili ya nyumba ya bwana wako.”
mchagueni aliye bora na anayestahili miongoni mwa mtoto wa bwana wenu na kumuweka kwenye kiti cha kifalme cha baba yake, na kupigania ufalme wa bwana wenu.”
4 Lakini wakaogopa sana na kusema, “Ikiwa wafalme wawili hawakuweza kupambana na Yehu, sisi tutawezaje?”
Lakini waliogopa na kusema miongoni mwao, “Tazama, wafalme wawili hawatasimama mbele ya Yehu. Hivyo tutasimamaje?”
5 Basi msimamizi wa jumba la mfalme, mtawala wa mji, na wazee na walezi wakatuma ujumbe huu kwa Yehu: “Sisi tu watumishi wako, na tutafanya kila kitu utakachosema. Hatutamteuwa mtu yeyote kuwa mfalme. Wewe fanya uonalo kuwa ni bora.”
Kisha yule mtu ambaye alikuwa kiongozi kwenye nyumba ya mfalme, na wale waliowalea watoto, wakatuma ujumbe kwa Yehu, kusema, “Sisi ni watumishi wako. Tutafanya chochote utakacho tuamuru. Hatutamfanya mtu yeyote kuwa mfalme. Fanya lile lililojema machoni pako.”
6 Kisha Yehu akawaandikia barua ya pili, akisema, “Ikiwa ninyi mko upande wangu na mtanitii mimi, twaeni vichwa vya wana wa bwana wenu, na mnijie huku Yezreeli kesho wakati kama huu.” Wakati huo wana sabini wa mfalme walikuwa wakiishi pamoja na viongozi wa mji wa Samaria, waliokuwa wakiwalea.
Kisha Yehu akaandika barua mara ya pili, akisema, “Kama mko upande wangu, na kama mtasikiliza sauti yangu, mtachukua vichwa vya watu wa wana wa mabwana wenu, na mje kwangu Yezreeli kesho mda kama huu.” Ndipo wana wa wafalme, sabini kwa hesabu, waliokuwa watu muhimu huko mjini, ambao walikuwa wakiwaleta.
7 Hiyo barua ilipowafikia, watu hawa wakawachukua wale wana sabini wa mfalme na kuwachinja wote. Wakaweka vichwa vyao ndani ya makapu na kumpelekea Yehu huko Yezreeli.
Hivyo barua ilipokuja kwao, waliwachukua wana wa wafalme na kisha kuwaua, watu sabini, wakaweka vichwa vyao kwenye vikapu, na kuivituma kwa Yehu katika Yezreeli.
8 Mjumbe alipofika, akamwambia Yehu, “Wameleta vichwa vya wana wa mfalme.” Ndipo Yehu akaagiza, “Viwekeni malundo mawili katika ingilio la lango la mji mpaka asubuhi.”
Mjumbe mmoja akaja kwa Yehu, akisema, “Wamevileta vile vichwa vya watoto wa wafalme.” Hivyo akasema, viwekeni kwenye mafungu mawili kwenye lango hadi asubuhi.”
9 Asubuhi yake, Yehu akatoka nje. Akasimama mbele ya watu wote na akasema, “Hamna hatia. Ni mimi niliyefanya shauri baya dhidi ya bwana wangu na kumuua, lakini ni nani aliyewaua wote hawa?
Asubuhi Yehu akatoka nje na kusimama, na kusema kwa watu wote, “Ninyi hamna hatia. Tazameni, nimefanya fitina dhidi ya bwana wangu na kumuua, lakini ni nani aliyewaua hawa wote?
10 Fahamuni basi kwamba, hakuna neno ambalo Bwana amesema dhidi ya nyumba ya Ahabu ambalo halitatimia. Bwana amefanya lile aliloahidi kupitia mtumishi wake Eliya.”
Sasa hakika tafakarini kwamba hakuna sehemu ya neno la Yahwe, lile alilonena Yahwe kuhusu familia ya Ahabu, itaanguka kwenye aridhini, kwa kuwa Yahwe amefanya kile alichokiongea kupitia mtumishi wake Eliya.”
11 Hivyo Yehu akaua kila mtu huko Yezreeli aliyekuwa amebaki wa nyumba ya Ahabu, ikiwa ni pamoja na wakuu wake, rafiki zake wa karibu, na makuhani wake. Hakuacha yeyote anusurike.
Basi Yehu akawaua wote waliokuwa wamebakia wa familia ya Ahabu katika Yezreeli, na watu wake muhimu wote, marafiki zake wa karibu, na makuhani wake, hakuna hata mmoja wao alisalia.
12 Kisha Yehu akaondoka kuelekea Samaria. Alipokuwa njiani karibu na nyumba ya kukatia manyoya ya kondoo, yaani, Beth-Ekedi ya wachunga kondoo,
Kisha Yehu akainuka na kuondoka; akaenda Samaria. Kadiri alivyokuwa akikaribia Bethi Ekedi ya wachungaji,
13 Yehu akakutana na watu wa jamaa ya Ahazia mfalme wa Yuda, akauliza, “Ninyi ni nani?” Wao wakasema, “Sisi ni jamaa ya Ahazia, nasi tumeshuka kuwasalimu jamaa ya mfalme na ya mama malkia.”
akamlaki na ndugu wa Ahazia mfalme wa Yuda. Yehu akawaambia, “Ninyi ni akina nani?” Wakajibu, “Sisi ni ndugu zake na Ahazia, na tunashuka chini kuwasalimia watoto wa mfalme na watoto wa Malkia Yezebeli.”
14 Yehu akaagiza, “Wakamateni wakiwa hai!” Kwa hiyo wakawachukua wakiwa hai, watu arobaini na wawili, na kuwachinja kando ya kisima cha Beth-Ekedi. Hakuacha yeyote anusurike.
Yehu akawaambia watu wake mwenyewe, “Wachukue wakiwa hai.” Hivyo wakawachukua wakiwa hai na kuwaua kwenye kisima cha Bethi Ekedi, watu wote arobaini na mbili. Hakumwacha hata mmoja wao akiwa hai.
15 Baada ya kuondoka hapo, alimkuta Yehonadabu mwana wa Rekabu, aliyekuwa akienda kumlaki. Yehu akamsalimu na kusema, “Je, moyo wako ni mnyofu kwangu kama moyo wangu ulivyo kwako?” Yehonadabu akajibu, “Ndiyo.” Yehu akasema, “Kama ndivyo, nipe mkono wako.” Yeye akampa mkono, naye Yehu akampandisha kwenye gari lake la vita.
Baada ya Yehu kuondoka huko, akakutana na Yehonadabu mwana wa Rekabu anakuja kukutana naye. Yehu akamsalimia na kisha akamwambia, “Je moyo wako uko na mimi, kama moyo wangu ulivyo pamoja na wako?” Yehonadabu akajibu, Ndio.” Yehu akasema, “kama ni ndio, nipatie mkono wako.” Kisha Yehonadabu akampatia mkono wake, na Yehu akampandisha Yehonadabu juu kwenye magari ya farasi pamoja naye.
16 Yehu akasema, “Twende pamoja ukaone wivu wangu kwa ajili ya Bwana.” Hivyo wakasafiri pamoja kwenye gari lake.
Yehu akasema, “Fuatana pamoja nami na uone wivu wangu kwa Yahwe.” Hivyo alikuwa na Yehonadabu akiendesha gari la farasi.
17 Yehu alipofika Samaria, akawaua wale wote waliokuwa wamesalia wa jamaa ya Ahabu, akawaangamiza, sawasawa na neno la Bwana alilosema kupitia Eliya.
Wakati alipokuja Samaria, Yehu akawaua wote waliobakia kutoka uzao wa Ahabu katika Samaria, hata akawaangamiza ukoo wa kifalme wa Ahabu, kama walivyokuwa wameambiwa kabla ya neno la Yahwe, ambalo aliloambiwa Eliya.
18 Kisha Yehu akawaleta watu wote pamoja na kuwaambia, “Ahabu alimtumikia Baali kidogo. Lakini Yehu atamtumikia zaidi.
Kisha Yehu akawakusanya watu wote akwaambia, “Ahabu alimtumikia Baali kidogo, lakini Yehu atamtumikia sana.
19 Sasa waiteni manabii wote wa Baali, watumishi wake wote na makuhani wake wote. Hakikisheni kwamba hakuna hata mmoja atakayekosekana, kwa sababu ninakwenda kutoa kafara kubwa sana kwa Baali. Yeyote atakayeshindwa kuja hataendelea kuishi.” Lakini Yehu alifanya hivyo kwa hila ili apate kuwaangamiza watumishi wote wa Baali.
Basi niitieni manabii wote wa Baali, wote wamwabuduo, na makuhani wake wote. Asikosekane mtu hata mmoja, kwa kuwa nina dhabihu kubwa nataka kutoa kwa Baali. Yeyote atakayeshindwa kuja hataishi.” Lakini Yehu alifanya haya kwa udanganyifu, kwa dhamira ya kuwaua wanaomwabudu Baali.
20 Yehu akasema, “Itisheni kusanyiko kwa heshima ya Baali.” Basi wakatangaza jambo hilo.
Yehu akasema, “Tengeni mda tuwe na mkutano kwa ajili ya Baali.” Hivyo wakalitangaza.
21 Kisha Yehu akapeleka ujumbe katika Israeli yote, nao watumishi wote wa Baali wakaja, hakuna hata mmoja ambaye hakufika. Wakasongana ndani ya hekalu la Baali hadi likajaa tangu mlango hadi mwisho wake.
Kisha Yehu akatuma Israeli yote na wamwabuduo Baali waje, hivyo basi hakuna mtu hata mmoja ambaye aliacha kuja. Walikuja kwenye hekalu la Baali, na ilijaa kutoka mwanzo hadi mwisho.
22 Naye Yehu akamwambia yule aliyekuwa mtunza chumba cha mavazi, “Leta majoho kwa ajili ya watumishi wote wa Baali.” Basi akawaletea majoho.
Yehu akamwambia yule mtu aliyekuwa anatunza kabati la nguo za makuhani, “Uwatolee mavazi wote wamwabuduo Baali.” Basi yule mtu akawatolea nguo.
23 Kisha Yehu na Yehonadabu mwana wa Rekabu wakaingia ndani ya hekalu la Baali. Yehu akawaambia watumishi wa Baali, “Tazameni kila mahali mhakikishe kwamba hakuna hata mtumishi mmoja wa Bwana aliye hapa pamoja nanyi, ila ni watumishi wa Baali tu.”
Basi Yehu akaingia pamoja na Yohonadabu mwana wa Rekabu kwenye nyumba ya Baali, na kisha akawaambia wanaomwabudu Baali, “Tafuteni na muhahakishe kwamba hakuna mtu hapa pamoja na ninyi kutoka watumishi wa Yahwe, lakini wamwabuduo Baali peke yao.”
24 Kwa hiyo wakaingia ndani ili kutoa kafara na sadaka ya kuteketezwa. Wakati huu, Yehu alikuwa amewaweka watu wake themanini akiwa amewapa onyo kwamba, “Ikiwa mmoja wenu atamwachia mtu yeyote ninayemweka mikononi mwake atoroke, itakuwa uhai wako kwa uhai wake.”
Kisha wakaenda kutoa dhabihu na sadaka ya kutekeza. Basi Yehu alichagua watu themanini ambao walikuwa wamesimama nje, na aliwaambia, Kama mtu yeyote miongoni mwa hawa watu ambao nimewaleta kwenye mikono yenu atoroke, yeyote atakayemwacha huyo mtu atoroke, maisha yake yatachukuliwa kwa ajili ya yule aliyeokoka.”
25 Mara baada ya Yehu kutoa sadaka ya kuteketezwa, akawaamuru walinzi na maafisa: “Ingieni ndani, waueni; asitoroke hata mmoja.” Basi wakawakatakata kwa upanga. Walinzi na maafisa wakazitupa zile maiti nje, kisha wakaingia mahali pa ndani pa kuabudia miungu katika hekalu la Baali.
Hivyo kisha baada ya mda mfupi Yehu alipomaliza kutoa sadaka ya kutekezwa, akamwambia mlinzi na manahodha, “Ingieni na muwaue. Msimwache mtu yeyote atoke.” Basi waliwaua kwa makali ya upanga, na mlinzi na manahodha wakawatupa nje na kwenda kwenye chumba cha ndani cha nyumba ya Baali.
26 Wakaileta ile nguzo ya kuabudiwa nje ya hekalu la Baali, na wakaichoma moto.
Wakazitoa nguzo za mawe ambazo zilikuwa kwenye nyumba ya Baali, na kisha kuzichoma.
27 Wakabomoa ile nguzo ya kuabudiwa ya Baali pamoja na hekalu la Baali, nao watu wakapafanya kuwa choo hadi leo.
Kisha wakazivunja zile nguzo za Baali, na kuiharibu nyumba ya Baali na kuifanya choo, ambacho kipo hadi leo.
28 Kwa hiyo Yehu akaangamiza kuabudiwa kwa Baali katika Israeli.
Hivi ndivyo ambavyo Yehu alivyomharibu muabudu Baali kutoka Israeli.
29 Hata hivyo, Yehu hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda, yaani kuabudu ndama za dhahabu huko Betheli ya Dani.
Lakini Yehu hakuacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo ilfanya Israeli kutenda dhambi-ambayo ni, kumwabudu ndama wa dhahabu katika Betheli na Dani.
30 Bwana akamwambia Yehu, “Kwa kuwa umefanya vyema kwa kutimiza yaliyo sawa machoni pangu, na umetenda kwa nyumba ya Ahabu yale yote niliyokuwa nimekusudia kutenda, wazao wako wataketi juu ya kiti cha enzi cha Israeli hadi kizazi cha nne.”
Hivyo Yahwe akamwambia Yehu, “Kwa kuwa umefanya vema kwa kufanya yaliyo sahihi kwenye macho yangu, na kumailiza kwenye nyumba ya Ahabu kulingana na yote yaliyokuwa kwenye moyo wangu, uzao wako utakaa kwenye kiti cha Israeli hadi kizazi cha nne.”
31 Lakini Yehu hakuwa mwangalifu kushika sheria za Bwana, Mungu wa Israeli, kwa moyo wake wote. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda.
Lakini Yehu hakujali kutembea kwenye sheria ya Yahwe, Mungu wa Israeli, kwa moyo wake wote. Hakugeuka kutoka kwenye dhambi za Yeroboamu, ambayo iliwafanya Israeli kutende dhambi.
32 Katika siku hizo, Bwana akaanza kupunguza ukubwa wa Israeli. Hazaeli akawashinda Waisraeli sehemu zote za nchi yao
Siku zile Yahwe akaanza kupunguza mikoa ya Israeli, na Hazaeli kuwashinda Waisraeli mipakani mwa Israeli,
33 mashariki ya Yordani, katika nchi yote ya Gileadi (eneo la Gadi, Reubeni na Manase), kutoka Aroeri karibu na Bonde la Arnoni kupitia Gileadi hadi Bashani.
kutoka Yordani upande wa mashariki, nchi yote ya Gileadi, Wagadi, na Wareubeni, na Wamanase, kutoka Aroeri, alipo karibu na bonde la Arnoni, kupita Geleadi hadi Bashani.
34 Kwa matukio mengine ya utawala wa Yehu, yote aliyofanya na mafanikio yake yote, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
Kama kwa mambo mengine yamhusuyo Yehu, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake, je hayakuandikwa kwenye kitabu cha matukio ya wafalme wa Israeli?
35 Yehu akalala pamoja na baba zake, naye akazikwa huko Samaria. Naye Yehoahazi mwanawe akawa mfalme baada yake.
Yehu akalala na wazee wake, na walimzika katika Samaria. Kisha Yehoahazi mwanaye akawa mfalme katika sehemu yake.
36 Muda Yehu aliotawala juu ya Israeli huko Samaria ilikuwa miaka ishirini na minane.
Mda ambao Yehu alitawala juu ya Israeli katika Samaria ulikuwa miaka ishini na nane.